January 08, 2013

WATANZANIIA TUNAWEZAJE KUISHI KWA GHARAMA KUBWA KILA MWEZI?


Na Yasinta Ngonyani, Sweden
Fikiri, matumizi nyumbani:- chakula, umeme, gesi, maji, soda au juisi za wageni. Ada za watoto zinazolingana na za vyuo vikuu. Na hapa nazungumzia ada za shule za binafsi sio zile za serikali  kwani tunajua unafuu wake. Matumizi mengine matibabu hospitalini, pesa ya walinzi kwa kila mwezi, sherehe za kuaga na kukaribisha mwaka mpya.
Zaka ya Kanisani na Misikitini, kupanda Mbegu/ Sadaka, Shukurani ya neno, ahadi na makusanyo, shukrani ya chakula cha Bwana kanisani, marekebisho ya Kitasa cha mlango kabla mwenye nyumba hajashtuka, gharama za marejesho ya mkopo wa Saccos kazini.
Tozo za Flying (wazoa takataka wa mikokoteni ambao huzitupa hapo hapo), Madalali wa nyumba, viwanja, pango la nyumba, fremu ya biashara na ofisi.
Mitandao ya simu (airtime vouchers), mafuta ya gari, walindaji na waoshaji magari. Daima kauli zao “oyaah sista/blaza, mdogo wako nipo apaaa.”
Tozo za kuegesha magari, makato ya mikopo, tozo za internet cafe ili uweze ku-surf. Rambirambi ya mfiwa mtaani kwetu, harusi ya ndugu yako wa ukoo na zawadi.
Bado sijamaliza kutaja, kuna Sendoff ya mtoto wa mdogo wake rafiki yako na zawadi, kumuaga mfanyakazi mwenzetu na zawadi, michango ya komunio ya 1 & 2 na kipaimara.
Michango ya birthday party na zawadi; Ndugu wa kule kijijini, mshahara wa hausigeli na hausiboi; matumizi ya Bodaboda, teksi na bajaji. Duka la dawa kwa mchaga, tuisheni ya mtoto, kuchangia wahanga wa mabomu na mafuriko. Mengine ni kwenda kumuona mtoto aliyezaliwa, kununua CD/DVD ya uzinduzi wa Kwaya yetu.
Chakula cha mbwa, mchango wa ujenzi wa kupanua Kanisa, kuchangia Uinjilisti Masasi, outing ya kitimoto, ujenzi wa Nyumba Mabwepande, Kuendeleza shamba Mkuranga (linalotaka kutaifishwa kwa kutoendelezwa). Na matumizi mengine kwa wale wenzetu wanaokwenda umbali wa Viti Virefu, moja moto, moja baridi. Maji ya Trafiki, Chai ya Nesi na Daktari, Kahawa ya Hakimu, Karani na PP.
Matumizi ya Vishoka waunganisha maji na umeme; Kidogo dogo cha mjumbe na mtendaji wa mtaa, makaribisho ya get together na dinner kwa rafiki wa kikazi ambaye hamjuani ila kweye simu tu.
Mchango wa matibabu ya mtoto nyumba ndogo kule Ngusero, mchango kidogo kwa rafiki aliyevamiwa na vibaka na kuumizwa vibaya. Gharama za malipo ya Mkulima Bar Moshi, manunuzi ya maji ya Kilimanjaro uwanjani Sheikh Amri Abeid, Ukiangalia mechi ya Yanga na JKT Oljoro, malipo kwa ajili ya Uji wa Shangazi, baada ya kazi Njiro jioni ya Alhamisi. Vipi manunuzi ya kandambili kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Hivi hali inakuwaje?
Mia mbili ya watoto wa mtaani au ombaomba, kitu kidogo cha wale wanaolazimisha kuosha kioo cha gari kwenye foleni barabarani. Umeme uliopanda bei, gesi iliyopanda bei, maji yaliyoadimika, bado contingency maana huu usafiri unaotembelea ball joint, bush, feni belt havijafa, hapo bado hujafanya service. Bado msosi wa mchana kazini hasa kama maofisi yetu akina Mama Ntilie na vyakula vyao vinapokaribiana bei za restaurants, bado mchango wa kitchen party na sare, kuna hii baby shower.
Na hapo bado hujatoa watoto outing jumapili, Upo wapi uwezekano wa kununua laptop mpya ambayo ni muhimu katika mfumo wa maisha ya kisasa. Desktop nyingine kwa ajili ya watoto nyumbani, rim mpya za gari ambazo zimeingia kwaajili ya ku-modernize gari lako kuu kuu. Vipi kuhusu gharama za kujipendekeza kwa kimwana wa kazini kwako ambaye amekubali kwenda nawe out leo.
Gharama za matibabu katika hospitali binafsi kwa kuwa madaktari wa serikali wapo katika mgomo. Dogo naye “Bro ninunulie basi japo kasimu ka promosheni, ile yangu imedondoka chooni” Mara “Bro/Sister Next week on Saturday shuleni tuna-visit snake Park na sina shilingi 3000 za mahudhurio”.
Mke naye nyumbani anaongeza yake, “Daddy leo Mwakasege yupo relini, vipi tutapitia? Hapo unatakiwa kujua kichwani mwako kuwa gharama ya taxi baada ya semina.
Vipi tozo za Toyo kwa kuwa nimeachwa na gari la ofisi (Staff Bus). Mwingine kama kawaida anakusubiri uwajibike kwa gharama zako hana muda wa kudhani unahitaji msaada. Mama yangu!
Ukigeuka huku na huko unajikuta nafuu yenyewe ni pale mwajiri anapokuongezea mshahara kwa 7% tu wakati inflation ni juu ya 19%. Ukifikiri kwa makini, unajiuliza Watanzania wanaishi vipi kwa mtindo huu?
Ndipo unapoimba "Mwokozi nitoe roho niepuke, hili balaaa." Napenda msomaji utafakari mwenendo wako wa matumizi kulingana na hali hali ya uchumi wan chi na jamii yetu.
Kama ukiyumba kwenye suala la kuweka akiba, basi maisha yako yatakuwa yanakabiliwa na ukosefu wa msingi wa muongozo au utakuwa unatumia gharama kubwa kwa mambo yasiyoweza kusaidia familia yako.

RAIS FRANCOIS BOZIZE ALIKUWA AKISUBIRI VITA ATIMIZE MAJUKUMU?


Na. Markus Mpangala, Lundu
Moja ya mambo yanayonikinaisha ni suala la mgogoro wa nchi ya Afrika ya Kati.
Serikali ya Bangui inaonekana lilala usingizi wa pono kiasi ambacho sasa baada ya mapigano ya muda mrefu na waasi wameamua kuitisha majadiliano huku serikali ya rais Bozize ‘ikiwatongoza’ waasi hao kwa mambo ambayo yaliapaswa kuwa kwenye ilani ya uchaguzi. 
Serikali ya mjini Bangui chini ya rais Francois Bozize inasema kuwa, kwa sasa imejipanga kwa dhati kutimiza majukumu yake kwa wananchi.
Serikali hiyo inasema katika majadiliano yake na waasi wan chi hiyo yatakayofanyika nchini Gabon, imekusudia kuwasilisha mipango thabiti ya maendeleo ya kiuchumi, mapenndekezo imara ya mabadiliko ya ndani ya jeshi la nchi hiyo na kadhalika.
Ikumbukwe Rais Bozize hivi karibuni alimtumua madarakani waziri wa ulinzi ambaye ni mtoto wake. Kwa upande wa waasi wan chi hiyo wanasema kuwa wanataka rais Bozize aondoke madarakani ili kurejesha amani ya nchi hiyo. Mazungumzo baina ya serikali na waasi yanafanyika baada ya miaka takribani miaka 12 ya kukosekana kwa amani, huku utawala wa Bangui ukiendelea kulemaa na kushindwa kutimiza makubaliano ya awali ya mwaka 2001.
Katika mazungumzo ya sasa, Jumuiya ya Nchi za Afrika ya Kati(CEEAC) imeratibu majadiliano baina ya Rais Bozize na waasi hao yatakayofanyika mjini Libraville nchini Gabon yakiwa na lengo la kumaliza mapigano ya pande hizo mbili.
Moja ya masharti yaliyowasilishwa na waasi ni kwamba lazima rais Bozize aondoke madarakani kwasababu ameshindwa kupata ufumbuzi na kutimiza makubaliano yaliyowahi kufikiwa huko nyuma.
Aidha, mwaka 2007 kulifanyika mazungumzo ya kusaka amani lakini hakukuwa na mwendelezo wowote uliofanyika chini ya rais Bozize. Ni jambo la aibu sana leo hii, Rais Bozize kuamua kuwasilisha mezani ajenda za kupata ufumbuzi ili kumaliza machafuko nchini mwake. Leo hii Rais Bozize anawasilisha mipango ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Afrika ya Kati, huku akihimiza mabaidliko ya kijeshi ndani ya jeshi la nchi hiyo.
Kimsingi Rais Bozize anaonekana kukosa dira ya kuongoza taifa hilo lililopo katikati ya bara la afrika. Sababu mapigano yake dhidi ya waasi yanafahamika kwa kipindi cha miaka kumi sasa, na ajenda zinazoelezwa na waasi ni hali mbaya ya wananchi, kukosekana wka matumaini ya kiuchumi na kadhalika. Lakini kwa upande wa Rais Bozize haonekani kuona kwamba yeye anaweza kuwa kikwazo cha kufikiwa makubaliano hayo.
Waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Kama ambavyo waasi wamesema, wanataka kuona Rais Bozize akiondoka madarakani ili kupata ufumbuzi, vivyo hivyo wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanavyopendekeza.
Hata hivyo kwa mtindo wa kutaka kukwepa majukumu, ni dhahiri rais Bozize anaweza kuwatupia lawama wasaidizi wake ili kuonekana hana hatia. Ni sababu hii ndio maana alimfukuza kazi mwanaye ambaye alikuwa waziri wa ulinzi na usalama wan chi hiyo.
Kumfukuza kazi waziri huyo hakukuweza kuwashawishi waasi wa nchi hiyo ili waone rais huyo anakusudia kuleta mabadiliko, bali waasi wanaona ni njia ya kujisafisha kwa sasa kutokana na kuachia machafuko kufikia kipindi kibaya sana.
Jambo jingine ni mabadiliko ya taratibu za uchaguzi wan chi hiyo. Ikumbukwe, waasi hawalalamikii taratibu za uchaguzi uliomuingiza madarakani rais Bozize bali wanalalamikia hali mbaya inayotokana na utawala wake. Kwa maana hiyo kutaka kufanya mabadiliko katika taratibu za uchaguzi anakusudia kuwaleta waasi hao katika ulingo wa siasa badala ya kuangalia njia za kukomesha mapigano ambayo yamesababisha watu kadhaa kufariki dunia na wengine kukosa makazi.
 Katika hali kama hiyo kwa vyovyote uchumi wa nchi lazima uzoroteshwe, kwani watu badala ya kutumia nguvu zao katika uzalishaji hivyo hutumia nguvu hizo matika kuyakimbia makazi yao au kuelekea uhamishoni. Sio kitu rais ambacho rais Bozize anaweza kuishawishi Afrika, lakini jambo la msingi ni kukubali kuwajibishwa kulingana na hali halisi inayoendelea nchini humo.
Wananchi wanapolalamikia hali mbaya ya kiuchumi huku rais wao akitumia muda mwingi na nguvu za kutosha kutaka kuwashawishi waasi waache mapigano, ni wazi ameshindwa kubaini kwua hata yeye ni sehemu ya tatizo la machafuko hayo.
Endapo yeye asingekuliwa sehemu ya tatizo basi tusingeona leo kuna machafuko yanaendelea nchini humo na tungeona serikali ya Bangui ikisifika kwa wananchi wake kutokana na juhudi za kuboresha na kuimarisha uchumi wake. Nadhani ni wakati wa Rais Francois Bozize kung’atuka madarakani, hivyo ikibidi kuitisha uchaguzi mkuu ambayo utashirikisha vyama vyote vya siasa na wananchi wa ujumla.

January 07, 2013

MUNGU ALIANZA UJASIRIAMALI TANGU KITAMBO NA WANAOTAKA KUFANIKIWA 2013


Na Albert Nyaluke Sanga, Iringa
Tangu siku Mungu anamuumba Adam, alimuumba kijasiriamali na alimwagiza akawe mjasiriamali. Unashangaa? Soma Biblia yako kitabu cha Mwanzo. Twende polepole utaelewa tu. Unajua neno Ujasiriamali/biashara linamaanisha nini? Ngoja nikujulishe. Biashara/Ujasiriamali inamaanisha, ubunifu wa uzalishaji (production), uongezaji wa ulichobuni ama kuzalisha (multiplication), usambazaji (distribution) na kutawala soko (dominion over market and ideas/innovation). Umeelewa enhee? Sasa turudi kwa Adamu. 
Mungu alipowaumba Adamu & Eva aliwambia hivi, "Enendeni mkazaliane, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kutawala vitu vyote". Wengi wanaposoma Biblia huwa wanadhani kuzaana ni "kupata watoto pekee"; lakini ukisoma English Bible (KJV) ina-highlight vizuri neno hili kuzaana; "Fruitful". Kuwa "Fruitful" inamaana "kutumia materials/rasilimali/akili ulizonazo ili kupata ama kutengeneza kitu chenye thamani zaidi", kwa lugha nyepesi ni 'uzalishaji (production). Tunaenda pamoja? 
Hebu turudi kwenye yale maagizo ya kijasiriamali ambayo Mungu aliwapa akina Adam na mkewe, "Enendeni mkawe wazalishaji (fruitful/production), mnachozalisha kikaongezeke (multiplication), mnachokiongeza mhakikishe kinajaa dunia yote (distribution), hivyo mnavyovijaza dunia yote hakikisheni mnaweza kuvitawala (dominion over market and ideas)" 
Haaa! haaa! Nimekupoteza? Usijali! Rudia kusoma pole pole, afu ujitahidi kuwa unasoma Biblia kwa tafakari; utaelewa! Sasa yoooote haya namaanisha nini? Ni hivi: Mungu alimuumba kila mwanadamu kufikiria na kuishi kijasiriamali. Si lazima kufanya ujasiriamali wa kupata fedha, lakini mtazamo wa kiujasiriamali utakupa ushindi wa maisha ya Kimungu wakati wote. ~SmartMind~

KWA WALE TU! WANAOTAKA KUFANIKIWA 2013!
Nimekuwa nikieleza mara nyingi kuwa; mafanikio katika maisha hayaji kwa lelemama! Iwe unataka uchumi mzuri, ajira nzuri, mke ama mume mzuri; ni lazima jasho likutoke. Hata hivyo sote tunatambua kuwa mafanikio yanaanza katika ufahamu wako. Namna unavyowaza inaamua namna unavyotenda, namna unavyotenda inadhihirika katika maisha uliyonayo hata sasa. Huwezi kudanganya! Tukiyatazama maisha yako, "automatically" tunajua mfumo wa mawazo na fikra zako. 
JE WAJUA? Kuwa mfumo wa mawazo yako ni matokeo ya mambo unayoyaingiza katika ubongo wako kupitia kusikia, kutazama na kusoma? Kama umenasa kwenye uhaba wa kifedha basi utambue kuwa ubongo wako umejaza "matango mwitu" kuhusu fedha, kama mapenzi yanakutesa, uwe na uhakika kuwa fikra zako zimejaa "upupu" kuhusu unavyotakiwa kubehave kwenye mapenzi. 
Soko kuu la Songea mjini
Kama upo kwenye ajira "isiyolipa" ama hujapata "japo pa kujishikiza"; basi ujue mtazamo wako kuhusu ajira na maisha "umejaa matope"!
UNAJIKWAMUAJE KUTOKA HAPO? Jibu ni rahisi! BADILISHA MTAZAMO NA NAMNA UNAVYOFIKIRI! Utabadilishaje? Jifunze kutoka kwa waliofanikiwa kufika unapotaka kwenda, Soma vitabu vinavyojenga fikra na mitazamo chanya, ama fanya yote mawili. Mimi ngoja nikusaidie moja: NITAKUPA VITABU VYA AINA HIYO! Kwa mwaka mzima nitakuwa nikituma vitabu viwili (2) kila mwezi kupitia baruabebe(email) vilivyopo katika mfumo wa pdf; kwenda kwa marafiki wote waliopanga kufanikiwa 2013. Kwa kuanza na mwezi huu Januari nitatuma vitabu vifuatavyo: 1) THE SCIENCE OF GETTING RICHER 2) COACH YOURSELF TO MAXIMUM EMOTIONAL INTELLIGENCE. Kwa rafiki unayehitaji ninapenda unijulishe email yako hapa (ama inbox) kisha utapokea vitabu hivi. KAMA UNATAKA KUFANIKIWA, KUJIFUNZA HAKUKWEPEKI. ~SmartMind~

KWA WATANZANIA KUZALIANA NI LAANA ........?


Na Salvatory Mkami, Dar es salaam
Mheshimiwa rais Kikwete mkatika hotuba yake mheshimiwa alieleza kuwa matokeo hayo ni ishara kwamba ifikapo mwaka 2016 kuna uwezekano wa idadi hiyo kufikia milioni 51 jambo ambalo linaweza kuwa ni mzigo kwa taifa, jamii na hata katika masuala ya uchumi.
Mheshimiwa Rais alizidi kufafanua kuwa jamii inapaswa kuyachukulia kwa uzito matokeo hayo hasa katika masuala ya kupanga uzazi pamoja na kuongeza bidii ya kufanya kazi.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, inaonesha kuwa kwa wastani, kila sekunde moja wanazaliwa watoto watano hapa duniani, na wakati huo huo watu wawili wanafariki dunia, achilia mbali zile mimba zinazoharibika.
Maana ya tofauti hiyo kati ya vizazi na vifo ni kwamba watu watatu wanaongezeka duniani kila sekunde moja. Ukizidisha idadi hiyo utagundua kwamba kuna ongezeko la watu 11,000 kwa saa na watu 265,000 kwa siku na hii inafanya dunia kuwa ongezeko la watu milioni 100 kwa mwaka.
Hivi sasa dunia ina watu wapatao bilioni 7. Mwaka 1750 kulikuwa na watu milioni 800 tu duniani. Kufikia mwaka 1850 idadi iliongeka na kufikia watu bilioni 1.8.

Mwaka 1950 idadi ya watu ikawa bilioni 2.5. Ilichukuwa miaka 50 idadi ya watu kufikia bilioni 6 yaani mwaka 2000. Ilikisiwa kwamba mpaka kufikia mwaka 2010 idadi ya watu hapa duniani itafikia watu bilioni 7, ikiwa ni ongezeko la watu bilioni 1 kwa muda wa miaka 10.
Lakini pia Ukiangalia mtiririko wa takwimu hizo utagundua kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa kasi hapa duniani kuanzia karne ya 19. Kwa mfano nchi yetu ya Tanzania iko chini ya kiwango cha ongezeko la watu hapa duniani ukilinganisha na nchi nyingine zilizoko dunia ya tatu. Tanzania ina ukubwa wa eneo la mita za mraba zipatazo 342,100, karibu sawa na Misri ambayo ina ukubwa wa mita za mraba zinazofikia 384,300.
Pamoja na kwamba tofauti ya ukubwa kati ya nchi hizi mbili ni ndogo sana lakini Tanzania imezidiwa kwa idadi ya watu karibu mara mbili na Misri. Kwani wakati Tanzania ikiwa na idadi ya watu wapatao milioni 44, Misri ina idadi ya watu wapatao milioni 83 kwa mujibu wa sensa iliyofanyika Julai 2012.
Ikiwa utaiunganisha Tanzania na nchi ya Benin iliyoko Afrika Magharibi ukubwa wake utalingana na nchi ya Misri, kukiwa na tofauti ndogo sana. Ukijumlisha idadi ya watu wa nchi ya Benin wanaokadiriwa kufikia watu milioni 9 (kwa mujibu wa sensa iliyofanyika Julai 2012) na idadi ya watu wa Tanzania unapata idadi ya watu wapatao milioni 53, ikiwa bado ni chini ya idadi ya watu wa nchi ya Misri.
Hii inaonesha bado nchi hii ina kiwango kidogo sana cha idadi ya watu ukilinganisha na nchi nyingine zilizo katika dunia ya tatu. Kwa hiyo sioni sababu ya serikali yetu kupiga kelele sana kuzuia watu wasizaane.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, imekadiriwa kwamba watoto milioni 1.6 huzaliwa kila mwaka hapa nchini. Na kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na wizara ya afya zinaonesha kwamba watoto wanaosajiliwa ni 140,000 kila mwaka ikiwa ni asilimia 10 tu ya watoto wanaozaliwa, hii inaonesha kwamba kuna idadi kubwa ya watoto wanaofia tumboni, na wale wanaofariki baada ya kuzaliwa inakuwa haijachukuliwa na kuingizwa kwenye takwimu za serikali.
Hata hivyo inakadiriwa kwamba watoto wapatao 51,000 hufariki baada ya kuzaliwa hapa nchini, na wakati huo huo 43,000 hufia tumboni kila mwaka.
Kwa mujibu wa takwimu hizo inaonesha kwamba bado tunayo safari ndefu ya kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa hapa nchini, kabla hatujaanza kupiga kelele ya watu kuzaa kwa mpango.
Hata hivyo chapisho hilo linabainisha kwamba mataifa makubwa yameanza kuonesha wasiwasi juu ya ongezeko la watu hapa duniani. Mataifa hayo yanadai kuwa ongezeko la watu linasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, na hivyo kutishia dunia isiwe salama.
Kwani kumekuwa hakuna udhibiti wa kutosha kiasi kwamba watu wamekuwa wakitawanyika kwa ajili ya kutafuta makazi na hivyo kuvamia maeneo ya misitu ya asili na vyanzo vya maji na kufanya uharibifu mkubwa mkubwa wa mazingira.
Imebainika kwamba iwapo watu hao watasogezewa miundo mbinu kama vile Barabara, shule, hospitali, na huduma mbali mbali za kijamii katika maeneo hayo ya hifadhi waliyoyavamia, itakuwa na maana ya kuhalalisha uharibifu wa mazingira.
Pia wataalamu hao wanadai kwamba ongezeko la watu haliendi sambamba na ujenzi wa miundo mbinu ambayo itasaidia kulinda uharibifu wa mazingira.
Labda niwaulize ndugu wasomaji, hivi nchi masikini na zile nchi tajiri zenye viwanda ni zipi hasa zinazoifanya dunia hii isiwe salama?
Wao wana viwanda wanazalisha sumu kila uchao huku wakitulisha vyakula na madawa yenye sumu ili kujikusanyia utajiri, halafu leo wanasema kuwa nchi masikini ndizo zinazochangia uharibifu wa mazingira na kuifanya dunia isiwe salama, huu ni uonevu wa hali ya juu.
HEBU TUANGALIE UPANDE MWINGINE WA SHILINGI WA KADHIA HII:
Kuzungumzia ongezeko la watu, unazungumzia ongezeko la soko, kwa maana ukuaji wa biashara, nguvu kazi, na ongezeko la viwanda, na hivyo ukuaji wa uchumi kuongezeka.
Kwani kwa jinsi idadi ya watu inavyozidi kuongezeka na ndivyo uchumi unavyozidi kukua, hebu angalia nchi kama ya China, India, Marekani na iliyokuwa Urusi kabla haijasambaratika, ukuaji wa uchumi katika nchi hizo ulitokana na kuwa na idadi kubwa ya watu.
Ila naomba nitahadharishe kidogo hapa, ninapozungumzia ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi nazungumzia nchi kutumia nguvu kazi katika kuzalisha na kuwa na serikali makini inayowawezesha wananchi wake kufikia malengo yao.

January 05, 2013

HATUA KWA HATUA YA AJALI YA BUS LA NEWFORCE ILIYOTOKEA NYORORO-IRINGA KAMA ILIVYOSHUHUDIWA NA EGBERT JEREMY


Kama inavyoonekana pichani bus la NewForce likiwa limepinduka kijiji cha nyororo mkoani Iringa

Mizigo ikitolewa ndani ya Bus baada ya kupinduka
Mashuhuda wa ajali hiyo.

Mwanamke anaonekana kwa mbali hapo akiwa ameanguka kutokana na bus kupinduka hivyo kukosa mwelekeo wa kujiokoa. 
Bus la NewForce likivutwa ili likae sawa barabarani baada ya ajali.

CHADEMA WANACHEZA NGOMA ZA CCM

 Na Markus Mpangala
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo katika maeneo mbalimbali nchini kuna mwenendo wa kisiasa za mabadiliko kwa kila upande. Chadema walisimamisha harakati za mikutano ya hadhara ya M4C iliyokuwa ikifanyika maeneo mbalimbali nchini.
Kimsingi kwenye ushindani lazima apatikane mshindi, na asiyekubali kushindwa siyo mshindani. Katika kila tukio ama masuala ya kisiasa yanayotokea hapa nchini, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010, Chadema ilionekana kwua mshindani mkali wa CCM



Uchaguzi huo mdogo unalipomalizika katika kata 29, ilishuhudia CCM ikipata ushindi wa Kata 22, huku Chadema ikiambulia Kata 5. Baadhi ya wapinzani wa Chadema wanadhani hilo ni pigo kubwa kuliko yoyote yaliyowahi kutokea katika siasa za ushindani baina ya CCM na Chadema.
Kila jukwaa ambalo waliweza kupita wana chadema walifanikiwa kujigamba kutokana na hali iliyojitokeza kwenye matokeo ya uchaguzi. Licha ya mgombea urais wa Chadema kutoapata ushindi wa kiti hicho lakini alileta changamoto kubwa kwa CCM.
Kuanzia hapo CCM wakawa wanavutwa kila jambo na Chadema. ilikuwa rahisi kubaini kuwa Chadema walikuwa wkaiongoza nchi kutokana na siasa zao za ushindani na namna walivyoweza kusimamia hoja. Hili lilijitokeza bungeni na katika majadiliano mbalimbali.
Chadema ilikuwa inaasisi hoja amabzo baadaye CCM ilionekana kufuata nyuma. Hata hivyo kuna mambo yamebadilika katika kipindi fulani cha mwaka huu katkati.
Kwanza suala la Meya wa iji la Arusha, kisha malumbano ya kawaida kuhusu Mbunge Maswa, John Shibuda ambaye alidaiwa kutamka kunuia kuwania urais, kisha suala la Zitto Kabwe kuwa miongoni mwa wa kero za chama bila kujali uanachama wake.
Pengine hayo hayakuweza kuitikisa Chadema kwani viongozi wake walikuwa makini na walijua katika siasa hakuna kanuni moja ya kuweza kufanikiwa. Suala la Mbunge wa Arusha mjini nalo lilikuwa moja ya mambo yaliyisababisha Chadema izungumzwe zaidi.
Lakini mahakama ya Rufaa imemrudishia Ubunge wake, Mheshimiwa Godbless Lema. Nadhani huu ni ushindi mwingine wa kwa Chadema. aidha, pamoja na ushindi huo kuna suala jingine lililoibuka tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo uliohusisha Kata 29.
Kuanzia wakati huu ndipo CCM wameamka na kuanza kupata mwanya wa kuzungumza kwa ushindani dhidi ya Chadema. ikumbukwe CCM walipoteza ubunge wao katika jimbo la Igunga ambapo mbunge wake Dk Dalily Kafumu alivuliwa Ubunge na Mahakama Kuu kanda ya Tabora.
Hayo yalitokana na jitihada za Chadema kupinga ushindi wa CCM. lakini kuna mambo yamebadilika kwa kiasi kikubwa baada ya chaguzi ndogo.
Suala la madiwani wa Ilemela mkoani Mwanza nalo linaweza kuwa sehemu ya hoja za CCM ambao wameweza kuzinduka kutokana na ushindi wa Kata 22 kote nchini. Sababu baada ya hapo CCM ilikuwa na chaguzi za ndani katika jumuiya mbalimbali.
Pia CCM iliweza kuchaguana katika Sekretarieti mpya ya kuendesha chama chao. Ujio wa Abdulrahman Kinana na Philip Mangula unaonekana kuwa moja ya nyenzo ambazo mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete amejaribu kurejesha imani kwa wanachama na wapigakura wao.     Kama nilivyowahi kuandika katika safu hii kuwa tunaona wazi kabisa, Jakaya Kikwete anairudisha CCM kwa wakomunisti kwa kutengeneza njia zilezile ambazo zilitumika na akina Mao Zedong.

Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini. 


Tangu kumalizika kwa chaguzi za ndani za CCM na kuteuliwa kwa Sekretarieti hiyo ninaona kabisa mabadiliko ya kimantiki kuhusu ushindani wa vyama hivi viwili, kwamba Chadema badala kuifanya CCM ifuate njia zake, sasa Chadema ndio inafuata mengi yanayosemwa na CCM. 

Hayo yanayosemwa bila kujali yana maana au yamejaa upuuzi. Kuna upepo fulani umevuma ghafla kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka huu. upepo huo umekifanya Chadema kuwa na hali ya kutafuta tafakari nyingi kuhusiana na mwenendo wao wa kisiasa. Wapo wanasiasa wenye mtazmao finyu ndani ya CCM waliweza kuihusisha M4C na zile Pick-Up za waasi wa Benghazi. Hayo yaliendelea sehemu mbalimbali nchini iwe kwenye vyombo vya habari ama mitandao ya kijamii. 
Hali hii iliachwa, na matokeo yake wapow aliofanikiwa kuwarubuni wananchi kwamba harakati za M4C zilikuwa na lengo la kuvuruga amani. Jambo jingine ambalo limebadilisha upepo huu ni mgogoro wa chinichini baina Chadema na Jeshi la Polisi.
Maandamano ya Morogoro yalisababisha maafa. Maandamano ya Iringa yalisababisha kifo cha Daudi Mwangosi. Kisaikolojia pekee mtu atauliza kwanini kifo kimetokea. Jibu lake litakuwa ni katika mkutano wa Chadema bila kujali muktadha wa kifo hicho.
Kwa mantiki hiyo hii ilikuwa inaleta ghasia kwa wananchi wa kawaida lakini kwa werevu walijua mwenendo wa siasa za harakati una faida zake hivyo licha ya mapungufu mbalimbali bado Chadema walipaswa kuheshimiwa.
Jambo zuri ni kwamba Chadema wamekiri kuwa wanalazimika kuachana na siasa za Harakati, hivyo kujipanga upya tangu kusitishwa kwa M4C. hekima hii imekisaidia sana Chadema ili kupumzisha akili za wnaanchi kutiwa hofu na kasi ya vurugu baina yao na jeshi la Polisi.
Yapo mambo ya msingi ambayo Chadema na Jeshi la Polisi wanaweza kusaidia katika kukuza demokrasia na uhuru wa kujieleza. Lakini haitoshi tu kulalamika kwamba Chadema ilisababisha ama Jeshi la Polisi lilisababisha.
Kila upande ukichukua wajibu wake nina uhakika haliweza kutokea tena, na endapo litatokea basi sababu za kutokea kwa vurugu hizo kutakuwa na zaidi ya siasa za kawaida tulizozizoea.
Lakini kingine ambacho kinasababisha Chadema ielekee kucheza ngoma za CCM ni hatua ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kusema baadhi ya vigogo wa vyama vya upinzani wanamiliki kadi ya CCM, kumejitokeza masuala mengi ndani ya Chadema.
Sio hilo tu bali hata taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa Chadema inapitia katika jaribio la kisiasa kutoka CCM. wakati CCM ikipima kina cha maji ya Chadema kwa kushambulia moja kwa moja kwenye ngome yao (Dk. Slaa), bado Chadema haijatoa majibu kwa hoja hizo zaidi ya mazungumzo ya hapa na pale.
Kisiasa hatua ya kutajwa Dk Slaa kumiliki kadi ya CCM kulikuwa na maana moja tu kutimiza falsafa ya aliyekuwa Rais wa Marekani Bill Clinton, kwamba ukitaka kumshinda adui yako basi shambulia ngome yake. CCM inaelewa aliyesababisha wakose kura nyingi kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 alikuwa Dk. Slaa kutokana na kukubalika na wengi.
Pili CCM imejaribu kuzingatia hoja ya nani ashambuliwe kisiasa ili kuweza kuidhoofisha Chadema. kimsingi kufanya malumbano au mashambulizi yoyote dhidi ya Chadema kupitia Dk. Slaa nina imani ni kujaribu kushambulia ngome ya Chadema.
Kwahiyo shambulizi hilo kwa Dk. Slaa ni jaribio la kupima uzito wa majibu ya Chadema namna ainavyoweza kukabailiana na njia mpya ya kupambana na CCM.
Bahati nzuri Chadema wametulia, ingawa wanasiasa chipukizi wameambukizana hisia na kuanza kucheza ngoma za CCM. hatua za viongozi wa Bavicha huko Mwanza, Mbeya au manyara, ni mwanzo wa kuonekana ukosefu wa msingi wa kushghulikia mashambulizi ya kisiasa.
Njia nzuri ya kudhibiti mashambulizi ni kuacha wakati upite, huku wahusika wakiacha kutumia muda mwingi kulumbana kwa hoja zinazowasilishwa. Kwahiyo Chadema watacheza ngoma za CCM kwa muda mrefu kama hawataelewa kwanini kuna mashambulizi dhidi ya Dk. Slaa.
Kwa vijana wenzangu wa Bavicha na chama chao kama hawatagundua hila za kisiasa sina shaka wanaweza kudhani kile wanachoshambuliwa wanatakiwa kukijibu kwa mashambulizi ya papo kwa papo.
Lakini njia nzuri ya kupambana kisiasa ni kuhakikisha wakati unapita ndipo unachukua nafasi ya kujibu mashambulizi kwa namna nyingine.
Mathalani, wakati wa uchaguzi wa Marekani, Mitt Romney alifanikiwa kumshambulia Barrack Obama kwa nguvu sana kwenye mdahalo wa kwanza.
Lakini wakati wa mdahalo wa pili Barrack Obama aliweza kumwadhibu Mitt Romney vibaya sana tena kwa kumgusa kutokana na kampuni yake ya Bain Capital kuendeleza wimbi la kuwakosesha ajira wamaerkani kwa kununua makampuni machanga kisha kuyafilisi.
Jambo jingine, am ana ambalo Chadema wakitaka kuepuka kuendelea kucheza ngoma za CCM ni kujifunza jinsi Obama alivyoweza kumshambulia Romney kwa hoja na “timing” ya hali ya juu.
Labda ingelikuwa kwenye ndondi basi tungesema Barrack Obama alipiga konde la “Chop” ya nguvu ambayo lililomdondosha Romney. Obama alisema wakati Romney aliwa Gavana aliongoza jopo la wabunge kusitisha uchimbwaji wa Makaa ya mawe, lakini miaka michache baadaye kampuni yake ikawa inaongoza kuhitaji uwekezaji wa makaa ya mawe.
Hilo linaweza kuchukuliwa kama njia ya kupambana kiasa. Lakini kwa hulka ya Bavicha bila utafiti wa kina watajikuta wakilazimisha Chadema kucheza ngoma za CCM, bila kuelewa dhumuni la kutungiwa nyimbo za kumnanga Dl. Slaa.
Sio yeye pekee, ilizuka nyingine kwamba Zitto Kabwe alihusika na rushwa kule Bungeni. Lakini Ripoti ya Mheshimiwa Ngwilizi ikaeleza kuwa kilichosemwa ilikuwa ulaghai.
Kwa maana nyingine ndani ya Chadema kuna wanasiasa walikwua wakicheza ngoma za CCM bila kujielewa. Na kwa mtindo huu, tunafanga mwaka kwa kuona Chadema wakiwa watulivu na kupanga mikakati kwamba mwaka 2013 hakuna kulala.
Lakini watambue hakuna kulala kokote kusiko na msingi wake. Itakuwa mbaya zaidi wakicheza ngoma za CCM, kwa kila shutuma dhidi ya wanasiasa wao wa ngazi za juu. Ni mtazamo tu. Nimemaliza.

January 02, 2013

TAARIFA KWA WAWEKEZAJI WAPYA KATIKA KILIMO CHA MITI YA MBAO, KARATASI NA NGUZO.


Fresh Farms & Tours (T), biashara tanzu ya Anesa Co.,Ltd (Nyaluke Business Empire); inajishughulisha na upandaji, utunzaji na uendelezaji wa mashamba ya miti ya mbao, karatasi na nguzo-mkoani Iringa. Vilevile inahusika na uvunaji na usambazaji wa mazao ya miti, (mbao na nguzo za umeme) sambamba na ufugaji. 
Fresh Farms ilianzisha programu maalumu, mapema mwaka jana; inayolenga kuwawezesha watanzania wengine kuwekeza katika kilimo cha miti kwa urahisi. Tayari makumi ya watanzania wamechangamkia fursa hii. Fresh Farms & Tours (T) tunapenda kuwaarifu wale wote wenye nia ya kuwekeza nasi; KWAMBA kuanzia tar 1, Feb, 2013 kutakuwa na mabadiliko ya bei na gharama za uendeshaji kwa mashamba ya miti. 
Mashamba tunayoyauza laki sita kwa sasa; bei mpya itakuwa milioni moja; na yale tunayouza laki nane gharama yake itakuwa milioni moja na nusu. Bei hizi hazitawaathiri wateja wa awali na wale ambao wamekwisha wasilisha oda zao. Fresh Farms & Tours (T) tunaendelea kuboresha huduma, taarifa na usaidizi kwa wote wanaowekeza nasi. 
Fresh Farms & Tours (T) tunakutakia heri ya Mwaka mpya wa 2013 na tunakukumbusha ile salamu yetu (motto); "Greening the world and Feeding People". 

IMETOLEWA NA:
Albert Nyaluke Sanga
Mtendaji Mkuu-Fresh Farms & Tours(T), (C) 2012

TOKA ANALOJIA HADI DIGITALI: NINI MAONI YETU?


John Mnyika, MB

Na John Mnyika, Dar es salaam
Naomba majibu yenu kwa kuzingatia kuwa kazi ya wabunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali: baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa kuhama kutoka analojia kwenda digiti kwa mkoa wa Dar es salaam; kwa watumiaji, nini faida na athari mlioanza kuzipata kwa wenye ving’amuzi? Na nini kikwazo kwa wengine ambao hamjahamia mpaka sasa? Na nini mnataka watoa huduma na mamlaka zingine kuzingatia? Katika hatua ya sasa, ni muhimu Tanzania Consumer Advocacy Society (TCAS) ifanye tathmini ya kina kwa niaba ya watumiaji kwa ajili ya hatua zake.  
Ikumbukwe kwamba Consumer Federation of Kenya ilikwenda mahakamani na kuzuia mitambo kuzimwa watumiaji tarehe 31 Disemba 2012, na mahakama imesitisha mpaka itakapofanya uamuzi wake wa msingi.
Kwa upande mwingine, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA-CCC) litumie mamlaka yake kwa mujibu wa kifungu cha 37 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano namba 12 ya mwaka 2003 na vifungu vingine vinavyohusika kushughulikia malalamiko yaliyotolewa kwa nyakati mbalimbali kwa kuzingatia tahadhari tuliyotoa kwa serikali bungeni miezi mingi iliyopita kuhusu athari zitazojitokeza kwa kutozingatiwa kwa maandalizi muhimu.

NB: John Mnyika ni mbunge wa jimbo la Ubungo