May 25, 2013

TUMETAYARISHA AJENDA GANI KWA OBAMA?

Markus Mpangala
Ziara ya Barrack Hussein Obama inaelekea kuwagusa wengi mno. Baadhi yetu tunaguswa na idadi ya watu watakaokuwepo kwenye ziara hiyo, ambao ni 700. Wengi wanajaribu kujiuliza ni kwanini Obama akae siku 4 nchini Tanzania. Lakini kwangu mimi muhimu sio siku zake atakazokuwepo hapa wala idadi ya watu atakaoambatana nao. Jambo muhimu kwangu ni Tanzania.
Naam, rais mstaafu George Bush alikaa hapa siku kama hizo hizo. Lakini wengi walidhani matokeo ya ziara yake ni siku chache ama zaidi. Sasa Obama anakuja, haendi Kenya, bali anakuja Tanzania. Hata hivyo tuendelee kufikiri zaidi kibiashara,uchumi na ushindani wa siasa za kimataifa baada ya ujio wa Xi Jinping.
Jambo muhimu kwetu ni kuangalia namna gani tutaweza kuzungumza na Obama katika masuala ya kibiashara na ushindani wa kimataifa kuhusu siasa na uwekezaji. Hatuwezi kuketi chini na kulalamika kuwa Obama anakuja na wageni wengi ambao hawana msaada kwetu. Lazima tutambue kuwa ujio huu unaitambulisha kwa namna nyingine nchi yetu ya Tanzania katika ulimwengu.
Wengi watakuwa wakijiulzia kwanini Rais huyo amekuja Tanzania na sio sehemu nyingine. Ni kweli kwamba Obama atakuwa na ziara katika maeneo mengine ambako anatarajiwa kuzungumza na viongozi mbalimbali. Katika mfumo wa siasa za kimataifa, ujio wa Barrack Obama ni mbinu ya kujaribu kufukuzana na China ambayo ilishamleta Rais wake Xi Jinping.

Rais huyo wa China aliihutubia dunia akiwa nchini Tanzania na alitumia lugha yao ya kichina. Sio hilo tu bali pia Rais huyo aliingia mkataba na nchi yetu ambayo mojawapo ni ujenzi wa bandari ya Bagamoyo ambapo China itakuwa msimamizi kwa kipindi cha miaka 50.
Kwa namna nyingine mkataba huu unaleta kizazi zaidi ya kioma kilichopo hapa nchini. Kwamba kizazi kijacho kitaachiwa urithi unaoonekana hivyo kuona manufaa ya uhusiano wa China na Tanzania. Kwa upande wa Obama, ziara yake lazima itakuwa na masuala ya sera za uchumi na kutengeneza njia ya maslahi yake kama ambavyo George Bush alifanya.

Kwahiyo ili kufanikisha yote haya lazima tukubaliane tunahitaji kushirikiana na wengi kote duniani hata kama washirika wetu wana desturi ya kuwa walaghai au kuwa na ksumba za kuwa nduli kama Idd Amin. Ili tuweze kuitangaza zaidi nchi yetu tunahitaji fursa kama hizi kujitokeza. Lazima tukubali tutaingaza nchi yetu mwaka huu kwa namna mbili kuu ambazo ni ujio wa Xi Jinping na Barrack Obama.
Lakini ujio huu sio kitu ambacho mwananchi anaweza kudhani sadaka bali anachojua ni wazi kuna maslahi yanafukuziwa hapa ambapo watanzania wana mali nyingi katika ardhi na mengineyo. Wananchi wanataka kujua ni ajenda gani ambazo tutaweza kuzungumza na Obama, au mwingine yeyote atakayekuja.

Tunafahamu ushindani uliopo kwa upande wa Mashariki ya Kati ambako mataifa haya ya China na Marekani yanajaribu kujenga misingi yao na kulinda maslahi yao. Sisi tunaonekana kuwa washirika wazuri wa mataifa haya. Lakini ingefaa zaidi nitoa angalizo kuwa katika ushirika huu lazima tukubaliane kuchukua hatua stahiki ili kuleta manufaa kwa wananchi wetu.

Sidhani kama tunahitaji kuelezwa mengi katika misingi yoyote iwe kijeshi, kiuchumi, kisiasa na kadhalika, yatupasa kuona kile ambacho tunatakiwa kukiona. Obama anakuja kulinda maslahi na kuendeleza misingi iliyoasisiwa na Bush. Obama anakuja kuwakilisha nchi yake, asilani tukaeti chini na kudhani tabasamu lake litakuwa la huruma kwetu.

Tunafahamu kuwa Marekani imejeruhiwa sana kiuchumi na inahitaji kujipanga na kuendeleza utawala wake kiuchumi. Kuna hali ya wazi kabisa afrika kuwa kitovu cha sera za nchi za mataifa mbalimbali kwahiyo hakuna njia ya mkato ambayo inatutweza kupata manufaa kama hii ya kuzungumza nao tukiwa na ajenda zenye maana mezani.

Lazima tujitarishe na kuamini kuwa ulinzi wa maslahi yetu ni jambo lenye maana sana hivyo hakuna sababu ya kuogopa kuweka sera zetu wazi mbele ya Obama na timu yake ya watu 700. Hakuna sababu yoyote ya kuhofia ujio huu kwanini kwa namna nyingine unaikumbusha dunia kuwa kuna taifa linaitwa Tanzania.
Ziara ya wkanza ya Obama akiwa Rais aliifanya nchini Ghana, ambako alizungumzia mengi sana. Sasa kwanino Obama ameichagua Tanzania? Lazima tukiri kuwa Ghana ni miongoni mwa nchi zenye ushawishi mkubwa sana kwa afrika magharibi ukiacha Nigeria hususani masuala ya uchumi na demokrasia. Kwa upande wetu Tanzania ni nchi yenye ushawishi mkubwa katika ukanda wa kusini mwa janwga la sahara.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinasimama mstari wa mbele kulinda maslahi ikiwemo kuendeleza misingi ya waasisi wa SADC. Tanzania ni nchi yenye ushawishi mkubwa sana katika ukanda huu na moja ya mambo yatakayojadiliwa sina shaka kabisa kuhusua hali ya Zimbabwe. Hali ya Zimbabwe sote tunaifahamu, na kwa eneo la kisiasa sina shaka kabisa itakwua moja ya ajenda za Obama katika ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara.

Ni wazi Jacob Zuma hana ushawishi wowote mbele ya Robert Mugabe ndiyo maana alisuswa alipotembelea Zimbabwe. Ni Tanzania ndiyo ilifanikisha uelewano chini ya Rais Kikwete ambaye akiwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika alifanikisha timu ya Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini kumaliza mzozo wa taifa hilo. Kwa maana hiyo watanzania lazima tukae chini na kuwahimiza watawala wetu wajipangie ajenda za msingi katika maongezi yao na Obama.

Lazima tukubali pia Obama anakuja kulinda maslahi ya nchi yake. Hakuna sababu zozote za kuficha hisia zetu, bali tuwahimize na kuwaambia twahitaji kuweka sera za wazi na zenye maslahi kwa taifa letu. Nafikiri yale yaliyoandaliwa na watawala wetu kuzungumza na Obama yanapaswa kuongezwa kwa kiwango chochote kile, ambacho iwe zaidi ya uwekezaji. Muhimu ni kusubiri ajenda yetu itakayowezeshwa na watawala wetu na kuinufaisha Tanzania.

May 23, 2013

SHAIBU NNUNDUMA ATEULIWA KUWA MKURUGENZI WA WILAYA YA NYASA

Na Hoops Kamanga, Mbamba Bay
Halmashauri ya Wilaya mpya ya Nyasa imepata mkurugenzi wake ambaye atasimamia shughuli za wilaya hiyo. Mkurugenzi huyo ni Shaibu Nnunduma, ambaye ni Afisa Kilimo kitaalamu, ameteuliwa kuongoza wilaya ya Nyasa baada ya kufanya kazi wka ufanisi mkubwa alipokuwa wilaya ya Mbinga.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Nyasa, Ndugu Shaibu Nnunduma alikuwa mkurugenzi wa wilaya ya Mbinga. Shaibu Nnunduma alikuwa Mkuu wa Idara ya kilimo Masasi kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Bukoba kisha akapelekwa wilaya ya Mbinga.

Nnunduma ana shahada ya kwanza na ya pili za kilimo ni mwenyeji wa mkoa wa Lindi. Anasifika kwa kufanya mabadiliko makubwa sana ya kimaendeleo katika wilaya ya Mbinga kwa muda aliofanya kazi wilayani humo. Mojawapo ni ujenzi wa barabara za lami katika mitaa na uwekaji wa taa za barabarani na sasa ujenzi wa stendi ya kisasa mjini Mbinga.
PICHANI; Shaibu Nnunduma akizungumza na wakulima kuhusu namna bora ya kilimo cha kisasa.

May 20, 2013

JAMES ZOTTO: WANAFUNZI NI WAZEMBE, WAVIVU KUPINDUKIA


Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
 
Hatua ya Serikali kufuta matokeo ya mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka 2012 yamepokelewa kwa hisia tofauti. Baadhi ya wataalamu wa sekta ya elimu wanaona serikali haikuwa makini kufanya uamuzi wa kufuta matokeo hayo, kwa madai uamuzi ulichukuliwa kisiasa zaidi badala ya taalamu. 
Baadhi ya wataalamu wanatetea ufanunuzi uliotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani nchini, Dk. Ndalichako. Katika baadhi ya mitihani wanafunzi waliandika mashairi ya nyimbo za muziki, wakachora picha za wachezaji mfano Lionel Messi na wengine wakachora picha za filamu za Zombi. 

Hali hii iliwashtua wengi na kuona mwelekeo mbaya wa sekta ya elimu nchini. Pamoja na wazazi kulalamikia hali hiyo bado wameshindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya watoto wao hivyo kuendelea kuilalamikia serikali. 

“Ni mkanganyiko tu! Serikali inatoa ufafanuzi ambao ukiuchambua unaona hauendani na hasira za Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani, Profesa Rwekaza Mukandala. Baraza limefanya kazi yake kitaalamu, lazima tuheshimu. Ningewaona wa maana sana kama wangekuja na suluhu ya kuondokana na matatizo mabovu.  Viongozi wa sasa walipata elimu bora zamani, lakini leo wanasimamia matokeo machafu, siasa na dini zinatuathiri katika kuiangalia NECTA,” 

Hayo ni maneno mazito ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, James Zotto. Hakuishia hapo, akaongeza kwa kuchambua zaidi uamuzi wa serikali juu ya kubatilisha matokeo hayo. 

James Zotto alitoa mfano muhimu ambao unahusisha baadhi ya wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao waliwahi kuomba kazi, lakini hawkauwa na weledi wa kutosha licha ya kuwa na matokeo mazuri sana katika vyeti vyao. 

“'Msomi mmoja alimaliza Chuo mkoa mmoja wa Kaskazini mwa Tanzania, akaomba kazi katika Idara yetu. Siku ya usaili nikamweleza ataje vitabu vitano alivyosoma katika fani yetu! Lakini cha kushangaza alishindwa kabisa. Nikamkumbusha tafiti za  Walter Rodney, akasema anafahamu. Huwezi amini nilimhoji tena, nikauliza What is the main thesis of  the book? Akashindwa kujibu, nikabaki kushangaa tu, nikajiuliza hivi hii elimu ikoje ambapo mtu ana matokeo mazuri lakini uwezo wake ni mbovu? Nikamuuliza kwa Kiswahili swali jingine, ‘Paradigm'  gani  ambayo Walter Rodney ameandika? Cha ajabu akashindwa kujibu. Sikuchoka, maana nilitaka afahamu umuhimu wa kuielewa fani yake sio matokeo yake kwenye vyeti tu, nikamuuliza kitabu gani anakipenda sana na  kinamvutia? Hakika alishindwa kujibu, ina maana hakuwa akisoma kitabu chochote, huku akijivunia matokeo mazuri kwenye vyeti vyake. Msomi huyo alikuwa GPA ya 4.6.” anasema Zotto.

“Leo hii serikali inafuta matokeo na kuwadekeza wanafunzi wavivu na wazembe kama hawa. Wahitimu Wwengi  laiti kama wangekutana na usaili Upya kabla hata ya kuonesha GPA zao, lazima wanataalamu tuone fedheha sana. Sisi wakati tunasoma tulikuwa tunataabikia katafuta shahada zetu, hawa wanafunzi wa siku hizi wanacheza sana ten asana, na hayo yaanzia huko chini ambako leo wanadekezwa na serikali nzima. Wanafunzi wa siku hizi wanapewa swali halafu wanamfuata mwalimu ofisini kuuliza, hivi hili swlai lina maana gani? Hawa wanafunzi wanauliza hivi wakati vitabu vipo lakini wanaona tabu sana, unadhani kusahihisha upya matokeo kutashindwa kuwadekeza?, anasisitiza Zotto.
Anaongeza kuwa, “Iko wapi Lambart, ambacho ni mkate wa somo la Jiografia, Kozlov, Wadada na Budere, na Walter Rodney? Sisi tulisoma haya yote tukiwa kidato cha tano na sita na tulipoyaona Chuo hatukushangaa. Tuliweza kutoa mifano na kuthibitisha hoja mbalimbali, ndipo tukaanza kukariri kurasa hadi kurasa eti leo wanafundisha wanafunzi majibu na maswali, ndio vitabu vyao vya leo. Uwezo wa kufikiri kwa kupambanua (Analytical thinking) umepungua sana,”

Alipotakiwa kueleza ni kwanini anadhani kuna tatizo la kupungua kwa uwezo, akasema, “Nimesama hayo kwakuwa nimejiuliza kwanini miaka ya hivi karibuni watu wamemaliza shahada na wanarudi kuunganisha shahada ya pili. Wengne hata kazi hawataki, nikajiuliza, je, ni hamu ya kuongeza elimu tu? Kazi ni shida? Ushindani mkubwa au kupanda madaraja kirahisi? Nikagundua kuwa elimu yetu haijajitoleleza vizuri kutatua matatizo. Je, hizo shahada za pili zimesaidia kutatua kama haya ya matokeo ya wadogo na watoto wetu huko sekondari? Hapo jibu ni hapana,” anasema James Zotto.

“Tumepoteza, the purpose of education, ambayo Mwalimu Nyerere alituachia. Binafsi nilijiona nimekamilika baada ya kumaliza kidato cha sita kuliko hata nilipomaliza Chuo Kikuu, tuliandaliwa kujitegemea kujenga hoja na kufanya kazi, lakini sasa naona kabisa kuna ombwe kubwa,” anasema Zotto

Anaongeza kuwa, “Mwalimu Nyerere alitaka elimu yetu iwe imekamilika kila hatua na kila hatua imsaidie mhitimu atatue  matatizo yake na ya jamii. Je, darasa la Saba la leo, Kidato cha Nne, cha Sita, Cheti, Stashahada vinajitosheleza? Nafikiri tutasoma hata Uzamivu na itakuwa bado. Itabidi tutafute elimu kubwa zaidi ya Uzamivu huenda ikatosha. Tujikague.”

“Labda nikuulize swali la kizushi, ungesikia Dk Ndalichako katangaza daraja la kwanza wamepata wanafunzi asilimia 80 na sifuri hakuna, kisha wengine wamepata asilimia 20 wapo katika, je ungempongeza Dk Ndalichako? Lazima niwe mkweli katika hili la kufutwa mitihani kwa vile wanafunzi hawa wa siku hizi nawafahamu, pia nafahamu kuwa Dk. Ndalichako ni mtu kati ya wachache wanaoheshimu  taaluma zao, waliposema walikubaliana wapitishe matokeo na NECTA ikatoa sahabu zake, mbina hatuambiwi waliyokubaliana ni yepi? Je, ina maana kuna matokeo ya makubaliano na yaliyotolewa na NECTA? Ndugu yangu tuna matatizo kwenye familia na uendeshaji wa elimu, siasa imeingia na dini pia. Halafu wanafunzi wenyewe hawa wavivu na wazembe tutarajie nini kama kila siku wanamfuata Mwalimu ofisini kuuliza maana ya swali wakati vitabu vipo?” ansema Zotto.