Zipo nchi kadhaa zilizomeguka kuunda pande zake, kwa mfano; Korea Kusini na Kaskazini au mabara ya Amerika Kusini na Amerika Kaskazini. Vilevile tumeona namna Somaliland inavyopigania kutambuliwa taifa huru tangu mwaka 1991.
Somaliland inaamini itakuwa taifa la 55 katika Bara la Afrika kwani imani yake ya kutambuliwa ni kubwa. Aghalabu mataifa mapya yanakuwa na mipango mingi huku watawala wakiwa na lengo la kuipasha nchi yao.
Sudan Kusini itazinufaisha Kenya, Uganda na jirani zake wengine, lakini bado shaka zipo juu ya uhusiano wake na Sudan Kaskazini. Kulikuwa na kazi kubwa sana hadi Rais wa Sudan, Omar El Bashir kuridhia matokeo ya kura za maoni ya kuundwa kwa taifa la Sudan Kusini.
Sababu kubwa ni mgogoro unaoendelea katika jimbo la Darfur, ambalo wakati fulani mamlaka za kienyeji zilieleza kutaka kujitenga. Jimbo la Darfur limekumbwa na machafuko kwa kipindi kirefu sana.
Aidha, tangu mwaka 2003 baada ya nchi za Magharibi kuingilia mgogoro huo umepanuka zaidi kuliko hali ilivyokuwa awali. Jimbo hilo limeweza kuwagawa wanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wanachama; Russia na China zimekuwa upande mmoja kupinga jitihada zozote za kutekeleza amri ya kukamatwa kwa Rais El Bashir wa Sudan iliyotolewa na mwendesha Mashtaka wa ICC, Luis Moreno Ocampo.
Russia na China ziliwahi kupiga kura ya turufu kupinga mpango wowote wa kijeshi dhidi ya serikali ya Khartoum, huku wanachama wengine Marekani,Uingereza na Ufaransa zikiazimia kutekelezwa kwa mpango huo.
Hata hivyo, mpango huo ulikwama baada ya kura hiyo. Lakini, Russia na China zinahusiana vema na Sudan Kaskazini na zimekuwa nchi zinazoendesha uchmbiaji wa mafuta nchini humo. Hivyo basi suala la msingi hapa ni mafuta ya Sudan Kaskazini, pamoja na jimbo lake la Darfur ambalo linasadikika kuwa na utajiri huo.
Pamoja na Darfur kuwindwa na nchi za kibeberu ili zichimbe mafuta, tayari kuna jimbo jingine ambalo linao utajiri huo. Jimbo hilo ni Abyei. Jimbo la Abyei hadi sasa linagombewa na mataifa haya mawili; Sudan Kaskazini na Sudan Kusini.
Kuna mgogoro unaendelea katika nchi hizi kuhusiana na jimbo la Abyei, lakini sababu kubwa ni utajiri wake wa mafuta. Kila nchi inaona ni lazima jimbo la Abyei iwe mali yake, na huo unakuwa mgogoro.
Kwa mujibu wa UN, mnamo Mei 26 mwaka huu Mji wa Abyei nchini Sudan uliteketea kwa moto huku watu wenye silaha wakipora mali. Mji huo na maeneo mengine umezungukwa na utajiri hivyo kugombewa na serikali ya Khartoum na Juba (Sudan Kusini)
Pamoja na operesheni ya UN nchini Sudan (UNMIS) kueleza inapinga vitendo vya uchomaji moto na uporaji kulikokufanywa na watu wenye silaha katika jimbo la Abyei, bado hali si nzuri baina ya Sudan Kaskazini na kusini.
Kulikuwa na mapigano makali baina ya pande hizo mbili; huku serikali ya Sudan Kusini ikitangaza bayana kwamba hatua za Sudan Kaskazini kutwaa jimbo la Abyei ni sawa na tangazo la vita kati yao kwakuwa jimbo hilo lipo upande wao.
Hadi Mei mwaka huu, Shirika la Madkatari wasio na Mipaka (MSF) lilitoa taarifa kwamba zaidi ya 20,000 wamekimbia makaazi yao. UN ilitoa amri kwa serikali ya Khartoum kuondoa vikosi vyake katika eneo la Abyei.
Jeshi hilo liliteka jimbo la Abyei, ambalo lipo mpakani kati ya Sudan Kusini na Sudan Kaskazini. Ujumbe maalumu wa UN uliotumwa mjini Juba, Sudan Kusini, kwa ajili ya kuzungumza na kiongozi wa eneo hilo, Salva Kiir, ulisema unaangalia kwa makini na kwa undani hali ilivyo katika eneo hilo.
Kana kwamba haitoshi, hivi karibuni Umoja wa mataifa umetangaza kuwa watu 600 wameuawa nchini Sudan Kusini kutokana na mapigano ya kikabila.
Mapigano haya yamefanyika katika jimbo la Jonglei ambapo jamii za Murle na Lou Nuer zilipigana. Kwa mujibu wa mwakilishi wa UN nchni humo, Hilde Johnson alisema mamia ya mifugo imeibiwa kutokana na mapigano hayo.
Taarifa zinaelezwa kuwa ng’ombe kati ya 26,000 hadi 30,000 wameibiwa katika mashambuliano hayo ya wizi wa mifugo. Ukifuatilia kwa umakini juu ya mgogoro huu wa kikabila halafu ukichunguza ule wa jimbo la Abyei ni dhahiri hali si nzuri baina ya nchi hizi.
Sababu Abyei kama tulivyoeleza awali, kuna utajiri mkubwa wa mafuta hivyo kila upande unahitaji kukuza uchumi wake. Pamoja kwamba UN iliamuru majeshi ya Sudan Kaskazini yaondoke, lakini jimbo la Abyei laweza kuwa Darfur mpya ikiwa hatua za makusudi hazitachukuliwa kumaliza mgogoro huo.
Wakati dunia imeshuhudia umwagaji damu na ukiukwaji wa haki za bindamu katika jimbo la Darfur kwa muda mrefu, bila shaka jimbo la Abyei linaweza kufuata mkondo huo. Mgogoro ulipoanza Darfur baina ya wafugaji na wakulima pamoja na upatikanaji mkubwa wa mafuta, mapigano yalizuka zaidi kama inavyotokea sasa Abyei.
Jimbo hili laweza kusababisha mgogoro mkali baina ya Sudan Kusini na Kaskizini, pengine kuvunja uhusiano wan chi hizi mbili. Ni wakati mwafaka, tena kungali mapema kwa watawala wa Juba na Khartoum kuchukua hatua za kukomesha au kumaliza kabisa mgogoro unaoendelea baina ya nchi hizo.
UN haitakiwi kutoa matamko pekee kwani hayana maana na hayatasaidia lolote kwa ustawi wa wananchi wa nchi hizi mbili. Kwasababu mgogoro huu, kwa vyovyote utawagawa wanachama wa Baraza la Usalama la UN, kwani watatazama maslahi yao.
Ni wazi baadhi ya wanachama wa Baraza hilo walioshindwa mpango wa kijeshi hapo awali, sasa watakuwa upande wa Sudan Kusini, hivyo kutanua mgogoro kutegemea mafuta ya Abyei.
Ni lazima tupige kelele, tukaripie na kuchukua hatua. Vinginevyo hali itakayojitokeza kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa itaathiri ustawi wa wananchi wa Abyei. Afrika kwanza, uhuru daima.


0 Changia Maoni:
Post a Comment
Andika maoni yako hapa kwa raha zako