February 12, 2013
MAFUNZO YA ELIMU YA UJASIRIAMALI-IRINGA USIKOSE
BIASHARA NA UCHUMI: UNAHITAJI 'GIA' YA UVUMILIVU KUMUDU BIASHARA
![]() |
| Albert Sanga, Iringa |
Makala haya ninayaandika leo ikiwa ni baada ya kumtembelea
Bw. Frank Mwaisumbe nyumbani kwake; jumapili mbili zilizopita na kubadilishana
nae mawazo. Bw. Mwaisumbe ni mfanyabiashara aliyepo mjini Iringa anaemiliki
kampuni inayohusika na uwakala wa safari za Anga, iitwayo Getterland Company
Limited na pia ni mmoja ya waasisi wa shirika la Mindset Empowerment
linaloendesha mashindano ya mbio za Ruaha Marathon.
Nilimfahamu Bw. Mwaisumbe zamani kidogo na kuna kitu cha
kusisimua hapa; kwa sababu ni mwalimu aliyenifundisha kozi ya masoko nikiwa
chuo kikuu Tumaini Iringa. Wiki iliyopita mtakumbuka nilieleza namna wasomi
wetu (wahadhiri, maprofesa na madaktari wa biashara) wanavyokwama kuzalisha
wafanyabiashara halisi; kwa sababu wanafundisha mambo ambayo wenyewe “hawayajui
kwa vitendo”.
Huyu Bw. Mwaisumbe ni mmoja ya wahadhiri ambao walinipa
hamasa kubwa sana kibiashara nikiwa chuo kikuu; kwa sababu alikuwa akifundisha
“biashara” halisi kwa sababu ni mfanyabiashara aliyefanya biashara nyingi sana
tangu kitambo. Vyuo vyetu nchini vinawahitaji watu wa jamii ya Bw. Mwaisumbe
katika kuwasaidia wahitimu wetu kujiajiri badala ya kulilia ajira ambazo
“hazipo”
Ninashirikiana kwa ukaribu sana na Bw. Mwaisumbe zaidi sana
katika shirika lake la Mindset Empowerment; ambapo mimi ni Mratibu
(Coordinator) wa shirika hili. Katika kushirikiana huku kuna mambo mengi sana
kuhusu uzoefu kibiashara ambayo nimekuwa najifunza kutoka kwake.
Jumapili hiyo niliyomtembelea tulitumia muda mwingi kujadili
mipenyo, staili, mbinu na mambo yanayosababisha wafanyabiashara mbalimbali
duniani kufanikiwa. Nilijifunza mengi sana katika mazungumzo yetu haya na
nikakumbuka visa vingi vilivyowahi kunipata katika harakati zangu kibiashara.
Katika kujadili tulibaini kuwa hakuna mfanyabiashara yeyote
duniani anaesimama mara moja kirahisi. Kila mfanyabiashara aliyefanikiwa
ukimfuatilia historia yake atakueleza namna alivyoanguka-anguka na kusimama,
namna alivyojaribu mambo mengi lakini akafanikiwa katika machache ama katika
moja bila kusahau namna alivyopokea upinzani mkali katika kufanikisha hilo
unaloliona limefanikiwa.
Binafsi ninakumbuka mtaji wangu wa kwanza niliupata (kwa
jasho langu mwenyewe bila kupewa na mtu) nikiwa na miaka 19 kwa kuchuuza
vitunguu kutoka pale Mang’ula Karatu na kuvipeleka Arusha mjini. Ilikuwa ni
biashara niliyoipatia kweli kweli kiasi kwamba nikaweka malengo ya kuanzisha
chuo cha mafunzo ya kompyuta na biashara.
Ndani ya mwaka mmoja nilifanikisha lengo langu hilo kwa
kufungua chuo hicho kule wilayani Mufindi. Nakumbuka thamani ya kile chuo ilikuwa takribani milioni
ishirini. Nilijiona niliyefanikiwa na kila nilikokuwa ninapita nilikuwa
ninapokea heshima na pongezi za mafanikio hayo hasa ikizingatiwa kuwa nilikuwa
nimezikamata “milioni” nikingali mdogo wa miaka 20 tu tena nikiwa ndio kwanza
nimehitimu kidato cha sita.
Ukweli ni kwamba saa niliyodhani kuwa “nime-win” kumbe ndio
saa ambayo nilikuwa naelekea kuanguka. Ile biashara ilianguka yote; ndani ya
miezi miwili tu nikawa sina kitu! Kufilisika kwangu kulitokana na mambo mawili.
Mosi; wafanyakazi niliowaajiri kuendesha chuo walijigeuza miungu watu, wakaanza
kuwanyanyasa wanafunzi na kuzembea kufundisha. Nilikuja kupewa taarifa mwishoni
mambo yakiwa yameharibika kabisa kuambiwa kuwa kati ya wanafunzi 104 waliokuwa
chuoni wamebaki wanafunzi nane tu!
Nilichanganyikawa na nikaenda haraka sana kuwatimua kazi,
lakini nilishakuwa nimechelewa na mambo yalikuwa yameshaharibika. Pili;
kulitokea shoti ya umeme (kwa uzembe wao) na ukaunguza sehemu kubwa ya vifaa
vya chuo kile zikiwemo kompyuta na vifaa vingine. Sikuwa na ujanja zaidi ya
kukifunga kile chuo na kukubali matokeo ya kufilisika.
Leo hii ninapojikumbusha kuhusu biashara ile namtafakari
mwandishi aitwaye Mchungaji Daktari Robert Schuller aliyeandika kitabu
kiitwacho, “Success is Never Final Failure is Never Ending”. (Kufanikiwa sio
kikomo na kushindwa sio mwisho). Anachomaanisha mwandishi huyu ni kuwa
ukifanikiwa usijisahau na ukianguka usikate tama.
Ukweli ni kwamba kwenye biashara kuna mapito mengi sana
kiasi ambacho mfanyabiashara unahitaji uvumilivu mkubwa mno kuendelea. Biashara
sio lelemama! Unaweza kutumia miaka mingi sana katika kujenga biashara zako na
kukusanya mali; lakini ukaja kupoteza kila kitu ndani ya dakika chache.
Huhitaji kukata tamaa, unahitaji uvumilivu na kuanza upya. Huo ndio
ujasiriamali na sifa ya mjasiriamali ni kutokukata tamaa.
Unadhani mchezo umeishia hapo? La hasha! Sikukata tamaa,
nilisimama na kuanza kujikongoja tena; safari hii nikaamua kufanya biashara ya
kukusanya na kuuza alizeti kule wilayani Njombe katika maeneo ya Irembula. Kama
kawaida; si rahisi kufanya biashara peke yako; ni lazima uwe na watu. Hata huko
kwenye alizeti nilikuwa na watu niliowaamini kunikusanyia na kunitunzia.
Mwanzoni nilienda vizuri; nikajisemea moyoni; loo! Biashara
si ndio hii? Kumbe nilikuwa nimepotea kwani mkasa mwingine ukanitokea. Nikiwa
nimekopa fedha kutoka kwa watu na kukusanya alizeti kwa wingi huku nikijua saa
ya kuuza nakuwa milionea; nikadhulumiwa mchana kweupe! Yule nilipotunza alizeti
akaauza alizeti magunia yote kisha akakimbia na fedha zote na hadi leo
ninapoandika makala hii ikiwa imepita miaka kadhaa sifahamu alipo.
Huu ukawa ni msiba mwingine kibiashara kwangu. Tena ni bora
angekuwa alikimbia na mtaji wangu pekee; lakini aliondoka na hela hata
nilizokopa; hii ina maana nilipoteza mtaji wote na nikabakiwa na madeni. Hii
ndio biashara, sikukata tamaa ndio maana hadi leo “nimekomaa” na biashara.
Kimsingi sina miaka mingi kiumri na wala sina miaka mingi sana katika biashara,
lakini kuna visa vingi mno vya kushindwa na kufanikiwa vilivyonitokea hadi
sasa; kiasi kwamba nikisema nivilete vyote gazeti zima halitatosha kwa juma
moja.
Hata hivyo; katika mikasa yangu miwili niliyoileta hapo juu
kuna mambo machache napenda uyajue ambayo Bw. Mwaisumbe amenisaidia sana
kuyajua. Mosi unapokuwa katika biashara unatakiwa uwe na imani isiyoteteleka ya
kuwa kuna siku utafanikiwa. Inawezekana ukawa unafanya biashara lakini haujui
“utatoka” lini.
Inawezekana
umeshapata hasara nyingi mno katika biashara zako; lakini kama ukibaki na imani
hii hakika ipo siku utafanikiwa tu. Bw. Mwaisumbe huwa anapenda kusema hivi
“Mtu aliyeanguka-anguka sana katika ujasiriamali, siku akiinuka, hataanguka
tena. Na mtu anaeanguka na kusimama hahofii kuanguka kesho kwa sababu anajua
ataamka tu”
Pili; asilimia kubwa ya sisi wajasiriamali tunaangushwa sana
na watu wengine, ediha tunaowaamini ama tunaowaajili ama tunaoamua kupanda nao
tunapopanda kibiashara. Pamoja na uweli huu; haimaanishi kuwa usiwaamini watu;
la hasha! Jambo la kufanya ni kuhakikisha unajitahidi kadiri uwezavyo kutafuta,
kushirikiana na kuajiri watu sahihi katika ujasiriamali wako. Itakumbukwa kuwa
nimewahi kuandika kupitia gazeti makala yenye kichwa; “Mjasiriamali na Sayansi
ya kuajiri wafanyakazi”
Tatu; unapofanya ujasiriamali ama kama unatamani kuingia
katika ujasiriamali hutakiwi kuogopa kupoteza mtaji ama hatua uliyonayo. Kitu
cha thamani katika ujasiriamali sio mali ama fedha unazofanikiwa kuzipata; bali
ni “akili ya fedha (financial IQ), kujiamini na uzoefu unaoupata kila
unapofanya biashara. Ni vema mjasiriamali kujenga ujasiri na kujiamini (spirit)
kiasi kwamba ujisemee kuwa “hata kama nikipoteza kila kitu nilichonacho leo,
ninaweza kurudisha na zaidi ya nilivyokuwa navyo”.
Niandikie: stepwiseexpert@gmail.com; 0719 127 901
February 11, 2013
CHOMBEZO: KILA MTU, MTU, MTU NA HAKUNA MTU
![]() |
| Markus Mpangala |
Hii ni hadithi kuhusu watu wanne waitwao Kila Mtu,Mtu, Mtu na Hakuna Mtu.
Kulikuwa na kazi muhimu kufanywa, na Kila Mtu alikuwa na uhakika kila mtu
angefanya kazi hiyo, lakini Hakuna Mtu aliyefanya hivyo. Mtu alipata hasira kuhusu hili, kwasababu
ilikuwa ni kazi ya Mtu. Kila Mtu aliwaza kuwa kila Mtu anaweza kufanya hivyo lakini
Hakuna Mtu aliyetambua kwamba kila mtu asingefanya hivyo. Na mwisho iliishia Kila Mtu kumlaumu Mtu wakati
Hakuna Mtu aliyefanya chochote ambacho Kila Mtu angeweza kufanya. Mwisho wa hadithi……
Haya sasa tafakari. Je wewe unatumia pesa zako
vizuri? Je una madeni mengi? Je wewe huachishwa kazi mara kwa mara? Nini sababu
zako za kuachishwa kazi? Au ni kwasababu ya kazi yenyewe au yule
aliyekupa kazi? Au ni kwasababu mazoea au tabia fulani ambayo unapaswa
kurekebisha?
Ikiwa hutumii vizuri pesa zako mwenyewe, je
utaweza kutumia pesa za familia? Je unatazama mambo yote kwa mtazamo mbaya? Tafakari mara nyingine. Jipe nafasi ya kufanya
hivyo huku ukijua kuwa kazi inahitaji uelewa, umakini na bidii. Sote tunajua kazi ni za kila mtu hapa duniani. Hakuna mtu ambaye anatarajia kazi ya mtu
itafanywa na mtu mwingine. Kila mtu anajua anahitajika kufanya kazi kwa bidii
ili asimtegee mtu au kumtegemea mtu.
Na kila mtu anahitaji kazi ili aishi vema,
hakuna mtu asiyehitaji familia bora. Kwahiyo ili kutimiza haya ni lazima
ujifahamu. Lakini ujue wajibu wako katika kazi yako. Na ufahamu mipaka ya kazi yako. Fahamu matumizi
yako ya kila siku ili usimlaumu mtu kwakuwa hakuna mtu atakayekusaidia. Fahamu
bajeti yako kwa siku,juma,mwezi, na mwaka. Lazima ujifahamu kila hatua unayokwenda mbele
maishani. Tambua kila mtu anafanikiwa endapo atafuata kanuni za msingi za
maisha.
Hakuna mtu anayependa kuona mtu anashindwa
kufanya kazi yake bila sababu, kwakuwa tu mtu anategemea kufanya hivyo. Na
asipofanya hivyo inakuwa shida na inamfanya mtu awe na hasira dhidi ya kila mtu. Pesa, kazi na maisha ni lazima viwe tofauti ili
kuongoza familia yako. Usitegemee mtu ataongoza familia yako. Hakuna mtu
atakayewaambia wanao wasome kwa bidii.
Ukihitaji kazi, basi hakikisha unayo hoja za
kusema kwa mtu. Je umekabiliana vipi na waombaji wapya wa kazi? Wangapi
wanatimiza wajibu wao katika kazi, maana kila mtu anataka kuona mtu anafanya
kazi yake ipasavyo. Je unalisaidiaje taifa kutokana na kazi yako?
Unafahamu kuwa kutoangalia mambo kijuu juu inakusaidia kujifahamu na kuongoza
vema ofisi yako au kupata kazi mpya?
Unatambua kuwa ndani ya ofisi yako kila mtu
anahitaji cheo ulichonacho? Hakika nakuambia hakuna mtu ambaye hataki kuona mtu
anaishi vizuri. Kila mtu anajua ni lazima afanye kazi na apendwe
na kila mtu. Mtu huona fahari pale anaposifiwa na kila mtu kutokana na
kuwajibika katika kazi yake. Kazi ya kila mtu ni mtu kuifanya kazi yake kwa
bidii na hakuna mtu ambaye anapenda kuharibu kazi yake.
Kwa hakika ndugu zangu mnatakiwa kuwa waelewe wa mambo na kila mtu ajue kuwa unaelewa. Mtu mwenye bidii ya
kazi na kujifunza mambo hachoki kuwatumikia watu, na kila mtu hupenda kufanyiwa
kazi zake vema. Usiwe mtu unayependezwa na mambo yaleyale au
kukubaliana kila jambo kwa mtindo na sababu zilezile. Uwe mtu ambaye kila mtu
anafahamu kuwa akihitaji ushauri basi atakuwa wa kwanza kuwajibika mbele ya
hadhira.
Jipe muda wa kujisomea, fanya tafakari kila
unachojisomea. Natambua kila mtu anachoka atokapo kazini, lakini hakuna mtu
ambaye anapenda kukaa tu ofisini kwake bila kufanya kazi yoyote. Timiza malengo yako kwa kuwatumia watu. Uwe
mtumishi wa kila mtu kulingana na cheo chako au nafasi yako kwa jamii. Kila mtu
anahitaji msaada wako wa nasaha na mengineyo, kwani duniani tupo kwaajili yaw
engine.
Wengine hawa ni kila mtu ambaye anajua umuhimu
wa kuwatumikia. Na hakuna mtu ambaye hajui umuhimu wa hili. Je unadhani kazi ya
mtu ni ipi? Na hadithi hii ya kila mtu inakupa funzo lolote?
Na inawezekana ndugu yangu umekata tama ya maisha. Lakini tambua kila mtu
amepitia kwenye milima na mabonde. Hakuna mtu aliyefika kileleni bila kuanguka.
Kila mtu anayepanda mlima Kilimanjaro kuna
mahali aliteleza au kuanguka. Hakuna mtu ambaye amefanikiwa bila kuchoka,
lakini unahitaji nidhamu zaidi ya kuchoka kuliko kuendelea kudhani kila mtu
anaweza tu kufanikiwa akikaa sebuleni na kuota amefanikiwa.
Unachotakiwa kufanya ni kusema katika kazi za
mtu basi wewe ni kila mtu na hakuna mtu anayeweza kuifanya kazi hiyo zaidi
yako. Waingereza wanaomsemo wao, simama uhesabiwe vinginevyo
kaa chini usahauliwe. Kwa maneno hayo inamaana
hakuna mtu muhimu katika maisha yako zaidi ya wewe. Hebu rudi juu usome falsafa
ya leo ya Kila Mtu, Mtu, Mtu na Hakuna Mtu. Halafu jifahamu wewe ni nani kati
ya hao wanne.
Madhumuni
Chombezo
Subscribe to:
Posts (Atom)



