March 23, 2008

Shamrashamra,Vifijo,Shangwe na Mbwembwe za Wanyasa

Jana nilikuwa na wanyasa hapa kijijini kwetu,jambo la kwanza nililojiuliza ni je wanyasa watakula nini au watasherekea vipi sikukuu hii ya pasaka kwa wakristo.Nikawafuata wazee wa mila wajuao desturi na tamaduni zetu ili wanipe mbwembwe na shamrashamra za kale kwa wanyasa.Nikaambiwa nyakati hizi kwa vijana ni hatari sana kwani mengi ambayo kale hayakuwapo yapo,hivyo shangwe hizo ziendane na kujihadhari japo kidogo.Zamani wazee wetu walikuwa wakitayarisha samaki kwa ajili ya wanyasa waishio mijini ili wakija kupumzika kwao waone kweli wapo nyasa,lakini kipindi hiki ile hali ya kujali imepungua na chanzo ni kubadilika kwa mfumo wa maisha ya mwanadamu.Basi unaambiwa wanyasa wanacharaza ngoma za Lendeku,madogori na nyingine nyingi,vijana walichangamka jana wakasahau machungu ya kulima nyakati hizi.watoto wanarukaruka kwa mikogo kuifurahia sikukuu hii,wamebeba virugu vya kutwanga wenzao{kama mchezo fulani hivi},wazee wanasema vijana wa siku hizi hawajiamini kama kale.Naambiwa vipi kujumuika kuselebuka mimi naulizia hayo mambo,nikajibu ni moja ya kusherekea pia kwani napata nasaha za wazee wa jadi wenye kila aina ya thawabu.Basi unaambiwa kuku wakienyeji wamechinjwa{hakuna kuku wa kisasa huku},mbuzi,ng'ombe na wengine waliwinda sungura na wanyama wengine kwa ajili ya kitoweo,hizi ni nyakati za wanyasa kusahau samaki kidogo na ugali wao wa muhogo lakini lazima samaki awepo ili kukamilisha unyasa wetu.Watu wamejazana wanafurahi sana jumamosi yenyewe kabla ya jumapili.Ni porojo za hapa na pale yaani kila mnyasa ni furaha tupu,mungu awalinde wanyasa wenzangu hawa.ngoja nikomee hapa kwa leo.

March 19, 2008

Machi Mwaka 2002;Yasinta Kwanini,kisa kinaendelea.

Nimerudi na kisa kileee kinachonihusu pengine zaidi ya kunihusu na kinawahusu wengine,mimi sijui.Hebu ngoja nikiandike tena hapa maana siyo mimi labda wengine kinawahusu.Mwezi machi 2002,Yasinta katoroka kwao,kamkimbia baba,mama na nduguze,wala hataki kusema anakokwenda.Nyumbani wazazi wanashangaa mwenetu tumpendaye kaondoka bila kuaga ni maajabu hayo.Yasinta katua Mbinga mjini,katulia stendi na raifikiye Vumilia wanapiga soga za hapa na pale lakini hatimaye mnyasa anatokea,ana-afro, katweta ghafla anajiuliza huyu binti vipi?Haya soga za hapa na pale wanakumbushana na mnyasa enzi wakiwa shule,lakini mnyasa anauliza kulikoni upo hapa? mara ghafla Yasinta anaomba "tafadhali ukiulizwa kuhusu kuniona mimi{yeye}usiseme".Mnyasa anashangaa kumbe binti katoroka nyumbani kumfuata mpenzi?Jamani kupenda tabu,mapenzi ni kikohozi kuficha huwezi aliimba Fresh Jumbe.Binti amependa hataki shule hataki kusikia maonyo ya wazazi,masikio kaziba pamba,mahaba yamekolea, lakini kwakuwa mnyasa anamjua vema akasaili hee mwenzangu nimesikia hutaki shule kulikoni?Sipewi jibu, nazungushwa huku na huko binti anajiona kumaliza kidato ni mwisho hakuna tena hamu ya shule kisa mapenzi mmh.Mwishowe mnyasa anashauri vipi uahirishe safari,looh.. akaambiwa alipe nauli aliyolipia tiketi kisha awezekuahirisha safari,mnyasa akaduwaa akasema huyu siku hizi kawa mbogo wa mapenzi.Lakini kwani mnyasa akawa anajua hapa anapenda lakini kwa mtindo huu acha ajifanye hana hizo hela,unajua shilingi ngapi?Watu wa Mbinga wanajua wakati huo nauli mpaka makao yetu makuu Songea ni....samahani sitasema.Binti anasafiri anakwenda kuonana na mpenzi wake,waubani wake, mwandani wake,yaani ampendaye.Mmh wapi bwana yako wapi hayo mapenzi mathubuti?kuna kuacha shule tena?Mbona yupo huko.......kwenye baridi anasoma,sijui kwa ari au ndiyo wasomi wetu wa siku hizi.Kifupi alicharukia mapenzi,akaona ganda la mua la jana........na masikitiko ya mnyasa kwa kuwa alimpenda basi katoa kauli za kulaani na bado zinamtesa,yako wapi mbona bado kasheshe inaendelea?Maisha ya Lundo yalikuwa ni simulizi murua.Ngoja nikomee hapa kwa leo.

March 17, 2008

Nyasa na Mambo ya nyakati hizi

Kipindi hiki ni cha masika kwa wanyasa wengi kwani hutumia kwa shughuli za kilimo na uvuvi pia.Ni kipindi cha wavuvi kufanya kazi mbili yaani uvuvi na kilimo kwani hii husadia kujipatia kitoweo na mlo wa uhakika katika maisha yao.Kwa kawaida hapa nyasa tunalima mihogo,mpunga na mazao mwengine pia hata viazi hupatikana.Sasa wakati huu kuna aina ya samaki ambao kupatikana kipindi kingine ni adimu hivyo watu wako makini na hilo kwani ndilo linalowafanya wawepo hapa nyasa.Juzi hapa nilikuwa kijiji cha Mbaha nikakutana na watu wanatoka mashambani na kujimwaga ziwani huku wakiwa na majembe yao.Nikwauliza vipi jamani majembe mpaka ziwani wakaniambia ni bora kuunganisha tu pale unapotoka shambani kwani ukienda nyumbani mwili huchoka hivyo kazi inendelea.Hawa jamaa walinishangaza kwani kazi waliyofanya ni ngumu lakini wanakwenda kutoa nyavu zao walizotega ili kupata mlo,yaani kwa mnyasa bila samaki hawezi kukamilisha siku.Kuna jamaa mmoja hapa alinidokeza kwamba imani juu ya samaki ni kubwa ndiyo maana wanyasa hawana tatizo la kuongezewa damu kwani wanakula mboga za majani za asili na aina ya mapishi yao ni ya asili hivyo hayana hata kemikali zozote.Mwingine leo kaniambia hata kama wengine watabeza lakini hawaondoki nyasa hata kidogo.Halafu kuna jamaa ananiuliza hapa pembeni hiki ninachoandika,wakati anayo kompyuta yake wala haoni haya kuchungulia maandiko haya ya wanyasa,nimemkasirikia halafu namtazama kama samaki wanaojificha kwenye makoro makubwa,unawajua,ni mandongo.Yani haachi eeeh wewe jamaani vipi.Kumbe mmatengo