March 13, 2013

UCHUMI NA BIASHARA: "UCHUMI" NDIO LUGHA YA AFRIKA MASHARIKI

Albert Sanga, Iringa

Wiki mbili zilizopita nimekuwa nikiandika waraka wa kiuchumi kwa wafanyakazi. Kwa ujumla wake waraka huo utakuwa ni mrefu hadi sehemu ya kumi. Kutokana na urefu huo nimejipangia kutouleta kwa mfululizo wa wiki zinazofuatana. Badala yake nitakuwa nikiuleta kwa wiki tofauti tofauti mpaka uishapo mwaka huu.

Leo ninapenda tuperuzi nafasi ya uelewa wetu sisi watanzania linapokuja suala la uchumi katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Unapotaja Afrika Mashariki ni kwamba kuna mambo ya msingi ambayo yanaushikilia uhusiano huu. Pamoja na mambo mengine nguzo kuu ya uwepo wa jumuiya hii ni suala la uchumi. Ndio maana tunaongelea soko la pamoja, kuunganisha sarafu zetu, kusafiri kwa mitaji pamoja na rasilimali watu.

Mambo mengine yanayojadiliwa na kushughulikiwa katika ushirikiano huu yanasaidia tu kuboresha lengo kuu la msingi; ambalo ni kuboresha uchumi wa ukanda huu. Kwa tafsiri ya mkato ni kuwa lugha ya Afrika Mashariki ni uchumi. Ili kunufaika na jumuiya hii ni lazima kuijua lugha hii, ni lazima kuyajua matendo ya kiuchumi, ni lazima kuelewa mwenendo wa kiuchumi na ni lazima kutambua nafasi ya mtu mmoja mmoja katika uchumi.

Wakinga tuna msemo mmoja usemao, “Kama wewe sio mchawi, hakikisha unamfahamu mganga mzuri”. Si lazima uwe mjuzi ama mtaalamu wa mambo ya uchumi na lugha za uchumi wa darasani ili kuijua lugha ya Afrika Mashariki; bali unaweza kujifunza na kujizoesha kutoka kwa ‘waganga’(wataalamu) na baadae nawe ukawa ‘mchawi’ (mtumiaji).

Je, watanzania tunaijua kwa kiasi gani lugha inayotumika Afrika Mashariki? Je, tunaelewa maana na matendo ya kufanya tunaposikia viashiria vya masoko ya hisa, masoko ya mitaji, sarafu ya pamoja, ushirikiano wa kodi na ushuru au tunapoambiwa mtiririko wa rasilimali watu? Kwa bahati mbaya sana ni kuwa kutojua lugha hizi hazitoi msamaha wa kuhurumiwa linapokuja suala la utekaji wa fursa zilizopo kwenye jumuiya hii.

Hebu tuangalie baadhi ya mifano michache ya lugha ya Afrika Mashariki. Unaposikia masoko ya mitaji na hisa kichwani kwako ni lazima kuje maneno kama DSE (Dar es Salaam Stock Exchange) , USE (Uganda Stock Exchange) na NSE (Nairobi Securities Exchange). Haya ni masoko ambayo kunatokea ununuzi wa hisa na ubadilishanaji wa mitaji pale.

Hapo kuna makampuni ambayo yanapeleka sehemu yake kuwa miliki ya umma hivyo unaweza kununua ama kuuza sehemu za makampuni hayo. Kujua kuhusu DSE, NSE, na USE hakuhitaji mpaka uwe unamiliki hisa ama mtaji pale isipokua mwenendo wake unaathiri sana uchumi wa eneo hili na hivyo kuathiri ustawi wako binafsi kiuchumi.

Nikisema habari za hisa na mitaji mtu anaweza kudhani ninaongelea masuala ya kitaalamu sana. Kumbuka kua ninaongelea lugha ya Afrika Mashariki. Namna makampuni yanavyojiandikisha na kuuza mitaji kwenye masoko ya hisa na mitaji kunaonesha mtiririko na mwelekeo wa mitaji katika ukanda mzima.

Nasi tunajua kua ulipo mzoga ndipo wakutanikapo tai. Tai wanajuaje kua sehemu Fulani kuna mzoga? Jibu ni rahisi, wanatumia harufu kutambua. Je, unajuaje kua Uganda ama Rwanda kuna fursa za kuwekeza?

Ni kwa kuangalia mwenendo wa mitaji na hisa kama moja ya kiashiria kati ya vingi vilivyopo. Ubaya ni kwamba hata kama wewe usipoisikiliza harufu ya “mzoga wa uwekezaji” wenzako kutoka nchi zingine za Jumuiya wataisikiliza harufu iliyopo hapa Tanzania nao watakusanyika.

Ninapoongelea habari za DSE, USE na NSE naelewa kuwa si rahisi sana kwa wengi kuelewa fursa zilizopo ndani yake pengine kutokana na historia ya uchumi na mazoea yetu. Wenzetu Kenye NSE ilianza (japo sio rasmi) mwaka 1954 wakati sisi DSE ilianza mwaka 1996.

Wanzetu wana uzoefu mkubwa na lugha hii wameizoea kwa kiasi kikubwa. Pale NSE makampuni yaliyojiandikisha ni zaidi ya 50 wakati hapa kwetu DSE kuna makampuni pungufu ya 20 tena mengine yakiwa ni yale yale ya kule Kenya (Cross listing).

Kwa upande wa Uganda hawana tofauti na sisi kwa maana ya kuanza, kwa ni USE ilianza 1997 lakini spidi yao ya kuijua lugha hii ni kubwa mno. Mwaka 2010 USE ilikua ni kinara wa masoko yote ya hisa Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kutumia kipimo cha ALSI (All Shares Index) ikiwa na mrejesho wa faida ya asilimia 74% kwa hisa zinazonunuliwa na kuuzwa.

Sina lengo la kukupitisha porini katika takwimu za kitaalamu lakini kuna kitu nataka tujifunze; Kenya walitangulia miaka mingi, Uganda ni wapya kama sisi lakini wanajifunza kwa kasi ya jabu. Wenzetu walishatangulia na wengine wanakimbia lakini sisi tunazinduka polepole mno.

Nikiri wazi kuwa mambo kama haya ya hisa na mitaji kiasili yaliibuka kutokana na ubepari, lakini kwa kua tumeamua “kuchanganyika” hatuna ujanja zaidi ya kuungana nao. Kumbuka kua, “Kama wewe sio mchawi hakikisha unawajua waganga wazuri”, hatuna ujanja inatakiwa tujifunze na kuizoelea lugha hii ili tuweze kuelewana na wenzetu wa hapa ‘Jumuiyani’

Katika robo ya mwaka jana makampuni mengi ya umma na binafsi katika nchi zote tano za Afrika Mashariki yameendelea kutoa ripoti zao za kifedha na kiutendaji kwa mwaka ulioishia Desemba, 2012. Hapa napo tunaweza kuitathmini hali yetu tuliyonayo katika lugha ya Afrika Mashariki kwa kuangalia namna tunavyozipokea ripoti hizo.

Nianze na namna jirani zetu Kenya wanavyozipokea ripoti hizo. Wakati makampuni 20 makubwa (yaliyopo kwenye 20 Shares Index) yakiachia ripoti zao nchini Kenya; kulikua na  gumzo mitaani kila mmoja akihaha kuzifuatilia, kuzisoma na kuzitafsiri. Wanahisa na wasio wanahisa wanataka kujua kampuni gani imefanya vipi, ipi imeizidi ipi, ipi ina fursa na gawio zuri kwa kuwekeza, ipi ina mikakati gani ya muda ujao na mengine mengi.

Gazeti moja la nchini Kenye lilipiga picha inayoonesha watoto wa sekondari katika mji wa Naivasha wakisoma ripoti ya mojawapo ya benki za biashara nchini Kenya. Walipoulizwa watoto hao mmoja wao alijibu hivi, “Mama ana hisa kwenye benki hii nataka nijue mwenendo wake”. Hapo ni Kenya!hadi watoto wa shule za sekondari wanaongea lugha ya Afrika Mashariki!

Hali ni tete kwa Tanzania kwa sababu ripoti za makampuni ya ndani ama ya wawekezaji huwa hazipokelewi kwa hamasa yeyote. Kwanza ni wachache ambao wanafuatilia ripoti hizo na achilia mbali uwezo wa kutafsiri maana na athari za ripoti hizo kwa Afrika Mashariki na watu wake.

Kule Rwanda na Burundi wenzetu ndio kwanza wanajenga upya nchi zao; hivyo sio rahisi sana kutoa hitimisho la moja kwa moja kuhusu hisia zao katika lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; lakini kiu yao ya kuinuka kiuchumi na kijamii inaonesha namna ambavyo wanaweza kutupita.

Unaposoma ripoti za makampuni haya (Financial Statements) kuna ishara zinatoa ikiwemo, “Nenda katafute ajira sehemu fulani”, “Nenda kawekeze kitu fulani mahali fulani”, “Ondoka mahali fulani kwa sababu pameharibika”. nakadhalika. Kwa kutozijua lugha hizi tunabaki tumeduwaa tusijue cha kufanya wala kwa kuelekea. Kwa kua wenzetu wanaelewa lugha na matendo ya Ki-Afrika Mashariki ni rahisi na itaendelea kuwawea rahisi kunufaika na lugha hii.

Tatizo letu watanzania wengi tunatumia malalamishi kama silaha ya kujiokoa na hatari za Afrika Mashariki. Juhudi zetu katika kuteka fursa za jumuiya hii zimeota matege na tumekua na mtazamo mdogo mno kuhusu mambo tunayotakiwa kufanya.

Kwa mfano; kitendo cha kukazana kujifunza Kiingereza ama kukazana kununua ardhi kwa ajili ya fursa za Afrika Mashariki sio kibaya lakini ni mtazamo mdogo sana. Tukiijua lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; tutaona na kuoneshwa mambo mengi sana yatupasayo ndani ya Jumuiya hii.

Kwa leo nikomee hapa, lakini natarajia kuendelea na chambuzi mbalimbali kuhusu biashara, ujasiriamali na uchumi katika mtazamo wa ki-Afrika Mashariki huko mbeleni.

Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi Afrika Mashariki!



March 11, 2013

MAONI YANGU KATIKA MIJADALA YA UHURU KENYATTA VS RAILA ODINGA, SHUKRANI KWA BEN SAANANE KUIBUA HOJA MUHIMU NA NYETI


Nakiri moja ya upumbavu mkubwa ni Barrack Obama kuwa kikaragosi kwake na serikali. Mwanzoni kupitia Hilary Clinton walisema wakenya wasichague watuhumiwa wa ICC yaani Kenyatta na Ruto. Baadaye akaja Barrack Obama akasema atawaunga mkono wakenya katika chaguo lao. UNAFIKI, na nilishawaambia watu Barrack Obama sio mwafrika kwa vile tunavyotaka kumtafsiri kama akina Jesse Owen, Jesse Jackson ambao ni zao la utumwa.

Obama hakuachagua lakini yeye sio zao la utumwa bali mapenzi tu wa binti na mvulana. hajui madhira ya akina jese jackson. kwa suala la kenya Raila Odinga nampenda harakati zake lakini bado naguswa na UZEMBE aliofanya na kudhani atashinda kirahisi. Nimeandika hili, inshallah itachapishwa wiki ijayo jumanne(TAZAMA). Odinga amejitakia sana, kwa njia zake alizopita tangu 2002, 2007 na 2013 sishangai kushindwa kwake.

Hata wengi walipomshinikiza Jaji Willy mutunga katika kesi ya Uhuru kenyatta na Ruto kutogombea, jaji mutunga alisema wanaopinga hawana hoja. Kimsingi Odinga alikuwa na timu dhaifu mno, wala hata CHADEMA sijui kupeleka nini au nini sijui bado Odinga alikuwa na timu dhaifu sana kuliko ile ya mwaka 2007 iliyojaa wababe wa siasa na wenye ushawishi. Hivi nani pale alikuwa na msaada kwa Odinga mwaka huu?

Sioni hata mmoja. Kwahiyo kuwalazimisha wakenya wamchague Odinga ni ukosefu wa heshima tu. wakenya sio wajinga, na wanaolalamika ni watu wa Kisumu tu. Ujinga aliofanya Odinga ahata akiongea na mimi nitamwambia ulifanya makosa haya na haya. kwahiyo CHADEMA kumsaidia Odinga ni kawaida na tunawaheshimu kwa hilo, lakini uamuzi wa mwisho ulikuwa mikoni mwa wakenya.

Sio Obama ambaye sio raia wa kenya. ....... sio mpiga kura wa kenya. kama alitaka Odinga ashinde alipaswa kuwa na adabu sasa. Marekani kutomtaja sio issue kabisa, haitabadilisha kitu, ni ujuha tu. wala Marekani ikitaja jina la kenyatta haina maana ndio inahalalisha. Marekani sio wakenya. 

Hayo mataifa yaliyowapongeza WAKENYA, na WAKENYA wamemchagua nani? Je, kupingwa matokeo mahakamani kunazuia kupongezwa kwa Uhuru Kenyatta ambaye ametangazwa na TUME? ....
na kama Raila Odinga akishinda hiyo kesi, kuna sheria inayozuia kutompongeza Raila Odinga? mimi nadhani USA kutotaja jina la kenyatta ni woga na udhaifu kiakili, sababu ilibidi hata pongezi wasitoe wasubiri hatima ya majibu ya mahakama. ... vilevile, mataifa ya magharibi kutotaja jina kenyatta au kutompongeza bado hakumanishi wao wana uhalali wa kuwamrisha wakenya wamchague nani. .....kwa upande mwingine kisiasa Odinga amejitakia ANGUKO.

KUFUKUZA MAKURUTA 95 WA JESHI LA POLISI HAITOSHI


Markus Mpangala

Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
Tukio la waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi kuwafukuza Makuruta 95 wa Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi kwa kile alichooita kugundulika kutumia rushwa kujipatia ajira, bado linaelea katika vichwa vya watu juu ya msingi wa maadili yetu.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Renatus Chalamila amehusishwa na rushwa katika kuajiri. Waziri Nchimbi amechukua hatua zaidi baada ya kumsimamisha kazi Kamishna huyo. Alisema pia taarifa za uchunguzi za Kamishna huyo, ambaye anashughulikia masuala ya ajira zimewasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete ambaye ana mamlaka ya kumfukuza kazi au uamuzi mwingine wowote.

Japokuwa waziri Nchimbi ametaja pia maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi ambao wamehusishwa na makosa mbalimbali lakini binafsi nimeguswa na huku chini kabisa (Makuruta). Kwa maana nyingine harakati za vijana 95 ambao wamefukuzwa na waziri Nchimbi waliokuwa wakitarajiwa kuingia kwenye ajira ya ndani ya Jeshi la Polisi, linatuletea swali la msingi juu ya maadili na namna tunavyojenga usalama wetu nchini. Hii ina maana katika Makuruta hao 95 tulikuwa na watu wenye tabia tofauti, lakini baya zaidi wamekutana katika msingi wa kutoa rushwa ili wapate ajira.

Namna nyingine tunajiuliza mfumo wetu wa jira katika sekta za ulinzi na usalama ukoje na nani anawajibika kuutengeneza pale unapokwenda kombo. Makuruta 95 ni wengi au hata wangelikuwa watano tu, lakini ukweli tunabakia katika mwenendo mbovu wa jamii iliyochoka kufuata kanuni hivyo kila kitu kinatakiwa kwenda ‘fasta fasta’. Ni tabia hii ya ‘fast tracking’ inatufikisha mahali pabaya kabisa na kushuhudia vijana wadogo wakijihusisha na rushwa.

Naam kufukuzwa kwao ni ushahidi wa wazi kabisa jamii yetu imeoza na hata wale viongozi kule juu akiwemo Kamishna Renatus Chalamila, ni taswira iliyoko huku kondeni. Kama CCP leo hii imegubigwa na vikwazo vya ajira mpaka vijana wetu watoe rushwa ina maana mfumo wetu wa kutumia rasilimali watu umegubikwa na maadili duni. Wengi wanatoa ajira kwa misingi ya jinsia, wajihi, rushwa, na kadhalika.

Kwa namna nyingine sio sifa nzuri kwa Jeshi letu adhimu la Polisi. Mwanazuoni wa masuala ya kijeshi Sun Tzu kwenye kitabu chake cha ‘The Art of War” anasema kama jeshi likiingia vitani kisha likapoteza mwelekeo basi wakulaumiwa ni Jenerali wa jeshi husikal Sun Tzu anasema iwapo jeshi likiwa kwenye gwaride linatii maagizo yote; kushoto geuka, kulia geuka, au mbelee tembeaaaa!

Waziri Nchimbi
Iweje jeshi hilo likapoteza umahiri huo ndani ya uwanja wa vita. Bahati mbaya Sun Tzu alisahau kuwa katika uwanja wa vita kuna matukio ambayo yanaweza kubadilisha mwelekeo au tabia za jeshi. Kama mwanajeshi hakuwa thabiti licha ya mafunzo yake, basi haitashangaza kuona siku moja akishindwa kuingia uwanja vita sababu tu ya kukosa misingi binafsi ya kulitumikia jeshi.

KWANINI JESHI LA POLISI LIWE NYENZO?
Moja makosa makubwa yanayofanyika katika jamii yetu ni kushindwa kuelewa watoto wetu wanatakiwa kufanya kazi gani katika maisha yao. Wapo wazazi ambao hawajui na watoto nao hawajui wafanye kazi gani hata wanapofika kidato cha nne. Wengi wao wakishapata matokeo ya mitihani yao ndipo huanza kujiuliza wafanye kazi gani.

Kwa Makuruta 95 waliokubali kutoa rushwa ina maana kuwa walikuwa wanataka kulitumia Jeshi la Polisi kama nyenzo ya kufanya kazi nyingine hapo baadaye. Mtu makini akichambua hili na kuangalia mwenendo wetu kwa Jeshi la Polisi, wapo wanaojiunga sio sababu ya mapenzi yao bali kwakuwa wanataka ‘kutoka’ kimaisha hivyo mwelekeo uliopo ni CCP Moshi. Sina shaka kabisa, Jeshi la Polisi linaweza kufanya uchunguzi wa mambo mbalimbali ikiwemo hili. Ni rahisi kukukotoa idadi ya wahitimu wa Jeshi la Polisi kila mwaka na wanakopelekwa na muda wao kazini.

Kisha Jeshi la Polisi linaweza kuanza kufuatilia wahitimu hao kama wameendelea na kazi ya Upolisi kwa muda gani na wanafanya nini baada ya kujiondoa katika jeshi la Polisi. Ninasema hivi kwakuwa katika nyakazi zetu Jeshi la Polisi kwa baadhi ya watu wanatafsiri kama sehemu ambayo wanakwenda vijana walioshindwa maisha hivyo kwa muda fulani wanajua wataweza kupata nyenzo ya kufanya kazi nyingine.

Ni wazi wengi waliowahi kujiunga Jeshi la Polisi kwa uadilifu wamedumu na wanaendelea kuheshimu taalumu yao. Lakini wapo wengine wanalitumia Jeshi la Polisi kama nyenzo ya kufanikisha mipango ya maisha. Ni kweli wana haki, lakini hawa vijana wetu baadhi yao wanaweza kabisa kuwa ndani ya jeshi la Polisi kisha baadaye wakipata njia za kufanya shughuli nyingine (baada ya kuelimishwa na au kulifanya jeshi kuwa mtaji).

Endapo Jeshi la Polisi limeweza kugundua Makuruta 95 wameingia kwa rushwa safari hii ni vema likafanya uchuguzi mwingine juu ya wahitimu wake na vituo vyao vya kazi. 

HASARA
Hakuna hasara kubwa kama watu kutumia idara za usalama kama nyenzo ya kufanikisha mipango yao. Tunahitaji askari waadilifu na wenye kuipenda kazi yao. Tunahitaji watu ambao sio tu watakuwa wakilalamikia mishahara midogo bali kutumia kidogo hicho kwa uadilifu na kulinda maslahi ya nchi yetu.

Lakini hakuna hasara kubwa inayotokea kama kitendo cha Makuruta 95 hao au wale waliowahi kupitia CCP Moshi na kadhalika wanaoingia maisha ya kawaida ya mtaani. Katika mazingira haya, “hisia” za ongezeko la Uhalifu haliwezi kukosekana kabisa. Na ili kukabiliana nalo ni vema kutafuta njia mwafaka za mkunusuru Jeshi letu la Polisi ili lisiwe na linakusanya tu kama kokoro na kujikuta limejaza askari wasiowaadilifu.

Ni mbaya, na hatutakuwa tumeokoa jamii inayoamua kufikiria RUSHWA kwanza ndipo ipate ajira. Ni vyema katika tukio la Makuruta waliofukuzwa wafuatiliwe na kuhojiwa zaidi, na iwapo wazazi wao walihusika kuchochea (kama) basi nao wanatakiwa kupitiwa na mkono wa sheria. Kuwafukuza Makuruta pekee hakutoshi mheshimiwa Waziri Nchimbi. Nimemaliza.