March 29, 2008

Wanyasa wangali wakiselebuka na Nyakati maalumu

Amini usiamini,utake usitake wanyasa ni wanadamu wanaofahamu namna ya kuzitumia hizi nyakati maalumu.Hawasiti kuselebuka kwa raha zao huku wakipiga ngoma za Lindeko,Madogoli n.k lakini kuna jambo nilisahau wakati naandika hapa kuhusu shamrashamra hizo,kuna aina fulani ya ngoma nilizisahau lakini kwa bahati mbaya,lakini nimekumbushwa na dadangu wa blogu ya Ruhuwiko{ngoja nitaandika ili uisome blogu yake},kanikumbusha Lizombe,Muhambo wa wamatengo,nami dakika hii nakumbuka Chomanga,mganda,makanya,sindo n.k
Kwa sasa huku Nyasa ni kama nyakati maalumu zipo kila siku kwani watu tunaselebuka kwa raha na kusahau uchungu fulani wa maisha{bila shaka unajua namaanisha nini}.Huku watu wajipa likizo isiyo na malipo,wanakunywa pombe zao za asili komoni,lihutapahi,mbege,chimpumu ya wamatengo na hizi zinazozalishwa huko mjini kifupi hazina soko hapa nyasa hazitakiwi.Basi jumapili ya pasaka yenyewe watu wamependeza,wafurahia siku hiyo,wanatabasamu hapa na pale wanakumbushana pasaka ya miaka iliyopita n.kWatu wanakumbuka mambo mengi ya kitamaduni ambayo yanawafanya waone fahali kuzaliwa na kuishi nyasa.Yaani mambo bado yanaendelea hapa watu hatujapumzika na wala nilipoibukia pale Mbinga sikapenda kukaa sana nikarudi nyasa ili nijionee furaha hizi.Siyo siri dadangu pale Sweden amekumbuka mengi anakosa nyakati hizi kwa wanyasa.Hii ndiyo nyasa watu wanajimwaga mitaani.Lakini kikubwa unywaji wa pombe hizi mjini hutumia mishkaki lakini hapa watu kama kawaida yao samaki maarufu kwa jina la "Kapili" yaani ni kama 'kachumbari' ya pombe kwa walevi na wanywaji .Samaki hawa wanakuwa wamekwisha kuchomwa na kukaushwa vyema basi inakuwa utamu juu ya utamu na pilipili pembeni yake.Wasiolewa kazi yao kukumbushana na kujadili maisha n.k kina dada wanajumuika kupiga gumzo na kina kaka maana ni nyakati maalumu hizi huja mara chache.Watu wanafurahia maisha acha wajifurahie

March 23, 2008

Shamrashamra,Vifijo,Shangwe na Mbwembwe za Wanyasa

Jana nilikuwa na wanyasa hapa kijijini kwetu,jambo la kwanza nililojiuliza ni je wanyasa watakula nini au watasherekea vipi sikukuu hii ya pasaka kwa wakristo.Nikawafuata wazee wa mila wajuao desturi na tamaduni zetu ili wanipe mbwembwe na shamrashamra za kale kwa wanyasa.Nikaambiwa nyakati hizi kwa vijana ni hatari sana kwani mengi ambayo kale hayakuwapo yapo,hivyo shangwe hizo ziendane na kujihadhari japo kidogo.Zamani wazee wetu walikuwa wakitayarisha samaki kwa ajili ya wanyasa waishio mijini ili wakija kupumzika kwao waone kweli wapo nyasa,lakini kipindi hiki ile hali ya kujali imepungua na chanzo ni kubadilika kwa mfumo wa maisha ya mwanadamu.Basi unaambiwa wanyasa wanacharaza ngoma za Lendeku,madogori na nyingine nyingi,vijana walichangamka jana wakasahau machungu ya kulima nyakati hizi.watoto wanarukaruka kwa mikogo kuifurahia sikukuu hii,wamebeba virugu vya kutwanga wenzao{kama mchezo fulani hivi},wazee wanasema vijana wa siku hizi hawajiamini kama kale.Naambiwa vipi kujumuika kuselebuka mimi naulizia hayo mambo,nikajibu ni moja ya kusherekea pia kwani napata nasaha za wazee wa jadi wenye kila aina ya thawabu.Basi unaambiwa kuku wakienyeji wamechinjwa{hakuna kuku wa kisasa huku},mbuzi,ng'ombe na wengine waliwinda sungura na wanyama wengine kwa ajili ya kitoweo,hizi ni nyakati za wanyasa kusahau samaki kidogo na ugali wao wa muhogo lakini lazima samaki awepo ili kukamilisha unyasa wetu.Watu wamejazana wanafurahi sana jumamosi yenyewe kabla ya jumapili.Ni porojo za hapa na pale yaani kila mnyasa ni furaha tupu,mungu awalinde wanyasa wenzangu hawa.ngoja nikomee hapa kwa leo.