22 March 2011

DADA KOERO, UNANILIZA!
Dada Koero,
Asante kwa salamu yako,

Dada Koero, juzi nilijawa furaha sana baada ya kupata barua yako. Kilichonifurahisha ni wewe kuhusudu kutumia shirika la posta kuniandikia barua. Mmh! Yaani siku hizi hata matumizi ya barua kwa njia ya posta watu hawataki, ati ni kizazi kipya.

Umenifurahisha sana. Nakutunuku upendo uliopevuka dada yangu, hakika malezi ya baba yetu yamekolea kwako. Si unajua mambo yale ya Posta na Simu, ukiandika barua inasota mwezi mzima, lakini ukiipata raha tupu, hamu ya kusoma inakutekenya yaani nakumbuka zamani!

Pia nikupe pongezi kwa majukumu maana nikisema pole nakukatisha tamaa dada yangu na ukumbuke baba alisema inawezekana timizi wajibu wako.

Najua majukumu ni muhimu maana malezi ya familia yetu sasa yameharibika, kiongozi wetu alikuwa na busara za bandia, kama hadithi za almasi za bandia, kwahiyo lazima dada yangu Koero uchukue jukumu hilo kutusaidia.

Halafu nikutoe shaka, najua hatujawasiliana kwa muda mrefu, lakini barua yako imenitosha,moyoni imetamalaki, imesahau kama hatukuwasiliana. Barua yako imekata kiu kinywa chapwa, sasa naisoma kila siku na umejaliwa mwandiko maridadi.

Dada umenikumbusha mbali uliponiambia umeniandikia barua ukitumia kibatari. Unakumbuka kidogo wakati baba akiwa hai tulikuwa tunatumia karabai kusomea pale shuleni? Umenikumbusha mbali kidogo, lakini baba alitupenda sana.

Nisikuchoshe dada yangu, nami nijikite katika dhumuni la barua yangu. Dada umeniambia mengi mazuri na yanafikirisha.

Nimekaa nikavuta kumbukumbu, nikakumbuka baba alipoona kiongozi wa familia anajitia kimbelembele enzi Che Nkapa akipewa taji. Baba alisema maneno haya; “mkiwaachia vijana hawa familia hii, mtapata shida huko.”

Halafu unakumbuka alimwuliza yule aliyekuwa msaidizi wake mwanzoni wa uongozi wa familia yule mwenye nywele nyeupe kama zeruzeru, baba akasema, “na wengine mmejikusanyia mali, wewe (akamnyooshea kidole) hizo mali unaweza kutueleza umepataje.”? Nakwambia hakujibu.

Sasa dada, tumejua kiongozi wa familia amevuruga familia nzima. Hebu nikueleze kidogo. Unajua wakati baba akiasa mengi ya busara aliona kwamba wapo viongozi wa familia ambao hawana lolote zaidi ya kunyakua madaraka.

Nakwambia sasa hivi najiuliza inakuwaje kiongozi anasema miaka mitano alikuwa anajifunza? Si unakumbuka mtu huyu alikuwa kiranja wakati tunaingia mkataba wa umye-mye wa AIPITIELO?

Nakwambia watu wengine wameingia kuongoza familia yetu kutimiza ndoto zao kama mtu anapoota kukuoa wewe dada yangu mpendwa, ati anajua Koero mlimbwende, wakati anajua ataishia kula ugali kwa harufu ya samaki mbasa.

Kalaghabahooo!! dada najua utamkumbuka baba mwenye nyumba yako (chyemeji chyemeji), mmmh! Halafu nasikia ana wivu eti dada ya kweli hayo? Tuache, utani huyo ndio chyemeji chyemeji wa ukweli, wivu wake analinda chake!

Jamani kiongozi wa familia juzi juzi alisema hamjui yule mwenye kanzu anayemiliki DowJones kama kweli mweeee ama kweli jamba jamba tunaipata, namkumbuka baba yetu.

Mimi nikamuuliza mama, eti mama kiongozi wa familia hii nani? Mama hakujibu. Nikaongeza, tunapofanya kikao cha familia tunaongozwa na nani? Mama hakujibu.

Sikunyamaza, nikasema hivi huyu jamaa anayetusumbua na DowJones aliingia wakati gani? Mama hakujibu. Niliendelea, hivi mama kiongozi wetu katika familia anapojiondoa kutohusika anafikiri tunamzungumzia binafsi bila familia yetu?

Nikachoka, nikapoa kama maji mtungini. Niligundua Mama anadonge la hasira. Nikaongeza, mbona kiongozi wa familia yetu ni mwepesi kwa mambo mepesi lakini amekuwa mzito kama gunia la maharagwe ya Ileje kwa mambo mazito na muhimu?

Mama akanikazia jicho kali. Dada utasema mimi nabishana, lakini mbona wakati wa maroroso ya DowJones alituambia eti hakuona ulazima wa kuongea, wakati wale Kyadema walipomchokoza kwa siku tisa ameongea upesi? Harara hizo za nini?

Dada, mwenzio nilimshiti tangu mwaka 2008 kusikiliza vikao vyake vya kila mwezi kwenye familia yetu. Niliona kila anachoongea ni mandondo tu ya watani wangu Wanyakyusa. Wala simfuatilii, nataka amalize muda wa kuiongoza familia hii aende zake! Apotelee mbali!

Dada, nikunong’oneze, lile likesi la DowJones na Tako na nesko ninalo, nililisoma hadi ukurasa wa 337 nikatupa uvunguni mwa teremka nikukaze, si unanikumbuka kile kitanda chetu cha urithi? Basi, hilo likesi ukilitaka nitalifyatua kopi.

Halafu familia ya Mzee Tusitusi, Msisiri na Libelibe tuwaachie wenyewe, lakini afadhali wale wa mzee Msisiri maana wamepoa na wana nidhamu kweli. Lakini dada nakwambia kwa mzee Libelibe na Tusitusi watanyolewa nywele kwa kisu haki ya mungu nakwambia.

Lile lijamaa la Tusitusi linaumwa kufua cha kuharisha! Ha! ha! ha! ha! Mmmh! Nacheka hadi mkojo umechuruzika, aibu!!

Lakini najiuliza wale wanaompinga mzee Libelibe walipata wapi silaha za kuteka ghala ya silaha pale Beghaza? Tuache hilo, la muhimu ni maisha ya wenzetu itakuwaje.

Hofu yangu hata mzee Libelibe akioondoka kuna watu wanataka minofu! Wakipata uchochoro tu wanachukua treni la michuzi. Patachimbika, lakini lawama kwa mzee Libelibe.

Sasa wamewakataa baba zao, sijui itakuwaje. Unafikiri na sisi tuwakatae eti dada, wewe unaonaje? Mmh! Mimi naona tufanye hivi, si unakumbuka baba alisema kila miaka mitano tuchague kiongozi.

Ngoja nakwambia jamba jamba ya mwaka jana, basi watakoma mwaka huo ujao wa kuchagua, halafu ule wa elfu 2 na 20 jamba jamba itakuwa kali, niamini. Sababu mimi na wewe ndio tutakuwa wazee wakushauri vijana wachague kiongozi wa familia yetu.

Pata picha sisi ndio tukiwa wazee wa kushauri unadhani utashauri wafanye nini kama siyo kumchojoa viwalo vyake na kumtandika bakora? Itakuwa mbindinge, ngumi jiwe, mstari kwa mstari hatutaweka mabano bali tutafungua mabano, hatutaki mfano.

Dada unajua sisi tuna utamaduni tofauti sana. Hata huyo kiongozi bandia wa familia anapowaogopa wale wavaa kombati ni aibu yake. Wale wavaa kombati wamegundua ili kuongea na familia lazima waje nyumbani kwetu tusogoe zaidi.

Lakini nina uhakika hawawezi kutushawishi tufanye kama kwa mzee Libelibe, Msisiri na Tusitusi maana wanajiheshimu kweli na wako makini wale. Wanafamilia najua hatuwezi kuchukia kiasi cha kumtaka kumzomea eti huyoooooo! Amefuliaaaa!!

Najua tumemkataa kwa kumpa jamba jamba mwaka jana na 60% zake. Si unakumbuka mwaka ule wa elfu 2 na 5 alipata 80%? Pima mwenyewe.

Halafu mwaka ule mara ya kwanza Beni Che Ukapa alipata watu milioni 17 walimchagua kuongoza familia yetu. Mara ya pili watu milioni 15. Niambie dada unagundua kitu gani hapo? Lakini mwaka ule elfu 2 na 5 kiongozi wa familia alipata 80% kwa watu milioni 9.

Unaona? Ushindi wa kishindo lakini watu wanasusa, wamegoma na hawataki. Unakumbuka wengine walilaumu eti ile tume ya kusimamia kuchagua haituambii umuhimu wa kuchagua? Watu wamesusa,wanaendesha mgomo baridi, hawataki na wanasubiri aondoke zake tu.

Nikomee hapa kwa leo. Nikipata nauli nitakuja. Msalimie mzee kifurushi pale magogoni.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako