15 September 2010

UWONGO WA MCHUNGAJI HAROLD CAMPING

Ninajibu swali la Oscar wa mjini Songea ambaye alituma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi usemao ‘Harold Camping mhubiri wa Radio Family wa Marekani anasema Mei 21-2011 watakatifu watakwenda mbinguni na hapo ndipo mwisho wa dunia’(mwisho wa kunukuu).

Niseme mapema kwamba, mahubiri ya aina hii siyo mageni kwangu, nimeyasikia mara nyingi sana, na mmojawapo ni mhubiri Benny Hinn wa hukohuko Marekani. Huyu alibashiri mengi kwamba yatatokea, lakini hakuna lililojiri hata moja. Soma uwongo wa Harold Camping katika kitabu chake; TIME HAS AN END.

Soma hapa makala nzima, USIPITWE

1 comment:

 1. Sina cha kuongezea isipokuwa tu kusema kwamba hata kanisa la Waadventista Wasabato limetokana (au pengine niseme limeathirika sana) na utabiri wa aina hii. Wao walitabiri kwamba dunia ingekoma tarehe 22 Oktoba 1844. Baadaye walidai kwamba walikuwa wamekosea mahesabu yaliyoko katika kitabu cha Danieli na wakapendekeza tarehe nyingine bila mafanikio yo yote.

  Ukristo wa leo umeingiliwa na umegeuka kuwa biashara kubwa sana. Watu wanauza maji, mafuta, vitambaa, miujiza na hata unabii. Hapa Marekani usingizi ukikugomea na uwe macho mpaka saa saba za usiku ndiyo utaona mengi. Wapo ambao mpaka wanaenda mbali na kusema kwamba uwatumie dola 1,000 na baada ya siku saba utapata muujiza mkubwa wa kufaidika kifedha. Usipopata muujiza wa aina hiyo basi wanakurudishia pesa zako (ingawa ukweli ni kwamba kiendacho kwa mganga huwa hakirudi). Mtu unaweza kujiuliza - tangu lini miujiza ya Mungu ikauzwa? Na wahubiri wengi wanaotamba katika runinga ni matajiri wa kutupwa (mmoja hapa alikuwa anachunguzwa kwa kujinunulia choo -ile sehemu ya kukalia tu - cha dola 15,000 kwa kutumia pesa za kanisa ambazo huwa hazitozwi kodi) na wakati huo huo wakiwahimiza wafuasi wao watoe kila kitu walicho nacho.

  Makanisa mengi yamegeuka kuwa kumbi za starehe tu na huwezi tena kusikia mahubiri ya kutubu dhambi na kuokoka. Mahubiri yaliyotawala ni yale ya kutajirika na kujifurahisha. Dhambi na wokovu wa bure kupitia kwa damu ya Yesu Kristo kamwe havitajwi kwani ukivitaja basi utawaudhi watu na wanaweza wasije tena kanisani kwako.

  Nadhani huu ni wakati wa KUSHIKA SANA TULICHONACHO kama vile tulivyokwishaonywa katika Biblia.

  Mada nzuri!!!

  ReplyDelete

Andika maoni yako