January 21, 2013

SETH DE JESUS GIOVANNI NA HUDUMA MPYA YA USHAURI WA KIMAPENZI


STRAIGHT TO YOUR PHONE ndio Service nimeizindua rasmi leo.Do you believe kuna True Love dunia ya leo???Je,unaamini you can fall inlove again baada ya kuumizwa sana???Unataka kujua jinsi ya kum-handle Mwanaume/Mwanamke unayempenda??Unataka kujua jinsi ya ku-deal na Mpenzi wako mkorofi na asiyekujali??
Yote haya utayapata Ukijiunga na Huduma hii ya SETH...Tutajadili kama tunavyojadili kwenye Wall hii lakini this time popote ulipo,huna haja ya ku-Log in Facebook kujua. Ukiwa mteja wa Mtandao wowote ule,iwe TIGO,AIRTEL,VODACOM au ZANTEL ukituma neno SETH kwenda 15678 utakuwa umejiunga na Huduma hii BURE!Hukatwi chochote kwa kutuma SMS hiyo!
Kuanzia sasa nitakuwa natuma Status ya Siku kwenye Simu yako ya Mkononi na utapokea ujumbe huo kama SMS...Najaribu kuyafanyia kazi Maoni yenu,kila mmoja kwa kadri Mungu anavyonijalia...
...SMS utaipata popote ulipo kwenye Simu yako na kama una tatizo au swali lolote,NITAKUJIBU!
SETH kwenda 15678,Please Support me on this one,NAWAPENDA! 

MRADI WA MAJI SAFI NA SALAMA KIGONSERA-MBINGA

Na Mwandishi Wetu, Kigonsera

Kigonsera ni miongoni mwa miji muhimu sana wilaya ya Mbinga. lkaini kwa kipindi kirefu baadhi ya wakazi wa mji huo walikuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji safi na salama. kwa sasa mradi mkubwa wa kusambaza maji safi na salama katika wilaya ya Mbinga umeshika kasi huku mji wa Kigonsera ukiwa miongoni mwa miji muhimu sana kiuchumi na biashara.
 Ni mji ambao upo pembezoni mwa barabara kuu iendayo Songea mjini kutokea Mbinga. Kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi, watu wengi hutumia mji huu kufanya biashara na zingine za ujenzi wa taifa, hivyo wanahitaji huduma muhimu sana ili kusogeza mbele maendeleo ya mji wao na taifa kwa ujumla.
       
Pichani msimami wa Mradi ndugu Egbart Jeremy akiwa katika intake ya maji safi na salama mjini Kigonsera, ikiwa ni moja ya miji ambayo inatakiwa kufanyiwa marekebisho ya kuleta uhuduma ya maji kwa wakazi wake.


     
Wahandisi wa maji wa wizara ya maji, mkoa wa Ruvuma na wilaya ya Mbinga wakikagua ujenzi wa tanki la maji lenye uwezo wa kubeba ujazo wa mita za ujazo mia mbili(200) katika mji wa Kigonsera. Tanki hilo lipo katika ujenzi na kampuni ya ujenzi ya Mwalongo Cont ya mkoani Njombe.

UHARIBIFU WA MAZINGIRA MDUNDUALO-MBINGA


Egbart Jeremy
Na Egbart Jeremy, Mbinga

Utunzaji wa mazingira umekuwa jambo muhimu sana. Kwa muda mrefu ripoti mbalimbali zimekuwa zikielezea juu ya umuhimu wa kutunza mazingira. Kuna wataalamu wa mazingira wamekuwa wakishughulikia ukaguzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali kwenye wilaya ya Mbinga. Miongoni mwao ni hapa pichani wataalamu wa mazingira wakikagua uharibu wa mazingira uliojitokeza kwenye maeneo mbalimbali.
Mathalani ni kijiji cha Mtundualo, kilichopo kwenye wilaya ya Mbinga ambako kunaendeshwa uchimbaji wa makaa ya mawe (TANCOAL). mtundualo ni miongi mwa maeneo yanayokaguliwa mara kwa mara kutokana na hali iliyowahi kujitokeza pia katika kijiji cha Ndumbi, kilichopo wilaya ya Nyasa.

Mtaalamu wa mazingira kutoka ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa wilaya, Egbart Jeremy akijadiliana jambo na ofisa usalama na mazingira kutoka mgodi wa makaa ya mawe(TANCOAL) kuhusu uchafuzi uliofanywa na 




Timu ya wataalamu wa mazingira wakikagua uharibu wa mazingira kijiji cha Mdundualo
                            
Mtaalamu Egbart Jeremy akikagua maji yanayodaiwa kuathiriwa na uchafuzi wa mazingira kutokana na uchimbaji wa makaa ya mawe(TANCOAL)

NINI SABABU YA UMASIKINI AU UTAJIRI WA NCHI?



Na Dkt. Hamisi Kigwangalla
Mnamo mwaka 1945 wakati vita kuu ya pili ya dunia ilipokuwa inaelekea kuisha, Korea ambayo ilikuwa iko chini ya utawala wa kikoloni wa Japan toka mwaka 1910 ilipata uhuru wake. Kabla ya hapo majeshi ya ukombozi ya Korea (Korean liberation army) yalikuwa na mpango wa kupigana na japan ili kudai uhuru wao. Kama bahati haikufikia kwenye kudai uhuru kwa vita lakini anguko la Japan kwenye vita kuu ya pili ya dunia ilifanya Korea ipewe uhuru wake bila mtutu wa bunduki. 
Ndani ya mwezi mmoja tu baada ya Japan kunyoosha mikono juu, Korea ilijikuta ikigawanywa mara mbili kwenye mstari unaojulikana kama ‘the 38th parallel north’ (nyuzi 38 kaskazini na sambamba na ikweta) na kuwa mamlaka mbili tofauti zenye ushawishi tofauti. Kusini ikiwa chini ya usimamizi wa Marekani na Kaskazini chini ya Urusi.
Amani ya kipindi cha vita baridi kati ya mamlaka hizi mbili iliisha katikati ya mwaka 1950 pale Korea ya Kaskazini ilipoamua kuivamia Korea ya Kusini na kufikia hadi kuuteka mji mkuu wa Korea ya Kusini, Seoul.
Leo hii nchi hizi zimekuwa dunia mbili tofauti kabisa. Korea ya Kaskazini ikiwa na mfumo tofauti kabisa wa kiuchumi na ile ya kusini. Pengine sababu pekee inayozitofautisha hizi Korea mbili, ambazo zamani zilikuwa moja na sawia kabisa katika kila Nyanja. Leo hii Korea ya Kaskazini hakuna ruhusa kuwa na simu ya mkononi inayotoa mawasiliano nje ya mipaka ya nchi, kuna watu wanaishi chini ya dola moja, kuna ugumu wa namna ya kusafiri kutoka sehemu moja mpaka nyingine, wakati ndugu zao wa Korea ya Kusini wanaishi maisha ya utajiri, ya uhuru wa kuwasiliana kwa simu za kiganjani, kwa mitandao na uhuru hata wa kusafiri na kufanya biashara na yeyote yule wa popote pale duniani – tunu ambazo zimewafanya leo hii wawe kwenye nchi ambazo zinahesabika kama ni za dunia ya kwanza.

Wakati Korea ya Kaskazini ikiishi kwa kutegemea misaada ya chakula na fedha kutoka nchi nyingine, Korea ya Kusini imejenga uchumi imara unaotokana na matumizi ya teknolojia na sayansi ya zama za sasa na imekuwa ni mfadhili wa nchi zinazoendelea kama Tanzania na hata Korea ya Kaskazini.

Ukiangalia kwa undani sana utabaini kuwa kinachotofautisha nchi hizi, zenye historia ya kufanana, zenye jiografia ya kunana, zenye watu wenye kuongea lugha moja, zenye dini, utamaduni na mila na desturi za kufanana, mienendo ya kufanana, kila kitu kinafanana, leo hii kinachowatofautisha si kingine zaidi ya ule mpaka uliowekwa kati yao (the 38th parallel north). Ni nini haswa kinachowafanya wa Kusini wawe matajiri na wa Kaskazini wawe maskini? Maisha ya watu wa Korea ya Kaskazini na yale ya watanzania hayana tofauti sana leo hii wakati yale ya ndugu zao wa Korea ya Kusini yanafanana kabisa na ya wazungu wa Ureno ama wa Hispania. Miaka ya kuishi ya mtu wa Korea ya Kaskazini ni kumi nyuma ya ile ya ndugu zao wa Korea ya Kusini, upande wa pili tu wa ule mstari.

Hizi tofauti zinazoonekana leo siyo za kihistoria. Na kwa hakika hazikuwepo kabla ya ile vita kuu ya pili ya dunia. Kilichotokea baada ya mwaka 1945 ni kwamba hizi serikali mbili, ya Kusini na ile ya Kaskazini zilifuata mifumo miwili tofauti ya kiuchumi, moja ilijenga mfumo wake kufuatia mfano wa kiliberali wa soko huria lililoruhusu uhuru wa masoko na mitaji kama ule unaofuatwa na nchi za magharibi na marekani, na nyingine, Korea ya Kaskazini, ilifuata mfumo wa kikomunisti.

Japokuwa marais wa kwanza wa Korea ya Kusini hawakuweka mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia, wengine wanasema kwa kuhofia kuvamiwa na mfumo wa kitawala wa kikomunisti uliokuwa unasambaa kwa kasi sana maeneo ya Asia wakati huo, walisimamia mfumo wa soko huria. Marais hao, Syngman Rhee, ambaye alisomea vyuo mashuhuri duniani vya Harvard na Princeton, na mwenzake Jenerali Park Chung-Hee, ambaye ni baba mzazi wa Rais wa kwanza wa kike wa nchi hiyo aliyeshinda uchaguzi mkuu juzi tu hapa, wameingia kwenye historia za marais waliotumia nguvu kuongoza nchi yao na ikafanikiwa.
Rais wa pili wa Korea ya Kusini atakumbukwa daima na watu wa Korea ya Kusini kwa kusukuma ruzuku na mikopo kwenye makampuni yaliyoonesha mwelekeo wa kufanikiwa. Kwa upande wa Korea ya Kaskazini, Kim Il-Sung, ambaye alikuwa kiongozi aliyeendesha harakati za kikomunisti za kupinga utawala wa kijapan alitawazwa kuwa Rais wa Korea ya Kaskazini mwaka 1947, na moja kwa moja aliwekeza nguvu zake katika kujenga mfumo wa kiuchumi ambao uliweka chini ya serikali kuu mamlaka yote ya kuandaa mipango ya kukuza na kuendesha uchumi wa nchi chini ya mfumo wa kikomunisti wa ‘Juche’. Rais Kim Il-Sung alizuia mfumo wa soko huria na hakukuwa na ruhusa ya kumiliki mali binafsi.

Hakuna jiografia, wala utamaduni, wala historia ya nchi inayoweza kuelezea tofauti ya kiuchumi kati ya nchi hizi mbili, ambazo si zaidi ya miaka 60 iliyopita zilikuwa nchi moja. Tukichukulia haya ‘maajabu ya Korea ya Kusini’ (the south Korean miracle) kama somo, tunapaswa tujifunze kitu, kwanza tuangalie ni nini chanzo cha kuendelea kwa Korea hii moja na kushidwa kwa nyingine? Majibu yake yanapatikana, kwa vyovyote vile kwenye mfumo wa kisiasa na kiuchumi uliofuatwa baada ya uhuru wa Korea kutoka chini ya utawala wa kikoloni wa Japan. 
Moja ilifuata mfumo wa soko huria na nyingine mfumo wa kikomunisti, je tofauti hizi za kimfumo zinaweza kutumika pia kuelezea utofauti wa kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya? Na je sababu hizi zinaweza kutumika kuelezea spidi ya ukuaji wa Uchumi wa nchi ya Rwanda? Sina jibu sahihi la maswali haya. Watanzania tuendelee kujipanga, pengine tusijidai sana na nafasi yetu kijiografia, kihistoria na hata kiutamaduni, maana jibu la umaskini wetu halipo huko, lipo kwenye mfumo wa kisiasa na kiuchumi tunaoufuata.
Mafanikio baina ya nchi kiuchumi yanatofautiana kwa sababu za tofauti ya aina za taasisi walizoweka kwenye nchi husika, sheria, kanuni na taratibu zinazoathiri uchumi walizotunga na namna ya motisha walizoweka kwa ajili ya watu wao. Angalia tofauti ya mtoto wa Korea ya Kaskazini na yule wa Korea ya Kusini, mmoja anakua huku akipata elimu ya uhakika na itakayomwezesha kushindana, anapata motisha ya kushindana kuingia kwenye ujasiriamali na anakuta kuna mazingira ya kumwezesha kufikia ndoto yake wakati mwingine hapati elimu stahiki na hana fursa ya kuanzisha, kumiliki mali na kuendesha biashara; ni yupi kati yao atakuwa na motisha ya kufanya ubunifu na kutafuta pesa?

Dkt. Hamisi Kigwangalla ni Mbunge wa Jimbo la Nzega, Mkoani Tabora. Amesoma shahada ya kwanza ya udaktari wa tiba, na ana shahada mbili za uzamili, moja kwenye afya ya jamii na nyingine kwenye uongozi. Na sasa anaandika tasnifu ya shahada yake ya uzamivu (Ph.D.) kwenye usawa, haki na uchumi, pia anamalizia kuandika kitabu chake kwenye sera za maendeleo.

WAPIGAKURA HABA, WALALAMIKAJI WAMEJAA POMONI


Na Markus Mpangala, Dar es salaam

Markus Mpangala
Wenyeji wa Latini Amerika ndio wavumbuzi wa neno “Suffragium”, ambalo walilitumia kuanzia karne ya 14. Maana ya neno hilo ni “haki ya kuchagua” au “Haki ya kuunga mkono”.

Ni ile hali ya mwananchi kuchagua viongozi, au masuala muhimu kitaifa. Tangu kuvumbuliwa kwa neno hilo ndipo dunia ilishuhudia taasisi za kisiasa zenye kujikita katika haki ya kuchagua au kuunga mkono wagombea mbalimbali katika chaguzi.

Kimsingi mkondo mkubwa wa siasa hizo ulijikita zaidi barani ulaya hususani jamii ya Warumi na Wagiriki hasa katika karne ya 17 na 18. Katika kipindi hicho wanafalsafa mbalimbali walikubali kuwa huo ulikuwa mtindo wa serikali binafsi ambapo mwananchi alikuwa na mamlaka ya kuwachagua viongozi anaowataka. 
Rais Nyerere
Wanafalsafa waliamini kuwa uchaguzi wowote unaofanywa na mwananchi (mpigakura) una lengo la kuunda serikali yake kwa mtazamo wake (Self government). Licha ya mabaidliko ya Kiliberali kuleta mfumo wa uchaguzi wa viongozi kupitia vyama vya siasa, bado muundo wa “self government’ umesalia katika serikali za kisasa duniani kote kupitia chaguzi zinazofanyikwa mara kwa mara kulingana na utaratibu wa nchi husika.
Mathalani Tanzania inafanya uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano, Malawi kila  baada ya miaka minne sawa na Marekani. uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Kongresi, Seneti, Madiwani na kadhalika wote hupitia kapu la mwananchi ambaye analazimika kuwapigia kura ili kuhalalisha mamlaka yao.

Kwahiyo, mamlaka ya mwananchi ya kupiga kura ni makubwa na ndiyo anayeamua kuwa mgombea fulani amepata kura nyingi kuliko mwenzake au wenzake(kama wanakuwa wengi). Baadhi ya nchi hurudia uchaguzi kama hakuna mgombea anayefikisha wastani wa kura zilizopangwa.
Liberia walirudia uchaguzi baada ya aliyeongoza Bi. Hellen Sirleaf kutofikisha asilimia 50, lakini duru la pili alifanikiwa kumshinda mshindani wake George Weah. Senegal pia Mack Sall alishinda uchaguzi baada ya Abdoulaye Wade kukiri kushindwa.
Kwa baadhi ya wanasiasa wapigakura ni nyenzo tu, lakini kimsingi wapigakura ni muhimu sana katika mfumo wa kidemokrasia. Hii inatokana na jinsi ushiriki wao unavyoweza kumfanya mgombea fulani kujivunia kura anazopata.

Hapa nchini Katiba yetu haizuii mgombea asiyefikisha asilimia 50 kuchukua madaraka. Kwa mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2000 haionyeshi kuwa mgombea urais wan chi yetu asipofikisha asilimia 50 basi anyimwe kutangazwa mshindi.

Bali Katiba yetu inampa nguvu yule aliyeongoza kupata kura nyingi bila kujali zimefika asilimia 50 au kidogo. Nadhani Katiba mpya inatakiwa kubainisha kwamba mshindi wa kiti cha urais anatakiwa kutangazwa tu akifikisha siyo chini ya asilimia 50.

Rais Mkapa
Tukisogea mbele kidogo tunaona kuwa katika uchaguzi wamwaka 2015 umekuwa gumzo mno kwa wananchi na mashabiki wa vyama vya siasa. Gumzo hili linatokana na hamasa mpya ambayo wananchi wameipata, na ndio maana ya haki ya kuchagua serikali waitakayo. 


Mwananchi amekuwa akiwapigia kura wagombea mbalimbali katika kiti cha urais, wabunge, madiwani na viongozi wa serikali za mitaa. Inaonekana kutoka utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tumekuwa na udhaifu mkubwa katika suala la upigaji kura.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1965, rekodi zinaonyesha kuwa waliojiandikisha kupigakura walikuwa watu 3,373,089. Katika uchaguzi huo waliopiga kura walikuwa watu 2,600,040 sawa na asilimia 77.1.

Mwalimu Nyerere alipata kura 2,410,903 sawa na asilimia 96.46, ambapo wapikura 88,600 sawa na asilimia 03.54 walimkataa, huku kura 100,537 zikiharaibika. Katika uchaguzi wa mwaka 1970, jumla wananchi waliojiandikisha kupiga kura ni 5,051,938.

Wapigakura waliompigia kura za ushindi Mwalimu Nyerere walikuwa 3,465,537 sawa na asilimia 72.2, huku kura 109,828 sawa na asilimia 03.07 zilimkataa, ambapo kura 74,388 ziliharibika.

Aidha, uchaguzi wa mwaka 1975 jumla watu waliojiandikisha kupigakura walikuwa 5,577,566, ambapo wapigakura 4,172,267 sawa na asilimia 93.25 walimpa ushindi Mwalimu Nyerere. Wapigakura 302,005 ambao sawa na asilimia 06.75 walimkataa Mwalimu Nyerere, huku kura 83,322 ziliharibika.

Katika uchaguzi wa mwaka 1980 jumla ya wananchi waliojiandikisha kupigakura walikuwa 6,696,803. Waliompigia kura Mwalimu Nyerere walikuwa 5,570, 883 sawa na asilimia 95.56, ambapo kura 295, 040 sawa na asilimia 04.44 zilimkataa, huku kura 157,019 ziliharibika.

Ukiangalia wastani wake utaona kuwa kuna kura zilikuwa zinaongezeka kwa kila uchaguzi. Mwaka 1965 waliomkataa Mwalimu Nyerere walikuwa  88,600, halafu kura 100,537 ziliharibika, kisha mwaka 1970 kura zilizomkataa zilikuwa 109,828 sawa na asilimia 03.07.

Kwa maana hiyo katika chaguzi hizo mbili Nyerere alishindwa kuwavutia wapigakura, kwani kutoka wapigakura 88,600 sawa na asilimia 03.54 waliomkataa  mwaka 1965 hadi wapigakura 109,828 ambao waliomkataa mwaka 1970 inaonyesha bado wananchi wetu hawakuwahi kuchukua uamuzi mgumu kupitia sanduku la kura.

Katika uchaguzi wa mwaka 1975 wapigakura waliomkataa Nyerere waliongezeka ambapo walikuwa 302, 005 sawa na asilimia 06.75. Lakini mwaka 1980 idadi ya waliomkataa Mwalimu Nyerere ilikuwa ndogo kuliko kwani wapigakura 259,040 walimkataa ingawaje alifanikiwa kushinda kwa wastani wa 95% ya uchaguzi huo.

Ali Hassan Mwinyi aligombea urais mwaka 1985 baada ya Mwalimu Nyerere kujiuzulu. Mwinyi alishinda kwa kura 4,778,114 sawa na asilimia 95.68 kati ya wapigakura 6,910,555 waliojiandikisha mwaka huo.

Kura zilizomkataa zilikuwa zilikuwa 215,626 sawa na asilimia 04.32, huku kura 188,259 ziliharibika. Uchaguzi wa mwaka 1990 wananchi waliojiandikisha walikuwa 7,296,553, lakini waliopiga kura walikuwa 5,198.120 sawa na asilimia 97.79%. Wapigakura 117,366 sawa na asilimia 02.21 walimkataa Ali Hassan Mwinyi.

Uchaguzi wa mwaka 1995 ulikuwa wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi. Mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa alishinda uchaguzi huo kwa jumla ya kura 4,026,422 sawa na asilimia 61.82 kati ya wapigakura 8,929,969 waliojiandikisha.

Wagombea wa vyama vya upinzani, Agustine Mrema (NCCR-Mageuzi) alipata kura 1,808,516 sawa na asilimia 27.77. Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) alipata kura 418,973 sawa na asilimia 6.43. John Cheyo alipata kura 258,734 sawa na asilimia 3.97. kura zilizoharibika katika uchaguzi huo zilikuwa 333,936.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2000 waliojiandikisha kupigakura walikuwa 10,088,484, ambapo kulikuwa na ongezeko la karibu milioni 1.2 ikilinganishwa na mwaka 1995. Benjamini Mkapa (CCM) alipata kura 5,863,201 sawa na asilimia 71.74. Profesa Lipumba (CUF) alipata kura  1,329,077 sawa na asilimia 16.26. Agustine Mrema alipata kura 637,115 sawa na asilimia 7.80. John Cheyo alipata kura 342,891 sawa na asilimia 4.20. wakati kura zilizoharibika zilikuwa 345,214.

Uchaguzi wa mwaka 2005 waliojiandikisha kupiga kura ni 16,401,694 yaani wapigakura walioongezeka ni milioni 6. Wapigakura 9,123,952 sawa na asilimia 80.28 ndio waliomchagua Jakaya Kikwete (CCM). Profesa Lipumba (CUF) alipata kura 1,327,125 sawa na asilimia 11.687. Freeman Mbowe (Chadema) alipata kura 663,756 sawa na asilimia 5.88. Augustine Mrema alipata kura 84,901 sawa na asilimia 0.75. katika uchaguzi huo, waliopiga kura walikuwa 11,875, 927 sawa na asilimia 72.4, huku kura zilizoharibika zilikuwa 310,460, kisha watu milioni 5 wakakosa kupiga kura.
Rais Mwinyi
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 jumla ya wapigakura walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.8, wakati waliojiandikisha walikuwa 11,511,020 sawa na asilimia 57.2. ukiangalia hesabu za kura kwa miaka yote utagundua kuwa hakuna wakati ambao wapigakura wetu walichukua uamuzi mgumu kubadilisha uongozi wa nchi hii.

Vilevile hakuna wakati ambao hakukuwepo na kura zilizoharibika. Hii ina maana kuna wapigakura haba, lakini walalamikaji katika nchi yetu hii wamejaa pomoni. Mathalani kama tunafika mahali tunasababisha kuharibika kwa kura, mfano mwaka 1965 (kura 100,537), mwaka 1970 (kura 74,388), mwaka 1975 (83,322), mwaka 1980 (kura 157,019), mwaka 1985(kura 188,259), mwaka 1990 (kura 109,796), mwaka 1995 (kura 333,936) mwaka 2000 (kura 345,314), mwaka 2005 (kura 310,460) na mwaka 2010 zipo kura zilizoharibika.

Katika hali kama hiyo bado wapo watu wamejaa kila kona ya nchi kazi yao kubwa ni kulalamikia hali fulani ndani ya taifa hili. Mlolongo wa kura zinazoonyesha hapo inaelekea CCM imekuwa chama kinachopata kura nyingi kila chaguzi.

Na wapigakura hao ni walewale ambao miongoni mwao wanaruhusu kura 333,936 kuharibika halafu wanalalamika hali duni au hali mbovu juu ya jambo fulani ndani ya nchi yetu au wengine hawapigi kura kabisa. Sijawahi kuona wananchi wa nchi hii wakichukua uamuzi mgumu kupitia sanduku la kura tangu mwaka 1965. Hivyo tunao wapigakura haba, ila walalamikaji wamejaa pomoni.

January 18, 2013

NIMEBOBEA KATIKA UFUGAJI WA NYUKI KWA NJIA ZA KISASA-ERNEST NDONDE

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

Miongoni mwa mabadiliko makubwa ya ufugaji wa nyuki ni ile hatua ya watu kuamua kujitoa kwa dhati kabisa kupata mafunzo ya ufugaji wa nyuki. Wengi tumezoea kuona njia za zamani ambazo zinawafanya baadhi ya watu wasio watalaamu kuelezea kuwa wanasumbuliwa na ufugaji wa nyuki pamoja na ulinaji asali kwa ujumla. 
Lakini kijana Ernest Ndonde kutoka Lundu alifanya mazungumzo na Lundunyasa Network, kuelezea juu ya utaalamu wake aliopata huko Mpanda wa kufuga nyuki. 
Yeye anasema wka sasa anakaribia kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki katika kijiji cha Mbaha ambacho ni kipo jirani kabisa na kijiji cha Lundu, katika tarafa ya Ruhuhu wilayani Nyasa. Ernest Ndonde aliamua kuchukua ujuzi wa kufuga nyuki wka njia za kisasa kutokana na mahitaji na mabadiliko ya namna ya kulina asali na wateja wake. 
Pia alichukua njia hiyo kuwa moja ya utaalamu ambao anaufanyia kazi katika maeneo mbalimbali ambayo wateja huhitaji mafunzo ya ufugaji nyuki kwa njia za kisasa. Akiwa mjini Mbinga alisema, "Niliamua kuchukua mafunzo hayo ili kufanya kazi hiyo kwa njia za kuboresha maisha ya watu na binafsi. Naelewa ufugaji wa nyuki haufanywi kwa njia za kisasa lakini sasa nina utaalau huo nitafanya na kila mmoja kulingana na mahitaji yake na popote nchini". 
Kwa mujibu wa bwana Ndonde ni kwamba ameona kuna haja ya kuwekeza kupitia ufugaji wa nyuki kuliko wote kutegemea upande mmoja ambao kwa kiasi fulani unazorotesha mahitaji na kuinuka kiuchumi kwa baadhi ya vijana. 
Lundunyasa Network ilimuuliza kama yuko tayari kufanya kazi za watu wengine ambao watahitaji utaalamu wake, yeye alisema haya, "Utaalamu wangu ninaufanya kwa yeyote anayehitaji. Jambo muhimu ni makubaliano ambayo yanaleta faida kwa pande zote, hivyo sote tutaweza kuinuka kiuchumi kwa kuifanya kazi kwa ufasaha zaidi. 
Alisema pia kwa wale wanaohitaji huduma zake za kutoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa wanaweza kuwasiliana naye kwa simu;  0759 965843, 0777665843, 0684965843 au 0655965843 au wka barua pepe; ernestndonde@ymail.com. Naam na Lundunyasa Network inamtakia kila la heri katika utaalamu wake huu mpya ili aweze kusaidia watanzania wanaopendelea kufugaji nyuki na wale wanaotarajiwa kufuga nyuki hapo baadaye.

January 15, 2013

MRADI WA MAJI KIJIJI CHA NG'OMBO WAKAMILIKA

Na Mwandishi  wetu, Ng'ombo
Wakazi zaidi ya 2450 wa kijiji cha Ng’ombo katika Kata ya Chiwanda wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wameondokana na adha iliyokuwa ikiwakabili ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji kijijini hapo,

Akizungumza na Lundunyasa Network, Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo Amos Mtweve alisema mradi huo ambao umejengwa kwa ufadhili wa UNDP kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira umegharimu jumla ya shilingi 298,346,700 na kwamba kuna vituo 23 ambavyo wakazi wa kijiji hicho watakuwa wakivitumia kupata maji.
Mhandisi Mtweve alisema kuwa kabla ya kujengwa kwa mradi huo wananchi walikuwa wakilazimika kutumia maji ya ziwa Nyasa kwa ajili ya kunywa, kupikia, na kuoga hali ambayo ilikuwa ikihatarisha usalama wa afya zao.
Alisema pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza wakati wote wa ujenzi wa mradi huo ikiwemo baadhi ya wananchi kutojitokeza kuchangia nguvu zao kama uchimbaji wa mtaro kwa ajili ya kulaza mabomba lakini bado mradi umekamilika kwa kwango kilichotakiwa.
“kukamilika kwa mradi huu kimsingi ni sifa kubwa kwetu kwani itawapa matumaini wafadhili wetu kufadhili miradi mingine hasa ikizingatiwa kuwa UNDP wamefadhili miradi michache ya maji hapa nchini ikiwemo huu wa kwetu,” alisema Mhandisi Amos Mtweve.

MIKOA YA MTWARA,LINDI NA RUVUMA TAFUTENI SULUHU KUFELI MITIHANI

Na Hamisi Magendela , Dar es Salaam
SIKU chache zilizopita wananchi wa mikoa ya kusini waliandamana kupinga uchimbaji wa bomba la gesi kutoka huko kwenda Dar es Salaam ambacho ingetumika kwa ajili ya kuzalisha umeme.
wanafunzi wakiwa darasani katika moja ya shule za msingi wilayani Nyasa
Umeme huo ambao ungezalishwa jijini Dar es Salaam ungetumika katika mikoa mbalimbali ya Tanzania hali ambayo inaaminika kuwa itasaidia kupungua ghalama za umeme na kufanya ukali wa maisha kupungua.
Sipingi mawazo yao kwani kila mmoja anafikilia kwa utashi wake japo ni vema wakaangalia faida kuliko na mafanikio yatakayopatika siku za usoni ikiwa gesi hiyo itasafilishwa kwa njia ya bomba kwenda Dar es Salaam.
Kikumbwa ambacho naweza kusema ni kwa wananchi wa mikoa ya kusini wanatatizo makubwa zaidi ya kuandamana kutaka manufaiko ya gesi wakati suala zima la elimu likiwa limewatupa mkono kiasi kwamba inatia simanzi kuona inashika nafasi 10 za mwisho katika ufauru wa matokeo ya kidato cha pili yalitangazwa juzi na Wizara ya Elimu na Mafunzo jijini Dar  es Salaam jana.
Licha ya kuwa ni aibu kwa wananchi pamoja na viongozi wa mkoa huo lakini naweza kusema kuwa ni kashfa ambayo katika miaka 50 ya Uhuru ijayo inatakiwa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha wanapata elimu ya kutosha na kuondoka na ujinga wa kukosa elimu.
Ingekuwa vema zaidi badala ya kulalamikia kuhusu gesi wangepiga kelele kwa kukosa elimu bora kwa wanachi wengi wa mikoa hiyo hali inawafanya kukosa nafasi nzuri katika viwanda vinavyojengwa katika mikoa.
Kwa maana nafasi nzuri ya ajira itakuwa ikishirikiliwa na wageni ambao wana elimu ya kutosha ya kukidhi mahitaji ya kazi inayohitajika kwa wakati huo na kufanya wenyeji kufanya kazi za hali ya chini kila siku.
Pia wananchi wa mikoa ya kusini umefikia wakati wa kusimama kidete kuhakikisha fursa iliyotangazwa na Serikali kuwa kuanzia sasa hakutakuwa na mwalimu atakaepangiwa kazi mijini kwa wanaotoka vyuoni.
Kwa maana hiyo ikiwa viongozi wa mikoa hiyo wakitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi wa kuzingatia elimu badala ya kung'ang'ani masuala ambayo kwa sasa hayasaidii sana katika miaka 50 ijayo.
Kusudio hilo la Serikali kupeleka walimu vijini linatokana na malalamiko kutoka sehemu hizo kuwa zimesahaurika kielimu kutokana na kukosa walimu wa kutosha hali inayofanya mikoa hiyo kushikia mikia katika matokeo ya mwisho kama ilivyo sasa kwa mikoa ya kusini.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu ilisema lengo la kufanya hivyo ni kupata uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 10 hali itakayosaidia kunyanyua kiwango cha elimu katika mikoa iliyo pembezoni mwaka nchi.
Hivyo naamini fursa hiyo ikiwa itatumiwa vema na wananchi wa huko itafanya viwanda vinavyojengwa sasa katika mikoa hiyo wenyeji kunufaika kazi zaidi kuliko wageni ndio madhumuni makubwa ya baadhi ya wawekezaji.
Kwa maana wapo wanaotoa ahadi kuwa ikiwa viwanda vyao vitamalizika waajili wenyeji kwa asilimia zaidi ya 60, lakini ikiwa hali ya elimu itaendelea kuwa hivyo ni dhairi wageni watakuwa na nafasi kubwa kuliko wazawa.
Viongozi wa mikoa ya pembezoni mwa Tanzania ikiwemo ya kusini kazi kwenu kuhakikisha mnahamasisha wananchi wenu wanatumia fursa inayotolewa na Serikali kupeleka walimu vijijini inatumiwa vizuri na matunda yaonekana.
Pia kwa Serikali ni vema ikatambu kuwa si walimu pekee wanahitajika katika mikoa hiyo iliyo pembezoni mwa Tanzania bali vyenzo za kufundishi nazo ni muhimu, itakuwa haina maana kupeleka walimu bila ya vitendea kazi na kuwajengea miondo mbinu mingine ikiwemi malazi bora.
Kwani upo uhushuhuda kuwa walimu wengi wanakacha kwenda kufundisha vijini kutokana na kutopatiwa mahitaji muhimu ya kibinadamu ikiwemo usafiri, nyumba nzuri za kuishi na kuishi katika maboma.
 Maoni: 0782839898