January 12, 2013

WANAWAKE NA WANAUME: HAKI SAWA NA USOMI

Jackline Mluge, Finland

Na Jackline Mluge, Finland

WANAWAKE VIPI? katika ulingo wa ndondi kuna raundi 1 hadi 12. zamani wakati raundi moja kwenda nyingine inapokwisha, kuna wanaume walikuwa wamevishwa suti au mavazi safi kutangaza raundi inayokuja ni ya ngapi. 
SIKU hizi WANAWAKE wanatumika kutangaza raundi huku wakiwa wamevishwa vichupi, au mavazi ambayo yanaonyesha nusu uchi kabisa, wanatembea kwa mikogo sana. Nini hicho? 
Hapa bongo utaona WANAWAKE wanavaa visuluwali vya mazoezi na kugeza kuwa mtoko wa siku, wanasema fasheni. Kila sehemu ya mwili huonekana, kama minyama au kiuno maridadi na kadhalika. WANAWAKE mnajidhalilisha ama? naendelea ....
Sasa hivi wanawake wanafanya kazi zote ambazo wanaume wanafanya. Ilikuwa zamani lakini si kwa sasa ila wanaume ndio wanao ji dhalilisha kwa sasa unakuta dumezima lina baka mtoto.Mimi na pingana kabisa haki sawa kwa jinsia zote
simpenzi wa nguo fupi lakini nadhani kila mtu ana uhuru wa kuvaa anachotaka hiyo siyo kujidhalilisha. 
Na kuhusu kujiuza kuna wanaume wanajiuza kwa akina mama wenye pesa tena wanapanga mstari unachagua kama nguo, na sasa wanawake wanajibadilisha kuwa wanaume na wanaume wanajibadilisha kuwa wanawake. Hao wanafunzi wanaojiuza wamezoea kujiuza sisababu hawajapata mkopo- mfano nasoma chuo cha Afya napata hela kidogo kutoka serikalini lakini muda wangu wa ziada nafanya kazi ya fani ninayosomea au hata nyingine kujipatia hela za matumizi na wakati huohuo na soma. 
Naamini unapokuwa chuo si mtoto tena umefikia umri wa kujitegemea kiamawazo lakini nia aibu mtu mzima kufundishwa kuacha umalaya, Hebu niambie wakimaliza chuo wasipopata kazi watalalamika kazi hakuna ngoja tuendelee kujiuza. 
Limenisikitisha sana kuona watu wenye elimu bado wanakili za kulalamika kitu fulani badala ya kuchagua njia mbadala ya kutatua matatizo yao mfano mnaweza kuanzisha kuuza sambusa hostel unajipatia pesa tatizo la wasomi wa Tanzania mtu akifika chuo hataki kufanya kazi mbaya mbaya anataka kufanya kazi hiyo hiyo aliyosomea huku kuna watu wanasomea uanasheria au uganga nk lakini utakuta wanafanya kazi ya kuuza baa kipindi wanasoma wakijipatia hela za kujikimi na mtu aoni aibu.Tanzania ehiii amka sasa acheni porojo.

January 11, 2013

CCM IMERUHUSU YENYEWE KUKABWA KOO NA UPINZANI


Na Markus Mpangala, Dar es Salaam

Kuna dhana moja kwamba vyama vya upinzani ni uadui. Kimsingi jambo hilo sio kweli na lazima tukemee kuwa kazi ya vyama vya upinzani ni kuikumbusha serikali kupitia chama kinachotawala. Hivyo basi kazi ya serikali ya CCM ni kuhakikisha kuwa masuala ya msingi ndani ya nchi yanafanyika ipasavyo. 
Haiwezekani wapinzani wakaibuka tu kutoka porini na kuanza kupinga ama kulalamikia jambo fulani. Lazima wameketi chini na kuona namna ambavyo CCM inakosea na makosa hayo ni dosari tu ambayo inatakiwa kufanyiwa kazi. Vivyo hivyo kazi ya CCM sio kulalamika kuwa kwanini wapinzani hawashiriki kutatua kero ya nchi yetu. Kazi ya vyama vya upinzani ile kukosoa na kukishambulia CCM maana yake wanatimiza wajibu wa kuikumbusha serikali ya CCM kuwa kuna mahali hapaendi vizuri. 
Kwahiyo Kazi ya mpinzani ni kukupinga. Dosari yako ni faida kwake. Yapo maeneo ambayo vyama vyote vinapaswa kushirikiana, mathalani lile kongomano lililoandaliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuhusu ulinzi, usalama na demokrasia, mbali ya Chadema kususia. Lakini neno kubwa hapa ni kwamba mpinzani akiona dosari zako ndio kete yake ya kupata ushindi.  
Ukitaka mpinzani wako asipate kete ya ushindi hakika unaziba mianya yote ya kumfanya apate kete. kwanza, hakika Ilani ya chama chako inatekelezwa, ahadi zote zinatimizwa. njia mpya za uchumi zinavumbuliwa maana watalamu wapo. mkondo mpya wa kuibua maendeleo unatakiwa kupatikana, vivyo hivyo unapaswa kuelewa kuwa anayesababisha vyama vya upinzani kupata la kusema ni chama tawala chenyewe. 
CCM ikijikita kwenye shughuli za kutimiza maazimio yake kwa wananchi, sidhani kama ni vibaya. MTAJI KISIASA, inawezekana hata Mheshimiwa mbunge wa Nzega alipokemea kuhusu uchimbaji madini na kuhimiza watu kugoma ni MTAJI PIA. Sijui wanasiasa wetu wanatafsiri namna gani juu ya mtaji wa kisiasa. Na kugoma ilikuwa hatua ya mwisho pale Nzega mjini Tabora ili serikali isikilize kilio cha wachimbaji wadogo wa madini. MUHIMU; CCM timizeni mliyokusudia kwa maendeleo ya wananchi. do it all utaona kama akina sisi huku pembeni kama tutakosoa. Ni faida kwenu na kwa wananchi sisi.

WILAYA YA MBINGA YAENDESHA KAMPENI YA UPANDAJI MITI

Ambroce Nkwera, Mbinga
Na Ambroce Nkwera, Mbinga

Wilaya ya Mbinga imeendendelea na kampeni kubwa ya upandaji miti kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hii. Hatua hii inalenga kulinda na kuhifadhi mazingira ya wilaya Mbinga ikiwemo kupambana na mabadiliko ya tabia nchi. Wananchi mbalimbali walijumuika katika kapeni hii ambayo imewahusisha watu wa kada mbalimbali, maofisa wa serikali na asasi binafsi wilayani hapa.
Wananchi wamehimizwa sana umuhimu wa kupanda miti kila wanapokata na hata pale wasipokata. kwa mujibu wa azimio la Halimashauri ya Wilaya Mbinga, kila mwananchi anataiwa kushiriki ikiwa sehemu ya mipango ya maendeleo ya uchumi kwa kulinda mazingira ya wilaya hii. mwandishi wa Habari hizi amefanikiwa kupata miti 700 ambayo amefanikisha kusafirisha hadi kijiji cha Mkali kilichopo katika wilaya ya Nyasa kwa lengo la kuendeleza kampeni ya kupanda miti. 
Kwa mujibu wa ratiba ya kampeni ya upandaji miti, itapita katika vijiji mbalimbali vinavyounda wilaya ya Mbinga huku uwezekano wa kampeni hizo kuhamia wilaya ya Nyasa ni mkubwa. Ikumbukwe kuwa wilaya ya Nyasa ni mpya ikwia bado inategemea watendaji kutoka wilaya ya Mbinga, hivyo kampeni hizo zitakwenda sambamba na uhamasishaji wa utunzaji mazingira kwa wilaya ya Nyasa ili kuepuka ukame unaoweza kutokea. Kampeni hii imevutia wengi na wananchi wamepanda miti ya kutosha.
Kulikuwa na mkakati wa upandaji miti na bado unaendelea, awamu ya kwanza waliotesha miti laki nne(400,000) yote wakawagawi wananchi bure na ikaisha awamu ya pili ndio hii, pia wamegawa miti karibu laki moja(100,000) na imeisha. Wananchi wameitikia mwito huu kwa ari kubwa sana. Tumegundua kuwa wananchi walikuwa wakikosa msukumo hivyo hatua hii imesaidia zaidi kufanikisha kusambaza habari za utunzaji wa mazingira kwa maendeleo yao.
Mipango mingine juu ya kusambaza na kuelimisha umuhimu wa upandaji miti inaendelea hapa Mbinga, huku halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na baraza la Madiwani na wabunge wake kuhakikisha mpango huu unakwenda safi na kuboresha mazingira. Aidha, tunatarajia mpango huu utafikishwa hadi wilaya ya Nyasa kama ilivyokusudiwa ili kukabiliana na ukame, pamoja na kuhifadhi mazingira. Tunawakaribishana wana Mbinga wote kutimiza ajenda hii ya kutunza na kuendeleza mazingira ili yawe bora kwa afya bora. Hilo litasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

UCHAWI: DHANA INAYOANGAMIZA JAMII YETU



Na John Chitanya, Nyasa

Mei 4, 2012 yalifanyika maandamano makubwa sana katika wilaya mpya ya Nyasa iliyogawanywa kutoka wilaya ya Mbinga. Nyasa ni wilaya ni kiserikali, lakini katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi inafahamika kama jimbo la Mbinga Magharibi. Maandamano yaliyofanyika yalilenga kuishinikiza serikali kumruhusu Mganga wa Kienyeji apewe  kibali cha kufanya kazi yake ya kuwaumbua wachawi wilayani hapa.
Maandamano yale yalionyesha na televisheni ya TBC1  wakazi wa mji wa Kilosa nje kidogo ya mji mdogo wa Mbamba Bay, kwa hakika ilikuwa fedheha kubwa kwa wananchi wa ukanda wa ziwa Nyasa na maeneo mengine yanayounda wilaya hiyo kwa upande wa mashariki ambayo yanakaliwa na jamii ya Wamatengo.
Kwa mtazamo wangu kama kuumbuana na kushika uchawi  wameshikana sana,  sasa tunataka maendeleo sio kuimba nyimbo za wachawi kuwanyima maendeleo baadhi ya watu.  
Watu wengi wanaamini kuwa kuna kasoro pale inapotokea jambo fulani likawa baya, basi linazungumzwa kuwa linatokana na kurogwa na wachawi.
Mganga wa kienyeji
Niliwahi kushuhudia tukio moja kwa moja ya familia iliyokuwa ikiendesha kikao cha kifamilia, kwamba binti mmoja wa shule ya msingi alishindwa kusoma na kuandika hivyo walipanga kwenda kwa Mganga wa Kienyeji ‘kumfungua” kwa madai alifungwa na watu wabaya(wachawi) asiweze kujua kusoma na kuandika.
Hakika suala hilo lilileta mtafaruku kwa wale waliofanikiwa kwenda shule, wakadai kuwa hilo ni suala la mwanafunzi mwenyewe wala halina uhusiano na kufungwa kwa misingi ya uchawi. Lakini ilishikiliwa uchawi ndio umemfunga binti yule. Hadi naandika makala hii juhudi za kumfikisha mwanafunzi yule kwa Mganga wa kienyeji zilikuwa zimesimishwa ila sina shaka zitaendelea kwani nia yao ipo na wanaonekana kuamiani sana uchawi umetumika kwa binti yule.
Matukio ya uchawi yamekuwa yakitangazwa sana hata wakati uchaguzi unapofanyika, kwani wagombea mbalimbali wanadaiwa kuwategemea waganga wa kienyeji, wapiga ramli na kuamua hatima ya harakati zao. Kwenye michezo ya mpira wa miguu na mingine suala la uchawi limekuwa likichukua nafasi kubwa bila kutegemea sayansi ya kuleta mafanikio.
Hatua za vigogo kuhangaika na kuwategemea waganga wa kienyeji inaleta ujumbe kuwa jamii yetu inakabiliwa sana na janga la uchawi na kutoamini nguvu zilizomo kwenye akili na miili yetu.
Leo hii ni vigumu kufanya jambo la maajabu kwa kutohusisha uchawi. Hapa ndipo mimi siku zote huamini mapinduzi ya maendeleo ya wilaya ya Nyasa na yale yenye kasumba za kutegemea wachawi yanapaswa kuanzia katika fikra zetu. Tuna mambo mengi ya kuyafanyia maandamano katika nchi hii, mfano umeme, bandari, barabara isiyoisha na mengine mengi, lakini wananchi wameshikilia na kuamini kuwa uchawi umesababisha wawe na maisha duni.
Hata hivyo tukio la mji wa Kilosa, waliohamasishwa mapema mwezi Mei, ili Mganga wa kienyeji kutoka Tanga walikamatwa na mamlaka zinazohusika. Mganga huyo alihamasisha vijana wa Mbamba Bay wafanye fujo kushinikiza apewe kibali ili atoe uchawi kwenye nyumba za watu, basi wale vijana wakavunja ofisi za serikali na kuchoma moto, huku  wakalazimisha kila familia kuchangia shilingi 5000.
Mamlaka zinazohusika zilifanikiwa kuzima jaribio hilo, na kuwakamata baadhi ya vijana waliohusika. Baadhi ya vijana yao ni mabinti watatu waliokamatwa kwa kosa la kuandamana bila kibali na kufanya vurugu, walishikiliwa mjini Kilosa, Mbamba Bay. Tukio hilo linaturejesha kwenye mjadala hivi masuala ya uchawi yanachukuliwaje kama turufu ya kufanya uhalifu au uvunjifu wa amani? Uchawi umekuwa ukizungumziwa sana katika jamii zetu.
Wafanyabiashara wanategemea uchawi, watu wa kawaida wanategemea uchawi, ina maana hata masuala yenye kuhitaji utaalamu yamepewa dhana ya uchawi. Jamii yetu imeshikilia dhana ya uchawi kama nyenzo ya kupata mafanikio. Wengi hushikilia sana kupiga ramli, wamekuwa wakishindwa kujielemisha na kupata ufumbuzi wa matatizo ya familia na jamii huku wakiamini matukio hayo yanatokana na uchawi. 
Idadi ya wapiga ramli nayo inaongezeka kila kukicha. Ulimwengu unatuacha nyuma, na kila mwenye mafanikio maishani anaweza kutazamwa kwa namna mbili; mosi aliiba mahli na pili amefanya uchawi. Hakuna watu wanaoamini kuwa juhudi hizo zimefanywa na mhusika. Kuna masimulizi mengi sana kwa wana jamii ya wilaya ya Nyasa kuhusiana na uchawi. Magari yakipinduka husemwa uchawi, hakuna anayesema kuwa barabara ni mbovu, wote husikilia uchawi.
Kuna mambo mengi yanatisha na bila juhudi za serikali kusambaza elimu kila jambo lingeonekana kwua uchawi. Na serikali yetu haiamini uchawi hivyo ni kosa la mtu kufanya fujo kama vijana wale kwa kisingizio cha uchawi. Sio hapa tu, hata Afrika Kusini, aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Pits Mosimame aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akijibu swali kwanini Bafana Bafana haijashinda mechi nyingi tangu achukue madaraka.
Naye  alijibu kwa urahisi kuwa shirikisho la soka la Afrika Kusini halijamlipa Sangoma (mganga wa kienyeji) tangu michuano ya kombe la dunia. Hali hiyo inaonyesha namna gani jamii imetawaliwa na uchawi. Kila kitu tunachofanya kinaonekana kimetokana na uchawi. Wachawi wamekuwa vikwazo kwenye mafanikio ya jamii yetu.
Dhana hii ya uchawi itaendelea kutuangamiza ikiwa juhudi za makusudi hazitachukuliwa. Kwa mtazamo wangu, naona uchawi ni sumu kali sana, lakini kama uchawi wa kisayansi basi nitasema kila nchi inao uchawi.
Nasema kila nchi inao uchawi kwa maana ya kisayansi kutokana na mila na desturi za nchi hiyo. Ujerumani walileta utabiri wa Pweza Paul, akatabiri ushindi kwa wahispania. Nao ni uchawi kama wapiga ramli za kisayansi sio mazingaombwe. Zipo nchi zinatumia uchawi wa kisayansi kwa njia ya maneno hususani katika dini,  “kuapishwa” au “kusimikwa”, kinachotendeka ni uchawi, ni mila na desturi za nchi husika na tamaduni zao. Mikoa ya kanda ya ziwa inakabiliwa na dhana hii ya uchawi imesababisha hofu kwa ndugu zetu albino, na wazee wenye macho mekundu. Wazee hao huuawa kwa kisingizio eti wachawi. Nionavyo uchawi uliosababisha watu wa mji wa Kilosa waandamane mapema mwezi Mei mwaka huu ni sumu kali sana, na kawaida sumu haiwezi kutibu ugonjwa mwingine, kwani huua.

John Chitanya ni mwandishi na mwalimu wa Miracle Center, mjini Songea. Niandikie: 0718 005557

NIDHAMU YA WALIMU WETU KAMA WANAMUZIKI WA BONGOFLEVA


Na John Chitanya, Nyasa
Naandika baada ya kufanya ziara fupi kutembelea shule ya sekondari ya Monica Mbega iliyopo Kata ya Mbaha katika Tarafa ya Ruhuhu. Nilianza safari yangu katka kijiji cha Lundu kuelekea Mbaha, ambapo umbali wake ni kilimita 1, niliwasili shuleni hapo yapata saa asubuhi.
Lengo la safari hiyo ni sehemu ya mkakati wa kutembelea shule zote za Kata katika Tarafa ya Ruhuhu, kisha shule za Tarafa ya Ruhekei kwenye wilaya mpya ya Nyasa. Nilipowasili shule hapo nilikusudia kuangalia mazingira ya shule na namna gani walimu wa shule hiyo wanavyowasilia katika uwajibikaji wao kwa wanafunzi na namna gani wanafunzi wanawajibika kwa walimu wao ili kujenga nidhamu na mafanikio ya shule.
Nidhamu baina ya mwalimu na mwanafunzi ndio msingi mkuu wa kulefa mafanikio ya shule yoyote.
Mpaka naondoka shuleni hapo saa moja na nusu sikufanikiwa kumuona mwalimu yeyote hata wa zamu hakuwepo, mazingira ya wanafunzi nao wapo kama wapo msibani hakuna shughuli za usafi wa mazingira. Nilijaribu kumhoji mmoja wa wanafunzi kama wamefanya ‘roll call’, nikaambiwa muda bado haujafika. Wakati huo ilikuwa saa moja na robo. Mpaka muda huo nilikuwa na wanafunzi wasiozidi 50.
Wanafunzi wa shule ya msingi Mango, wilayani Nyasa. 
Picha kwa Hisani ya Tanzglo
Na kati yao hapakuwa na mwenye saa. Picha hiyo unatarajia patakuwa na hali nzuri kimasomo, wajibu na nidhamu kati ya mwalimu na mwanafunzi? Kwahiyo hali nzuri ya kitaaluma kwa shule kama hiyo sio jambo linaloweza kutokea, kwa vile mwanafunzi hurithi tabia za wakubwa naamini wanafunzi watakuwa katika hali gani kitabia na kitaaluma toka kwa walimu hao? Kama mwalimu ni mvivu kuwahi shule unatarajia atapanda mbegu gani kwa wanafunzi wake? Nilipojaribu kutaka kujua kama walimu wanakaa mbali na maeneo ya shule niliambiwa wote wanakaa ndani  ya mita 100 toka shuleni hapo. Je unatarajia nini kwa shule kama hiyo?
Nilifanya ziara hiyo kwakuwa mwezi wa pili nilikuwa katika kikao cha tathmini ya matokeo ya mitihani ya taifa kwa kidato cha pili na nne. Nilienda kwa niaba ya mzee kwa wanafunzi. Katika matokeo ya kidato cha pili walikuwa wanafunzi sio chini ya 47, lakini waliovuka wastani ni wanafunzi watatu tu. Katika matokeo ya kidato cha nne hawakuzidi wanafunzi 37, lakini waliopata vyeti kwa daraja la nne kwa pointi  29-33 ni wanafunzi 6 pekee na wanafunzi waliobaki walifeli.
Wakati ule mkuu wa shule alijitetea kwenye kikao cha tathmini kuwa shule haikuwa na walimu  wa kutosha kwani walikuwa watatu tu. Kwa sasa shule hiyo ina walimu 8 bado hawatoshi. Kama walimu 8 hawafiki darasani kwa muda mwafaka wakiwa walimu 20 itakuwaje hali ya shule hiyo? Sitakosea nikisema walimu hao ipo siku watafika shuleni saa sita mchana kwa kufuata muda wa vipindi vyao tu? Leo nimekumbuka msemo wa walimu  wa siku hizi  ni walimu wa bongofleva wanafika shuleni wamevaa suluali za jeans. Na wao wanajitetea kuwa ualimu sasa sio wito bali kazi, na kama wito ulikuwa zamani sana. Sijui, natafakari tu.

•    John Chitanya, ni mwandishi na mwalimu wa Miracle Center iliyopo Songea. Maoni: 0718 005557

January 08, 2013

WATANZANIIA TUNAWEZAJE KUISHI KWA GHARAMA KUBWA KILA MWEZI?


Na Yasinta Ngonyani, Sweden
Fikiri, matumizi nyumbani:- chakula, umeme, gesi, maji, soda au juisi za wageni. Ada za watoto zinazolingana na za vyuo vikuu. Na hapa nazungumzia ada za shule za binafsi sio zile za serikali  kwani tunajua unafuu wake. Matumizi mengine matibabu hospitalini, pesa ya walinzi kwa kila mwezi, sherehe za kuaga na kukaribisha mwaka mpya.
Zaka ya Kanisani na Misikitini, kupanda Mbegu/ Sadaka, Shukurani ya neno, ahadi na makusanyo, shukrani ya chakula cha Bwana kanisani, marekebisho ya Kitasa cha mlango kabla mwenye nyumba hajashtuka, gharama za marejesho ya mkopo wa Saccos kazini.
Tozo za Flying (wazoa takataka wa mikokoteni ambao huzitupa hapo hapo), Madalali wa nyumba, viwanja, pango la nyumba, fremu ya biashara na ofisi.
Mitandao ya simu (airtime vouchers), mafuta ya gari, walindaji na waoshaji magari. Daima kauli zao “oyaah sista/blaza, mdogo wako nipo apaaa.”
Tozo za kuegesha magari, makato ya mikopo, tozo za internet cafe ili uweze ku-surf. Rambirambi ya mfiwa mtaani kwetu, harusi ya ndugu yako wa ukoo na zawadi.
Bado sijamaliza kutaja, kuna Sendoff ya mtoto wa mdogo wake rafiki yako na zawadi, kumuaga mfanyakazi mwenzetu na zawadi, michango ya komunio ya 1 & 2 na kipaimara.
Michango ya birthday party na zawadi; Ndugu wa kule kijijini, mshahara wa hausigeli na hausiboi; matumizi ya Bodaboda, teksi na bajaji. Duka la dawa kwa mchaga, tuisheni ya mtoto, kuchangia wahanga wa mabomu na mafuriko. Mengine ni kwenda kumuona mtoto aliyezaliwa, kununua CD/DVD ya uzinduzi wa Kwaya yetu.
Chakula cha mbwa, mchango wa ujenzi wa kupanua Kanisa, kuchangia Uinjilisti Masasi, outing ya kitimoto, ujenzi wa Nyumba Mabwepande, Kuendeleza shamba Mkuranga (linalotaka kutaifishwa kwa kutoendelezwa). Na matumizi mengine kwa wale wenzetu wanaokwenda umbali wa Viti Virefu, moja moto, moja baridi. Maji ya Trafiki, Chai ya Nesi na Daktari, Kahawa ya Hakimu, Karani na PP.
Matumizi ya Vishoka waunganisha maji na umeme; Kidogo dogo cha mjumbe na mtendaji wa mtaa, makaribisho ya get together na dinner kwa rafiki wa kikazi ambaye hamjuani ila kweye simu tu.
Mchango wa matibabu ya mtoto nyumba ndogo kule Ngusero, mchango kidogo kwa rafiki aliyevamiwa na vibaka na kuumizwa vibaya. Gharama za malipo ya Mkulima Bar Moshi, manunuzi ya maji ya Kilimanjaro uwanjani Sheikh Amri Abeid, Ukiangalia mechi ya Yanga na JKT Oljoro, malipo kwa ajili ya Uji wa Shangazi, baada ya kazi Njiro jioni ya Alhamisi. Vipi manunuzi ya kandambili kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Hivi hali inakuwaje?
Mia mbili ya watoto wa mtaani au ombaomba, kitu kidogo cha wale wanaolazimisha kuosha kioo cha gari kwenye foleni barabarani. Umeme uliopanda bei, gesi iliyopanda bei, maji yaliyoadimika, bado contingency maana huu usafiri unaotembelea ball joint, bush, feni belt havijafa, hapo bado hujafanya service. Bado msosi wa mchana kazini hasa kama maofisi yetu akina Mama Ntilie na vyakula vyao vinapokaribiana bei za restaurants, bado mchango wa kitchen party na sare, kuna hii baby shower.
Na hapo bado hujatoa watoto outing jumapili, Upo wapi uwezekano wa kununua laptop mpya ambayo ni muhimu katika mfumo wa maisha ya kisasa. Desktop nyingine kwa ajili ya watoto nyumbani, rim mpya za gari ambazo zimeingia kwaajili ya ku-modernize gari lako kuu kuu. Vipi kuhusu gharama za kujipendekeza kwa kimwana wa kazini kwako ambaye amekubali kwenda nawe out leo.
Gharama za matibabu katika hospitali binafsi kwa kuwa madaktari wa serikali wapo katika mgomo. Dogo naye “Bro ninunulie basi japo kasimu ka promosheni, ile yangu imedondoka chooni” Mara “Bro/Sister Next week on Saturday shuleni tuna-visit snake Park na sina shilingi 3000 za mahudhurio”.
Mke naye nyumbani anaongeza yake, “Daddy leo Mwakasege yupo relini, vipi tutapitia? Hapo unatakiwa kujua kichwani mwako kuwa gharama ya taxi baada ya semina.
Vipi tozo za Toyo kwa kuwa nimeachwa na gari la ofisi (Staff Bus). Mwingine kama kawaida anakusubiri uwajibike kwa gharama zako hana muda wa kudhani unahitaji msaada. Mama yangu!
Ukigeuka huku na huko unajikuta nafuu yenyewe ni pale mwajiri anapokuongezea mshahara kwa 7% tu wakati inflation ni juu ya 19%. Ukifikiri kwa makini, unajiuliza Watanzania wanaishi vipi kwa mtindo huu?
Ndipo unapoimba "Mwokozi nitoe roho niepuke, hili balaaa." Napenda msomaji utafakari mwenendo wako wa matumizi kulingana na hali hali ya uchumi wan chi na jamii yetu.
Kama ukiyumba kwenye suala la kuweka akiba, basi maisha yako yatakuwa yanakabiliwa na ukosefu wa msingi wa muongozo au utakuwa unatumia gharama kubwa kwa mambo yasiyoweza kusaidia familia yako.

RAIS FRANCOIS BOZIZE ALIKUWA AKISUBIRI VITA ATIMIZE MAJUKUMU?


Na. Markus Mpangala, Lundu
Moja ya mambo yanayonikinaisha ni suala la mgogoro wa nchi ya Afrika ya Kati.
Serikali ya Bangui inaonekana lilala usingizi wa pono kiasi ambacho sasa baada ya mapigano ya muda mrefu na waasi wameamua kuitisha majadiliano huku serikali ya rais Bozize ‘ikiwatongoza’ waasi hao kwa mambo ambayo yaliapaswa kuwa kwenye ilani ya uchaguzi. 
Serikali ya mjini Bangui chini ya rais Francois Bozize inasema kuwa, kwa sasa imejipanga kwa dhati kutimiza majukumu yake kwa wananchi.
Serikali hiyo inasema katika majadiliano yake na waasi wan chi hiyo yatakayofanyika nchini Gabon, imekusudia kuwasilisha mipango thabiti ya maendeleo ya kiuchumi, mapenndekezo imara ya mabadiliko ya ndani ya jeshi la nchi hiyo na kadhalika.
Ikumbukwe Rais Bozize hivi karibuni alimtumua madarakani waziri wa ulinzi ambaye ni mtoto wake. Kwa upande wa waasi wan chi hiyo wanasema kuwa wanataka rais Bozize aondoke madarakani ili kurejesha amani ya nchi hiyo. Mazungumzo baina ya serikali na waasi yanafanyika baada ya miaka takribani miaka 12 ya kukosekana kwa amani, huku utawala wa Bangui ukiendelea kulemaa na kushindwa kutimiza makubaliano ya awali ya mwaka 2001.
Katika mazungumzo ya sasa, Jumuiya ya Nchi za Afrika ya Kati(CEEAC) imeratibu majadiliano baina ya Rais Bozize na waasi hao yatakayofanyika mjini Libraville nchini Gabon yakiwa na lengo la kumaliza mapigano ya pande hizo mbili.
Moja ya masharti yaliyowasilishwa na waasi ni kwamba lazima rais Bozize aondoke madarakani kwasababu ameshindwa kupata ufumbuzi na kutimiza makubaliano yaliyowahi kufikiwa huko nyuma.
Aidha, mwaka 2007 kulifanyika mazungumzo ya kusaka amani lakini hakukuwa na mwendelezo wowote uliofanyika chini ya rais Bozize. Ni jambo la aibu sana leo hii, Rais Bozize kuamua kuwasilisha mezani ajenda za kupata ufumbuzi ili kumaliza machafuko nchini mwake. Leo hii Rais Bozize anawasilisha mipango ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Afrika ya Kati, huku akihimiza mabaidliko ya kijeshi ndani ya jeshi la nchi hiyo.
Kimsingi Rais Bozize anaonekana kukosa dira ya kuongoza taifa hilo lililopo katikati ya bara la afrika. Sababu mapigano yake dhidi ya waasi yanafahamika kwa kipindi cha miaka kumi sasa, na ajenda zinazoelezwa na waasi ni hali mbaya ya wananchi, kukosekana wka matumaini ya kiuchumi na kadhalika. Lakini kwa upande wa Rais Bozize haonekani kuona kwamba yeye anaweza kuwa kikwazo cha kufikiwa makubaliano hayo.
Waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Kama ambavyo waasi wamesema, wanataka kuona Rais Bozize akiondoka madarakani ili kupata ufumbuzi, vivyo hivyo wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanavyopendekeza.
Hata hivyo kwa mtindo wa kutaka kukwepa majukumu, ni dhahiri rais Bozize anaweza kuwatupia lawama wasaidizi wake ili kuonekana hana hatia. Ni sababu hii ndio maana alimfukuza kazi mwanaye ambaye alikuwa waziri wa ulinzi na usalama wan chi hiyo.
Kumfukuza kazi waziri huyo hakukuweza kuwashawishi waasi wa nchi hiyo ili waone rais huyo anakusudia kuleta mabadiliko, bali waasi wanaona ni njia ya kujisafisha kwa sasa kutokana na kuachia machafuko kufikia kipindi kibaya sana.
Jambo jingine ni mabadiliko ya taratibu za uchaguzi wan chi hiyo. Ikumbukwe, waasi hawalalamikii taratibu za uchaguzi uliomuingiza madarakani rais Bozize bali wanalalamikia hali mbaya inayotokana na utawala wake. Kwa maana hiyo kutaka kufanya mabadiliko katika taratibu za uchaguzi anakusudia kuwaleta waasi hao katika ulingo wa siasa badala ya kuangalia njia za kukomesha mapigano ambayo yamesababisha watu kadhaa kufariki dunia na wengine kukosa makazi.
 Katika hali kama hiyo kwa vyovyote uchumi wa nchi lazima uzoroteshwe, kwani watu badala ya kutumia nguvu zao katika uzalishaji hivyo hutumia nguvu hizo matika kuyakimbia makazi yao au kuelekea uhamishoni. Sio kitu rais ambacho rais Bozize anaweza kuishawishi Afrika, lakini jambo la msingi ni kukubali kuwajibishwa kulingana na hali halisi inayoendelea nchini humo.
Wananchi wanapolalamikia hali mbaya ya kiuchumi huku rais wao akitumia muda mwingi na nguvu za kutosha kutaka kuwashawishi waasi waache mapigano, ni wazi ameshindwa kubaini kwua hata yeye ni sehemu ya tatizo la machafuko hayo.
Endapo yeye asingekuliwa sehemu ya tatizo basi tusingeona leo kuna machafuko yanaendelea nchini humo na tungeona serikali ya Bangui ikisifika kwa wananchi wake kutokana na juhudi za kuboresha na kuimarisha uchumi wake. Nadhani ni wakati wa Rais Francois Bozize kung’atuka madarakani, hivyo ikibidi kuitisha uchaguzi mkuu ambayo utashirikisha vyama vyote vya siasa na wananchi wa ujumla.

January 07, 2013

MUNGU ALIANZA UJASIRIAMALI TANGU KITAMBO NA WANAOTAKA KUFANIKIWA 2013


Na Albert Nyaluke Sanga, Iringa
Tangu siku Mungu anamuumba Adam, alimuumba kijasiriamali na alimwagiza akawe mjasiriamali. Unashangaa? Soma Biblia yako kitabu cha Mwanzo. Twende polepole utaelewa tu. Unajua neno Ujasiriamali/biashara linamaanisha nini? Ngoja nikujulishe. Biashara/Ujasiriamali inamaanisha, ubunifu wa uzalishaji (production), uongezaji wa ulichobuni ama kuzalisha (multiplication), usambazaji (distribution) na kutawala soko (dominion over market and ideas/innovation). Umeelewa enhee? Sasa turudi kwa Adamu. 
Mungu alipowaumba Adamu & Eva aliwambia hivi, "Enendeni mkazaliane, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kutawala vitu vyote". Wengi wanaposoma Biblia huwa wanadhani kuzaana ni "kupata watoto pekee"; lakini ukisoma English Bible (KJV) ina-highlight vizuri neno hili kuzaana; "Fruitful". Kuwa "Fruitful" inamaana "kutumia materials/rasilimali/akili ulizonazo ili kupata ama kutengeneza kitu chenye thamani zaidi", kwa lugha nyepesi ni 'uzalishaji (production). Tunaenda pamoja? 
Hebu turudi kwenye yale maagizo ya kijasiriamali ambayo Mungu aliwapa akina Adam na mkewe, "Enendeni mkawe wazalishaji (fruitful/production), mnachozalisha kikaongezeke (multiplication), mnachokiongeza mhakikishe kinajaa dunia yote (distribution), hivyo mnavyovijaza dunia yote hakikisheni mnaweza kuvitawala (dominion over market and ideas)" 
Haaa! haaa! Nimekupoteza? Usijali! Rudia kusoma pole pole, afu ujitahidi kuwa unasoma Biblia kwa tafakari; utaelewa! Sasa yoooote haya namaanisha nini? Ni hivi: Mungu alimuumba kila mwanadamu kufikiria na kuishi kijasiriamali. Si lazima kufanya ujasiriamali wa kupata fedha, lakini mtazamo wa kiujasiriamali utakupa ushindi wa maisha ya Kimungu wakati wote. ~SmartMind~

KWA WALE TU! WANAOTAKA KUFANIKIWA 2013!
Nimekuwa nikieleza mara nyingi kuwa; mafanikio katika maisha hayaji kwa lelemama! Iwe unataka uchumi mzuri, ajira nzuri, mke ama mume mzuri; ni lazima jasho likutoke. Hata hivyo sote tunatambua kuwa mafanikio yanaanza katika ufahamu wako. Namna unavyowaza inaamua namna unavyotenda, namna unavyotenda inadhihirika katika maisha uliyonayo hata sasa. Huwezi kudanganya! Tukiyatazama maisha yako, "automatically" tunajua mfumo wa mawazo na fikra zako. 
JE WAJUA? Kuwa mfumo wa mawazo yako ni matokeo ya mambo unayoyaingiza katika ubongo wako kupitia kusikia, kutazama na kusoma? Kama umenasa kwenye uhaba wa kifedha basi utambue kuwa ubongo wako umejaza "matango mwitu" kuhusu fedha, kama mapenzi yanakutesa, uwe na uhakika kuwa fikra zako zimejaa "upupu" kuhusu unavyotakiwa kubehave kwenye mapenzi. 
Soko kuu la Songea mjini
Kama upo kwenye ajira "isiyolipa" ama hujapata "japo pa kujishikiza"; basi ujue mtazamo wako kuhusu ajira na maisha "umejaa matope"!
UNAJIKWAMUAJE KUTOKA HAPO? Jibu ni rahisi! BADILISHA MTAZAMO NA NAMNA UNAVYOFIKIRI! Utabadilishaje? Jifunze kutoka kwa waliofanikiwa kufika unapotaka kwenda, Soma vitabu vinavyojenga fikra na mitazamo chanya, ama fanya yote mawili. Mimi ngoja nikusaidie moja: NITAKUPA VITABU VYA AINA HIYO! Kwa mwaka mzima nitakuwa nikituma vitabu viwili (2) kila mwezi kupitia baruabebe(email) vilivyopo katika mfumo wa pdf; kwenda kwa marafiki wote waliopanga kufanikiwa 2013. Kwa kuanza na mwezi huu Januari nitatuma vitabu vifuatavyo: 1) THE SCIENCE OF GETTING RICHER 2) COACH YOURSELF TO MAXIMUM EMOTIONAL INTELLIGENCE. Kwa rafiki unayehitaji ninapenda unijulishe email yako hapa (ama inbox) kisha utapokea vitabu hivi. KAMA UNATAKA KUFANIKIWA, KUJIFUNZA HAKUKWEPEKI. ~SmartMind~

KWA WATANZANIA KUZALIANA NI LAANA ........?


Na Salvatory Mkami, Dar es salaam
Mheshimiwa rais Kikwete mkatika hotuba yake mheshimiwa alieleza kuwa matokeo hayo ni ishara kwamba ifikapo mwaka 2016 kuna uwezekano wa idadi hiyo kufikia milioni 51 jambo ambalo linaweza kuwa ni mzigo kwa taifa, jamii na hata katika masuala ya uchumi.
Mheshimiwa Rais alizidi kufafanua kuwa jamii inapaswa kuyachukulia kwa uzito matokeo hayo hasa katika masuala ya kupanga uzazi pamoja na kuongeza bidii ya kufanya kazi.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, inaonesha kuwa kwa wastani, kila sekunde moja wanazaliwa watoto watano hapa duniani, na wakati huo huo watu wawili wanafariki dunia, achilia mbali zile mimba zinazoharibika.
Maana ya tofauti hiyo kati ya vizazi na vifo ni kwamba watu watatu wanaongezeka duniani kila sekunde moja. Ukizidisha idadi hiyo utagundua kwamba kuna ongezeko la watu 11,000 kwa saa na watu 265,000 kwa siku na hii inafanya dunia kuwa ongezeko la watu milioni 100 kwa mwaka.
Hivi sasa dunia ina watu wapatao bilioni 7. Mwaka 1750 kulikuwa na watu milioni 800 tu duniani. Kufikia mwaka 1850 idadi iliongeka na kufikia watu bilioni 1.8.

Mwaka 1950 idadi ya watu ikawa bilioni 2.5. Ilichukuwa miaka 50 idadi ya watu kufikia bilioni 6 yaani mwaka 2000. Ilikisiwa kwamba mpaka kufikia mwaka 2010 idadi ya watu hapa duniani itafikia watu bilioni 7, ikiwa ni ongezeko la watu bilioni 1 kwa muda wa miaka 10.
Lakini pia Ukiangalia mtiririko wa takwimu hizo utagundua kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa kasi hapa duniani kuanzia karne ya 19. Kwa mfano nchi yetu ya Tanzania iko chini ya kiwango cha ongezeko la watu hapa duniani ukilinganisha na nchi nyingine zilizoko dunia ya tatu. Tanzania ina ukubwa wa eneo la mita za mraba zipatazo 342,100, karibu sawa na Misri ambayo ina ukubwa wa mita za mraba zinazofikia 384,300.
Pamoja na kwamba tofauti ya ukubwa kati ya nchi hizi mbili ni ndogo sana lakini Tanzania imezidiwa kwa idadi ya watu karibu mara mbili na Misri. Kwani wakati Tanzania ikiwa na idadi ya watu wapatao milioni 44, Misri ina idadi ya watu wapatao milioni 83 kwa mujibu wa sensa iliyofanyika Julai 2012.
Ikiwa utaiunganisha Tanzania na nchi ya Benin iliyoko Afrika Magharibi ukubwa wake utalingana na nchi ya Misri, kukiwa na tofauti ndogo sana. Ukijumlisha idadi ya watu wa nchi ya Benin wanaokadiriwa kufikia watu milioni 9 (kwa mujibu wa sensa iliyofanyika Julai 2012) na idadi ya watu wa Tanzania unapata idadi ya watu wapatao milioni 53, ikiwa bado ni chini ya idadi ya watu wa nchi ya Misri.
Hii inaonesha bado nchi hii ina kiwango kidogo sana cha idadi ya watu ukilinganisha na nchi nyingine zilizo katika dunia ya tatu. Kwa hiyo sioni sababu ya serikali yetu kupiga kelele sana kuzuia watu wasizaane.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, imekadiriwa kwamba watoto milioni 1.6 huzaliwa kila mwaka hapa nchini. Na kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na wizara ya afya zinaonesha kwamba watoto wanaosajiliwa ni 140,000 kila mwaka ikiwa ni asilimia 10 tu ya watoto wanaozaliwa, hii inaonesha kwamba kuna idadi kubwa ya watoto wanaofia tumboni, na wale wanaofariki baada ya kuzaliwa inakuwa haijachukuliwa na kuingizwa kwenye takwimu za serikali.
Hata hivyo inakadiriwa kwamba watoto wapatao 51,000 hufariki baada ya kuzaliwa hapa nchini, na wakati huo huo 43,000 hufia tumboni kila mwaka.
Kwa mujibu wa takwimu hizo inaonesha kwamba bado tunayo safari ndefu ya kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa hapa nchini, kabla hatujaanza kupiga kelele ya watu kuzaa kwa mpango.
Hata hivyo chapisho hilo linabainisha kwamba mataifa makubwa yameanza kuonesha wasiwasi juu ya ongezeko la watu hapa duniani. Mataifa hayo yanadai kuwa ongezeko la watu linasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, na hivyo kutishia dunia isiwe salama.
Kwani kumekuwa hakuna udhibiti wa kutosha kiasi kwamba watu wamekuwa wakitawanyika kwa ajili ya kutafuta makazi na hivyo kuvamia maeneo ya misitu ya asili na vyanzo vya maji na kufanya uharibifu mkubwa mkubwa wa mazingira.
Imebainika kwamba iwapo watu hao watasogezewa miundo mbinu kama vile Barabara, shule, hospitali, na huduma mbali mbali za kijamii katika maeneo hayo ya hifadhi waliyoyavamia, itakuwa na maana ya kuhalalisha uharibifu wa mazingira.
Pia wataalamu hao wanadai kwamba ongezeko la watu haliendi sambamba na ujenzi wa miundo mbinu ambayo itasaidia kulinda uharibifu wa mazingira.
Labda niwaulize ndugu wasomaji, hivi nchi masikini na zile nchi tajiri zenye viwanda ni zipi hasa zinazoifanya dunia hii isiwe salama?
Wao wana viwanda wanazalisha sumu kila uchao huku wakitulisha vyakula na madawa yenye sumu ili kujikusanyia utajiri, halafu leo wanasema kuwa nchi masikini ndizo zinazochangia uharibifu wa mazingira na kuifanya dunia isiwe salama, huu ni uonevu wa hali ya juu.
HEBU TUANGALIE UPANDE MWINGINE WA SHILINGI WA KADHIA HII:
Kuzungumzia ongezeko la watu, unazungumzia ongezeko la soko, kwa maana ukuaji wa biashara, nguvu kazi, na ongezeko la viwanda, na hivyo ukuaji wa uchumi kuongezeka.
Kwani kwa jinsi idadi ya watu inavyozidi kuongezeka na ndivyo uchumi unavyozidi kukua, hebu angalia nchi kama ya China, India, Marekani na iliyokuwa Urusi kabla haijasambaratika, ukuaji wa uchumi katika nchi hizo ulitokana na kuwa na idadi kubwa ya watu.
Ila naomba nitahadharishe kidogo hapa, ninapozungumzia ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi nazungumzia nchi kutumia nguvu kazi katika kuzalisha na kuwa na serikali makini inayowawezesha wananchi wake kufikia malengo yao.