Markus Mpangala |
Hii ni hadithi kuhusu watu wanne waitwao Kila Mtu,Mtu, Mtu na Hakuna Mtu.
Kulikuwa na kazi muhimu kufanywa, na Kila Mtu alikuwa na uhakika kila mtu
angefanya kazi hiyo, lakini Hakuna Mtu aliyefanya hivyo. Mtu alipata hasira kuhusu hili, kwasababu
ilikuwa ni kazi ya Mtu. Kila Mtu aliwaza kuwa kila Mtu anaweza kufanya hivyo lakini
Hakuna Mtu aliyetambua kwamba kila mtu asingefanya hivyo. Na mwisho iliishia Kila Mtu kumlaumu Mtu wakati
Hakuna Mtu aliyefanya chochote ambacho Kila Mtu angeweza kufanya. Mwisho wa hadithi……
Haya sasa tafakari. Je wewe unatumia pesa zako
vizuri? Je una madeni mengi? Je wewe huachishwa kazi mara kwa mara? Nini sababu
zako za kuachishwa kazi? Au ni kwasababu ya kazi yenyewe au yule
aliyekupa kazi? Au ni kwasababu mazoea au tabia fulani ambayo unapaswa
kurekebisha?
Ikiwa hutumii vizuri pesa zako mwenyewe, je
utaweza kutumia pesa za familia? Je unatazama mambo yote kwa mtazamo mbaya? Tafakari mara nyingine. Jipe nafasi ya kufanya
hivyo huku ukijua kuwa kazi inahitaji uelewa, umakini na bidii. Sote tunajua kazi ni za kila mtu hapa duniani. Hakuna mtu ambaye anatarajia kazi ya mtu
itafanywa na mtu mwingine. Kila mtu anajua anahitajika kufanya kazi kwa bidii
ili asimtegee mtu au kumtegemea mtu.
Na kila mtu anahitaji kazi ili aishi vema,
hakuna mtu asiyehitaji familia bora. Kwahiyo ili kutimiza haya ni lazima
ujifahamu. Lakini ujue wajibu wako katika kazi yako. Na ufahamu mipaka ya kazi yako. Fahamu matumizi
yako ya kila siku ili usimlaumu mtu kwakuwa hakuna mtu atakayekusaidia. Fahamu
bajeti yako kwa siku,juma,mwezi, na mwaka. Lazima ujifahamu kila hatua unayokwenda mbele
maishani. Tambua kila mtu anafanikiwa endapo atafuata kanuni za msingi za
maisha.
Hakuna mtu anayependa kuona mtu anashindwa
kufanya kazi yake bila sababu, kwakuwa tu mtu anategemea kufanya hivyo. Na
asipofanya hivyo inakuwa shida na inamfanya mtu awe na hasira dhidi ya kila mtu. Pesa, kazi na maisha ni lazima viwe tofauti ili
kuongoza familia yako. Usitegemee mtu ataongoza familia yako. Hakuna mtu
atakayewaambia wanao wasome kwa bidii.
Ukihitaji kazi, basi hakikisha unayo hoja za
kusema kwa mtu. Je umekabiliana vipi na waombaji wapya wa kazi? Wangapi
wanatimiza wajibu wao katika kazi, maana kila mtu anataka kuona mtu anafanya
kazi yake ipasavyo. Je unalisaidiaje taifa kutokana na kazi yako?
Unafahamu kuwa kutoangalia mambo kijuu juu inakusaidia kujifahamu na kuongoza
vema ofisi yako au kupata kazi mpya?
Unatambua kuwa ndani ya ofisi yako kila mtu
anahitaji cheo ulichonacho? Hakika nakuambia hakuna mtu ambaye hataki kuona mtu
anaishi vizuri. Kila mtu anajua ni lazima afanye kazi na apendwe
na kila mtu. Mtu huona fahari pale anaposifiwa na kila mtu kutokana na
kuwajibika katika kazi yake. Kazi ya kila mtu ni mtu kuifanya kazi yake kwa
bidii na hakuna mtu ambaye anapenda kuharibu kazi yake.
Kwa hakika ndugu zangu mnatakiwa kuwa waelewe wa mambo na kila mtu ajue kuwa unaelewa. Mtu mwenye bidii ya
kazi na kujifunza mambo hachoki kuwatumikia watu, na kila mtu hupenda kufanyiwa
kazi zake vema. Usiwe mtu unayependezwa na mambo yaleyale au
kukubaliana kila jambo kwa mtindo na sababu zilezile. Uwe mtu ambaye kila mtu
anafahamu kuwa akihitaji ushauri basi atakuwa wa kwanza kuwajibika mbele ya
hadhira.
Jipe muda wa kujisomea, fanya tafakari kila
unachojisomea. Natambua kila mtu anachoka atokapo kazini, lakini hakuna mtu
ambaye anapenda kukaa tu ofisini kwake bila kufanya kazi yoyote. Timiza malengo yako kwa kuwatumia watu. Uwe
mtumishi wa kila mtu kulingana na cheo chako au nafasi yako kwa jamii. Kila mtu
anahitaji msaada wako wa nasaha na mengineyo, kwani duniani tupo kwaajili yaw
engine.
Wengine hawa ni kila mtu ambaye anajua umuhimu
wa kuwatumikia. Na hakuna mtu ambaye hajui umuhimu wa hili. Je unadhani kazi ya
mtu ni ipi? Na hadithi hii ya kila mtu inakupa funzo lolote?
Na inawezekana ndugu yangu umekata tama ya maisha. Lakini tambua kila mtu
amepitia kwenye milima na mabonde. Hakuna mtu aliyefika kileleni bila kuanguka.
Kila mtu anayepanda mlima Kilimanjaro kuna
mahali aliteleza au kuanguka. Hakuna mtu ambaye amefanikiwa bila kuchoka,
lakini unahitaji nidhamu zaidi ya kuchoka kuliko kuendelea kudhani kila mtu
anaweza tu kufanikiwa akikaa sebuleni na kuota amefanikiwa.
Unachotakiwa kufanya ni kusema katika kazi za
mtu basi wewe ni kila mtu na hakuna mtu anayeweza kuifanya kazi hiyo zaidi
yako. Waingereza wanaomsemo wao, simama uhesabiwe vinginevyo
kaa chini usahauliwe. Kwa maneno hayo inamaana
hakuna mtu muhimu katika maisha yako zaidi ya wewe. Hebu rudi juu usome falsafa
ya leo ya Kila Mtu, Mtu, Mtu na Hakuna Mtu. Halafu jifahamu wewe ni nani kati
ya hao wanne.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako