January 02, 2013

TAARIFA KWA WAWEKEZAJI WAPYA KATIKA KILIMO CHA MITI YA MBAO, KARATASI NA NGUZO.


Fresh Farms & Tours (T), biashara tanzu ya Anesa Co.,Ltd (Nyaluke Business Empire); inajishughulisha na upandaji, utunzaji na uendelezaji wa mashamba ya miti ya mbao, karatasi na nguzo-mkoani Iringa. Vilevile inahusika na uvunaji na usambazaji wa mazao ya miti, (mbao na nguzo za umeme) sambamba na ufugaji. 
Fresh Farms ilianzisha programu maalumu, mapema mwaka jana; inayolenga kuwawezesha watanzania wengine kuwekeza katika kilimo cha miti kwa urahisi. Tayari makumi ya watanzania wamechangamkia fursa hii. Fresh Farms & Tours (T) tunapenda kuwaarifu wale wote wenye nia ya kuwekeza nasi; KWAMBA kuanzia tar 1, Feb, 2013 kutakuwa na mabadiliko ya bei na gharama za uendeshaji kwa mashamba ya miti. 
Mashamba tunayoyauza laki sita kwa sasa; bei mpya itakuwa milioni moja; na yale tunayouza laki nane gharama yake itakuwa milioni moja na nusu. Bei hizi hazitawaathiri wateja wa awali na wale ambao wamekwisha wasilisha oda zao. Fresh Farms & Tours (T) tunaendelea kuboresha huduma, taarifa na usaidizi kwa wote wanaowekeza nasi. 
Fresh Farms & Tours (T) tunakutakia heri ya Mwaka mpya wa 2013 na tunakukumbusha ile salamu yetu (motto); "Greening the world and Feeding People". 

IMETOLEWA NA:
Albert Nyaluke Sanga
Mtendaji Mkuu-Fresh Farms & Tours(T), (C) 2012

TOKA ANALOJIA HADI DIGITALI: NINI MAONI YETU?


John Mnyika, MB

Na John Mnyika, Dar es salaam
Naomba majibu yenu kwa kuzingatia kuwa kazi ya wabunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali: baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa kuhama kutoka analojia kwenda digiti kwa mkoa wa Dar es salaam; kwa watumiaji, nini faida na athari mlioanza kuzipata kwa wenye ving’amuzi? Na nini kikwazo kwa wengine ambao hamjahamia mpaka sasa? Na nini mnataka watoa huduma na mamlaka zingine kuzingatia? Katika hatua ya sasa, ni muhimu Tanzania Consumer Advocacy Society (TCAS) ifanye tathmini ya kina kwa niaba ya watumiaji kwa ajili ya hatua zake.  
Ikumbukwe kwamba Consumer Federation of Kenya ilikwenda mahakamani na kuzuia mitambo kuzimwa watumiaji tarehe 31 Disemba 2012, na mahakama imesitisha mpaka itakapofanya uamuzi wake wa msingi.
Kwa upande mwingine, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA-CCC) litumie mamlaka yake kwa mujibu wa kifungu cha 37 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano namba 12 ya mwaka 2003 na vifungu vingine vinavyohusika kushughulikia malalamiko yaliyotolewa kwa nyakati mbalimbali kwa kuzingatia tahadhari tuliyotoa kwa serikali bungeni miezi mingi iliyopita kuhusu athari zitazojitokeza kwa kutozingatiwa kwa maandalizi muhimu.

NB: John Mnyika ni mbunge wa jimbo la Ubungo

December 29, 2012

SCHOLARSHIPS ANNOUNCEMENT.


SCHOLARSHIPS ANNOUNCEMENT.
Applications are invited for qualified Tanzanians from the Public
Service to apply for the following training program from the
Government of India:-
· “Promotion of Rural Micro-Enterprises”
Dates: 7 – 20, March, 2013
Website: SOMA HAPA. kWA TAARIFA ZAIDI INGIA HAPA KUSOMA ZAIDI: BONYEZA

SIKU NILIPOHOJIWA NA DANIEL R. GINGO


Daniel Gingo akionyesha moja ya kitabu alichoandika.
NB: Wiki kadhaa zilizopita rafiki yangu huyu aliamua kujadiliana nami jambo muhimu kuhusu sekta ya habari hapa nchini. Haya ndiyo tuliyoongelea japo kwa ufupi kutokana na muda mchache. Karibuni........
DANIEL GINGO: Kuna huu mfumo ambao vyombo vyetu vinautumia kutuhabarisha habari za Ulimwengu kwa mfano: Gazeti la The Gurdian, linaweza likawa na kurasa hata sita zilizosheheni habari kutoka Reuters, BBC, UPI, AP na Xinhua ya China.
TBC: inaweza kusheheni habari kutoka RT au Al-Jazeera, ITV inaweza ikawa na habari za CNN, BBC, na vipindi kibao ambavyo hatujavitengeneza hapa nchini, na wakati mwingine tunavilipia. Je, mfumo huu unavinufuaisha vyombo vyetu vya habari au tunakuwa victims?
MARKUS MPANGALA: Nadhani kila TV inakuwa na makubaliano na kituo cha nje. Kuna mikataba ya kurusha matangazo baina ya TV zetu na za nje.
Kama STAR TV na DW. .....kimsingi hii ni moja hasara kubwa tunayopata katika sekta ya habari na jamii yetu. Sababu CNN, DW, BBC, RT na wengineo hawana muda wa kuonyesha vipindi vya TV zetu.
Hili ni tatizo kubwa sana nadhani TCRA inatakiwa kuwa na mchakato wa kupiga marufu au kupunguza muda wa vipindi vya TV za nje. Channel Ten wao wana SKY NEWS.
Kwa kweli ni hasara sababu badala ya kumuonyesha mkulima wa kisasa sisi tunaonyesha Beckham akiwa mitaa na watoto wake.
Kwa kweli mimi hata DIRA YA DUNIA nimeshindwa kukiangalia sababu malengo ni yale yale kuwa afrika chafu na makamasi.
DANIEL GINGO: Hasara inakujaje kwetu hapo?
MARKUS MPANGALA: Kwanza, tunapoteza nafasi ya kuhabarisha habari nyingi za kwetu. Pili, tunashindwa kuzitangaza habari zetu kupitia hao hao tunaokubaliana nao kurusha vipindi vyao.

Markus Mpangala katika tafakari zaidi kabla ya kujibu maswali.
DANIEL GINGO: Na wao wanafaidikaje?
MARKUS MPANGALA: Lazima tuchukue nafasi ya kuonyesha mambo ya kwetu, sio kuhamisha tu ya nje na kuyaleta.
Kwa mfano kama TV inakuwa na saa 4 za kuonyesha mambo ya Russia. je Russia wanatumia saa ngapi kuonyesha ya kwetu?
Kwa maana nyingine sisi kazi yetu ni kubebeshwa tu habari za CNN, BBC na kuzirusha huku, lakini wao hawana muda na habari za mkulima wa viazi kule mbeya.
DANIEL GINGO: Tena wakati mwingine tunazipokea bila hata kuzihariri, zikiwa za uongo wanazirusha hivyo hivyo. Nikuulize swali la nyongeza?
MARKUS MPANGALA: Na ukweli kabisa huo. Ili kupunguza lazima TCRA ichukue hatua, wengi wanadhani China ni wajinga kuzuia CNN, BBC, Facebook na mengine kujaza habari zao kule China. Lakini naona walikuwa na hekima zaidi. Siku hizi habari zingine mbovu kabisa kwenye hizoTv za nje basi tu.
DANIEL GINGO: Lakini. Ikiwa TCRA watafanyia kazi ushauri huo, unadhani tunaweza kumudu kujaza nafasi zilizoachwa wazi na CNN, BBC, Hollywood nk?
MARKUS MPANGALA: Tunaweza kabisa. tunayo mambo mengi nchi hii hayatangazwi. Mfumo wetu wa habari bado unategemea, sio kujitegemea kuendesha mambo.
Ninaposema kutegemea ni ile hali ya kungojea matukio au habari fulani, badala ya kujitegemea kwakuwa na vipindi vingi vyenye tija kwa taifa.
Nina uhakika CNN au nyingine haiwezi kuwa kila kitu nchini. Hakika nakuambia, tunaweza kuwa na habari nyingi iwapo vyombo vyetu vya habari vitaanza kujitegemea.
DANIEL GINGO: Ninamaanisha hivi: Je, vyombo vyetu vya habari vina pesa na nyezo za kutosha kwenda Rubili kule Kagera, Rusumo kule Ngara, Kizorogoto kule Morogoro, Makiungu kule Singida, Kilindi kule Handeni, Kerenge kule Korogwe nk kwa ajili ya ku-cover matukio?
MARKUS MPANGALA: Naam ndio maana nimesema vyombo vyetu vinaendeshwa kwa Kutegemea sio Kujitegemea. Kwahiyo kujitegemea ni kama hivyo unavyosema, je vitaweza kwenda ku-cover story kule? Mimi nadhani inawezekana, na kilichokosekana ni msukumo.
Hawa Mwananchi kuna mtindo fulani wanaufanya kwa upande wa magazeti yao. Wana kitu fulani wanakionyesha lakini najua inahitaji gharama sana.
Hata hivyo ukitaka kuleta ufanisi katika vyombo vyetu lazima bajeti zao ziwe za kutosha kwa kuwekeza kwa ku-cover story sio posho na mengineyo. Tulichokosa ni Dhamira. Matokeo yake, Tunajikuta tunategemea tu.

'KUMRUDISHA MWAFRIKA KWENYE ASILI YAKE: MRADI MGUMU KULIKO YOTE"

Mimi na mzee Kamara Kusupa, hii leo Ofisini, mambo ya kuhariri kitabu chake kipya.

Kwa muda mrefu tumeshuhudia maandiko mengi kuhusiana na sisi waafrika. Yapo maandishi kama ya akina Cheikh Anta Diop, Dk. Elly Kamugisha, Franz Fanon, Julius Nyerere, Leopold Senghor na wengineo. Lakini jambo kubwa lililokuwa likijadiliwa ni nani hasa huyu MWAFRIKA. Mathalani wengi wanakubaliana kwamba mwafrika ni mtu mweusi, hivyo kuwatenga waarabu, wahindi, wazungu na wabarbaig ambao kimsingi nao wamejikuta wakiwa wamezaliwa katika bara ya Afrika. Msomi Dk Harrith Ghassany yeye alihoji nini asili ya Afrika na akaelezea kuwa ni kutoka kule Tunisia.
Dk Harrith alisema hayo kwenye kitabu chake cha KWAHERI UHURU, KWAHERI UKOLONI: ZANZIBAR NA MAPINDUZI YA AFRABIA. Ni moja ya changamoto alizotoa ambao kila mwenye udadisi atajikuta akishughulisha ubongo wake. Wapo wachambuzi makini kama Joseph Mihangwa ambaye kwa sasa maandiko yake yanapatikana katika gazeti la RAIA MWEMA, amekuwa akihojia mara kwa mara juu ya asili ya afrika na kuelezea mambo kadhaa yaliyowahi kutokea huko nyuma. Yote haya yanatuletea swali la msingi MWAFRIKA huyu ni nani?
Hata hivyo dunia imebadilika sana na kila kona inatusaidia kujua nini hasa kinachopaswa kusemwa kwa dhati na moyo safi kwa nyakati za sasa. Kuna wazungu wamezaliwa Afrika Kusini, Tanzania na wengine nchi nyingine za Afrika. Je hawa watakwenda wapi ikiwa hawajui asili zao zilikuwa namna gani. Ni kama ambavyo Waafrika wanavyojiuliza ni namna gani wataweza kurudi Afrika ambako hawajui waanzie wapi.

Ni vigumu leo kumwelezea Cliford Harris au T.I arudi afrika kutoka Marekani. Ni vigumu vilevile kumweleza Lennox Lewis arudi barani afrika. Ni vigumu kumwambia Danny Jordan wa Afrika Kusini kwamba uchotara wake sio kitu arudi kwenye asili ya makaburu. Au ni vigumu kumwambia Hellen Zille mwenyekiti wa chama cha upinzani cha D.A pale Afrika Kusini na gavana wa jimbo la Cape Town, kwamba arudi kwa wazungu wenzake. Hii ni moja ya mabadiliko makubwa ya mipaka ya nchi ambayo imeshindwa kuzuia mahusiano ya wanadamu kutoka nchi moja hadi nyingine au kutoka jamii ya nchi moja kwenda jamii ya nchi nyingine. Leo mwafrika anaweza kuzaa na mchina au Mkorea hivyo ni vigumu mtoto atakayezaliwa kutotambuliwa kuwa mwafrika, na kuangalia asili. 
Lakini wapo watu wanaojaribu kujiuliza ni namna gani wanaweza kuwakumbusha waafrika wenzeo kuwa Mwafrika alikuwa na asili yake. Ni mwafrika alikuwa wa kwanza kuwasilia Marekani kabla ya christopher Columbus, ambapo ushahidi mwingine uliandikwa na Profesa Ivan Sertima kwenye kitabu chake "THEY CAME BEFORE COLUMBUS". 
Nikiwa na mzee Kusupa. Duh anahamu mpaka amevunja meza.
Hata ukisoma 'voyage' mbalimbali za Columbus kumejaa mengi ya kushangaza na kwanini yanachukuliwa kuwa kama yalivyo?. Tukiacha hilo tunajikuta tunaangalia sisi Waafrika ni nani na asili yetu ikoje. Dhana ya uhai inakuwa kubwa na inachukua mkondo mkubwa sana, hivyo basi kitabu cha KUMRUDISHA MWAFRIKA KWENYE ASILI YAKE; MRADI MGUMU KULIKO YOTE hakika kinakuletea baadhi ya majibu ya maswali ambayo kila mara watu wanajiuliza. 
Hii inaonekana kuanzia kwenye DINI, SIASA, UTAMADUNI, na mengine mengi kuhusu Afrika yetu. Mwandishi wa kitabu hicho MWINJILISTI KAMARA KUSUPA anatuelezea mengi kwamba kuna makosa kadhaa yanafanyika, na amekuwa akisogea mbele kidogo zaidi ya anapoishia mwanazuoni kama Ali Mazrui. 
Kila jamii imekuwa kwenye asili yake, na inakuwa vigumu kurudi kwenye asili yake. Nini ambacho Kamara Kusupa anatuelezea kwenye kitabu hicho, hakika tunapaswa kuwa watulivu na kuvuta subira kwamba ni moja ya kitabu chenye mafunzo mengi kwa watu wa Afrika. Je, dini za waafrika ni zipi? Mfumo wa utawala wa waafrika ni upi? Msingi wao na dhana ya uhai vikoje? Uhusiano wao na jamii za nje ukoje? Je, mwafrika ataepuka dhahama ya mabadiliko ya kijamii duniani? Je, mwafrika ataweza kurudi katika asili yake? 
Nadhani ni moja ya mambo ya kusisimua na hakika yatakuwa na hamasa kwa wasomi na wananchi wengine. Ikumbukwe hicho kitakuwa kitabu cha tatu kutoka kwake, kwani alishaandika vitabu viwili; MAISHA YANGU GEREZANI, na kingine HII NDIYO TANZANIA TUNAYOITAKA. Kitabu cha pili nilishiriki kwa kiasi kikubwa, na sasa nashiriki pia kuhariri na kuweka lugha bora yenye hadhi kwa wasomaji makini. Ninadhani wasomaji watafurahia zaidi. Na tuseme basi kama kweli tutaweza kurudi kwenye asili yetu au ni mradi mgumu?    MWINJILISTI KAMARA KUSUPA atatujibu hilo, usikose kukisoma kitabu hicho.

AZIMIO LA ZANZIBAR LILISAHAU B.E.E


Na Markus Mpangala 



Azimio la Zanzibar linafahamika kuwa nyenzo iliyotumika kuua lile la Arusha.
Ingawaje viongozi wetu hawasemi walichokubaliana kule Zanzibar, lakini hali haijifichi na inaonekana tunazidi kusonga mbele.
Kuna mtikisiko wa kijamii unaendelea kwa sasa, kutoka kwenye mitazamo na maisha ya ujamaa hadi kwenye kiwango cha chini cha ubepari. Bahati nzuri ni kwamba ujamaa upo mioyoni mwetu yaani ndio maisha ya watanzania.
Ni kwa sababu hii ndiyo maana Mwalimu Nyerere aliuita ujamaa wa kiafrika. Sasa basi, katika azimio la Zanzibar viongozi wetu bila shaka walikusudia kufanya mabadiliko katika uchumi. Bahati mbaya mabadiliko hayo yalikuwa yanafanyika kwa kudanganywa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Dunia.
Walichodanganywa viongozi wetu ni sera za asasi hizo kuwa mwongozo wa uchumi wetu. Halafu hali ikiwa mbaya wanachofanya ni kulaumu kuwa nchi imeshindwa. Sera za IMF na WB hazijali mazingira ya mwanadamu wa kitanzania.
Maeneo mengi imetokea hali hiyo na hivyo kuongeza kiwango cha ufukara kwa wananchi katika nchi husika. Ufukara huo unachochewa zaidi na jinsi sera inavyopuuza hali halisi ya mazingira ya nchi na utamaduni wa watu.
Sera za IMF na WB zinatokana na uzoefu wa nchi za Ulaya na Amerika. Kule wataimba nyimbo kuwa ruzuku ni muhimu kwa mkulima na wanakwenda nchi zetu za Afrika na kusema kama, ‘utampatia ruzuku mkulima basi unampunguzia uwezo wa kuwa mbunifu.’
Lakini hatujiulizi kwanini wakulima wa Ulaya wanapewa ruzuku na kadhalika. Sera za IMF na WB ndizo zilisababisha azimio la Zanzibar kuonekana kituko mbele wa wajuzi wa mambo.
Azimio hilo lililo katika kibarua cha Azimio la Arusha halikuja na mbinu mbadala ya kuweka msingi wa kukuza uchumi. Badala yake likaja na mageuzi ya uchumi katika mkondo wa sera za IMF na WB.
Kimsingi hilo lilikuwa kosa na dosari kiuchumi. Serikali yetu haikumwandaa au haikuhodhi moja kwa moja uchumi. Bali ikadanganywa na IMF na WB kuwa jambo muhimu ni kufungua milango ya mageuzi ya uchumi.
Milango iliyofunguliwa sio ile ambayo ilifunguliwa na chama cha siasa cha ANC cha Afrika Kusini. Chama cha ANC kilifungua milango ya mageuzi ya uchumi kwa sera yake, misingi yake na baadaye kikawa kinapokea ushauri tu.
Sera kubwa ambayo iliing’arisha ANC ni B.E.E. ( Balack Economic Empowerment). ANC ilikuwa wazi kabisa, hata kama sera hiyo iliwalenga watu weusi wa Afrika Kusini, na kuwatenga wazungu ambao ni raia halali wa nchi hiyo, lakini kilichofanyika ni kuziba pamba masikioni.
ANC ikasema inatambua kuwa B.E.E inaonekana kama inabagua lakini ni wajibu wao kutimiza uwezeshaji wa watu weusi katika mitaji ya kiuchumi. Mazao ya ANC ndio Tokyo Saxwalle, au familia ya kina Khoza.
Mfanyabiashara Tokyo Saxwalle anafahamika kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa na wawekezaji wa kiwango cha juu kutoka jamii za waafrika. Ni kutokana na sera hiyo iliwezesha kuibua wafanyabishara, wawekezaji na wajasiriamali wengine ambao walifanya kila jitihada kwa kutumia sera ya B.E.E kufanikiwa.
ANC ikasema lazima watu weusi wawezeshwe. Tafsiri sahihi hapa ni kuwawezesha wazawa. Hali hiyo ilitokana na miaka mingi ya utawala wa kaburu kuwanyonya na kuwakandamiza watu weusi. ANC ilipania, ikathubutu, ikatimiza dhamira yake.
Ni sababu hiyo tunaona baadhi  wawekezaji wakubwa waafrika kutoka Afrika Kusini, vinginevyo ubaguzi ulioanzishwa na makaburu ungeendelea kuwafanya waafrika wabaki hohehahe.
Mfano wa pili ni Chujusong, Korea Kaskazini. Tangu mwaka 1925 Korea Kaskazini chini ya chama cha kikomunisti ilifanya jitihada kubwa ya kujenga uchumi huku ikitanganza kuwa ni Jamhuri ya Kisoshalisti.
Chujusong ni mpango wa kujitegemea kiuchumi. Msingi mkuu ulikuwa kuhakikisha mitaji ya kiuchumi inakuwa huru ili kuondokana na utegemezi kutoka nje. Sera hiyo ilichukua ngumu na kuhodhi mwenendo wa nchi hiyo kujenga uchumi wake.
Polepole mabadiliko makubwa yakajitokeza hadi Korea Kaskazini tunayoiona leo. Hapa kwetu sera ya wazawa tu ilitushinda, na kwakuwa tulikuwa tumekosa uelewa wa kutosha tukadhani sera hiyo inabagua.
Laiti tungelikuwa na msimamo na uelewa wa kutosha kuwa huo siyo ubaguzi sababu hata wageni walioingia nchini mwetu waliwabagua wenyeji. Kwahiyo ili kukabaliana na pengo lililokuwepo zama za ukoloni, ilipaswa serikali ya awamu ya pili ilipofungua milango kuruhusu mageuzi ya kichumi, itunge sera za B.E.E.
Mpango wa kuwawezesha waafrika sio dhambi. Mpango wa kuwawezesha wazawa sio dhambi. Wazawa hao maana yake tuwe na wawekezaji sampuli ya Reginald Mengi.
Watu wa aina yake tuwe nao wengi ili kuimarisha mitaji ya serikali na uchumi wetu. Tusipokuwa na misingi inayoakisi ustawi wa taifa kiuchumi, itawezesha fedha nyingi za Tanzania kuishia mikononi mwa wadokozi. 
Na wadokozi wengine tulipowajua wakati wa miaka ya 1990 ntumejikuta sasa nchi inabomolewa benki yake. Sasa baada ya kuipoteza misingi hii tumejikuta tunahamasisha ujasiriamali.
Tunahangaika na ujasiriamali sababu wakati wa kufungua milango ya mageuzi ya uchumi hatukujua mageuzi hayo yanafanyikaje na uchumi utakuwaje.
Milango iliyofunguliwa ikawa ni kuruhusu wachuuzi ambao walidhaniwa wawekezaji, wakawa wanachuma mali za watanzania. Sasa, akili inapoibuka kipindi hiki tunajikuta kumbe wakati tunazika azimio la Arusha tulipaswa kutamka kwakuwa lazima tuwezeshe wazawa. Lazima watu weusi wawezeshwe kwenye mitaji. Na iwe sera sio huruma. Kwa sasa tumejikuta tunao wawekezaji wengi kutoka nje, halafu wawekezaji wa ndani bado uwezo wao  sio mkubwa sababu hawakuwa sehemu ya mageuzi ya uchumi yaliyofunguliwa wakati ule.
 Nionavyo, tunatakiwa kuwa na sera za kuondokana na uchuuzi wa kijasiriamali. Lazima tujenge uwezo kwa wazawa. Lazima tuwaige ANC kwa sera ya Black Economic Empowerment. Tujiulize, hivi kuna ofisi ngapi za Benki ya Dunia na IMF katika nchi za Kiarabu? Jibu hakuna ofisi hizo kwakuwa hazihitajiki. Tafakari. Nahitaji changamoto. 

UTAJIRI WA GESI ASILIA: TUWASIKILIZE WATANZANIA WA MTWARA NA LINDI. TUSIWAPUUZE



Na Zitto Kabwe, Dar es Salaam
Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.
Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona. 
Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa.
Mtwara na Lindi wanataka nini?
Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la hasha.
Sio dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? 
Tumesahau ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho? Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya Tumbaku.
Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali huru ya Tanzania? Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye Gesi asilia.

Mtwara na Lindi wanakosea wapi?
Madai yao halali na mimi binafsi na chama changu tunayaunga mkono. Lakini kuna mahala lazima waelimishwe. Watu wa Mtwara pia wanapaswa kuelewa kuwa juhudi zao zisiwatenganishe na Watanzania wengine kwani bado utajiri wa Taifa unafadisha kikundi cha Watanzania wachache sana. Watu wa Mtwara wanahitaji kuungana na watu wa Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga na watu wa Kagera kudai utajiri wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya kunufaisha kundi dogo la watu. Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na Watanzania wengine kuzuia uporaji wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi kijacho. Watu wa Mtwara wasijitenge wakawa peke yao na Gesi yao. Nguvu ya mnyonge ni umoja.
Serikali isiyosikia
Serikali ina hoja kuhusu kujenga Bomba la Gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya Watanzania. Kwa kuwa hii asilimia 14 ndio wenye sauti basi watu wa Mtwara wataonekana hawana hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara mbilimbili kuhusu mradi huu wa Bomba? Tunaambiwa na Wataalamu kwamba kuna uwezekano mkubwa mwakani gesi asilia ya kiasi cha futi za ujazo trillioni 20 itakuwa imegunduliwa katika Kitalu namba 7( block 7) ambacho kipo mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Temeke. Iwapo gesi nyingi hivi itakuwa hapa Dar karibu kabisa na mitambo ya kuzalisha umeme, mradi huu wa Bomba unaojengwa kwa trillioni za shilingi utakuwa na maana tena? Huu mkopo utakuwa na tija?
Serikali imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba Dar dhidi ya gharama za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na kuusafirisha umeme kwenda maeneo mengine ya Tanzania? Serikali imeangalia faida ya kujenga gridi nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na bwawa la Mtera? Leo bwawa la Mtera lisipozalisha hata megawati moja hata Dar es Salaam izalishe megawati alfu kumi umeme hautakuwapo maana uti wa mgongo wa gridi ni Mtera! Kwa nini tusiwe na gridi nyingine yenye uti wa mgongo Lindi au Mtwara?
Picha zote kwa hisani ya Said Msonga
Tuwasikilize watu wa Mtwara
Watanzania sio mabwege tena. Kuwaita watu wa Mtwara ni wahaini, wapuuzi au watu hatari haisaidii kujenga Taifa moja lenye watu huru. Serikali na wadau wote wa sekta ya Gesi likiwemo Bunge washirikiane na watu wa Mtwara kuhusu miradi ya gesi asilia. Tuwe na Azimio la Mtwara, tamko la kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa Gesi bila kuathiri umoja wa Taifa letu.
Ujio wa Sera, Maono na Uongozi Mbadala
Sasa hivi wananchi wa Mtwara kama wananchi wa sehemu nyingine wanahitaji maono mbadala, uongozi mbadala, sera mbadala na mwelekeo mbadala wa kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao, utazingatia raslimali zilizopo na utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika kutengeneza mfumo wa kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima.
Ni kwa sababu hiyo naamini chama changu ni jibu sahihi kwa matamanio na kiu ya wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine nchini. Ikumbukwe kuwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2010 tulielewa haja ya kuangalia mikoa hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa mwelekeo wa kipekee katika sera.  Bado tuna makusudio hayo tunapoelekea 2015 na tukishika Dola wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine zote zilizoachwa pembezoni mwa mafanikio wajue kuwa wamepata rafiki na mshirika wa karibu wa kushirikiana nao kuleta maendeleo.
Siyo katika suala la gesi tu bali katika nishati, maji, elimu, miundombinu, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii. Mtwara kama ilivyo mikoa mingine ina raslimali za kutosha kuweza kuwainua wananchi wake kimaisha, na zaidi ya yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi. Hili ambalo ni kweli kwa Mtwara ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara, Katavi, Lindi n.k.
NB: ZITTO KABWE ni mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema.

December 27, 2012

MIKONO NA MOYO WA NATHAN MPANGALA KUWAFANYA WATOTO WENYE SARATANI KUTABASAMU

Nathan Mpangala akiwa anawafundisha watoto kuchora michoro mbalimbali. 
Nathan Mpangala ni miongoni mwa watanzania wanaogusa mioyo ya watu kutokana na kazi zao za sanaa. Wengi wanakumbuka michoro ya katuni za Kijastibikozi na mingine mingi sana. 
Yeye ndiye mwasisi wa michoro ya katuni za Daladala ambazo huchapishw ana gazeti la MAJIRA hapa nchini. Tasnia ya uchoraji imemfikisha katika nchi mbalimbali kuhudhuria mihadhara ya kuelimisha jamii akiwa miongoni mwa waandishi wa habari wanaotumia vipaji vyao kufikisha ujumbe kwa njia ya sanaa za michoro. Moja ya kazi zake kubwa zinazoonekana kote nchini kupitia Televisheni ya ITV ni kibonzo cha MTU KWAO. 
Kibonzo hivyo hubeba ujumbe mbalimbali wenye nia ya kuelimisha na kuburudisha jamii. Kutokana na kipaji chake, Nathan Mpangala anarudisha faida anayopata kwa kazi hiyo kwenda kwa jamii. 
Amekuwa akifanya hivyo kupitia programu ya WAFANYE WATABASAMU akiwa na lengo la kuwaliwaza watoto wote wanaougua saratani nchini. Juhudi hizo ni kutokana na mapenzi yake kwa jamii na nchi kwa ujumla. Kama anavyoonekana pichani akiwa na watoto hao, pamoja na mchoro mwingine upande wa kulia unavyoonyesha watu wasiofikiria jamii yao. 
Hakika Mikono na moyo wa NATHAN MPANGALA umekuwa faraja kwa wazazi wa watoto na watoto hao kwa ujumla. Nawe waweza kuchangia juhudi zake kwa kuungana naye katika WAFANYE WATABASAMU.


Anaelezea zaidi safari yake .............
UCHORAJI UMEPAMBA MOTO. Baadhi ya watoto wanaendelea na matibabu ya saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, wakijimwayamwaya wakati wakichora. Kupitia Program ya Wafanye Watabasamu, nilitembelea watoto hao kuwapa zawadi kisha kuchora nao. 
Katika ziara hiyo niliyoambatana na baadhi ya wachoraji katuni na marafiki wa Wafanye Watabasamu tuliwazawadia watoto zawadi kisha kuchora nao. Kwa niaba ya watoto, nawashukuru ndugu na marafiki wa Programu ya Wafanye Watabasabu kwa zawadi mbalimbali walizochangia ambazo zimefanya ziara hiyo kuwa ya mafanikio. Pia nawashukuru sana marafiki na wachoraji wote waliojitokeza na kuungana nami Muhimbili. Picha na michoro mbalimbali iliyochorwa na watoto hayo iko njiani.