November 07, 2012

WAZEE WA KYELA WATOA USHAHIDI KUHUSU MGOGORO WA ZIWA NYASA



Wazee wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, wameunga mkono hoja ya serikali kwamba, mpaka wa Tanganyika na Malawi, upo katikati ya ziwa hilo, wakisema ndivyo walivyoelezwa na wazee wao walipokuwa vijana.

Walisema hayo mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alipokutana nao ili kupata ushahidi kuhusu mpaka halali wa nchi hizo.

Waziri Membe akiongea na wazee wa Kyela katika ziara yake ya kuzungumza na wazee kuhusu mipaka ya Ziwa Nyasa. Picha: Subi Sabato/Wavuti

Mzee Edwin Kasirati (75) alisema alizaliwa na kulikuta ziwa hilo na wakati wakiwa vijana walielezwa na wazee wao kuwa mpaka wa Tanganyika na Malawi ni mto Songwe, ambao unaingia ndani ya Ziwa Nyasa.
Alisema mwaka 1961 Wamalawi wenyewe walikiri kwamba, mpaka ni katikati ya ziwa na mto Songwe.
Mzee Michael Mwang’onda (70) alisema tangu wakiwa wadogo walikuwa wakielezwa na wazee wao kwamba, mpaka wa Tanzania (wakati huo Tanganyika) ni huo huo uliopo katikati ya ziwa kama ilivyo na  wameendelea kuulinda hadi sasa.
Alisema wanavyoelewa ni kwamba, Tanzania ndiyo inayomiliki eneo kubwa la ziwa hilo linalofikia theluthi mbili ya ziwa lote na Malawi wanalo eneo dogo ikilinganishwa hata na Msumbiji.
Mwang’onda alisema kama ni kulalamika, basi wangelalamika wananchi wa Msumbiji, ambao ndio wanafuatia kwa kumiliki eneo kubwa la ziwa na wala siyo Malawi.

wazee wa Kyela wakimsikiliza waziri Membe
Alisema hivi karibuni ziwa hilo limepanuka na kumega eneo lao, akidai kuwa hata makaburi ya mababu zao hivi sasa yamefunikwa na maji umbali wa zaidi ya kilometa mbili ndani ya ziwa Nyasa, hivyo haiwezekani ziwa lote ni mali ya Malawi. 
Katika safari yake ya kukusanya ushahidi, tayari Waziri Membe amekwishapita katika mikoa ya ya Ruvuma, hususan wilayani Mbinga na Mbeya katika wilaya ya Kyela, ambako alikutana na wazee mbalimbali na kuzungumza nao.
Awali, akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya, Waziri Membe alisema serikali haitarudi nyuma kushugulikia mgogoro wa mpaka baina yake na Malawi ndani ya ziwa hilo na kwamba, inataka kufikia mwaka 2015 suala hilo liwe limepata ufumbuzi.
Alisema licha ya Serikali ya Malawi kusuasua kuhudhuria vikao vya kuzungumzia mgogoro huo, Serikali ya Tanzania haitalifumbia macho suala hilo kabla ya kulipeleka katika Mahakama ya Kimataifa (ICJ).

wavuvi wakivua samaki katika ziwa Nyasa
Akiwa wilayani Kyela, Waziri Membe alizungumza na wananchi wa Kata ya Katumba Songwe na Matema akiwataka waendelee kuishi kwa amani na utulivu na asitokee mtu kwenda kuwatisha na kuwadanganya kwamba kuna hatari yotote katika mpaka huo.
Alisema serikali inalitambua tatizo hilo na inalifuatilia kwa makini ili kulipatia ufumbuzi na ndio sababu hivi sasa yeye anakwenda kwa wananchi na kuzungumza na wazee kwa nia ya kupata ushahidi utakapelekea kupata suluhu.
Alisema hata Rais Kikwete alitoa kauli ya kuwaahidi Watanzania kwamba, kabla ya kumaliza uongozi wake anahitaji suala hilo liwe limepata ufumbuzi ili wananchi wa eneo hilo waendelee kuishi bila wasiwasi, kwa amani na utulivu.
Aliwahakikishia wananchi hao kuwa hata kama suala hilo litapelekwa ICJ, lazima Serikali ya Tanzania itashinda kutokana na ushahidi unaotolewa na wazee katika maeneo mbalimbali anakopita. CHANZO: SOMA ZAIDI, HABARI ZINGINE SOMA HAPA KUHUSU NYASA NA WAZEE WA KYELA

CHANZO: HABARI NA EMMANUEL LENGWA
CHANZO: NIPASHE

UJENZI WA MACHINJIO MBINGA NA SOKO LIWETA


Katika kuboresha huduma za jamii, kuna mengi huwa yanafanyika. Miongoni mwake ni kujenga Machinjio yenye ubora na mazingira salama kwa afya za wanadamu. Wilaya ya Mbainga imefanikiwa kujenga machinjio katika eneo la mbinga mjini. Machinjio hii itasaidia kuondokana na mazingira duni ya kuchinjia wanyama mbalimbali wanaopelekwa sokoni kuuzwa. Picha ya chini inaonyesha sehemu ya kusafishia utumbo katika Machinjio hayo mjini Mbinga.


Picha ya chini: eneo la Machinjio hayo, mjini Mbinga. Kama tulivyoeleza awali kuwa machinjio hii itawanufaisha sana wafanyabishara wa nyama na watumiaji kutokana na ubora uliopo, kulingana na kanuni za AFYA.

UJENZI WA SOKO
Ujenzi wa Soko la Kijiji cha Liweta. Ujenzi huo upo katika awamu ya kwanza. Unatarajiwa kukamilika mapema mwakani ili kuhakikisha wakazi wa kijiji hicho wanaweza kuwa na Soko lenye kiwango kizuri baada ya kutokuwepo kwa Soko kwa muda mrefu. ni njia moja wapo ya kuweka mazingira safi na kuwawezesha wauzaji wadogowadogo kuuza bidhaa zao katika mazingira mazuri.

November 02, 2012

AMBROCE NKWERA, KIZAZI KIPYA CHA WILAYA YA NYASA NDANI YA MAHAKAMA

Miaka mingi sana imepita wazee wetu wazaliwa wa wilaya za Mkoa wa Ruvuma wemekuwa wakifanya kazi katika sekta mbalimbali, lakini hawana muda wa kutosha kufikiria kurudi nyumbani Nyasa na kufanya kazi karibu na wakazi wao. Lakini wapo vijana wenye tofauti kiasi kikubwa na wazee kama Prof. Nkoma (TCRA), Prof Mpangala (UDSM), Jaji Samatta(Mahakama Kuu), Mataka(ATC) na wengine wengi sana ambao waliozaliwa na kukulia wilaya Nyasa. Aidha, inapendeza pia kuona mzaliwa wa wilaya ya Nyasa James Zotto, akifanya utafiti wake wa masomo ya juu(Masters) katika suala la Utatuzi wa mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa baina ya Malawi na Tanzania. Zotto ni mzaliwa wa mji wa Liuli katika wilaya ya Nyasa.
                                      
                                        AMBROCE NKWERA KAZINI MAHAKAMANI
Hata hivyo kijana AMBROCE NKWERA yeye alisukumwa na nia ya kuwatumikia watu wa wilaya ya Nyasa, lakini amejikuta akipangiwa wilaya ya Mbinga ambayo zamani ilikuwa pamoja na Nyasa. Kwa hakika sio hatua mbaya, bali lengo lake liliongozwa na kuwatumikia watu wa ukanda wa Mkoa wa Ruvuma hususani wilaya za Songea, Tunduru, Mbinga na Nyasa au Ludewa(Iringa).
Baada ya serikali kutangaza nafasi za kazi ya Uhakimu kwa wilaya kadhaa za Nyasa, ndipo kijana huyu akachukua uamuzi wa kuomba nafasi hiyo. Na hadi sasa anaitumikia jamii ya Tanzania hususani wilaya ya Mbinga hivyo kukamilisha ujenzi wa Taifa. Labda swali hapa ni kwanini aliamua 'KURUDI NYUMBANI' ambayo ni sera yetu nami nikiwa mfuasi wake?
Sababu kubwa ni kwamba kuna wafanyakazi waliowahi kuajiriwa na kupangiwa wilaya ya Mbinga ama maeneo ya Wilaya za mkoa Ruvuma halafu hawaendi kufanya kazi vituo vya kazi. Hii ilikuwa ikimkera na kuona kuna haja wazaliwa wa maeneo hayo wenye sifa kuomba kazi ili warejee na kuwatumikia watu wa nyumbani kwao. 

                                          
                                                     AKITOKA KAZINI
Lengo hilo lilifanikiwa baada ya Mahakama kuu kumwajiri AMBROCE NKWERA na kumwapisha huko wilayani Lushoto mkoa wa Tanga. Kwa sasa yeye anatumikia taifa kupitia wilaya ya Mbinga ambayo ni jirani na nyumbani kwao wilaya ya Nyasa.  Yeye ni miongoni mwa walioshauri kuanzishwa mahakama maalumu ya kuwahukumu watu wote wanaoshtakiwa kwa kosa la Ufisadi ambayo anasema sawa na wahujumu uchumi (tutachapisha mahojiano yake siku zijazo).
Kwa hakika anastahili sifa na kupongezwa sababu uamuzi wake licha ya shahada yake ya sheria, akaona kuna haja ya kwenda kufanya kazi maeneo ambayo wengi hawataki kufanya kazi, maana huwa wanaripoti na kuondoka moja kwa moja, hawarudi tena. 
AKIFURAHIA MANDHARI YA MBINGA
Sasa, roho yake imetulia atakuwa HAKIMU mzuri sana, mikono yake itatenda haki na sera yake ya kushawishi wasomi ambao ni wazaliwa wa Wilaya ya Nyasa au Mbinga na nyingine za mkoa wa Ruvuma kwamba ni vyema wakarudi nyumbani kuwatumikia wananchi wao kuliko kulalamikia wageni wanaotoka mikoa mingine kutopendelea kufanya kazi maeneo ya mkoa huo. Mabadiliko na maendeleo yatawafikia watu kwa watu kufanya jitihada za kufanya kazi kwa bidii. Hongera sana Mgosi wa Ndimba AMBROCE NKWERA.