February 26, 2013

NAFASI YA KAZI KWA VIJANA WA KITANZANIA. CHANGAMKIA FURSA HII SASA



ANESA COMPANY LIMITED
P.O.BOX 1295, IRINGA. Mobile +255 719 127 901

TANGAZO LA KAZI
Anesa Co.,Ltd ni kampuni ya kitanzania iliyosajiliwa na BRELA na kisha kupewa leseni ya kuendesha biashara mbalimbali kwenye maeneo ya Kilimo, Ufugaji, Majengo na Nyinginezo. Kampuni ina masikani yake mkoani Iringa huku ikiendesha shughuli zake katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Dodoma. Kwa mwaka 2013 kampuni imepanga kujitanua; hivyo inahitaji wafanyakazi wapya, vijana wenye ari, wabunifu, waaminifu na wenye weledi wa hali ya juu; ili kufanikisha mikakati ya kuitoa kampuni kutoka ngazi moja kwenda nyingine. Kampuni inayofuraha kutangaza nafasi za kazi katika maeneo yafuatayo:

A)MENEJA MAUZO/MASOKO.
SIFA ZA MWOMBAJI
1.                  Awe na elimu ya cheti, diploma au digrii katika masomo ya biashara. Wale waliodurufu (specialize)kozi za masoko, ugavi au utawala watapewa kipaumbele.
2.                  Awe na umri wa miaka kuanzia 25-35
3.                  Awe ni mbunifu, mpana katika uelewa wa masuala ya biashara, awe ni mchapa kazi na anayeweza kujisimamia. Mwombaji ajiridhishe kuwa ni mwaminifu na anayeweza kutumia vichache na kuzalisha vingi.
4.                  Awe na ufahamu wa kutosha kuhusu taratibu za uendeshaji wa makampuni.

B) MUHASIBU
SIFA ZA MWOMBAJI
1                    Awe na elimu ya cheti, diploma au digrii katika masomo ya uhasibu.
2                    Awe na umri wa miaka 21-35
3                    Awe na ufahamu wa kutosha kuhusu taratibu, kanuni na sheria za makampuni
4                    Awe na uzoefu ama uelewa wa kinadharia wa kukokotoa mizania ya mirejesho ya kodi za makampuni kwa mujibu wa kanuni na taratibu za TRA.
5                    Awe ni mbunifu, mwaminifu, anayejituma na anayeweza kujisimamia mwenyewe.

C) KATIBU MAHSUSI (OFFICE SECRETARY)
SIFA ZA MWOMBAJI:
1.                  Awe ni wa jinsia ya kike
2.                  Awe na elimu ya kuanzia kidato cha nne na awe na cheti cha mafunzo ya kompyuta au ya ukatibu mahsusi (secretarial certficate)
3.                  Awe na umri wa miaka 22-29
4.                  Awe na uzoefu usiopungua miezi sita katika shughuli zinazofanana ama kukaribiana na nafasi hii.
5.                  Awe ni mchangamfu, mkarimu, mwaminifu na anayejituma


D)  DEREVA
SIFA ZA MWOMBAJI
1.                  Awe na umri miaka 25-40
2.                  Awe na leseni class E na kuendelea
3.                  Awe na uzoefu wa kuendesha magari ya mizigo kwa miaka isiyopungua mitatu
4.                  Awe mwaminifu na anayeweza kujisimamaia

MISHARA NA MARUPURUPU.
Kampuni ina sera nzuri ambazo zinampa nafsi mfanyakazi kufurahia mazingira ya kazi huku akilipwa mshahara bora na stahiki zinazopendeza.

JINSI YA KUTUMA MAOMBI.
1.                  Waombaji wote watume barua za maombi zikiwa zimeambatanishwa na maelezo yao (CV), vivuli vya vyeti pamoja na picha ndogo moja (passport size). Maombi hayo yatumwe kwa “Meneja Utawala” kupitia baruapepe: anesagroup@yahoo.com
2.                  Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 10/Machi/2013, saa 12 jioni.
3.                  Wale watakaopita katika mchujo wa awali ndio watakaoitwa kwenye usaili.
4.                  Usaili utafanyika Isimila Hotel, Iringa mjini katika tarehe ambayo itajulishwa kwa wale watakaoitwa kwenye usaili.

IMETOLEWA NA:
MENEJA UTAWALA
ANESA CO.,LTD,
25/FEBRUARI/2013

UCHUMI NA BIASHARA: WARAKA WA UCHUMI KWA WAFANYAKAZI


Na Albert Sanga, Iringa

Leo nina neno na wafanyakazi waliopo katika sekta mbalimbali; za umma na za binafsi. Nimeamua kuandika waraka huu wa uchumi leo kwenda kwa wafanyakazi kutokana na sababu kuu tatu. Mosi, uwepo wa mbinyo wa kuongezeka kwa gharama za maisha ikilinganisha na vipato halisi vya wafanyakazi.

Pili, kuwepo kwa uwezekano wa wafanyakazi kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali. Tatu, hata kama wafanyakazi wasipoona umuhimu wala ulazima wa kuongeza vipato vyao; bado wafanyakazi ni moja ya kundi linaloweza kuliokoa taifa hili kwa kutengeneza maelfu ya ajira ikiwa wataamua kufanya hivyo.
Wafanyakazi wengi (japo yaweza kuwa sio wote) watakubaliana na mimi ya kwamba mishahara na marupurupu yanayotolewa ajirani hayatoshelezi mahitaji ya kimaisha. Gharama za maisha zimekua juu, mfumuko wa bei unazidi kutikisa nchi na imefika mahali watu hawaelewi waishi vipi.

Upandaji wa maisha hauendani na ongezeko la mshahara, malengo ya kimaisha sio tu kwamba hayatimii; lakini hayawezi kutimia kama mtu utaendelea kutegemea namna ile ile ya kipato-mshahara na marupurupu.

Yapo mambo mawili ningependa kila mfanyakazi afahamu. Cha kwanza ni kuwa; mabadiliko tunayoshuhudia nchini, ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha na mfumuko wa bei ni mabadiliko ambayo yanaukumba ulimwengu mzima na sio Tanzania pekee.

Kwa maana hiyo, utatuzi wa suala hili ni kuachana na kufikiria kienyeji (local thinking) badala yake watu tufikirie kiupana (global thinking). Sambamba na hilo ni vema mtu mmoja mmoja kuwa na mtazamo chanya kuhusu ramani ya maisha kwa ujumla.

Cha pili ni kuwa; siasa haziwezi kuamua hatma yako isipokua umeziruhusu kufanya hivyo. Labda niiseme falsafa yangu kuhusu siasa ndipo naweza kueleweka zaidi; “Politics has nothing to do with my destiny”. Maana ya falsafa yangu hii ni kwamba siasa zinaweza kunizuia kwa muda kufika ninakotaka, lakini haziwezi kunizuia milele.

Nikisema hivi simaanishi ninaukana umuhimu wa siasa katika ustawi wa kiuchumi kwa wafanyakazi na mtu mmoja mmoja. Isipokuwa ninachotaka turekebishe ni ile hali ya kudhani siasa zitafanya kila kitu maishani mwetu.
Nimeyataja mambo hayo mawili ili kusafisha njia ya kuelekea kwenye fikra pevu kuhusu uhuru wa kiuchumi kwa wafanyakazi. Kila mfanyakazi ni vema akafahamu kuwa usalama wa maisha yake hauwezi kuletwa na ongezeko la mshahara. Bila kulitambua na kulikubali hili tunaweza kuwa shidani; kwa sababu mara nyingi mtaji wa wanasiasa kupatia kura huwa ni ongezeko la mishahara!
 

Wanauchumi tunafahamu vizuri mchezo unaotokea pindi serikali inapoongeza mishahara, pasipo kuongeza tija ya uzalishaji. Iko hivi, unapoongeza mzunguko wa fedha, (unbalanced injection of money into circulation) mfano kwa kuongeza mishahara kinyume na mizania ya kiuchumi; ikiwa hakuna tija katika uzalishaji basi unakuwa ukiibua mfumuko wa bei (inflation).

Kuanzia mataifa madogo mpaka makubwa hadi nikiandika makala hii yanasumbuliwa na kusuasua kwa uchumi. Wanapojaribu kushusha ‘inflation’ wanajikuta wametengeneza uhaba mkubwa wa ajira, wanapojaribu kumimina ajira mitaani wanajikuta mfumuko wa bei unainua pembe zake.

Hata hivyo nikiri kuwa inawezekana kuleta msawazo wa ujazo wa fedha na mfumuko wa bei; lakini kufanikiwa kwake kunategemea visababishi vingi mno (simulation factors) ambavyo kutokana na utamaduni wa nchi yetu kiuchumi; sio rahisi kuvifanikisha vyote. Yote katika yote; hizo ni lugha na misamiati ya wachumi; lakini ni nini maana yake kwa mfanyakazi?

Hayo juu yanatupa kutambua kwamba kumbe usalama wa maisha ya mfanyakazi utapatikana kwa kujifunza mbinu za kuutumia mshahara kidogo anaoupata kuzalisha mifumo, bidhaa na huduma zitakazomwongezea tija. Hili linaweza kufanikishwa kwa mfanyakazi kuanzisha miradi midogo midogo nyumbani au mikubwa mahali pengine, kufungua biashara na hata kutumia vipawa alivyonavyo nje ya ajira yake kuzalisha fedha.

Nianze sasa na yale mambo matatu yaliyonisukuma kuwaandikia waraka huu, nikianza na lile la kwanza. Udogo wa mishahara isiyoendana na gharama za maisha unazidi kuleta msiba katika nchi yetu.

Hebu fikiria, mfanyakazi analipwa mshahara mdogo ambao akishalipa kodi ya nyumba, akanunua chakula, akafanya matumizi mengine ya msingi; kila mwisho wa mwezi anajikuta ana madeni. Tangu Januari hadi Desemba mfanyakazi huyu anakua ni mtu sio tu wa madeni ila ni madeni yanayoongezeka. Hana tumaini la kujikwamua kesho wala keshokutwa.

Kutokana na hali hii tumezalisha wafanyakazi wengi ambao wajibu wao wameugeuza kama hisani makazini, ndio hawa ambao hawawezi kukuhudumia mpaka umewapa chochote. Wengine wameendelea ‘ku-survive’ kwa kuunga unga, wanaishi kwa mizinga kila wakati na kila sehemu. Huwezi kuwalaumu; wanalazimishwa na mazingira yanayowakabili.

Nchi sasa hivi imejipatia ‘mamilionea’ bandia ambao wamepata fedha zao kwa njia ya kughushi mikataba, kupewa hongo, kupokea rushwa kubwa na ndogo pamoja na wizi wanaoufanya makazini. Wakishapata fedha hizo ndipo wanajenga majengo makubwa makubwa, wananunua magari ya kifahari na kuishi maisha ya kifalme. Wengi wetu tumeingia katika mtego wa kuwasifu watu wa namna hii ya kwamba ni ‘wajanja’, ‘watafutaji’, ‘wenye akili’, ‘matajiri’ na majina mengine yenye sifa.

Kuna atahri mbili kubwa mfanyakazi unaposhawishika kupata mafanikio kwa njia zisizo halali. Mosi ni kwamba unaliangamiza taifa na  kuwadhulumu wengine. Pili, unaharibu utu wako wa ndani na kupoteza amani ya rohoni. Iko hivi; kikawaida uovu humrudia muovu, wema humrudia mwema.

Ukijikusanyia mali ama fedha kwa njia ya wizi, rushwa, hongo ama ujanja-ujanja; utajikuta unaishi maisha yasiyokua na amani kunakopelekea kukosekana kwa furaha maishani mwako. Kikawaida mtu unapaswa uwe na mafanikio yanayoleta utulivu katika roho na nafsi yako; kinyume na hapo haina maana ya kuwa na mafanikio.

Najua wapo watu mnaowafahamu ambao wametajirika kwa njia za mikato; nanyi mnaona kama wanaishi maisha mazuri yenye  furaha; ukweli wanaujua wenyewe kama ambavyo tunathibitishiwa na wataalamu wa ukuaji wa kiroho, saikolojia na maumbile; ya kwamba uovu humrudia mwovu.

Unaweza kutumia rushwa kutajirika lakini malipo ukayapata kupitia mgogoro wa ndoa na kudharaulika; ndio maana huwa sishangai ninapoona watu wengi wakitafuta furaha kupitia ngono na ulevi; wengi wao njia walizotumia kupata mafanikio waliyonayo zimewapa ‘garantii’ ya kutokua na furaha maisha yao yote!

Kwa nini ninasema haya yote? Ni kwa sababu ninataka tuangalie upande wa pili ya kwamba tupende ama tusipende ni lazima wafanyakazi wote wafanikiwe ili kukabiliana na yanayowakabili maishani; lakini mnafanikiwaje? Ndipo hapo ambapo ninataka tuyaone maisha katika mwanga wa ujasiriamali

Kila mfanyakazi anastahili kuishi maisha ya ushindi wa kiuchumi!
stepwiseexpert@gmail.com;    0719 127 901

February 20, 2013

FRESH FARM WAMEREJEA TENA KATIKA UWEKEZAJI WA MITI YA MBAO NA NGUZO


Kampuni ya Anesa Co.,Ltd kupitia biashara yake tanzu ya Fresh Farms(T); kwa kushirikiana na kikundi cha “Rudisha Uumbaji wa Mungu kwa Kupanda Miti (RUMM)-Kilolo;” tukiwa mkoani Iringa, tumezindua programu maalumu iliyolenga kuwawezesha watanzania wengi kuwekeza na kumiliki mashamba ya miti ya mbao na nguzo kwa urahisi kabisa.

1.  Progamu hii inaitwa “GREEN THE WORLD and BECOME RICH” ambapo tunauza mashamba yenye miti (miti pamoja na ardhi) kwa utaratibu wa mtu kulipa kidogo kidogo kwa kadiri ya kipato chake. Kiwango cha chini cha kununua ni ekari tano, ambapo utatakiwa kulipa walau asilimia 50% ya bei yote; kisha fedha inayobaki utaendelea kuilipa kwa awamu kwa kadiri utakavyokubaliana na kampuni

2.  Tupo Iringa mjini na Kilolo (kijiji cha Mwatasi), na mashamba yapo maeneo mbalimbali katika wilaya za Mufindi na Kilolo. Yapo mashamba yenye miti kuanzia ya mwaka mmoja hadi minne, na bei zake ni kuanzia tsh. 700,000(laki saba) hadi 2,000,000 (milioni mbili) kutegemeana na umri wa miti husika. Bei zote zinajumuisha (miti pamoja na ardhi)

3.  Miti ya mbao inachukua miaka kati ya 7 hadi 10 tangu kupandwa hadi kuvunwa. Wastani wa faida unayoweza kupata kwa ekari moja ya miti iliyokomaa ni tsh milioni tisa hadi kumi na tano (kama ungekuwa unauza leo). Gharama ya kuhudumia ekari moja kwa mwaka haizidi laki mbili. NOTE KWA WALE WAGENI KUHUSU KILIMO HIKI CHA MITI: Pamoja na taarifa hizi, kampuni inahamasisha watu ambao ni wageni kabisa na taarifa zihusuzo miti; kutafuta taarifa zaidi na zaidi kutoka vyanzo mbalimbali kuhusu kilimo-biashara hiki; ili kujiridhisha kabla ya kufanya maamuzi ya kiuwekezaji.

4.  Mnunuzi akishafika na kuyatazama mashamba (au kama anayafahamu mazingira yalipo mashamba); akishajiridhisha, atasaini mkataba wa makubaliano ya kimalipo kati yake na kampuni, kisha ataanza malipo mara moja. Baada ya kukamilisha malipo yake, utafanyika utaratibu wa kupata hati za kimila/mikataba ya kiumiliki kutoka mamlaka ya baraza la ardhi la kata/kijiji kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa ardhi ya vijiji ya mwaka 1999.

5.  Fresh Farms(T) tukiwa na falsafa ya “Greening the world and Feeding People”; lengo letu ni kuhakikisha tunawasaidia mamia ya watanzania kutumia fursa ya uboreshaji mazingira; kwa kuwekeza vitega uchumi vya mashamba vinavyowahakikishia kipato kikubwa sasa na siku za usoni.

6   Kampuni itaendelea kutoa usaidizi wa uangalizi na utunzaji wa mashamba yote yanayonunuliwa kutoka kwetu kwa utaratibu rahisi na nafuu kabisa. Nia yetu ni kuona kuwa kila anayewekeza; avune faida ya uwekezaji wake. Hivyo, hauhitaji kuhofu juu ya usalama wa shamba utakalonunua, popote utakapokuwepo utajihakikishia kuwa “investment” yako inafanyiwa juhudi kubwa kuhakikisha inakua.

7.  Programu na ofa hii ni ya muda maalumu, imeanza tarehe 15, Februari, 2013 na itamalizika, Aprili, 14, 2013. Programu hii inaweza kukoma kabla ya tarehe ya ukomo, ikiwa ekari zilizotengwa zitaisha mapema. Hivyo kwa yeyote anayehitaji tunashauri kuwasiliana nasi mapema.

Mawasiliano:
Iringa:                   Mkurugenzi, Albert Sanga (0719 127 901, 0766 742 414), albertnyaluke@yahoo.com

Dar es Salaam:     Meneja Masoko, Markus Mpangala (0764936655), mwanazuoni27@gmail.com