April 23, 2008

Kutoka Nyasa + Marekani =Kurudi Teja

Ndiyo kuna jamaa mmoja hapa amenishangaza kama siyo kuniacha hoi,ni kisa hiki lazima nikiweke hapa ili tuelimishane wanyasa.Huyu jina lake maarufa la Kessi.Kipindi cha nyuma alifanikiwa kuwepo nchini Marekani kwa Joji Kichaka,akiwa huko aliishi na dada yake.Lakini pamoja nia nzuri {sina hakika kama ni nzuri} ya dada yake kuishi naye huko jamaa kawa ovyoovyo hata haeleweki.Akaanza kubwia madawa ya kulevya,akapiga kete hizo kwa kipindi kadhaa mpaka akawa mwendawazimu sasa.Basi jamaa karudi nyasa hapa kawa kituko heshima yake imetoweka siyo kama awali,akili yake haina tofauti na kichaa shauri ya madawa hayo,hajiwezi kwani maisha ameyachezea sana.Alipokuwa hapa nyasa kipindi cha nyuma na baadaye kupata nafasi ya kwenda kwa akina Joji Kichaka hakuwa hivyo,ila sasa hali ni mbaya,usicheke tafadhali.Siyo siri hali ya Kessi ni mbaya ,akili yake ovyoovyo wala hajielewi shauri madawa ya kulevya yamemwathiri .kwasasa anaweza kuongea na kucheka pekee yake kwa siku nzima huku akikumbuka namna alivyokuwa akibwia kete za madawa ya kulevya na rafiki zake.Hivi wewe unayesoma hapa hiki kisa kinakukuna sana?unajifunza nini?unatumia madawa ya kulevya?na hii hata hiyo bangi mnayotumia vijana wa kisasa eti ni fasheni au kuongezea mzuka,midadi n.k kumbukeni ukichaa unawanyemelea karibuni.Madawa ya kulevya ni hatari jihadharini sana,ndiyo maana nasema kutoka nyasa+marelani=kurudi.

April 20, 2008

Ziwa Limechafuka,Wanyasa na Ngalawa Tu

Nilikaa juu ya jiwe nikiangaza huku na huko kuwatazama wanyasa wanavyohaha katika shughuli zao za maisha ya hapa na pale.Nikaona ngalawa zinaumiza vifua vya wanyasa kwani hali siyo nzuri katika ziwa kwa sasa.Hakika ziwa nyasa limechafuka namaanisha dhoruba kali sana wiki hili,kila myasa/mvuvi unayemuona kanuna,kafura kama chatu ghadhabu imejaza vibaba wala haimithiriki zaidi ya hapo,hawacheki.Ziwa linanguruma mawimbi makali makali,nyavu zinapotea nyakati hizi shauri maboya yanazama kwa kushindwa kuhimili nguvu ya mawimbi.Lakini pamoja na kuchafuka kwa ziwa hilo hakuna hata mvuvi anayethubutu kusema atabaki nyumbani kujipumzisha au kurejesha zana za uvuvi nyumbani ili kupisha dhoruba hiyo,wapi bwana sahau kabisa habari ya wanyasa kuogopa dhoruba nyakati hizi au kuacha ngalawa ili kukosa kitoweo,hakuna mnyasa anayefikiri kula nyama za kuku wasiokomaa,wanaotafunika hata mifupi,wanaokuzwa kwa kudungwa sindano,wanatia kinyaa kuwala,au chipsi za huko mijini.Wanyasa wanaelewa uzuri wa kuwa wajuzi wa ziwa hili ambalo wenyewe wanasadiki kuwa hakuna ziwa lenye dhoruba kali ulimwenguni zaidi ya hili.Hakuna aliyeka chini kuacha ngalawa au kuacha kupanda mitumbwi.Yaani uvuvi unaendelea kana kwamba ziwa lipo shwari wakati "limekasirika" utafikiri limedungwa sindano ya kukasirika.Yote hao ni kitoweo cha asili hiki utamu adimu huu.