March 19, 2013

GEOPOLITICS: YA RAIS AL BASHIR KUMNUSURU UHURU KENYATTA?


Markus Mpangala
IWAPO Raila Odinga wa Muungano wa CORD atashindwa kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Kenya, basi Uhuru Kenyatta ataapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo. Bahati mbaya zaidi, suala linalojitokeza sasa ni namna diplomasia ya Kenya itakavyokuwa hapo baadaye.

Kuna nchi zimempongeza Uhuru Kenyatta kwa kupata ushindi; Tanzania, Zimbabwe, Afrika Kusini, Rwanda na Uganda, huku Marekani ikikwepa kutaja jina lake. Si hoja kuu kujadili uamuzi wa serikali ya Barrack Obama kukwepa kumtaja Uhuru Kenyatta.

Pamoja na hayo Uhuru Kenyatta na William Ruto wamefunguliwa mashtaka katika Mahakama Kimataifa ya Uhalifu(ICC). Hata hivyo, kesi yao itaendeshwa mjini Arusha hapa nchini baada ya serikali kukubali maombi ya ICC kuwa nchi mwenyeji. Mjadala mkubwa uliopo ni juu ya diplomasia ya Kenya  chini ya Uhuru Kenyatta na William Ruto ambao walikuwa wakiungwa mkono na Mwai Kibaki, huku Daniel Arap Moi akimuunga mkono Musalia Mudavadi.

Kote Afrika kuna mazungumzo kila kona wakihoji jinsi Uhuru Kenyatta anavyoweza kuwaumiza wananchi wa Kenya ikiwemo suala la kuwekewa vikwazo. Kwanza tunatakiwa kutambua Uhuru Kenyatta alipigiwa kura kihalali na aliingia kwenye mchakato wa kugombea urais kwa njia halali kabisa baada ya Mahakama Kuu nchini Kenya, chini ya Jaji Willy Mutunga kutupilia mbali madai ya kuzuiwa kwa wanasiasa hao kugombea urais.

Uhuru Kenyatta
Tangu wakati huo kuliibua hofu, lakini kulingana na siasa za Kenya, ukabila umeshika kasi hivyo makabila ya Kalenjin na Kikuyu yanaonekana kushinda uchaguzi huu baada ya William Ruto (mkalenjin) na Uhuru Kenyatta (mkikuyu) kushika madaraka. Hivyo hadi leo diplomasia ya Kenya inaelekea kuleta mjadala na kudhaniwa kunaweza kutokea mgogoro na nchi za kigeni hivyo kuhatarisha maisha ya wakenya.
Lakini muhimu ni kufahamu kuwa Kenyatta alipigiwa kura na wakenya, hivyo ulikuwa uamuzi wao juu ya kumchagua au kumwacha. Jambo la kuelewa hapa ni kwamba Uhuru Kenyatta anaingia kwenye nafasi ya urais (iwapo Mahakama haitabatilisha matokeo) akiwa na swahiba wake William Ruto.

UMOJA WA AFRIKA vs ICC
Umoja wa Afrika utalazimika kufikiria zaidi juu ya suala la Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. AU inaendesha Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (African Court on Human and People’s Right), yenye makao makuu mjini Arusha.  Mahakama hii iliidhinishwa nchini Ethiopia na kugharamiwa na serikali ya Tanzania. Dhumuni la Mahakama ya ACHPR ni kuwa na Mamlaka ya kusikiliza na kuzitolea uamuzi kesi za makosa ya Jinai sawa na Mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (uhalifu wa vita na haki za binadamu) yaani ICC (International Criminal Court) yenye makao makuu The Hague, Uholanzi.  

Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (ACHPR) inaongozwa na Jaji Gerald Niyungeko (Rais wa Majaji), Jaji Sophia Akuffo (Makamu) Jaji Elsie Nwanuri na Jaji Robert Eno (Msajili wa Mahakama hiyo).  Kwa mujibu wa AU, Mahakama ya ACHPR itakuwa na mamlaka kamili ya kutolea uamuzi wa; (i). Makosa dhidi ya Ubinadamu (Crimes against Humanity), (ii). Makosa ya kivita (War Crimes) na mamlaka yote ya kusikiliza makosa ya Jina.
Aidha, kulingana na uanzishwaji wa ICC, kuna kesi ambazo zinatolewa uamuzi The Hague, Uholanzi, lakini zinaweza kufanyiwa uamuzi na Mahakama ya Haki za Binadamu inayofanya kazi barani Afrika mjini Arusha, Tanzania. Madhumuni ya ICC ni; (i). kusikiliza makosa ya ukandamizaji (Crime of Genocide), (ii). Makosa dhidi ya Ubinadamu (Crimes against Humanity), (iii). Makosa ya Kivita (War Crimes), (iv). Makosa ya Uchokozi (Crime of Aggression), (v). Makosa ya uvunjaji wa Sheria za Kimataifa.

Mahakama ya ICC ilianzishwa rasmi mwaka 2002 baada ya makubaliano yaliyofanyika mwaka 1998 kwa kazi tulizoainisha hapo juu. Kuundwa kwa ICC ni zao la Mkataba wa Roma (Rome Statue) wa Julai 1, 2002. Kumekuwa na shutuma nyingi dhidi ya Mahakama ya ICC, lakini sasa bara la Afrika limeamua kujibu mapigo kwa kufanya kweli na kuanzisha  Mahakama yao. Mwaka 2009, Mahakama ya ICC ilianzisha mchakato wa uchunguzi wa uhalifu wa kivita katika nchi za DRC, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kenya, Afghanistan, Colombia, Ivory Coast, Chad na Georgia. ICC iliamua kutoa hati ya mashtaka dhidi ya Rais Omar Al Bashir kwa madai anahusika na mauaji ya yanayofanyika katika jimbo la Darfur, Sudan.
Aidha, ICC ilimhusisha Rais Bashir na wanamgambo wa Janjaweed. Kwa mujibu wa Ripoti yake, ICC ilisema Sudan siyo sehemu ya Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC kulingana na Mkataba uliounda Mahakama hiyo), hivyo kiongozi wake (Bashir) hawezi kukamatwa kwa mfumo wa Mahakama hiyo. Lakini ICC ikasema inachukua jukumu la kumtia mbaroni Rais Bashir kulingana na uamuzi wa Baraza la Usalama (United Nation Security Council) Namba.1593 la Machi 31, 2005, kutokana na hali ya maafa ya jimbo la Darfur. Azimio hilo linalofanya kazi chini ya Sura ya VII ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) ndilo lilitumiwa na ICC kutaka kumkamata Rais Bashir kulingana na hali mbaya ya Jimbo la Darfur.
Jean Ping, Mkuu wa zamani wa Tume ya Umoja wa Afrika
Wanachama 11 waliounga mkono azimio hilo, halafu China, Algeria na Brazil zikapinga. Hata hivyo, uamuzi wa ICC unadaiwa kuchochewa zaidi na Marekani ambayo siyo mwanachama wa Mahakama hiyo, bali ilitumia nafasi yake ya mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, na mvuto wa ICC katika hatua zake za kulinda haki za Binadamu. Hivyo kikao cha 111 cha ICC kikaidhinishwa kukamatwa kwa Rais Bashir. Lakini kwa upande wa nchi za Afrika kupitia Umoja wa Afrika zilipingana na ICC, huku zikishutumua ICC kuchukua mkondo wa nchi za kibeberu kuingilia kadhia ya Darfur.

Hati ya kukamatwa Rais Bashir ilitolewa Machi 4, 2009 haiwezi kutekelezwa kwa namna yoyote kwa mujibu wa AU hali ambayo ilileta malumbano makali. Malumbano yalichochewa zaidi baada ya serikali ya Marekani kutangaza kuunga mkono Rais wa Sudan kufikishwa The Hague. Taarifa za serikali ya Marekani zilitolewa na Robert Wood, Hilary Clinton na mwakilishi wa Marekani nchini Sudan, Jenerali Scot Gration ambao waliwakilisha maoni ya serikali yao kuhusu Hati ya kukamatwa kwa Rais Bashir. Awali  mwaka 2007, ICC ilitoa Hati ya kukamatwa kwa waziri mmoja wa zamani wa serikali ya Sudan.

UMOJA WA AFRIKA ULIVYOMTETEA RAIS BASHIR
Ripoti ya Januari 9, 2012 ilieleza waziwazi hatua ya ICC kumkamata Rais Omar al Bashir ni batili.  AU ilipinga hatua ya ICC kuzishinikiza nchi za Malawi na Chad kutoa “maelezo”  kwanini ziliruhusu Rais wa Sudan, Omar al Bashir kuzitembelea huku zikifahamu kuwa ICC imetoa Hati ya kukamatwa kwao. AU ilikosoa kwa vipengele vya sheria iliyotumika na ICC kuzishinikiza  kutoa “maelezo” kwa nchi za Chad na Malawi. Taarifa ya AU yenye Kumb. Namba. 002/2012, iliyojibu taarifa mbili za ICC;- Mosi ni taarifa yenye  Kumb. Na. CC-02/05-01/09-139, pili; yenye  Kumb. ICC-02/05-01/09-140 Desemba 12 na 13, 2011, inaeleza kwanini haikubaliani na uamuzi wa ICC.

Lakini  ICC ilieleza kuwa hatua za Malawi na Chad kumkaribisha Rais Bashir ni kukiuka Ibara ya 87(7)  ya ICC, pamoja na Baraza la nchi wanachama pamoja na Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa. Aidha, ICC ilisema Malawi na Chad zilikiuka Ibara ya 27(2) na 98(1) zilizounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa Mamlaka ya Kiongozi wa nchi kutekeleza agizo la ushirikiano na Mamlaka ya ICC.

Kwa hiyo ICC,  ilikuwa ikimshutumu marehemu Bingu wa Mutharika wa Malawi (Joyce Banda alibadilisha baadaye) na Idrissa Derby wa Chad wanadaiwa kukiuka Ibara ya 98(1) kwa kutotimiza “agizo la ushirikiano” kwa mamlaka yao mbele ya ICC. Hata hivyo, Umoja wa Afrika haukuweza ulisema Malawi na Chad ni wanachama wa AU wapo chini ya Ibara ya 23 (2) ya Sheria (Constitutive Act) ambayo inawataka nchi wanachama kuheshimu na kuzingatia Sera zinazounda Umoja wa Afrika.  
AU ikasema kulingana na Ibara ya 27(2) ambayo inaelezea taratibu maalumu za uundwaji wa ICC;- kwamba hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa lazima zizingatie nafasi ya mhusika iwe kitaifa au kimataifa, hivyo mahakama haitakiwa kuingilia suala hilo. Ibara hiyo inajieleza kuwa ni ‘taratibu za jumla za Jinai’ lakini hatua zozote za kisheria hazichukuliwi kama kigezo cha kumkamata mhusika, vinginevyo kulingana na uhusiano baina ya ICC dhidi ya mtuhumiwa (Rais Bashir/Uhuru Kenyatta) kama inavyoelezwa kwenye Ibara ya 98(1).

Ibara hiyo inasema mamlaka ya jumla, hatuwezi kusema Mahakama za ndani hazijumuishwi, hivyo lazima ICC inatakiwa kuwa na adabu mbele ya sheria za Kimataifa (Interanational Law Helsinki Final Act) na sheria za Mahakama ya ndani. Kwa mantiki hiyo, hapa tunajikuta tukimleta Uhuru Kenyatta ambaye ni mshtakiwa wa ICC, je, atalindwa na Constitutive Act kama ilivyokuwa kwa Rais Bashir? Labda tofauti iliyopo Kenya ni mwanachama wa ICC na Sudan sio mwanachama wa mahakama hiyo. Pia Uhuru Kenyatta ameshtakiwa akiwa mwanasiasa wa kawaida sio mkuu wa nchi kama sheria za Umoja wa Afrika zinavyoagiza. Ni mtihani kwa diplomasia ya Kenya na Afrika.

BIASHARA NA UCHUMI: WAFANYAKAZI 'WAZEMBE" NI MSIBA KWA WAJASIRIAMALI

Na Albert Sanga, Iringa

Mwishoni mwa mwezi Februari nilikuwa nikisafiri kutoka wilaya ya Mvomero kuelekea Kilombero mkoani Morogoro. Nilipofika Morogoro mjini niliingia kwenye basi moja ambalo linafanya safari zake kati ya Morogoro mjini na Ifakara.

Muda niliokata tiketi katika basi hilo ilikuwa ni saa tisa na nusu jioni, lakini ndani ya hilo basi nilikutana na abiria ambao walikata tiketi majira ya saa tatu asubuhi! Kila abiria aliyekuwa anakata tiketi pale alikuwa akidanganywa muda wa kuondoka kwa basi husika.  Wale waliokata tiketi saa tatu asubuhi waliambiwa basi lingeondoka saa nne na mimi wakati ninakata tiketi saa tisa na nusu niliambiwa kuwa basi linaondoka saa kumi kamili!

Kilomita mbili baada ya kuondoka stendi kuu ya Morogoro majira ya saa kumi na moja jioni; kondakta akatutangazia abiria ya kwamba basi hilo halitaendelea na safari ya Ifakara kwa sababu idadi ya abiria ni wachache. Kondakta akadai kuwa kutokana na uchache wa abiria tuliomo “haitawalipa” kulipeleka basi huko.

Walichofanya wakakodi basi dogo na kuamuru abiria tuingie humo. Kwa bahati mbaya sana idadi ya abiria tuliokuwemo kwenye basi la awali tulikuwa ni wengi kushinda idadi ya siti za hili basi dogo. Abiria wengi waliokosa siti wakalazimika kusimama wakati tiketi zao zilikuwa zinaonesha nambari ya siti kwa basi la awali.

Abiria tusio na makuu ndio tulioingia kwenye basi lile dogo lakini kuna ambao waliwasha moto kuhusu “uhuni” wa basi lile na wakakataa katakata kubadilishiwa gari eti kwa sababu ya kusema “hailipi”. Nilimsikia abiria mmoja akisema maneno yafuatayo kwa hasira na ukali mwingi;

“Kama ingekuwa basi limeharibika ningekubali, lakini mnaleta uhuni wa kusema eti haitawalipa, kwani mnavyoomba leseni SUMATRA si mlijua kuna siku mtapata abiria na siku nyingine mtakosa? Imeandikwa wapi katika leseni ya kuwa abiria wakiwa wachache katika basi, safari iahirishwe? Nitakufa na ninyi ili niwafundishe adabu muache kutuonea. Mnadhani watanzania wa siku hizi ndio wale wa zamani wa kuwapelekesha kama maboga?”

Baada ya kuona pamekuwa pa moto, wafanyakazi wa lile basi kubwa ilibidi wawavute pembeni wale abiria waliowasha moto na kuzungumza nao. Sielewi walifikia muafaka gani lakini abiria wale walishikilia msimamo wa kutoingia kwenye basi lile dogo. Tuliondoka Morogoro mida ya saa moja kasoro jioni huku abiria wote wakiwa wanalalamika, kujiapiza na kupiga sana kelele.

Katika siti niliyokaa ndani ya lile basi dogo kulikuwa na mama mmoja ambae baada ya kumsalimia alinieleza kuwa anaona sura yangu kama sio ngeni. Nilipomueleza kuwa huenda aliniona kwenye gazeti la Jamhuri, alishtuka mno na kusema, “Hee, kumbe wewe ndio Sanga? Wawoo!”
“Kila wiki nazisoma makala zako” Kisha akauliza kwa hisia kali, “Kwa nini hujawapigia kelele hawa wahuni (wenye basi) wakati wewe ni mwandishi? Hivi unajua ungejitambulisha kwao na kuwapiga mkwara, wangeogopa sana na wasingefanya uhuni waliotufanyia?”

Yule mama niliendelea kuongea nae njia nzima, lakini kwa swali lake la hisia nilimjibu hivi, “Wakati abiria wote mlikuwa mkipiga kelele na kulilaani hili basi, mimi fikra zangu zilikuwa kwa mmiliki wa hili basi. Huko aliko nina uhakika hafahamu kuwa vijana wake wanamuharibia biashara. Katika masuala kama haya huwa ninafunga kinywa changu na kusali nikimuombea mjasiriamali mwenye biashara husika.”

“Kwa sababu ninafahamu kama mwenye basi hili angekuwepo hapa; asingetumia lugha ya kibabe, asingeonesha ukaidi na asingekubali kuona jina la basi lake linachafuliwa”. Nikaendelea kumueleza, “Siwezi kutumia uwezo wangu wa kuandika kwa ajili ya kuchafua biashara ama makampuni ya wengine hata kama wawe wamekosea vipi.”

“ Ninaamini kuwa kuwalinda wajasiriamali wenzangu ni eidha kuandika mema yao ama kukaa kimya kwa makosa yao. Msimamo wa kukaa kimya inapotokea uvurundaji kama wa lile basi lililotushusha unaweza kuonekana ni kutokuwajibika; lakini sikufichi mamangu; kabla sijaandika chochote kuhusu biashara ama kampuni yeyote; huwa kwanza najiuliza hivi:

“Je, hiki ninachoandika kama ningekuwa ni mimi, biashara yangu ama kampuni yangu inaandikwa hivi, ningejisikiaje? Majibu ya swali hili ndiyo hutengeneza makala zangu zote za biashara na uchumi unazozisoma. Nafahamu kuwa viatu vya ujasiriamali ni vizito; mtu anaweza kukurupuka kukusema vibaya pasipo kufahamu ikiwa wewe unahusika moja kwa moja ama laa. Nipo makini sana na kalamu yangu”

Mimi nilishuka Kilombero na yule mama aliendelea na safari yake ya Ifakara, lakini safari ile ilinipa kutafakari na kuwahurumia wajasiriamali wengi. Nikaikumbuka kampuni nyingine ya mabasi ambayo siku hizi siioni tena. Wafanyakazi wa kampuni ile enzi zile ikiwa kileleni iking’aa walikuwa na nyodo kupindukia.

Siku moja nilikuwa nilikuwa na ndugu yangu mmoja mfanyabiashara aliyepo Tunduma na tukafika katika ofisi zao kukata tiketi za kwenda Dar es Salaam. Mkatisha tiketi akatuambia kuwa tiketi zimeisha.

Siku za baadae nilikuja kuambiwa kuwa wafanyakazi wa mabasi yale walikuwa na mtindo wa kumtazama mtu mavazi na mwonekano wake kabla ya kumpa tiketi. Ukivaa rafu rafu hupewi tiketi! Kitendo hiki kilisababisha atu wengi kuhisi wanadharauliwa na hivyo wakaanza kusambaza maneno mabaya kuhusu mabasi yale.

Kilichotokea? Kuna wakati basi la watu sabini lilikuwa likiondoka stendi likiwa na abiria saba tu! Katika mazingira kama haya ambayo unaendesha kampuni ama biashara kwa hasara haiwezekani ukastahimili katika soko.
Kwenye ujasiriamali wafanyakazi ni pasua kichwa kweli kweli. Uzembe, ujinga na upumbavu wa wafanyakazi wengi umesababisha wajasiriamali wengi kutoendelea, kuyumba ama kufilisika kabisa.

Unaweza kutafuta mtaji kwa jasho jingi sana na ukaanzisha duka, unamuweka mfanyakazi auze hapo lakini wengi hawawi waaminifu. Kama ni duka anaweza kuanza kufuja mali ama kuiba. Shemeji zangu wahehe huwa wanamsemo huu, “Mtu anakuja kuomba kazi akiwa ananyenyekea na kuweka mikono nyuma, lakini akishapata anaanza kuiweka mikono mbele na anaweza kukufokea hata wewe bosi wake”!

Kwa hawa wafanyakazi wazembe jambo  baya kuliko yote ni pale inapotokea hawaheshimu, kuwathamini wala kuwajali wateja. Wafanyakazi vimeo huwa hawana uchungu na biashara yako, iwe unauza ama hauuzi, iwe unapata hasara ama faida, hawajali! Wanachojali wao ni mshahara wao unaowalipa, basiii!

Usiombe biashara yako ikaingia kwenye tanuri la kusemwa vibya, utajuta. Mathalani, lile basi liliotufanyia uhuni pale Morogoro kila abiria alikuwa akijiapiza kuwa hatakaa apande tena lile basi na wengine wakaweka nadhiri ya kuwajulisha ndugu, marafiki na jamaa zao kuhusu hatari ya basi lile kwamba halifai kupandwa. Unategemea nini kwa majaliwa ya kampuni ile kama sio kushuhudia kupungua kwa abiria wanaopanda mabasi yao?

Kama hili tumeshalifahamu ya kuwa wajasiriamali tuna hatari ya wafanyakazi wazembe kutufilisi, Je, tufanyaje? Kulalamika haitatusaidia! Kusema tumuachie Mungu ni uzembe! Kuendelea kuvumilia ni kujirudisha nyuma!  Tupende ama tusipende wajasiriamali tunalazimika kuchukua hatua za makusudi za kutuwezesha kuwa na wafanyakazi bora watakaojenga biashara pamoja nasi na sio wale wanaobomoa.

Nilichogundua ni kuwa wajasiriamali wengi hatujui namna ya kuajiri pamoja na namna ya kuwafundisha wafanyakazi. Wengi wetu huwa tunazoazoa bora wafanyakazi. Na kinachotuponza ni kupenda vya dezo. Tunapenda kuwabeba ndugu zetu wa karibu bila kujali ubora wao, ili mradi tu tuwe tunawalipa kidogo ama kutowalipa kabisa.

Fikiria wewe unamiliki basi ama duka halafu unamuweka ndugu yako asiye na uwezo wala vigezo vya kufanya kazi kwa ustadi, unategemea nini? Sana sana ataanza kujitukuza na kujiona yeye ndie kila kitu katika biashara husika. Hata majigambo yake kwa wengine itakuwa ni cheo chake cha undugu kwako.

Inabidi ufike wakati ambapo mjasiriamali unapiga hesabu za biashara yako halafu unatafuta wafanyakazi wa kiwango na vigezo kuhimili biashara yako. Hakuna maana ya kusema eti unabana matumizi ya kuwalipa watu mishahara ilhali unaelekea kufilisika.

Nimewahi kueleza namna ya kuwatendea wafanyakazi tunaowaajiri katika makala iliyokuwa na kichwa, “Mjasiriamali na Sayansi ya kuajiri”. Mara zote nimekuwa nikiwatahadharisha wafanyabiashara na wajasiriamali kuepuka mtego wa kuwa wadhulumaji kwa wafanyakazi wao.
Mara zote mfanyakazi unaemuajiri katika biashara zako huwa anafahamu kiwango cha faida unayozalisha. Kitendo cha wewe kumlipa kiduchu kinazalisha sumu mbaya sana. Matokeo yake ni kukuibia, kupoteza morali wa kazi na hatimaye kuwavuruga wateja wako.

Nihitimishe kwa kuwasihi wajasiriamali kuwa makini tunapoajiri watu katika biashara zetu kwa sababu wengine wanaweza kugeuka mawakala wa shetani kutufilisi. Niwatakie kila raheri katika mapambano makali ya kiujasiriamali

stepwiseexpert@gmail.com , 0719 127 901


March 18, 2013

NAFASI ZA KAZI KWA VIJANA WA KIKE NA KIUME 20 KAMA "VOLUNTEERS" KATIKA RUAHA MARATHON..!!


Shirika la Mindset Empowerment waandaaji wa mashindano ya RUAHA MARATHON inawashukuru wasimamizi wa shughuli zake kwa upande wa DAR ES SALAAM, Markus Mpangala na Kambi Mbwana, pamoja na akina dada waliojitokeza kuwania nafasi ya kazi pale Mlimani City, Dar es Salaam. 

Nimepewa taarifa kuwa walijitokeza kwenye interview ni mabinti zaidi ya 50 na wamechujwa na kupatikana mabinti watano (5) ambapo mmoja kati yao atachukua nafasi hiyo na wanne kuwa reserve kwa majukumu mengine ndani ya Ruaha Marathon. Tunayo furaha kutangaza tena nafasi 20 za kazi za kujitolea (volunteers) kwa vijana wa KIUME na wa KIKE kwa ajili ya kufanikisha mashindano haya tarehe 25/May/2013, mkoani Iringa.

ENEO LA KAZI: Iringa mjini & Iringa vijijini, kwenye njia (route) za mashindano
MAJUKUMU: Kufanya kazi katika vituo vya marathon siku hiyo ya mashindano
UKOMO: Kazi hii ni ya kujitolea kwa siku moja TU (siku hiyo ya mashindano)
SEMINA: Wiki moja kabla ya siku ya mashindano kutakuwa na semina kwa volunteers wote, kwa ajili ya ujuzi wa kufanikisha majukumu yao.

FAIDA: Pamoja na posho (allowance) atakayopewa volunteer siku hiyo, vile vile atapewa cheti cha kimataifa kinachoonesha kujali, uzoefu na ushiriki wake katika miradi ya kijamii (Ikumbukwe kuwa Ruaha Marathon inafanyika mwaka huu kwa ajili ya kuchangisha fedha za ujenzi wa shule na kituo cha michezo kwa watoto walemavu, Tanzania). Volunteers wote watakuwa ni watu wanaofikiriwa kwanza (first priority) kila zinapotoea nafasi za kazi za kudumu katika Shirika la Mindset Empowerment.

VIGEZO: Yeyote anaependa kuwa volunteer anatakiwa awe anajua kungea na kuandika lugha ya kiingereza kwa ufasaha. Pia awe na ufahamu mzuri kuhusu mambo mbalimbali. Wafanyakazi pia Wanafunzi & wahitimu wa vyuo vikuu/vyuo mbalimbali na wengineo wanaoweza kufika, waliopo/au wenye makazi Iringa mjini wanahamasishwa wasipitwe na fursa hii adhimu

KUTUMA MAOMBI: Tuandikie email: nyalukemarathon@yahoo.com au tuma sms au piga katika +255 719 127 901. Unapoandika/kutuma sms zingatia: 1) Andika majina yako yote matatu, 2) Elimu yako/mahali unaposoma au unapofanyia kazi. 3) Umri wako 4) Jinsia yako. Baada ya kukutuma maombi yako; tutakujulisha hatua inayofuata. Maombi tunaanza kupokea leo tarehe, 17/March/2013

IMETOLEWA NA: Albert Nyaluke Sanga, Mratibu-Ruaha Marathon/Mindset Empowerment, 2013~(C)

NANI KASEMA KLABU YA SIMBA HAINA HELA?


Na Ezekiel Kamwaga

Nauli ya bei nafuu kabisa kutoka Dar-Luanda-Dar ni dola 1000 kwa kichwa. Simba imekwenda Angola pasipo kutembeza bakuli kwa mtu. Na wote waliosafiri wakalipwa posho kwa USD (si kwa fedha za madafu). Fedha hizo ni mara kumi ya zile ambazo wachezaji walikuwa wakilipwa miaka minne hadi sita iliyopita wakiwa safarini na Simba....

 Leo inazushwa kwamba eti Simba haina fedha za kwenda Kagera ndiyo maana inapita Dodoma, Tabora, Shinyanga kucheza ndondo!!!!!! Inachekesha. Gharama ya mafuta, kwa sababu Simba ina basi lake, haifikii hata nauli ya mtu mmoja kwenda Angola... Sasa vije leo isemwe eti Simba haina fedha za kwenda Mwanza? Yaani za kwenda Angola zipo ila za Mwanza hakuna? Kuna sababu kubwa mbili kwanini timu inakwenda Kagera TARATIBU. 

Mosi, zaidi ya nusu ya wachezaji waliosafiri wanatoka TIMU B na wengine hawajawahi kufundishwa na Patrick Liewig. Benchi la ufundi liliona ni vema hawa wapate nafasi ya kujaribiwa katika mechi ya kirafiki ili wajue kocha anahitaji nini na kocha awafahamu zaidi wachezaji wake. Ikumbukwe pia, kiufundi, Simba haikutakiwa kuwa na mechi kwa wiki zaidi ya mbili kutokana na ratiba iliyozingatia ushiriki wake kwenye Ligi ya MABINGWA.

Hiyo ni sababu ya kiufundi. Kuna sababu ya 2 ambayo ni ya kimantiki. Kwamba Simba ni klabu ya Watanzania wote na si wale walioko Dar es Salaam na mikoa yenye timu za Ligi Kuu. Kuna mikoa kama Tabora ambayo Simba haijacheza kwa takribani miaka 10 lakini wapo Wana Simba ambao wangependa kuiona. Vivyo hivyo kwa Shinyanga ambapo tulipata sapoti kubwa sana tulipokwenda mwaka jana. 

Tunahitaji kuwafurahisha wapenzi wetu wa kona zote. Tunahitaji pia kutengeneza fan base kubwa zaidi hata kwa watoto ambao wataiona Simba ikicheza Tabora.... Mwaka jana tulipeleka Kombe letu katika baadhi ya mikoa. Mara baada ya kumalizika kwa ligi msimu huu, tuna mpango wa kwenda kwenye mikoa ambayo Simba haijakwenda kwa miaka mingi... Mikoa kama vile Rukwa, Kigoma, Singida, Mara, Iringa n.k... 

Jamani huko kote kuna washabiki wa Simba na watafurahi kuiona ikicheza mbele ya macho yao. TUNASUBIRI KWA HAMU pia tuambiwe tunaenda kucheza ndondo wakati huo ! Watu wanafikiri Man United inakwenda China kufanya mazoezi pekee!!!! Hapana, inakwenda kutangaza brand yake ili wapate pa kuuza merchandise yao... Tutakwenda kote itakakowezekana, INSHALLAH... Ili mradi Simba ikianza kufanya biashara huko tuendako, na wakati huo utafika tu, tusianze kuulizana tulimtumia MGANGA gani kufanya biashara ya merchandise yetu vizuri.... Hiki ndicho kile rafiki yangu John Shibuda huwa anakiita kwa maneno mawili tu; FIKRA MCHAKATO....

March 13, 2013

UCHUMI NA BIASHARA: "UCHUMI" NDIO LUGHA YA AFRIKA MASHARIKI

Albert Sanga, Iringa

Wiki mbili zilizopita nimekuwa nikiandika waraka wa kiuchumi kwa wafanyakazi. Kwa ujumla wake waraka huo utakuwa ni mrefu hadi sehemu ya kumi. Kutokana na urefu huo nimejipangia kutouleta kwa mfululizo wa wiki zinazofuatana. Badala yake nitakuwa nikiuleta kwa wiki tofauti tofauti mpaka uishapo mwaka huu.

Leo ninapenda tuperuzi nafasi ya uelewa wetu sisi watanzania linapokuja suala la uchumi katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Unapotaja Afrika Mashariki ni kwamba kuna mambo ya msingi ambayo yanaushikilia uhusiano huu. Pamoja na mambo mengine nguzo kuu ya uwepo wa jumuiya hii ni suala la uchumi. Ndio maana tunaongelea soko la pamoja, kuunganisha sarafu zetu, kusafiri kwa mitaji pamoja na rasilimali watu.

Mambo mengine yanayojadiliwa na kushughulikiwa katika ushirikiano huu yanasaidia tu kuboresha lengo kuu la msingi; ambalo ni kuboresha uchumi wa ukanda huu. Kwa tafsiri ya mkato ni kuwa lugha ya Afrika Mashariki ni uchumi. Ili kunufaika na jumuiya hii ni lazima kuijua lugha hii, ni lazima kuyajua matendo ya kiuchumi, ni lazima kuelewa mwenendo wa kiuchumi na ni lazima kutambua nafasi ya mtu mmoja mmoja katika uchumi.

Wakinga tuna msemo mmoja usemao, “Kama wewe sio mchawi, hakikisha unamfahamu mganga mzuri”. Si lazima uwe mjuzi ama mtaalamu wa mambo ya uchumi na lugha za uchumi wa darasani ili kuijua lugha ya Afrika Mashariki; bali unaweza kujifunza na kujizoesha kutoka kwa ‘waganga’(wataalamu) na baadae nawe ukawa ‘mchawi’ (mtumiaji).

Je, watanzania tunaijua kwa kiasi gani lugha inayotumika Afrika Mashariki? Je, tunaelewa maana na matendo ya kufanya tunaposikia viashiria vya masoko ya hisa, masoko ya mitaji, sarafu ya pamoja, ushirikiano wa kodi na ushuru au tunapoambiwa mtiririko wa rasilimali watu? Kwa bahati mbaya sana ni kuwa kutojua lugha hizi hazitoi msamaha wa kuhurumiwa linapokuja suala la utekaji wa fursa zilizopo kwenye jumuiya hii.

Hebu tuangalie baadhi ya mifano michache ya lugha ya Afrika Mashariki. Unaposikia masoko ya mitaji na hisa kichwani kwako ni lazima kuje maneno kama DSE (Dar es Salaam Stock Exchange) , USE (Uganda Stock Exchange) na NSE (Nairobi Securities Exchange). Haya ni masoko ambayo kunatokea ununuzi wa hisa na ubadilishanaji wa mitaji pale.

Hapo kuna makampuni ambayo yanapeleka sehemu yake kuwa miliki ya umma hivyo unaweza kununua ama kuuza sehemu za makampuni hayo. Kujua kuhusu DSE, NSE, na USE hakuhitaji mpaka uwe unamiliki hisa ama mtaji pale isipokua mwenendo wake unaathiri sana uchumi wa eneo hili na hivyo kuathiri ustawi wako binafsi kiuchumi.

Nikisema habari za hisa na mitaji mtu anaweza kudhani ninaongelea masuala ya kitaalamu sana. Kumbuka kua ninaongelea lugha ya Afrika Mashariki. Namna makampuni yanavyojiandikisha na kuuza mitaji kwenye masoko ya hisa na mitaji kunaonesha mtiririko na mwelekeo wa mitaji katika ukanda mzima.

Nasi tunajua kua ulipo mzoga ndipo wakutanikapo tai. Tai wanajuaje kua sehemu Fulani kuna mzoga? Jibu ni rahisi, wanatumia harufu kutambua. Je, unajuaje kua Uganda ama Rwanda kuna fursa za kuwekeza?

Ni kwa kuangalia mwenendo wa mitaji na hisa kama moja ya kiashiria kati ya vingi vilivyopo. Ubaya ni kwamba hata kama wewe usipoisikiliza harufu ya “mzoga wa uwekezaji” wenzako kutoka nchi zingine za Jumuiya wataisikiliza harufu iliyopo hapa Tanzania nao watakusanyika.

Ninapoongelea habari za DSE, USE na NSE naelewa kuwa si rahisi sana kwa wengi kuelewa fursa zilizopo ndani yake pengine kutokana na historia ya uchumi na mazoea yetu. Wenzetu Kenye NSE ilianza (japo sio rasmi) mwaka 1954 wakati sisi DSE ilianza mwaka 1996.

Wanzetu wana uzoefu mkubwa na lugha hii wameizoea kwa kiasi kikubwa. Pale NSE makampuni yaliyojiandikisha ni zaidi ya 50 wakati hapa kwetu DSE kuna makampuni pungufu ya 20 tena mengine yakiwa ni yale yale ya kule Kenya (Cross listing).

Kwa upande wa Uganda hawana tofauti na sisi kwa maana ya kuanza, kwa ni USE ilianza 1997 lakini spidi yao ya kuijua lugha hii ni kubwa mno. Mwaka 2010 USE ilikua ni kinara wa masoko yote ya hisa Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kutumia kipimo cha ALSI (All Shares Index) ikiwa na mrejesho wa faida ya asilimia 74% kwa hisa zinazonunuliwa na kuuzwa.

Sina lengo la kukupitisha porini katika takwimu za kitaalamu lakini kuna kitu nataka tujifunze; Kenya walitangulia miaka mingi, Uganda ni wapya kama sisi lakini wanajifunza kwa kasi ya jabu. Wenzetu walishatangulia na wengine wanakimbia lakini sisi tunazinduka polepole mno.

Nikiri wazi kuwa mambo kama haya ya hisa na mitaji kiasili yaliibuka kutokana na ubepari, lakini kwa kua tumeamua “kuchanganyika” hatuna ujanja zaidi ya kuungana nao. Kumbuka kua, “Kama wewe sio mchawi hakikisha unawajua waganga wazuri”, hatuna ujanja inatakiwa tujifunze na kuizoelea lugha hii ili tuweze kuelewana na wenzetu wa hapa ‘Jumuiyani’

Katika robo ya mwaka jana makampuni mengi ya umma na binafsi katika nchi zote tano za Afrika Mashariki yameendelea kutoa ripoti zao za kifedha na kiutendaji kwa mwaka ulioishia Desemba, 2012. Hapa napo tunaweza kuitathmini hali yetu tuliyonayo katika lugha ya Afrika Mashariki kwa kuangalia namna tunavyozipokea ripoti hizo.

Nianze na namna jirani zetu Kenya wanavyozipokea ripoti hizo. Wakati makampuni 20 makubwa (yaliyopo kwenye 20 Shares Index) yakiachia ripoti zao nchini Kenya; kulikua na  gumzo mitaani kila mmoja akihaha kuzifuatilia, kuzisoma na kuzitafsiri. Wanahisa na wasio wanahisa wanataka kujua kampuni gani imefanya vipi, ipi imeizidi ipi, ipi ina fursa na gawio zuri kwa kuwekeza, ipi ina mikakati gani ya muda ujao na mengine mengi.

Gazeti moja la nchini Kenye lilipiga picha inayoonesha watoto wa sekondari katika mji wa Naivasha wakisoma ripoti ya mojawapo ya benki za biashara nchini Kenya. Walipoulizwa watoto hao mmoja wao alijibu hivi, “Mama ana hisa kwenye benki hii nataka nijue mwenendo wake”. Hapo ni Kenya!hadi watoto wa shule za sekondari wanaongea lugha ya Afrika Mashariki!

Hali ni tete kwa Tanzania kwa sababu ripoti za makampuni ya ndani ama ya wawekezaji huwa hazipokelewi kwa hamasa yeyote. Kwanza ni wachache ambao wanafuatilia ripoti hizo na achilia mbali uwezo wa kutafsiri maana na athari za ripoti hizo kwa Afrika Mashariki na watu wake.

Kule Rwanda na Burundi wenzetu ndio kwanza wanajenga upya nchi zao; hivyo sio rahisi sana kutoa hitimisho la moja kwa moja kuhusu hisia zao katika lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; lakini kiu yao ya kuinuka kiuchumi na kijamii inaonesha namna ambavyo wanaweza kutupita.

Unaposoma ripoti za makampuni haya (Financial Statements) kuna ishara zinatoa ikiwemo, “Nenda katafute ajira sehemu fulani”, “Nenda kawekeze kitu fulani mahali fulani”, “Ondoka mahali fulani kwa sababu pameharibika”. nakadhalika. Kwa kutozijua lugha hizi tunabaki tumeduwaa tusijue cha kufanya wala kwa kuelekea. Kwa kua wenzetu wanaelewa lugha na matendo ya Ki-Afrika Mashariki ni rahisi na itaendelea kuwawea rahisi kunufaika na lugha hii.

Tatizo letu watanzania wengi tunatumia malalamishi kama silaha ya kujiokoa na hatari za Afrika Mashariki. Juhudi zetu katika kuteka fursa za jumuiya hii zimeota matege na tumekua na mtazamo mdogo mno kuhusu mambo tunayotakiwa kufanya.

Kwa mfano; kitendo cha kukazana kujifunza Kiingereza ama kukazana kununua ardhi kwa ajili ya fursa za Afrika Mashariki sio kibaya lakini ni mtazamo mdogo sana. Tukiijua lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; tutaona na kuoneshwa mambo mengi sana yatupasayo ndani ya Jumuiya hii.

Kwa leo nikomee hapa, lakini natarajia kuendelea na chambuzi mbalimbali kuhusu biashara, ujasiriamali na uchumi katika mtazamo wa ki-Afrika Mashariki huko mbeleni.

Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi Afrika Mashariki!