March 19, 2008

Machi Mwaka 2002;Yasinta Kwanini,kisa kinaendelea.

Nimerudi na kisa kileee kinachonihusu pengine zaidi ya kunihusu na kinawahusu wengine,mimi sijui.Hebu ngoja nikiandike tena hapa maana siyo mimi labda wengine kinawahusu.Mwezi machi 2002,Yasinta katoroka kwao,kamkimbia baba,mama na nduguze,wala hataki kusema anakokwenda.Nyumbani wazazi wanashangaa mwenetu tumpendaye kaondoka bila kuaga ni maajabu hayo.Yasinta katua Mbinga mjini,katulia stendi na raifikiye Vumilia wanapiga soga za hapa na pale lakini hatimaye mnyasa anatokea,ana-afro, katweta ghafla anajiuliza huyu binti vipi?Haya soga za hapa na pale wanakumbushana na mnyasa enzi wakiwa shule,lakini mnyasa anauliza kulikoni upo hapa? mara ghafla Yasinta anaomba "tafadhali ukiulizwa kuhusu kuniona mimi{yeye}usiseme".Mnyasa anashangaa kumbe binti katoroka nyumbani kumfuata mpenzi?Jamani kupenda tabu,mapenzi ni kikohozi kuficha huwezi aliimba Fresh Jumbe.Binti amependa hataki shule hataki kusikia maonyo ya wazazi,masikio kaziba pamba,mahaba yamekolea, lakini kwakuwa mnyasa anamjua vema akasaili hee mwenzangu nimesikia hutaki shule kulikoni?Sipewi jibu, nazungushwa huku na huko binti anajiona kumaliza kidato ni mwisho hakuna tena hamu ya shule kisa mapenzi mmh.Mwishowe mnyasa anashauri vipi uahirishe safari,looh.. akaambiwa alipe nauli aliyolipia tiketi kisha awezekuahirisha safari,mnyasa akaduwaa akasema huyu siku hizi kawa mbogo wa mapenzi.Lakini kwani mnyasa akawa anajua hapa anapenda lakini kwa mtindo huu acha ajifanye hana hizo hela,unajua shilingi ngapi?Watu wa Mbinga wanajua wakati huo nauli mpaka makao yetu makuu Songea ni....samahani sitasema.Binti anasafiri anakwenda kuonana na mpenzi wake,waubani wake, mwandani wake,yaani ampendaye.Mmh wapi bwana yako wapi hayo mapenzi mathubuti?kuna kuacha shule tena?Mbona yupo huko.......kwenye baridi anasoma,sijui kwa ari au ndiyo wasomi wetu wa siku hizi.Kifupi alicharukia mapenzi,akaona ganda la mua la jana........na masikitiko ya mnyasa kwa kuwa alimpenda basi katoa kauli za kulaani na bado zinamtesa,yako wapi mbona bado kasheshe inaendelea?Maisha ya Lundo yalikuwa ni simulizi murua.Ngoja nikomee hapa kwa leo.

March 17, 2008

Nyasa na Mambo ya nyakati hizi

Kipindi hiki ni cha masika kwa wanyasa wengi kwani hutumia kwa shughuli za kilimo na uvuvi pia.Ni kipindi cha wavuvi kufanya kazi mbili yaani uvuvi na kilimo kwani hii husadia kujipatia kitoweo na mlo wa uhakika katika maisha yao.Kwa kawaida hapa nyasa tunalima mihogo,mpunga na mazao mwengine pia hata viazi hupatikana.Sasa wakati huu kuna aina ya samaki ambao kupatikana kipindi kingine ni adimu hivyo watu wako makini na hilo kwani ndilo linalowafanya wawepo hapa nyasa.Juzi hapa nilikuwa kijiji cha Mbaha nikakutana na watu wanatoka mashambani na kujimwaga ziwani huku wakiwa na majembe yao.Nikwauliza vipi jamani majembe mpaka ziwani wakaniambia ni bora kuunganisha tu pale unapotoka shambani kwani ukienda nyumbani mwili huchoka hivyo kazi inendelea.Hawa jamaa walinishangaza kwani kazi waliyofanya ni ngumu lakini wanakwenda kutoa nyavu zao walizotega ili kupata mlo,yaani kwa mnyasa bila samaki hawezi kukamilisha siku.Kuna jamaa mmoja hapa alinidokeza kwamba imani juu ya samaki ni kubwa ndiyo maana wanyasa hawana tatizo la kuongezewa damu kwani wanakula mboga za majani za asili na aina ya mapishi yao ni ya asili hivyo hayana hata kemikali zozote.Mwingine leo kaniambia hata kama wengine watabeza lakini hawaondoki nyasa hata kidogo.Halafu kuna jamaa ananiuliza hapa pembeni hiki ninachoandika,wakati anayo kompyuta yake wala haoni haya kuchungulia maandiko haya ya wanyasa,nimemkasirikia halafu namtazama kama samaki wanaojificha kwenye makoro makubwa,unawajua,ni mandongo.Yani haachi eeeh wewe jamaani vipi.Kumbe mmatengo

March 13, 2008

Samaki anaujanja Mezani?

Moja ya mitaala ya maisha ya Wanyasa ni uvuvi.Huu ni ukurasa mkuu wa kijana wa kinyasa kujifunza au kuusoma vyema uvuvi atake asitake.Mtaala huu huvutia sana ikiwa unazingatia kanuni zake.Wanyasa wengi wanawafundisha watoto wao namna ya kuoposha samaki au kutega nyavu na mambo mengine yahusuyo uvuvi.Kwa kijana wa kinyasa kuvua samaki ni fahari na ni utamaduni murua kwa maisha yake ya kila siku.Huu unamaana kwamba huwezi ukamweka samaki mezani halafu akaleta ujanja kwani ujanja wake ni kabla ya kufika hapo vinginevyo ameliwa.Kuzaliwa kijana wa kinyasa halafu akakwepa angalao kujifunza namna ya kuvua samaki ni kukiuka tamaduni na utaratibu wa Wanyasa.Ndiyo maana nilianza kublogu kuhusu nyasa yaani kuwapa watu kitu tofauti na mambo ya wanasiasa.Kwa mnyasa na mtoto wake maisha hayo wala siyo mateso bali ni fahari na nuru ya kutumikia utamaduni wake wa kila siku.Kijana anajifunza mbinu za kuvua samaki katika vipindi tofauti toka kipindi cha kiangazi na aina ya samaki wake,masika aina ya samaki wake na vipindi vingine ambavyo kwa wanyasa hufahamu mbinu na uelekeo wa samaki n.kMitaala nina maanisha kwamba utaratibu kamili wa kila siku kwa wavuvi wa samaki,hivyo ili mtoto wa kinyasa afuate kanuni au asifuate basi asizaliwe nyasa.Kutozaliwa nyasa labda unaweza kuleta ujanja mezani,lakini kwa mtoto wa kinyasa hana ujanja kwani tayari amezaliwa eneo lenye ubora wa kutukuza tamaduni zake.Ukiwaona wanyasa lazima utagundua kwani hawapendi ujanja wa mezani bali wao hushindana na mawimbi ya ziwa lenye mawimbi kuliko yote duniani la Nyasa,je wewe uliyezaliwa nyasa unaweza kuleta ujanja?Je samaki anaujanja mezani? kilichobaki ni kuliwa tu,na kijana wa kinyasa lazima uvua samaki tu hata kama atapa shahada za uzamili za mbinguni lakini aliwahi kuvua au siyo wanyasa wenzangu.msikasirike haya mawazo tu..!!!!!