February 20, 2013

FRESH FARM WAMEREJEA TENA KATIKA UWEKEZAJI WA MITI YA MBAO NA NGUZO


Kampuni ya Anesa Co.,Ltd kupitia biashara yake tanzu ya Fresh Farms(T); kwa kushirikiana na kikundi cha “Rudisha Uumbaji wa Mungu kwa Kupanda Miti (RUMM)-Kilolo;” tukiwa mkoani Iringa, tumezindua programu maalumu iliyolenga kuwawezesha watanzania wengi kuwekeza na kumiliki mashamba ya miti ya mbao na nguzo kwa urahisi kabisa.

1.  Progamu hii inaitwa “GREEN THE WORLD and BECOME RICH” ambapo tunauza mashamba yenye miti (miti pamoja na ardhi) kwa utaratibu wa mtu kulipa kidogo kidogo kwa kadiri ya kipato chake. Kiwango cha chini cha kununua ni ekari tano, ambapo utatakiwa kulipa walau asilimia 50% ya bei yote; kisha fedha inayobaki utaendelea kuilipa kwa awamu kwa kadiri utakavyokubaliana na kampuni

2.  Tupo Iringa mjini na Kilolo (kijiji cha Mwatasi), na mashamba yapo maeneo mbalimbali katika wilaya za Mufindi na Kilolo. Yapo mashamba yenye miti kuanzia ya mwaka mmoja hadi minne, na bei zake ni kuanzia tsh. 700,000(laki saba) hadi 2,000,000 (milioni mbili) kutegemeana na umri wa miti husika. Bei zote zinajumuisha (miti pamoja na ardhi)

3.  Miti ya mbao inachukua miaka kati ya 7 hadi 10 tangu kupandwa hadi kuvunwa. Wastani wa faida unayoweza kupata kwa ekari moja ya miti iliyokomaa ni tsh milioni tisa hadi kumi na tano (kama ungekuwa unauza leo). Gharama ya kuhudumia ekari moja kwa mwaka haizidi laki mbili. NOTE KWA WALE WAGENI KUHUSU KILIMO HIKI CHA MITI: Pamoja na taarifa hizi, kampuni inahamasisha watu ambao ni wageni kabisa na taarifa zihusuzo miti; kutafuta taarifa zaidi na zaidi kutoka vyanzo mbalimbali kuhusu kilimo-biashara hiki; ili kujiridhisha kabla ya kufanya maamuzi ya kiuwekezaji.

4.  Mnunuzi akishafika na kuyatazama mashamba (au kama anayafahamu mazingira yalipo mashamba); akishajiridhisha, atasaini mkataba wa makubaliano ya kimalipo kati yake na kampuni, kisha ataanza malipo mara moja. Baada ya kukamilisha malipo yake, utafanyika utaratibu wa kupata hati za kimila/mikataba ya kiumiliki kutoka mamlaka ya baraza la ardhi la kata/kijiji kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa ardhi ya vijiji ya mwaka 1999.

5.  Fresh Farms(T) tukiwa na falsafa ya “Greening the world and Feeding People”; lengo letu ni kuhakikisha tunawasaidia mamia ya watanzania kutumia fursa ya uboreshaji mazingira; kwa kuwekeza vitega uchumi vya mashamba vinavyowahakikishia kipato kikubwa sasa na siku za usoni.

6   Kampuni itaendelea kutoa usaidizi wa uangalizi na utunzaji wa mashamba yote yanayonunuliwa kutoka kwetu kwa utaratibu rahisi na nafuu kabisa. Nia yetu ni kuona kuwa kila anayewekeza; avune faida ya uwekezaji wake. Hivyo, hauhitaji kuhofu juu ya usalama wa shamba utakalonunua, popote utakapokuwepo utajihakikishia kuwa “investment” yako inafanyiwa juhudi kubwa kuhakikisha inakua.

7.  Programu na ofa hii ni ya muda maalumu, imeanza tarehe 15, Februari, 2013 na itamalizika, Aprili, 14, 2013. Programu hii inaweza kukoma kabla ya tarehe ya ukomo, ikiwa ekari zilizotengwa zitaisha mapema. Hivyo kwa yeyote anayehitaji tunashauri kuwasiliana nasi mapema.

Mawasiliano:
Iringa:                   Mkurugenzi, Albert Sanga (0719 127 901, 0766 742 414), albertnyaluke@yahoo.com

Dar es Salaam:     Meneja Masoko, Markus Mpangala (0764936655), mwanazuoni27@gmail.com

February 19, 2013

SIASA ZA KITOTO; WAKUBWA NA WATOTO


                                             
Markus Mpangala
Ndugu zangu waungwana, kama kuna kitu tumejilemaza katika nchi yetu hii ni ile hali ya kujitumbukiza katika janga la kufikiria matatizo tu. Wapo watu wanafikiria kila kukicha na kusubiria tatizo litokee ndio wanakuwa wa kwanza kupayuka. Kuna mchezo mbovu katika sasa zetu unaendelea hapa nchini. mwanasiasa anahama chama kimoja kwenda kingine akiwa na lundo la TUHUMA. Mathalani mwanasiasa anahama CHADEMA anakwenda CCM. Au anahama CUF anakwenda ADC, au anahama CHADEMA anakwenda CUF.
Au anahama ADC na kwenda TLP. Kila siku utasikia eti nilitumika kuwadanganya watanzania au wapigakura. Kwa wale wataalamu wa kusoma tabia za watu wanabaki wanajiuliza, hii ni tabia mpya au udhiafu wa kutokomaa kifikra? Sababu mwanasiasa anapohamia chama kingine kisha anakuwa na kapu la TUHUMA ni moja ya udhaifu mkubwa wa ukomavu wake kisiasa. Ni udhiafu na tumekuwa tukijipongeza kwa upuuzi huu kwamba ndio ugangwe wa kuonekana ni wanasiasa weledi.

Haikatazwi kuhama chama, haikazwi kutoa TUHUMA. Lakini moja ya udhaifu wa mwanasiasa au mkoamavu kifikra, na aliyejipika akajiivisha kisha chama/siasa zikamfanya aive hawezi kutoa lundo la TUHUMA kwa chama anachohama. Ni utoto na siasa za kitoto kuanzia watoto hadi wakubwa. Hayo ni dhahiri yanaonyesha namna gani tumeshindwa kutengeneza wanasiasa wenye ushindani badala yake tumekuwa na idadi kubwa ya wanasiasa wapika majungu, wivu wa kujinga na kadhalika.

Nakiri ni makosa makubwa sana katika siasa zetu. Nitatoa mifano midgo tu, Tambwe Hizza alirudi CCM akitokea chama cha CUF. Wakati anarudi CCM alisema kuwa kule CUF alitumika vibaya na alidanganya mengi, ingawaje hakutaja alichotumiwa au alichodanganya. 

Kwa mkondo ule wanasiasa wanaorudi CCM wanasema hilo hilo. Akihama CHADEMA kwenda CCM, au akihama CCM kwenda CHADEMA anatamka ukakasi kuwa wapo watu ambao wanasababisha matatizo ndani ya chama na wkamba wao wanaamua kuhama. Utoto mkubwa umeenea na ni aibu sana kwa mwanasiasa kijana kuigia siasa za kikoloni ambazo zimekuwa na ubainafsi na kushindwa kutengeneza misngi. Angalia hii pia, Arcado Ntagazwa alipohamia CHADEMA alisema sababu ni maovu ya CCM.
Ni kwamba kwa mkondo uleule wa Tambwe Hizza ambaye aliamua kuondoka CUF kisha akakabidhiwa kitengo cha PROPAGANDA cha CCM, akidai alitumika vibaya. Hii nchi yetu inachekesha mwanasiasa anahamia chama kingine anakishutumu kile anachotoka. Kuna haja gani dada yangu mpendwa Juliana Shonza kumwambia mwenyekiti wa CCM kuwa alipokuwa CHADEMA alitumika vibaya? Natambua wapo wanasiasa shupavu, na Juliana Shonza anaelekea kuwa shupavu, lakini moja ya dosari alizokumbana na kuangukia kwenye tope la mtindo wa lundo la TUHUMA.

Nasema hilo sababu huyu ni mwanasiasa kijana na anakuwa msingi wa vijana kuchukua uamuzi wa kuhamia kwingine. Lakini ushauri wa msingi haifai kabisa kuhamia chama kingine ukiwa na shutuma ambazo zinakuweka katika darubini ya uangalizi huku watu makini ndani ya chama wanabaki wakitoa gego na fizi kwa kujiuliza, tumfanyeje mtu huyu? Je kama mwanasiasa alitumika vibaya atokako, ataweza kuaminika aendako? sichelei kusema hizi ni siasa dhaifu sana. Hakuna sababu ya kujaza orodha ya maovu ndio umahiri wa kuhamia chama kingine, nadhani ni siasa za kitoto.

Wazee wetu wamekuwa waasisi wa siasa za kitoto kama hizi, maana rcado Ntagazwa angeliweza kutumia weledi kuhamia CHADEMA. Profesa Abdallah Safari naye angetumia weledi kuueleza umma sababu za kuhamia CHADEMA. Mabere Marando angetumia weledi kuhamia CHADEMA.Vivyo hivyo ilipaswa kuangaliwa kwa wanasiasa wengine ili kuondokana na mtindo unaomea siku hizi eti ukihamia chama kipya unatakiwa kuonekana u mtakatifu na kutubu 'madhambi' ya utokako, lakini wale wanaokupokea kwanza wanapoteza imani juu yako.

Kisha wanachofanya kukukejeli na kukuona u mtumwa wa siasa na umekosa misingi. Muhimu tutengeneze wanasiasa ambao wanajua nini maana ya siasa, na nini ushindani wa kisiasa. Lau hata wakihamia vyama vingine wawe na uhodari wa hoja sio kutegemea kuwatusi au kuwatuhumu wengine. Aibu, acheni siasa za kitoto kwa wakubwa na watoto.

UCHAGUZI MKUU: HOFU YA MACHAFUKO YAREJEA KENYA

Dorine Otinga

Na Dorine Otinga, Eldoret, Kenya

MDAHALO ulimalizika vizuri mapema Jumatatu wiki iliyopita hapa Kenya, huku wagombea wote wakionyesha uwezo mkubwa.
Martha Karua, Raila Odinga, Peter Kenneth, Uhuru Kenyatta ni wagombea waliovuta hisia za wananchi wa Kenya kutokana na uwezo wao wa kujibu hoja na kuelezea sera zao iwapo watafanikiwa kushika madaraka.

Takribani wananchi 328 waliotazama mdahalo huo kwa njia ya runinga wanakubali kuwa ushindani wa wagombea umekuwa mkubwa. Pia mdahalo umeboresha uelewa wananchi wa Kenya kujua ni mgombea gani anafaa kuwa rais badala ya Mwai Kibaki.Siku chache zilizopita baada ya mdahalo, Taasisi mbalimbali za utafiti ziliendesha zoezi la kura za maoni juu ya uamuzi wa wakenya kuchagua rais Machi 4, mwaka huu.
Watu 92% wamekubali kuwa mdahalo kwa njia ya runinga ulisaidia kujua mbinu na uwezo wa kujieleza wa wagombea wao. Wengine 24% walilazimika kubadili mawazo yao kwaajili ya wagombea waliodhani watawachagua. Kwahiyo, mdahalo umeleta changamoto kwa wagombea kuweza kuwapata wapigakura sahihi ili kuibuka na ushindi. Wapigakura hawa 34% ina maana wamebadili mawazo kutoka kwa mgombea mmoja kwenda kwa mwingine.

Uhuru Kenyatta
Pengine wapo waliopanga kumchagua Musalia Mudavadi au Raila Odinga na Uhuru Kenyatta, lakini kutokana na kuwatazama na kuwasikiliza kupitia mdahalo, ni wazi wananchi wamebadili mitazamo juu ya wagombea hao. Profesa James Kiyiapi alitangaza mageuzi ya elimu ya hapa Kenya. Raila Odinga alitangaza mageuzi 18 ya kimaendeleo ambayo atayafanyia kazi ipindi akingia madarakani kuongoza wakenya; elimu bure, afya, na uwajibikaji sekta ya umma. Naye Martha Karua amekusudia kupambana na ufisadi unaolitafuta taifa letu kwa miaka mingi sasa. Kwenye mdahalo huo wagombea ambao hawakufua dafu ni Musalia Mudavadi, Paul Muite na Mohamed Abduba Diba.

Mvuto wao kwa wapigakura bado dhaifu, haitegemewi kama wataweza kumudu ushindani wa Uhuru na Odinga. Wakenya 27% wanadhani Uhuru Kenyatta atashinda uchaguzi. Wakenya 26% wanaamini Peter Kenneth atashinda kutokana na kufanya vizuri kwenye mdahalo. Vilevile 22% ya wakenya wanaamini Raila Odinga atashinda uchaguzi na yeye ndiye bingwa wa ushawishi hadi sasa akiwa na mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka.

Halafu kuna 12% wanapenda kuona Martha Karua akishinda kuchukua uongozi. Sasa baada ya kuona hiyo, na sasa tuone suala nyeti ambalo linagusa sana wagombea wa urais hapa Kenya. Kwanza, suala la kisiwa cha Migingo ambalo limeleta ugomvi na Uganda ya Yoweri Museven. Kenya na Uganda zingeweza kuingia vitani kutokana na kuzozania kisiwa cha Migingo ambacho kimsingi ni chetu hapa Kenya.
Yoweri Museven alinuia kupeleka majeshi kisiwani Migingo, lakini alisahau kuwa hata sisi Kenya tunaweza hilo. Mwai Kibaki alilaumiwa kupuuza sana suala la kisiwa cha Migingo lakini ni vema anaondoka madarakani huku mapigano baina ya Kenya na Uganda hayakutokea. Suala hili linachukuliwa kama hatua nzuri ya kulinda amani, lakini haieleweki iwapo mshindi wa urais Machi 4 atavumilia kama Mwai Kibaki alivyofanya kwa kisiwa cha Migingo.
Hili ni suala la nje ya mipaka ya Kenya yetu, lakini yapo mengine yanashiria kuleta mapigano baada ya uchaguzi. Hofu hii imejaa kwa wengi miongoni mwa wakenya.
Dalili mojawapo ni mapigano ya kikabila kule Tana River ambako watu 140 walifariki dunia kutokana na ugomvi wa kuwania mifugo. Hili la Tana River lazima itakuwa moja ya dalili za kutoelewana kwa wakenya hivyo ukabila kuchukua nafasi hata kwenye uchaguzi huu. Yapo maeneo ambayo yanaongoza suala la kabila hapa Kenya.
Raila Odinga
Mfano, ingawa si sehemu zote, lakini Rift Valley Province kuna ukabila sana. Hofu ni vita baada ya uchaguzi kutokana na makabila kutoelewana kabisa. Kwa Rift Valley Province ina makabila nyingi, lakini kabila lenye watu wengi ni Kalenjin na Wakikuyu, ambao hawajawahi kusikizana kabisa.

Sasa hawa Wakalenjin na Wakikuyu wamekuwa mwiba kwa miaka mingi kila mmoja akiona yeye ni bora kuliko kabila lingine. Eneo jingine ni Nyanza Province ambalo kuna kabila la Wajaluo. Nyanza hasa eneo la Kisumu City huwa machafuko makubwa yanatokea kwani wenyeji wake wamekuwa wakifukuza makabila wasiyotaka pamoja na kuchoma maduka ya wahindi. 
Kule Nyanza Province Wahindi ni wahanga wa kwanza wa machafuko kwani maeneo yao ya biashara yamekuwa yakiharibiwa sana. Imekuwa hivi kwa miaka mingi na sasa Wahindi hawa wanaona ufikapo uchaguzi ni nyakati zao za kufunga biashara kwa wale wenye uwezo wanahama kabisa Kenya yetu.
Wengine huenda huko India na wengine huishi nchi za kigeni kwa muda na uchaguzi ukimalizika kwa amani wanarejea. Eneo jingine ni Eldoret ambalo lipo Western Kenya. Kwanza hapa huwa na hali mbaya zaidi. Hapa Eldoret inasemekana kuna watu wamekusanya silaha na kujiandaa kwa mapigano baada ya uchaguzi Machi 4. Sio Al Shabab wala magaidi wowote bali ni watu wa kabila la Kalenjin wanasemekana kuhifadhi silaha kuwadhuru makabila mengine baada ya uchaguzi iwapo kutakuwa na ukosefu wa amani.

Martha Karua
Haya maeneo mawili Rift Valley Province na Nyanza Provine yanakuwa na machafuko sana, inatia hofu sisi wananchi wa Kenya namna gani tutaweza kuishi. Wakenya wenyewe hawapo tayari kuona wanamaliza uchaguzi halafu wanaingia kwenye machafuko kama mwaka 2007 baada ya uchaguzi. Hatupo tayari kuwa na machafuko ila kwa dalili zilizopo inatia hofu hatima ya uchaguzi itakuwaje mwaka huu. Kingine ni hata wagombea kuamiani kuwa kutegemea makabila yao ndio siri ya ushindi, huku wakisahau inaleta picha mbaya na kusababisha machafuko.

Raila Odinga anawafuasi wengi na anategemewa kushinda uchaguzi. Uhuru Kenyatta ndiye anampa ushindani mkubwa manake ‘ruuning mate’ wake William Ruto hushawishi Wakalenjin wenzake kumuunga mkono Uhuru Kenyatta. Ruto hatumii sera ya kushawishi kwa Wakalenjin bali anatumia ukabila wake ili kuwashawishi Wakalenjin waweze kumchagua Uhuru Kenyatta. Mimi natokea kabla la Luhya, lakini kura yangu iko wazi nitampa Uuru Kenyatta na ‘running mate’ wake Willaim Ruto ili waweze kushinda bila kujali, Uhuru ni kabila la Embu na Ruto kabila la Kalenjin.

Sisi Luhya tunatokea eneo la Western Kenya kama nilivyosema kuhusu Nyanza Province na hofu ya machafuko. Raila Odinga anazo sera nzuri kwa wakenya, lakini Uhuru Kenyatta anaweza kumtisha kwani ameleta sera ambayo itamfanya aungwe mkono na wasomi wengi wa Kenya, kuanzia wanafunzi wa vyuo vikuu, wahadhiri, na watu wa sekta ya elimu kwa ujumla.
Uhuru Kenyatta atapata kura yangu sababu ameahidi akishinda ataondoa Parallel Program kwa University ili wanafunzi wote waliofuzu walipe pesa sawa. Parallel program ni mwanafunzi ambaye hakupata alama B ya pointi 61 lakini anafuzu kuwa University anajilipia zaidi ya laki moja kama karo chuoni. Kwa sera hii Uhuru Kenyatta anapata kura yangu na atafanikiwa kupata kura nyingi za watu wa sekta ya elimu kwani atawaondolea ubaguzi wakenya katika elimu.

Wengi wanakosa kulipiwa karo sababu hawana alama Ba, hivyo hujilipia kiasi cha pesa wenyewe chuoni. Ninaamini Raila Odinga anaweza kushinda uchaguzi huu, ingawa wakati uliopita tuliamini na hakushinda kwani ilisemekana Mwai Kibaki aliiba kura.
Lakini ushindani anaotoa Uhuru Kenyatta si uchwara kwani amekuwa mwerevu kuelezea makusudio yake pindi akiingia madarakani, ambayo yanaonyesha kabisa kuwaunganisha wakenya.
William Ruto
Kuna jambo lingine limejitokeza siku chache zilizopita kabla ya uchaguzi ambalo linatia hofu ya machafuko. Kama kura zinaibwa maana yake itachochea machafuko, mfano juzi gari ya Mkuu wa IEBC (Electoral and Boundaries Commission), Isaac Hassan alipigwa risasi, uzuri hakuwa ndani hivyo hilo nalo linaashiria kuna mambo yatajitokeza baada ya uchaguzi hasa hawa Wakikuyu na Kalenjin wanapenda fujo na hawajawahi kuelewana.

Sasa ukiangalia mapigano ya Tana River, watu 140 wamekufa sababu za kikabila na kugombea mifugo. Halafu hali mbaya ya mji wa Garrissa mpakani mwa Somalia na hapa Kenya, kisha miji ya Kisumu na Siaya pamoja na eneo la Kibera mjini Nairobi, ni dalili za wazi kuna mambo uchaguzi ujao.Ni eneo la Kiberra kule Nairobi ndipo machafuko yalipoanzia mwaka 2008, tunakumbuka hili na Wakikuyu walikuwa na chokochoko dhidi ya Wakalenjin. Mzee Daniel Arap Moi naye ni mkalenjin amekuwa akisisitiza wakalenjin waache mapigano dhidi ya wakikuyu lakini hakuna dalili za kumaliza suala hili.

Moi anakula pensheni yake ya randi milioni 2.5 sawa na pauni 175,000 anamuunga mkono Musalia Mudavadi, badala ya Uhuru Kenyatta ambaye alimuunga mkono mwaka 2002.
Kubadilika kwa Moi kumuunga mkono Mudavadi wa kabila la Luhya ni wazi ameamua kubadili mbinu za kisiasa baada ya kuona hakuungwi mkono na wagombea wengine. Moi pamoja na hotuba zake, lakini hawezi kumaliza hofu ya machafuko  baada ya uchaguzi.

Na kwakuwa nitakuwa Voters Clerk uchaguzi wa Machi 4, nadhani nitapata wasaa mzuri zaidi kuyasoma mawazo ya wapigakura na mwenendo mzima wa uchaguzi wetu hapa Kenya.
Lakini hofu kubwa itakuwa kwa wafuasi wa Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, kati ya Wakalenjin, Wajaluo na Wkikuyu. Kuna hofu ya mchafuko hapa. Kwa mfano, Februari 15, Raila Odinga alitembelea watu wa jamii ya Embu ambako ni kabila la Uhuru Kenyatta, kulitokea rabsha, kama si juhudi za Polisi, basi Odinga angetimuliwa kwani wanamtaka Uhuru Kenyatta tu.

Dorine Otinga ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton nchini Kenya na atakuwa miongoni mwa wasimamizi wa uchaguzi ujao.

UCHUMI NA BIASHARA: "NJIA BORA YA KULINDA BIASHARA ZAKO"

Albert Sanga, Iringa

Wiki iliyopita niliandika makala iliyokuwa na kichwa “Unahitaji gia ya uvumilivu kumudu biashara”. Kwenye makala hiyo nilieleza visa kadhaa vilivyowahi kunitokea katika harakati zangu za kibiashara. Mamia ya wasomaji kutoka pande zote za nchi wameonesha kuguswa mno na yaliyowahi kunitokea.

Wengi wamenitumia ujumbe, mfupi, wameniandikia baruapepe na kunipigia simu nyingi wakinipa pole na ushauri mbalimbali. Hata hivyo ninapenda kuutambua mchango ya msomaji mmoja ambae alinitumia meseji kwa simu. Mchango wake ndio msingi wa makala hii ya leo.
Msomaji huyu ni Mchungaji Ency Mwalukasa wa Dar es Salaam. Mch. Mwalukasa anasema, “Halo kaka ALBERT! Nimefurahia sana shuhuda za mapito katika biashara zako. Hata kwenye huduma ya MUNGU mapito ni hivyo hivyo. Nimeguswa nikushirikishe kinga na ulinzi wa mali na fedha zetu: ni kumtolea  Mungu fungu la kumi au zaidi.”

“Kwa kufanya hivi inaleta ulinzi na baraka. Malaki 3:8-12. Mungu ameahidi unapotii ni lazima atende. Au asilimia Fulani ya fedha na mali zako wape wahitaji utazidishiwa na kupokea ulinzi wa mali na fedha zako. Mtu wa Mungu ni lazima upate mafanikio ya kudumu” Mwisho wa kunukuu.

Ninapoendelea na makala haya ninasukumwa kuweka wazi mambo mawili ili nisilete migongano ya kifikra na kimaslahi. Mosi; ninapenda nitangaze maslahi yangu kiimani. Mimi ni mkristo niliyezaliwa mara ya pili. Kwa  hiyo leo ninaandika ulinzi wa biashara zetu kwa mtazamo wa tamaduni na sheria za kibiashara lakini pia kutoka katika Biblia. Pili; si lengo langu kuhubiri katika makala haya; hivyo kama nitarejea mafundisho ya kidini ijulikane kuwa ni nukuu tu za kutusaidia.

Kama alivyosema Mchungaji Ency Mwalukasa ni kweli kuwa mfanyabiashara unatakiwa kutoa fungu la kumi pamoja na sadaka nyingine. Kiimani, utoaji wa sadaka huleta ulinzi wa kiroho katika biashara zako. Ukiacha ulinzi, utoaji wa sadaka huachilia nguvu za uweza wa Kimungu katika fahamu na fikra za mfanyabiashara anaetoa sadaka; kiasi ambacho kunakuwa na mtiririko wa mawazo ya kibiashara (costant flow of business ideas), unakuwa mbunifu na unakuwa na nguvu za kuendelea mbele hata vinapotokea vikwazo kibiashara.



Mimi ni msomi wa masuala ya biashara lakini pia najivunia uzoefu nilionao na ninaoendelea kuupata kwa kufanya biashara kwa vitendo. Hata hivyo; kule madarasani na kwenye vitabu vya biashara kuna jambo eidha linafichwa ama linapuuzwa. Jambo hili ni nafasi ya Mungu katika kumfanikisha mtu kibiashara.

Watu wanapofundishwa masomo ya biashara hawaambiwi kuwa ukitaka kuwa na mafanikio ya kweli ni lazima uanze kuimarika kiroho (spiritual mindset). Mimi kamwe sitaacha kuitaja na kufundisha wazi nafasi ya Mungu katika mafanikio ya watu.
Kwa sababu kama tukiwaficha watu kuhusu Mungu tutakuwa tunajenga mafanikio yasiyo ya kudumu. Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa, “Mtu yeyote anayepata mafanikio ya kifedha ama mali, ikiwa hajaijenga roho yake kwa kuwa na uhusiano mzuri na Mungu; basi mtu huyo ameuchuma msiba”

Pengine changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi ni namna gani ya kutoa hizi sadaka. Mathalani, sadaka ya fungu la kumi ni asilimia kumi ya faida unayoipata katika biashara. Sasa, utajuaje asilimia kumi ya kumtolea Mungu ikiwa haujui unapata faida ya shilingi ngapi kwa wiki, kwa mwezi, au kwa mwaka?

Asilimia kubwa ya wajasiriamali na wafanyabiashara nchini wanaendesha biashara kienyeji na kwa kubahatisha. Wengi hawajui ni faida gani anazalisha kwa wiki, mwezi au mwaka na hili linatokana na kutokuwa na utamaduni imara wa kutunza kumbukumbu.. Jambo hili ni hatari sana linapokuja suala la kumtolea Mungu sadaka; kwa sababu utajikuta eidha unamwibia Mungu au unamuongezea unapotoa sadaka. Ni heri ukamzidishia Mungu kuliko kumwibia!

Binafsi nilijifunza mapema sana uhusiano uliopo kati ya sadaka na mafanikio ya mtu kibiashara. Kitu ambacho kilinitesa kwa muda mrefu sana ilikuwa ni namna ya kujua nimtolee Mungu kiasi gani; kwa sababu biashara nyingi nilikuwa nazifanya kimazoea, kwa kukisia. Nilipokuwa nachanganyikiwa zaidi ni pale inapotokea faida imerudi ‘juu kwa juu’ katika mzunguko na ikaongezea kwenye mtaji.

Unapofika muda wa kutoa sadaka nabaki nimechanganyikiwa maana sielewi mtaji ni kiasi gani na faida ni shilingi ngapi kwa muda gani. Huenda hata mimi nilikuwa mmoja ya watu waliokuwa wanamwibia Mungu sadaka. Lakini kwa sasa nimepata mwarobaini. Nilikuja kubaini kuwa biashara ili zifanikiwe na ukitaka usigombane na Mungu wako kwa “kumdokolea” sadaka; ni vema kuendesha biashara katika mifumo rasmi.

Ndipo nilipoamua kusajili kampuni ambapo biashara zangu zote ninaziendesha kikampuni. Uzuri wa kufanya biashara katika mifumo rasmi ni kwamba; unalazimika kuwa na utaratibu wa uendeshaji biashara, utunzaji wa kimahesabu na mipango ya biashara iliyochambuliwa (business plan). Pale kwenye kampuni huwa ninapata fedha kwa njia mbili. Mosi; ni kupitia mshahara ninaolipwa kila mwezi. Pili ni gawio la faida inayotokana na mchanganuo wa idadi ya hisa ninazomiliki.

Nimetaja habari ya mshahara ninaolipwa kila mwezi. Wengine wanaweza kushangaa kidogo, inakuwaje kampuni ya kwangu halafu tena ninalipwa mshahara? Hapa ndipo ambapo wajasiriamali wengi huwa wanateleza. Unapokuwa na biashara hata kama iwe ndogo kiasi gani, unatakiwa uwe unajilipa mshahara kiwango maalumu na sio kutumia faida ama fedha ya mtaji kadiri unavyojisikia.

Sasa linapokuja suala la sadaka sisumbuki. Katika ule mshahara ninaolipwa (ama uite ninaojilipa) kila mwezi ninatenga fungu la kumi na kumalizana na Mungu. Vile vile inapokuja suala la gawio la faida za hisa, iwe faida itarudi kukuza mtaji ama nitaichukua; ni kwamba kabla ya chochote ninatenga asilimia kumi na ninamalizana na Mungu. Hii nimeona inanisaidia sana na niwe muwazi; ninauona ulinzi wa Mungu katika biashara na mipango yangu mingi.

Ninapoeleza habari za sadaka na mafungu ya kumi mtu anaweza kusema, Huyu Sanga mbona analeta habari za kiroho hapa? Kwa taarifa yako ulinzi wa biashara zetu kwa njia ya sadaka unatajwa hata katika sheria na taratibu za biashara.

Waanzilishi wa sheria na taratibu zote zinazotumika katika biashara duniani pote ni Waingereza. Wao katika sheria hizi wanashauri na kulazimisha kuwa biashara inapozalisha faida; ni vema ikarudisha sehemu ya faida yake kwa jamii inayoizunguka. Faida hii ndio sadaka. Tena mjasiriamali usisubiri mpaka uwe na mamilioni ili kutoa sadaka. Anza na hiyo faida ndogo unayozalisha hata kama ni shilingi mia tano, toa!

Biashara yako inapowasaidia watu kuna mambo mawili yanatokea. Mosi; biashara yako inakaa akilini na mioyoni mwa watu kwa hiyo unaendelea kuwa na wateja waaminifu. Pili; biashara yako inakuwa inaheshimika na jamii unayoisaidia kwa sababu wanajua kuwepo kwa biashara yako ndio kupona kwao hivyo watailinda kwa nguvu zote.

Pamoja na juhudi zetu za utaalamu na kanuni za kuzingatia kibiashara, mjasiriamali usisahau kuwa njia bora ya kulinda biashara zako ni wewe pamoja na biashara yako kumtolea Mungu sadaka, kuwasaidia wahitaji na kupeleka sehemu ya faida kuongeza thamani za maisha ya jamii inayokuzunguka.

Wajasiriamali tunahitaji ushindi
0719 127 901, stepwiseexpert@gmail.com

TAKUKURU NA MAHAKAMA YA UHUJUMU UCHUMI


Markus Mpangala

Na Markus Mpangala
“Katika kesi nyingi za rushwa, zimekuwa zikilalamikiwa sana na wananchi na kwa kuliona hilo mara zote nimekuwa nikimshauri Jaji Mkuu, Othman Chande kuanzisha Mahakama Maalumu za kesi ya rushwa kama ilivyo Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki,”.
Hayo ni maneno ya Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah akizungumza wakati wa Mafunzo ya Walezi na wenyeviti wa klabu za wapinga rushwa jijini Dar es salaam.
Dk. Hoseah ameibua hoja niliyowahi kuwasilisha baada ya mahojiano yangu na Hakimu Ambroce Nkwera, siku chache tu baada ya kuajiriwa kuwa hakimu wilayani ya Mbinga, mkoani Ruvuma.
Mahojiano hayo yalitokana na kuibuka wka tuhuma za rushwa wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini uliowasilishwa bungeni  kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, na kutawaliwa na tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge katika Kamati ya Bunge  ya  Nishati na Madini.
Katika mjadala huo Wizara ya Nishati na Madini na Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi, walifichua mambo mbalimbali ya ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya wabunge kupitia kamati zao, ambayo baadaye yalishindwa kuthibitishwa kutokana na Kamati ya Ngwilizi kuwasafisha wabunge waliotuhumiwa.
Hakimu Ambroce  Nkwera ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, alieleza kwa kina juu ya mchakato wa kuanzisha Mahakama maalumu ya rushwa ambayo aliita Mahakama ya Wahujumu uchumi. Nini alichosema wakati huo na ambacho kinasadifu tamko la Dk. Hoseah,  fuatilia mahojiano haya;-
SWALI: Ndugu Ambroce Nkwera, shutuma za kupokea rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge, bila shaka umezisikia. Kuna Kamati za Bunge zinalalamikiwa kwa vitendo vya rushwa, mfano Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC). Nini tafsiri yako katika suala hilo?
JIBU: Nimesoma taarifa nyingi kuhusiana na shutuma hizo. Kimsingi hizo ni shutuma, kwahiyo kuna mamlaka zinazohusika na ufuatiliaji wake. Mathalani Spika wa Bunge, Anna Makinda amewasilisha suala hilo mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi.
Spika ametumia madaraka ya kupeleka suala hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1). Sasa kumbuka ile ni kanuni ya 53(2) na 58(3)(f) inasema malalamiko juu ya vitendo vya rushwa kwa baadhi ya Kamati za Bunge na wabunge, lazima Spika atumie kanuni hizo.
Siyo hapo tu, Spika wa Bunge anayo madaraka ya kuvunja kamati inayotuhumiwa ama kama zipo nyingi zinazotuhumiwa zitavunjwa. Sikushangaa Spika alipoiagiza Kamati ya Ngwilizi kutengeneza code of ethics ili mbunge yeyote atakayetuhumiwa, hatua dhidi yake zichukuliwe.
Sasa, tunachoona ni matumizi ya ile kanuni 113(3) inayompa madaraka Spika kuvunja kamati zinazolalamikiwa kwa vitendo vya rushwa. Hapo Kamati ya Nishati na Madini ikavunjwa. Kwahiyo uchunguzi unaofanywa na Kamati ya Ngwilizi, utatupa majibu.
SWALI:Umeeleza kanuni za Bunge zilitumika kuvunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Nini mtazamo wako kwa ujumla katika suala la vitendo vya rushwa bungeni?
JIBU: Mimi, nimeshtushwa kama watanzania wazalendo wengine. Napata wasiwasi sana na hii nchi mwisho wake itakuwaje, na siyo mwisho tu bali hali ya maisha itakuwaje kwa watanzania.
Hivyo ni hofu ya kila mmoja, ingawa ni kipindi cha mpito, ninayo hofu eneo la muhimili wa pili wa dola limeingiliwa na ubadhirifu. Lazima tutafute njia za kukomesha hilo. Na hilo lisiwe interim decision maana athari zinaweza kushamiri kwa wananchi.
SWALI: Umedokeza suala la interim decision, unasema iepukwe, nini unachokusudia au unachomaanisha hapo?
JIBU: Ok! Nazungumzia uamuzi wa mpito. Hii interim decision ni mbaya, usifikiri kutafuta suluhisho na  kukomesha ubadhirifu kwa tafsiri ya kushutumiwa baadhi ya wabunge, hata sekta zote wapo na wanatakiwa kutafsiriwa ni wala rushwa. Suluhisho la muda mfupi hatuwezi kufanikiwa hata kidogo kwa suala la rushwa.

SWALI: Unadhani wananchi wanachukulia uzito wowote katika suala la tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge?

JIBU:Huu sio wakati wa mwaka 1947. Uzito upo siyo lazima wananchi wapayuke, kwamba mtu afike barabarani aanze kusema nakerwa na rushwa ama inakera wabunge kutuhumiwakwa  vitendo vya rushwa.
Matokeo yake unaweza kuyaona katika uchaguzi, nadhani patakuwa na mabadiliko bila kujali chama. Natoka kusoma taarifa zao hapa, nashauri kwa kurudia hii sio interim decision, tuwe au tuanzishe Mahakama za wahujumu uchumi, mimi nadhani zitakuwa na msaada sana katika haya mambo ya rushwa.

SWALI: Kwanini Mahakama ya uhujumu uchumi. Muundo wa Mahakama hiyo utakuwaje, sababu tunazo mahakama zinazofanya kazi vizuri tu?

JIBU:Katika Mahakama Kuu kuna kitengo au division ya biashara, division ya kazi na wangeanzisha kitengo cha ku-deal (kushughulikia) na economic embezzlement, kwenye nchi nyingine zipo mahakama hizo, zimefanikiwa sana. Na hapa hilo linawezekana tukiwa na dhamira ya kukomesha rushwa nchini. Dhamira tu ndio msingi.

SWALI: Hebu, kabla hujaendelea,  ina maana katika mahakama za kawaida, hatuwezi kuwafungulia mashtaka hao unaosema wahujumu uchumi?

JIBU: Kama nilivyosema mwanzo, suala la mgawanyo tu hapa, kama ipo division ya kazi na biashara, basi nayo ujuhumu uchumi iwe division peke yake. Sasa, mahakama za kawaida siyo vibaya ila tupanue mitazamo yetu. Mimi naona wahujumu wana uwezekano wa kushinda kesi mahakama za kawaida.
Kwanza sheria yenyewe haiweki nguvu au adhabu kali kwa tafsiri zangu za uhujumu uchumi. Mifano ipo, na mimi natafsiri ni uhujumu uchumi, kuna mifano ya watu ambao wamefungwa jela kwa miaka michache kutokana na sheria zetu, hasa  kwenye mahakama za kawaida.

SWALI: Kwahiyo, hapa tatizo ni kushinda kesi na kiwango cha adhabu tu, na pia hizo sheria haziwezi kuboreshwa na kutumika mahakama za kawaida?

JIBU: Naongelea sheria inayowahukumu watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na adhabu zake. Mahakama za kawaida naona wengi wanapata adhabu ndogo. Ingawa ni adhabu lakini bado tunahitaji kukomesha rushwa, na maana ya kukomesha ni pamoja na kutoa adhabu kali, hivyo  na sheria za ku-deal  na wahujumu zipatiwe mahakama yake. Hata zile sheria za zamani alizotumia Sokoine (Waziri Mkuu, Edward Sokoine), tutumie na kuongeza kulingana na mazingira ya sasa na huko mbele, tutengeneze sheria na mahakama za kukomesha wala rushwa, wanazorotesha nchi.
SWALI: Unasema sheria za kushughulikia  wahujumu uchumi zipo. Ni sheria gani hizo?
JIBU: Kuna hii Economic and Organized Crime Act, lakini sijui kama hasa wanatumia, kwani ni sheria ya zamani sana. Pia hii nyingine ya Penal Code inaweza kutumika. Lakinitukisema economic and organized crime Act, inabidi ujue sheria hiyo ilikuwa inatumika sana wakati wa Rais Julius Nyerere, ni hiyo iliyotumiwa pia na WaziriMkuu, Edward  Sokoine kuwashika walanguzi na wahujumu uchumi.Hivyo utaona kuwa tuanzie pale alipoishia mzee Sokoine.
Lakini Penal Code wahujumu wanakuwa wanapelekwa tu katika mahakama za kawaida. Mimi naona haitoshi kabisa kukomesha suala hili, napendekeza lazima tufanye jambo dhidi ya wahujumu, nasisitiza lazima tumrejee Sokoine kutengeneza njia mwafaka kukomesha wala rushwa.
Spika wa Bunge Anna Makinda
SWALI: Lakini, unadhani tunao Majaji wa kutosha kuhudumia Mahakama ya uhujumu uchumi au tuanze mchakato mpya wa mafunzo mapya yao?
JIBU: Siyo kweli kwamba Majaji hawatoshi, labda tufahamishane, majaji wapo, nahawa wana weledi tofauti kwenye taaluma hii ya sheria. Kwahiyo, wale majaji wenye weledi wa mambo ya uchumi watapewa eneo hilo, na jukumu lao litakuwa mahakama ya wahujumu uchumi.
Ni mpango wa kimkakati na kiutendaji zaidi, na hapa tusizungumzie vikwazo kwamba hatuna fedha, bali tujikamue kadiri tuwezavyo. Mfano, serikali yetu imeonyesha pesa zipo za kutosha linapokuja suala nyeti, angalia kama kwenye Tume ya kukusanya maoni ya wanachi kupata Katiba Mpya inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, wana nyenzo za uhakika, dhamira imo serikalini, labda tutapata katiba mpya.
Lakini siamini kama suala la mahakama hii itatufanya tushindwe sababu ya fedha. Tuweke dhamira tu, yote yanawezekana. Zipo nchi zinawashughulikia ipasavyo wahujumu uchumi, nazo zilikuwa na dhamira mbali ya majaji wachache kama tatizo lilikuwepo au la.
Mfano tufanye comparison (tulinganishe) hapa na nchi za China, Thailand, Marekani, Uingereza au Scotland tuone wanawafanya nini wahujumu uchumi ili nasi tuwe na mwarobaini wa kukomeshwa rushwa. Angalia, mfano kule Thailand ulimuona Thaksin Shinewatra, alikuwa waziri mkuu wa nchi ile. Lakini akituhumiwa na kufunguliwa mashtaka ya vitendo vya rushwa.
Hapa lazima tuelewe hawa PCCB ya bwana Edward Hosea (Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini) ndio wanajua suala gani au kesi gani ni ya aina ya uhujumu. Yupo DCI, Manumba, hivyo wale wengine kule kwa DPP anakuwa tayari amepelekewa kesi inayopaswa kwenda Mahakama ya uhujumu uchumi, ikiwepo.
Sio hilo tu, hapa tunataka pia watu werevu, well trained katika PCCB ili tusiharibu mpango wenyewe. Lazima tuwe na mahakama hizo kila kanda ya nchi yetu. Uhujumu ni janga baya sana kwa nchi, haya yanayotokea ni kilelezo cha jamii. Tuchukue hatua, hatuchachelewa.