April 05, 2013

WANAFUNZI SHULE YA MSINGI KWAMBE WAPEWA CHAKULA CHA MCHANA


WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI KWAMBE WILAYA YA NYASA WAKIPATA MLO WA MCHANA SHULENI HAPO,JITIHADA ZA AFISA ELIMU NDUGU MATHIAS MKALI KUPUNGUZA UTORO MASHULENI KWA KUANZISHA SHULE ZOTE WILAYANI MBINGA ZITOE CHAKULA CHA MCHANA.HONGERA KWA NYANJA BOY HUYO

April 04, 2013

DARASA HURU: CCM KAENI CHONJO NA JULIANA SHONZA NA MTELA MWAMPAMBA

Daniel Gingo

Kuna wakati ukiangalia siasa wanazofanya Juliana Shonza na Mwampamba (na hasa Mwampamba) wanachofanya sio siasa, wanachokifanya ni utoto! Tena unaweza kudhani kwamba inawezekana CHADEMA walipumua baada ya hawa jamaa kuondoka huko.

Niliwahi kusema kwamba utoto wanaoufanya sasa hivi utakitokea puani CCM, kama baadhi yenu hamtaki kuniamini kwa kudhani kwamba nina chuki na CCM basi mimi na ninyi tunyamaze kwa sasa, tusubiri wakati ukifika utasema.

Kwa Juliana mpaka kesho sijui kilichomtokea, namfahamu kama dada aliyekuwa akimpenda na kumtumikia Mungu kule Mabibo, kilichotokea kwake sikijui, BWANA AJUA!

KWA MFANO WAULIZENI MASWALI HAYA:
1. Kama wakiwa CHADEMA walikuwa wakijua njama zote za mauaji zilizokuwa zikipangwa au kutekelezwa na CHADEMA nini kiliwafanya washindwe kuinuka na kusema kama kweli walikuwa wazalendo kwa Taifa hili? Kwa nini waje waanze kutoa tuhuma hizo leo magazetini na mitandao kama humu?

2. Kama walijua njama za uhalifu zilizokuwa zikifanywa na CHADEMA na wakaficha ‘uovu’ huo ni vipi leo watashindwa kuficha uovu wa CCM pindi utakapofanywa? Nini kitawazuia kuficha madudu ya CCM dhidi ya wananchi wa Tanzania?

3. Katika njama na mikakati ya ‘uovu’ ya CHADEMA wao walishiriki kiasi gani na kwa kiwango gani? Je, ni kweli hawakushiriki mipango iliyotelekezwa? Nini kiliwafanya wajiondoe huko huku wakijua kuwa walishiriki kupanga njama hizo? Je, walikosa walichoahidiwa?

4. Kama waliweza kuwasiliti wenzao wa CHADEMA na leo wanakuja kuwaanika hadharani, watuambie kwa nini tusiionye na kuitahadharisha CCM kukaa chonjo na vijana hawa? Kama waliwasaliti CHADEMA na leo wanafichua siri ambazo walishiriki wote Nape Nnaye ana uhakika gani kwamba nay eye hatakuja kuumbuliwa siku za mbeleni?

MWISHO
a. Narudia leo kuionya CCM, iwe macho na vijana hawa, na sio CCM tu, hata vyama vingine kwa ajili ustawi wa Demokrasia nchini, viache kushabikia watu wanapoacha vyama vyao na kuja kuwa mavuvuzela kwenye vyama vipya!
b. Sina uhakika kama CHADEMA haijawatuma vijana hawa kuivuruga CCM, lakini mashaka yangu ni makubwa juu ya hilo.

MANABII MNAO, LAKINI HAMUWASIKILIZI!!!!

KIKUNDI CHA HABARI CHAKUTANA KUWEKA MIKAKATI


Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba, Angellah Kairuki amewataka wanachama wa kikundi cha waandishi wa habari cha kujikomboa kiuchumi (Habari Group) kupendana na kuaminiana ili kukifikisha kikundi hicho mbali.


Kairuki ambaye pia ni mlezi wa Habari Group, alikitaka kikundi hicho kutokuwa wachoyo wa kusaidia waandishi wa habari wengine wenye nia ya kuungana na kufanikiwa kimaisha.

Akizungumza na kikundi hicho Dar es Salaam juzi, alisema ili mtu afanikiwe ni lazima awe mwenye upendo na kusaidia wengine pale penye mwanya wa kufanya hivyo na kuwataka wanachama wote kuwa na moyo wa kujitolea kwa ajili ya kikundi.  "Sitopenda kusikia kikundi hiki kimekufa kwa sababu ya mifarakano na chuki miongoni mwenu kwani kwa kufanya hivyo hamtofikia malengo mliyokusudia," alisema Kairuki.


 Aliongeza kuwa wakati anaingia madarakani aliweka vipaumbele kwa wafanyakazi wa majumbani, madereva wa aina zote, wafanyakazi wa mashambani, wahudumu wa baa na nyumba za wageni, walinzi na waandishi wa habari.  Na kwamba ameanza kushughulikia haki mbalimbali za makundi hayo, ambapo kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kuishinikiza serikali kusaini mkataba wa kuridhia haki za wasichana wa majumbani.

Aliwapongeza waandishi wa habari kwamba pamoja na changamoto nyingi wanazokutana nazo, lakini hawakati tamaa na wamekuwa wakifanya kazi yao kwa moyo mmoja na kwa bidii. 

Kama mkakati wake wa kuwasaidia waandishi wa habari, alisema atasimamia Habari Group ili wawe mabalozi wazuri kwenye mambo mbalimbali kwa jamii, ikiwemo kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali, kuwapa elimu ya umuhimu wa cheti cha kuzaliwa, sambamba na kushirikiana nao bega kwa bega kwenye mambo muhimu ya kijamii.

"Kuwasidia kwenu ni miongoni mwa malengo yangu niliyojiwekea ya kupigania haki ya baadhi ya makundi ambyo nimeona haki zao kama wafanyakazi hazitekelezwi,"aliongeza.

MGODI UNAOTEMBEA: WAMEAMUA KUIWEKA TANZANIA KIKAANGONI.

Kambi Mbwana, Dar es salaam

KABLA ya kuanza kufikiria labda kuna mkono wa mtu au Taifa kutoka nje ya nchi yetu, vyema tukaelewa kuwa siku zote mvunja nchi ni mwananchi mwenyewe, hasa kwa kuangalia jinsi baadhi yao wanavyokosa uzalendo kwa kutenda vitu visivyokuwa vya kiungwana.

Watu hao wamekuwa wakiendeleza kufanya vitendo vya kushangaza na kuogopesha kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni njia moja wapo inayolitangaza Taifa letu vibaya nje ya nchi.

Tangu kupata Uhuru uliopatikana kwa harakati za viongozi wetu, akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wapambanaji wengine, Tanzania ilijipambanua kuwa ni kisima cha amani.
Katika kulinda msingi huo, wananchi walielimishwa au kupewa kauli mbiu ya namna gani wanavyotakiwa waishi kwa ajili ya kuishi kwa amani na upendo ili kukuza uchumi wa nchi yetu.
Ni kweli kabisa. Kiu hiyo ilidumu kwa miaka mingi, ingawa sasa naanza kuona kuwa hali hiyo imekwisha. Anayesema kuwa nchi hii bado ni kisiwa cha amani, hakika anatumia lugha nzuri kwa kuhofu anayewaeleza hivyo wataondoa woga kwa sababu moja ama nyingine.
Kwanini nasema hayo? Taifa letu sasa lipo kwenye matatizo makubwa ya vurugu za kidini, siasa na mambo mengine ambayo yote kwa pamoja yanawaweka wananchi kwenye wasiwasi mkubwa.

Kumekuwa na matukio mengi ya kutisha. Katika kulielezea jambo hilo la machafuko ya Tanzania, wengi watawataja watu maarufu au wale ambao matukio yao yamegusa watu wengi. Lakini ukweli ni kwamba hao wanaotajwa ni wachache kati ya wengi ambao labda kwa kutokuwa maarufu kwao, au kutojulikana kwa madhira yaliyowakuta, kunawafanya wasionekane yale yaliyowatendewa.

Ingawa watu watawataja watu kama vile Mwandishi Daudi Mwangosi, mtu aliyepoteza maisha kwa staili ya kutisha kupita kiasi. Mbali na Mwangosi, bado wapo watu kama vile Daktari Stephen Ulimboka, Mhariri wa Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006 (Ltd), Absalom Kibanda ambao matukio yao ya kutekwa na kuteswa yamewagusa watu wengi na kuendeleza msemo kuwa Tanzania sasa si kisiwa cha amani.

Mbali na watu hao, ambao kwa mapenzi ya Mungu wameendelea kubarikiwa uhai, wapo ambao wamepoteza maisha, akiwamo Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Visiwani Zanzibar. Padri huyu aliuagwa na kuibua hisia nzito sambamba na kuzidi kueneza chuki kwa miongoni mwa jamii ya Kitanzania. Pamoja na yote hayo, bado wapo wananchi ambao wamekuwa wakiishi bila kuvumiliana kwa sababu za ajabu, hasa huu wimbo wa kuchinja unaoendelea kuimbwa kwa lugha za chuki na kukiathiri kizazi cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tangu kuzaliwa kwa Taifa hili, likipita katika vipindi tofauti kwa viongozi tofauti waliokuwa na mapenzi makubwa kwa wananchi wao, watu waliishi kwa upendo na kuvumiliana kupita kiasi. Si kama ukatili haukuwapo, huenda ulikuwapo, ila si kama ulivyokuwa sasa kiasi cha watu kushikwa na mihemko na kutenda bila hata kuogopa vyombo vya Dola katika mazingira wanayotaka wao.

Hii si njia nzuri ya kuzalisha amani kwa Watanzania. Zaidi tunaendeleza chuki, fitina, majungu na kusababisha sumu mbaya ya vurugu ambazo kuna siku zitashindwa kumalizwa.
Katika kutafuta nufumbuzi juu ya machafuko ambayo mengi huibuka kwa kupita mgongo wa dini na siasa, baadhi ya watendaji wa serikali, wanashindwa kutumia busara, hekima na utu juu ya kumaliza migogoro hiyo.

Kuna siku tutashuhudia watu wakiingia barabarani kufanya uhalifu, maana tayari walishazoea na kuona kuwa hakuna wa kuwazuia kwa namna moja ama nyingine.
Katika kuliangalia Taifa lenye amani, hatupaswi kuchekea kauli za uchochezi zinazotoka kwa mtu yoyote, iwe ni mwanasiasa au kiongozi wa dini ambaye hana uzalendo na wananchi wake. Huo ndio ukweli. Mihemko yako haiwezi kutufanya tuone upo sahihi hata pale utakaposimama kwa kupitia cheo chako cha kidini au kisiasa kuhamasisha vurugu hatari kwa Taifa hili.

Hatuwezi kwenda hivyo. Bado hatuna uchumi unaotufanya tulinge kuwa tutakuwa pazuri hata kama baadhi ya watu watafanya vurugu, wataharibu miundo mbinu yao kwasababu ya kuhamasisha ujinga kutoka kwa mtu mmoja asiyekuwa mzalendo. Kwa mfano, wapo watu ambao wanabishana juu ya nani yupo sahihi katika suala zima la kuchinja. Sakata hili lilibuliwa na Waziri Stephen Wasira, alipokuwa anazungumza jijini Mwanza.

Mengi yaliendelea kuibuka hasa pale Wasira alipojikuta akitoa ufafanuzi kuwa mwenye mamlaka ya kuchinja ni Waislamu. Kauli ya Wasira isingeleta matatizo kama watu watatumia akili na uzalendo kufuatilia suala hili. Kuna uwezekano mkubwa kuwa huenda Wasira amezungumza hivyo kwasababu ndio utaratibu uliozoeleka kwa Watanzania wengi. Hata wachungaji, mapadri walikuwa wakitaka kufanya shughuli inayoshirikisha watu wa jamii tofauti, vitoweo vyao vilikuwa lazima vichinjwe na Waislamu.

Pamoja na yote hayo, watu ambao ni jamii ya Wakristo hawakulazimishwa pia wachinjiwe na Waislamu kama hawajaona hilo linafaa, ingawa tatizo litakuwa pale wanapochinja wao na kuwalisha wengine. Kumbe leo wapo watu wanaotaka wachinje, basi sakata hilo linastahili viongozi wakae na kushirikisha makundi ya kijamii hasa kwa viongozi wao wa dini, Mashekhe, Mapadri na wengineo.

Wakati hayo yakiendelea, watu wanahoji. Je, vurugu hizo mwisho wake ni wapi? Ingawa wapo wanaosema kuwa vurugu hizi zina mkono wa mtu, wakimaanisha watu wanaotumiwa na wengine kutoka nje ya nchi, lakini bado hainifanyi nishindwe kuwataja watu hao kama majuha na wasiokuwa na uzalendo katika Taifa lao.

Watu hao ambao lengo lao kubwa ni kuiweka nchi katika mtihani mzito, hasa katika kiu ya kuilinda amani yake, hawastahili kuchekewa hata mara moja, maana wanavyoendelea kuchekewa, ndivyo sumu hiyo inavyozidi kuenea na kuota mizizi hata kwa wale wasiokuwa na tabia hiyo.

Kila mtu wakiwamo viongozi wa serikali, chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa upande wa Bara na Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wa Visiwani kuendelea kuwa wakali kwa kundi lolote, mtu yoyote anayefanya uvunjifu wa amani kwa makusudi kwa faida anayoijua mwenyewe.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe kuwa vinakuwa mstari wa mbele, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kulinda amani na mustakabali wa Tanzania.

Leo tunaona ni kawaida, lakini ikiendelea hivi, kila mmoja ataona ana uhuru wa kufanya kila analotaka, hivyo kusababisha machafuko, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, hasa tatizo hilo linapopitia kwa mlango wa dini au vyama vya siasa, kama vile Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine vya siasa vilivyosajiliwa katika nchi yetu.

Huu ndio ukweli wa mambo. Tusipokuwa makini, kujua nini cha kufanya kwa ajili ya nchi yetu, hakika hatutakuwa na kizazi chenye uzalendo, kinachoithamini amani kwa ajili ya kulinda utu na heshima za watu.

Tuna wajibu wa kulijua hili, maana inapotokea machafuko makubwa, wanaoathirika ni akina mama na watoto, hivyo ni wazi hawa wanaofanya vitendo vya unyama kwa wenzao, wale wananaokesha kubuni namna ya kufanya vurugu za kidini na kisiasa wafikie wakati waone imetosha kwa ajili ya kuendeleza wimbo wetu wa Tanzania kisiwa cha amani.

MAONI: kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087

April 03, 2013

GHASIA ZA TUNDUMA, HALI SIO NZURI SANA


Ghasia zinazoendelea katika mji wa Tunduma ulioko mkoani  Mbeya zimechochea uharibifu kijamii. Tunduma haiko katika hali nzuri.

Vurugu kama hizo ziliwahi kutokea mjini Mwanza na kuhusisha wamumini wa imani ya kikristo na Kiislamu. Mauaji yalitokea na serikali ilifanya juhudi kuwakamata wahusika.  

Hapa mwakilishi wa Blogu ya Lundunyasa, anaelezea kwa ufupi sana juu ya kile kinachoendelea mjini humo.

Ni kwamba inaelekea hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu uchinjaji bado haijaeleweka, hivyo wakristo bado walikuwa na msuguano na wenzao juu ya nani achinje. 
Tamko la Polisi lilisema waislamu waendelee kuchinja sasa leo alfajiri vijana wa kikristo walienda machinjoni na kumgawia kichapo cha kutosha mchinjajiwa kiislam ambaye alifanikiwa kutoroka. 

Baada ya hapo wakristo nasikia ndiyo wakaanza hizo fujo ikiwemo pamoja na kufunga barabara, kuharibu msikiti, kubomoa nyumba ya polisi mmoja aliyejenga uraiani, wameandamana na biblia mikononi kudai haki ya kuchinja. 

Polisi wa Tunduma kazi imewaelemea na ikabidi nguvu itoke mkoani na RPC yupo huko sasa hivi. Juzi kanisani Padre mmoja alitoa kauli kuwa kama hawa watu wanataka kuchinja basi watuchinjie na kitimoto.

Kisa kikuu ni kwamba madalali wa mifugo wamegoma kupima nyama zinazochinjwa na wakristo, hivyo wakristo wanahoji kwanini iwe hivyo. Pia mtaani mabucha ya nyama zilizochinjwa na waislamu zimeganda hakuna wanunuzi.

Raia ilibidi wakimbilie mahakamani kwa kuona kwamba ndiyo sehemu pekee ya usalama kwao, hivyo ikalazimu mahakama kuhairishwa ili kuepusha balaa. Kale kamchezo kakuchoma matairi na kufunga barabara kakawa ndiyo mchezo wa kawaida.

KIM POULSEN ANASTAHILI MKATABA MNONO TAIFA STARS



Hivi karibuni kocha mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametoa mipango mizuri kwa maendeleo ya soka. Kim ameliambia shirikisho la soka nchini kuwa anahitaji kuona kikosi cha timu ya taifa ya vijana Serengeti Boys ikishiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara. 

Kocha Kim anasema, mpango wake ni kutaka kuona wachezaji hao wanakuwa wanacheza mechi za ushindani kwa kila wiki ya mwezi ili kuweza kujijenga kiushindani na kimbinu. Kwa mujibu wa kocha huyo, anasema kama wachezaji wa Serengeti Boys wataweza kucheza mechi moja kwa wiki, kisha wakafanikiwa kushiriki michuano yote ya Ligi Kuu basi hakuna shaka kabisa watakuwa kwenye ushindani mkali watakapopewa nafasi ya kuchezea timu ya wakubwa.
Kocha Kim anasema, wachezaji hao vijana wanatakiwa kuchezea timu ya taifa kwa muda kisha wakifikisha umri wa  kuvuka Serengeti Boys basi watarudishwa kwenye klabu zao ili kupisha wengine waweze kutumika katika kikosi hicho na kushiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Dhumuni la kocha huyo ni lilelile kuwafanya wachezaji wengi vijana wakipata nafasi na kucheza soka la ushindani wakati wote. Pia kocha Kim anakusudia kujenga kikosi bora cha miaka ijayo hivyo hakuna wasiwasi kuwa kati ya mwaka 2015 au 2017 tanzania inaweza kabisa kushiriki michuano ya Kombe la mataifa ya Afrika pamoja na kombe la dunia mwaka 2018 nchini Russia au 2022 nchini Qatar. 

Nilipotafakari programu hiyo upesi nikakumbuka namna kocha Marcio Maximo alivyoweza kuishirikisha timu ya taifa ya vijana kwenye michuano ya kombe la taifa ambalo linashirikisha mikoa yote ya jamhuri ya muungano wa Tanzania. Moja ya faida hizo ni kumjengea uwezo mshambuliaji wa TP Mazembe, Thomas Ulinwengu ambaye alishiriki kikamilifu kwenye michuano hiyo. 

Kwa wengine sasa wanaona Thomas Ulimwengu amekuwa mshambuliaji hatari na hodari zaidi, lakini njia alizopitia zimemjengea umakini na uhodari katika soka, ambako sasa anaweza kupambana na washambuliaji hatari klabuni kwake kama Kaluyituka, Given Singuluma, na wengineo. 

Kwa mtazamo wangu uamuzi wa kocha Kim kuliagiza shirikisho la soka nchini TFF kuhakikisha Serengeti Boys inashiriki mechi za Ligi Kuu Tanzania bara kuna lengo moja tu kuhakikisha anakuwa na kikosi imara zaidi cha timu ya taifa ya wakubwa(Taifa Stars). 

Ukiangalia rekodi za kocha Kim na namna anavyoweza kujenga kikosi chake katika timu ya taifa, hakika amekuwa kocha wa kipekee sana. nasema hivi sio kwasababu ya matokeo mazuri, bali muundo wake wa utendaji kazi na namna anavyoweza kutufahamisha makosa yetu kwa hekima. 

Kim anajua kabisa tulichokosa ni misingi ya soka la vijana kwahiyo anachofanya ni kuhakikisha tunakuwa na hazina ya kutosha katika soka la vijana kupitia timu ya taifa. Wakati Kim akisema hayo wenyewe tunafahamu kuwa tuna michuano miwili muhimu sana ambayo inawajenga vijana lakini bado haionekani kuwa imara kiushindani. Mfano michuano ya Copa cocacola na michuano ya Uhai. 

Hii ni michuano inayohusisha timu za vijana ambazo kwa namna moja ama nyingine zinapata faida, lakini hakuna mwendelezo wake. Kwahiyo kocha Kim amegundua moja ya sababu za kushindwa kuwa na mwendelezo ni gharama za uendeshajiu, kwahiyo anaamua kupunguza gharama hizo kwa kuitumia timu ya taifa ili iweze kusaidia kuzalisha wachezaji imara. 

Pia anaikumbusha TFF kuwa hakuna njia ya mkato kama inataka wachezaji wazuri zaidi ya kuwekeza ikibidi shirikisho lenyewe kuwa na kituo chake. Kwa mantiki hiyo badala ya kuwkusanya vijana huko mitaani na kuwapeleka uwanja wa Karume, kocha Kim anatumia timu ya taifa kama mahali pevu ambapo pataleta hamasa kwa vijana na kuongeza ujuzi wao kipindi wakirudi kwenye klabu zao. 

Pili, hii itazisaidia timu zetu kama Yanga na Simba ambazo mara nyingi zimekuwa zikisubiri wachezaji walioko timu ya taifa ndio wawasajili. Namna gani kocha Kim ataweza kuwaendeleza wachezaji watakaofanya vema kwenye kikosi cha Serengeti Boys? Hilo litateguliwa kwa kumuongezea mkataba mpya ambao utamfanya ajikite zaidi kutengeneza timu imara za timu za taifa akishirikiana na makocha wazawa. 

Nimalize kwa kusema, hakuna jambo baya kama tutaruhusu kuondoka kwa kocha Kim Poulsen wakati huu ambapo ametuonyesha falsafa bora kabisa ya soka letu. Ni vyema TFF na serikali zinaona umuhimu wa kuongeza mkataba mnono kwa kocha huyu. Muhimu tuache blah blah katika hili.

STRAIN THEOTY/CRIMENOLOGY VS UDINI NA DINI=CUHUMI?



Wataalamu kama Robert Merton waliwahi kusistiza umuhimu wa uhalifu katika jamii. Lakini kwa wataalamu hao hao wanasema, ikiwa njia za kujipatia pato zikibanwa au zikibinywa uhalifu ni kitu kinachochukua nafasi ambapo watu hutafuta pato kupitia njia zozote zile ikiwemo uhalfu. 
 
Wakasema kuwa kuna umuhimu wa uhalifu sababu unaileta jamii pamoja. Jamii inakuwa kwenye kutafuta njia mwafaka kumaliza uhalifu, lakini lazima jamii hiyo ijitolesheleze ndipo tunaweza kuufanya uhalifu kumalizika. .......

Naam kama nchi yenu haiongelei suala la ukuzaji uchumi, itaongelea nini? Kama tumeshuhudia watu kule Mwanza wanauana kisa HAKI YA KUCHINJA na kuvaa mavazi ya DINI kisha kumwaga damu, nini tafsiri yako? Je, umewaona wanaoshiriki zoezi la kuuana ni watu wa namna gani? ....je wale wanawezaje kuachwa katika faili la UCHUMI? Hatuna uchumi imara lakini hatutakiwi kuacha kutafuta UCHUMI imara.   

@Nakupenda sana nchi yangu TANZANIA. 

Hatutendi haki hata kidogo kutoandika 'aya' za uchumi wetu ambayo ndio msingi wa taifa letu na kumwachia Rais wetu Kikwete akihutubia mambo machache. Labda afadhali hayo machache kuliko kukosa kabisa. Kama tunataka kujenga utamaduni wa kutomwambia basi tunajenga taifa la watu wasioweza kufikiri au taifa la watu wanaopendelea mambo mepesi. 

Hatukatai kuona kuwa hotuba ya rais wetu haiwezi kuwaridhisha watu wote, lakini mimi naona kuna haja pia kuwakumbusha wale wote wanaohusika kuwa, wajaribu na waweze kufanya kitu ambacho kinaakisi jamii yao. Kama tunakubaliana kwamba uhalifu ni kitu kinacholeta jamii pamoja, na kwamba lazima jamii ijitosheleze basi yatupasa kujiuliza itajitosheleza katika lipi na kwanini? 

Lazima tumfanye rais wetu awe 'mgumu' kwa maana mtu 'mzito' kwa hoja nzito. Kwahiyo tusitegemee kuwa Rais anaweza kufanya hilo pekee bali lazima tusaidie, lazima kumfanya awe bora sababu ni mali yetu na tunajivunia yeye. Lakini kama kuna watu wanadhani kukosoa hotuba ya Rais ni dhambi ati sio saizi yetu hatuba budi kusema labda akina sisi tunaokosoa tumechanganyikiwa na tunakaribia kuchojoa nguo. 

Ni jambo baya sana tunapoona kila mtu anadhani waandishi wa hotuba ya Rais wanajua kila kitu. Lakini wanayo fursa ya kupata tafiti za kisasa za uchumi, makabrasha na kadhalika ili kuweza kuelezea jambo la msingi kuhusu hali ya maisha ya watu wetu. 

Ni vigumu sana kuamini kuwa Rais wetu anaandikiwa hotuba nusu, labda wenzetu walisahau, ila nakumbusha kama huijui jamii yako basi unaelekea kuchanganyikiwa. Turuhusu waandishi wa hotuba ya rais wawe hodari kwa kuwajengea hoja zenye maana sio kuwatusi. Tuwape nafasi ya kujisahihisha sababu wao sio miungu hata kidogo..

SERIKALI YASHIKILIA MSIMAMO SAKATA LA LOLIONDO



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI     kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema haitabidili kamwe  maamuzi iliyotoa kuhusu Pori Tengefu la Loliondo, mkoani Arusha na kuwataka wanaharakati wanaochochea mgogoro wa ardhi katika eneo hilo kuacha mara moja.

Tamko hilo la serikali, limekuja muda mfupi baada ya watu mbalimbali kutoa maoni yao kwenye mitandao na vyombo vya habari kwamba uamuzi wa
serikali kuhusu pori tengefu si sahihi.

Tamko la serikali lilitangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki hivi karibuni kwamba, wameacha  kilomita za mraba 25,000 kwa ajili ya wananchi na serikali imechukua kilomita za
mraba 15,00 kwa ajili ya kutunza rasilimali za nchi.

Alifanya hivyo kwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya 16 Vifungu Na. 4, 5 na 6 na kwamba muda mrefu viongozi wa wizara wamekuwa wakikutana na wananchi na viongozi wa mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro kujua kero zilizopo ili zitatuliwe na ndio imewezesha serikali kufanya uamuzi alioufanya.

"Ukweli ni kuwa Waziri Kagasheki alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu kupunguza eneo la pori tengefu la Loliondo kwa mujibu wa sheria inayompatia waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila
kuathiri uhifadhi,"alisema George Matiko, ambaye ni msemaji wa wizara.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, Matiko alisema tamko lilizingatia tafiti mbalimbali ikiwemo utafiti wa  Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro wa Loliondo ikiwemo ya Waziri Mkuu iliyoundwa mwaka juzi.

Aliongeza kuwa eneo la kilomita za mraba 1,500 litaendelea kumilikiwa na wizara kwa mujibu wa sheria na kwa kutambua kuwa ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori, mapito ya wanyamapori na vyanzo vikuu  vya maji kwa hifadhi mbalimbali ikiwemo Serengeti.

Alisisitiza ardhi iliyobaki baada ya kuondoa eneo la pori tengefu la Loliondo itasimamiwa na vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999 na wananchi watawezeshwa ili waanzishe Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika ardhi hiyo kwa manufaa
yao.

"Tanzania inajali uhifadhi lakini pia inajali maslahi ya wananchi, ndiyo maana asilimia 25 ya eneo la nchi hii limehifadhiwa bila kuwepo migogoro. Hakuna migogoro kati ya wananchi na Serikali, kwa kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa uhifadhi kwao na kwa vizazi vijavyo.

Ndiyo maana wananchi wanachangia kwa kiwango kikubwa katika kufanikisha uhifadhi,"alimaliza Matiko.