Mlimbwende Salha Israel amekabidhiwa zawadi ya gari aina ya Jeep Patriot lenye thamani ya shilingi milioni 72 na fedha taslimu shilingi milioni 8. Binti huyo ana miaka 18 ambapo alianzia kwa kunyakua taji la mrembo bora wa wialaya ya Ilala, atawakilishi nchi yetu kwenye mashindano ya urembo ya dunia yatakayofanyika nchini Uingereza.
Mshindi wa pili ni Tracy Sospeter aliyekuwa akiwakilisha mkoa wa Shinyanga na kuzawadiwa shilingi milioni 6.2. Mshindi wa tatu alipewa shilingi milioni 4, mshindi wa nne alipewa shilingi milioni 3 huku mshindi wa tano akipewa shilingi milioni 2.4.
Warembo walioingia katika hatua ya 15 bora walizawadiwa shilingi milioni 1.2 kila mmoja. Warembo walioshiriki mwaka huu ni 30 kutoka mikoa yote ya Tanzania. Mwaka huu tumeshuhudia mashindano haya yakifanyika kwa mara ya 18 tangu yalipoanzishwa mwaka 1994.
Shindano la mwaka huu limevunja rekodi ya mlimbwende Sylvia Bahame ambaye aliibuka mshindi na kukabidhiwa zawadi ya gari aina ya Nissan Hardbody yenye thamani ya shingili milioni 55 na fedha taslimu shilingi milioni 7.
Mshindi wa mwaka jana mlimbwende Geneveva Mpangala alikabidhiwa zawadi ya shilingi milioni 20 na gari maarufu kwa jina la Mkoko lenye thamani ya shilingi milioni 10.
Shindano la mwaka huu tunaweza kusema limefanikiwa sana katika upande wa zawadi kwa washiriki kuanzia mshindi wa kwanza hadi 30. Kwa mantiki hiyo washiriki hawakutangaza tu jina la wadhamini bali wamenufaika na ushiriki wao. Hii ni aina ya ajira isiyokuwa rasmi ambayo inawasaidia warembo walioshindwa kutwaa taji hilo kupata kazi au mwanzo mzuri wa maisha yao. Ukikokotoa kiwango cha zawadi walizokabidhiwa warembo hao, kisha ukageukia Ligi kuu Tanzania Bara kuna jambo unaweza kulishangaa.
Udhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara siyo mnono kama zawadi zinazotolewa kwa warembo hao. Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania anajinyakulia kombe na shilingi milioni 30. Pia kuna zawadi za mchezaji bora, mlinda mlango bora, kocha na kadhalika.
Kwa maana hiyo Ligi Kuu inayojumuisha imu 14 inashindana kupata shilingi milioni 30 kwa msimu mzima. Mechi za Ligi Kuu ni 28, ambazo huchezwa nyumbani na ugenini.
Katika mechi hizo timu zote zinazoshiriki zinabanwa na mkataba ulioingiwa kati ya TFF na wadhamini kwamba timu hizo zinalazimika kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini zikiwa kifuani.
Jezi zinazotumiwa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zinatolewa na mdhamini hali ambayo imezisaidia baadhi ya timu kuwa na jezi za uhakika. Hata hivyo jezi zinazotumika katika ligi Kuu Bara zinafanana sana. Kuna tofauti ndogo sana kati ya jezi ya Coastal Union ya Tanga na Simba ya Dar es salaam.
Ni klabu ya Azam pekee inayoonekana kuwa na jezi tofauti. Sasa, katika mechi moja baina ya timu mbili, kuna wachezaji 22 wanaokuwa katika vikosi vya kwanza. Katika benchi kunakuwa na wachezai 6 kwa kila upande ambao wanakuwa tayari kuchukua nafasi za walioanza.
Kwa maana hiyo kunakuwa na wachezaji 34 katika mechi hiyo. Halafu, kuna makocha; mkuu na msaidizi wake pamoja na meneja wa timu ambao huvaa nguo za michezo zinazotolewa na wadhamini. Tukumbuke wadhamini wanataka neombo yao ikae mbele.
Hadi hapo utapata jumla wa wahusika 34 kwa timu mbili ambao huvaa jezi zenye nembo ya wadhamini kwa mwaka mzima. Lakini kwa shindano la warembo la saa 6 tu linawapatia shilingi milioni 80, huku bingwa wa Ligi Kuu anavuna shilingi milioni 30.
Hesabu ya wanaovaa jezi za wadhamini ni kwa mchezo mmoja, lakini kwa mechi tano bila shaka idadi ni kubwa mno. Idadi hiyo hailingani na zawadi zinazotolewa na wadhamini. Ni kama biashara isiyo na hesabu zozote zenye maana yeyote.
Mathalani, saa 6 zinatoa mshindi wa milioni 80, lakini mechi 28 kwa mwaka mzima zinatoa zawadi ya shilingi miliono 30. Halafu kwa golikipa bora zawadi ni shilingi milioni 1.2. kwa mantiki hiyo, zawadi ya golikipa bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara ni sawa na zawadi ya mrembo aliyeshika nafasi ya 6 mwaka huu.
Sababu mshindi wa pili ni milioni 6.2, mshindi wa tatu ni milioni 4 na yule wa nne ni miloni 3. Awali nimeonesha namna washindi walivyotuzwa, kwahiyo mshindi wa 6 hadi wa 15 wa mashindano ya urembo nchini alipata shilingi milioni 1.2.
Golikipa wa Yanga, Yaw Berko ambaye ni raia wa Ghana alishinda taji la golikipa bora, kwahiyo zawadi yake ni sawa na mshindi wa 6 wa Miss Tanzania. Je, udhamini kama huu kwenye soka hususani Ligi Kuu Tanzania bara una manufaa yeyote?
Je, TFF ilipoingia mkataba huo haikujua kuwa ni mdogo? Nasema hivi kwasababu Yanga waligomea kuchukua jezi zinazotolewa na wadhamini kwa hoja kwamba zina nembo nyekundu ambayo ni rangi ya wapinzani wake wa jadi, Simba.
Ukifuatilia sababu za Yanga ni kweli walitakiwa kusimamia imani yao na utamaduni wa rangi za klabu yao. Vilevile tulihabarishwa kwamba Yanga ilikuwa kwenye mazungumzo na kampuni moja ya simu za mkononi ili iwe mdhamini wake, lakini upesi TFF itamka kuwa suala hilo halikubaliki.
Bila shaka hilo ni fundisho tosha, ndiyo maana mapendekezo mapya ya mdhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuanzia msimu ujao neombo yake itawekwa mabegani.
Haya ni mapinduzi makubwa na ushindi wa Yanga. Mathalani, Liverpool inadhaminiwa na benki, wakati mdhamini mkuu wa EPL ni benki pia. Sasa, ukikokotoa hesabu za zawadi za wadhamini ni wazi kuna njaa sana katika vilabu vyetu vya ligi kuu.
Pamoja na kupokea kile kinachopatikana kutoka kwa wadhamini, kwa hakika udhamini uliopo ni janga kubwa. Ndiyo maana naunga mkono mapendekezo mapya ili mdhamini ajaye atambue hilo. TFF inatakiwa kujifunza sana kwenye mashindo ya Miss Tanzania.
Ni kwanini shindano linalodumu kwa saa 6 tena siku moja, mshindi wake anapewa kitia cha milioni 80? Je, TFF inakiri kwamba Miss Tanzania ni bora kuliko Ligi Kuu Bara?
Kama TFF inakataa basi ihakikishe udhamini unaokuja una manufaa au wadhamini waliopo wakitaka kuongeza mkataba basi wafuate masharti ya shirikisho hilo. Udhamini katika Ligi Kuu siyo hisani, ni biashara. Je, Miss Tanzania ni bora kuliko Ligi Kuu Tanzania Bara?


0 Changia Maoni:
Post a Comment
Andika maoni yako hapa kwa raha zako