Na James Zotto, University of Dar es Salaam
Ndugu zangu watanzania, naamini mnafuatilia vizuri tatizo la mpaka wetu wa ziwa Nyasa na Malawi! Na pia mmefanikiwa kusikia au kusoma hotuba ya Waziri wa Mambo ya nje, Benard Membe. Nilishtushwa kidogo na hotuba hiyo. Niharakishe kusema, mimi napenda utaifa wangu na uzalendo wangu. Lakini napenda sana kutetea mambo yangu kwa kukubali ukweli, kujua hali halisi, kukubali hata zile zinazonipinga, ili nami nijipange kujenga joja. Niongeze tu kuwa, eneo hili nafanyia study yangu ya PhD. Sidhani kama nipo sahihi zaidi na lengo langu si kusema nani anamiliki nini!
James Zotto akiwa pembezoni mwa ziwa Nyasa.
Ukweli ninaofahamu, tatizo si kubwa sana kama tunavyolifikiri, na pengine tutachukua muda kupitia nyaraka zote muhimu.
Kwanza, tunahitaji kwenda Idara ya Kumbukumbu ya Uingereza(Public Records Office). Pili tunapaswa kufuatilia Colonial Archives Potsdam, Ujerumani.
Aidha, tufuatilie pia Malawi National Archives, Tanzania National Archives, Maktaba Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM) na Chancellor College Malawi. Ninaamini ubishi utaisha kwa kuwa nyaraka zote zipo.
Naomba nianze kujadili kwa kuweka angalizo katika suala hili ili ikilazimika, Malawi wasalimu amri kwa njia yoyote tutakayoamua, nitasema hapo baadaye.
Angalizo lenyewe: ziwa Nyasa liligawanywa na mabeberu wa Kiingereza, Kijerumani na Kireno. mkataba wa mwaka 1890 uitwao Anglo-German Agreement, unasema mpaka wa uliokuwa miliki ya Ujerumani au kwa kiingereza German East Africa (Tanzania Bara ya leo) na Nyasaland (Malawi ya leo) unapita kando kando ya ziwa Nyasa kutoka mto Ruvuma(mkoani Ruvuma) mpaka mto Songwe(mkoani Mbeya).
Mkataba huo upo katika nyaraka nyingi sana. Mathalani katika Sheria za Kimataifa (International Law) wanafahamu jambo hilo na sina shaka ndugu zetu wanasheria wa kimataifa (International Lawyers) wanaelewa nini nazungumza!
Sehemu nyingine ilikuwa ya mkataba ilikuwa mwaka 1891 kati ya Ujerumani na Ureno. Kulingana na mkataba huo, walikubaliana kuwa mipaka ilianzia mto Ruvuma kuelekea Portuguese East Africa (Msumbiji ya leo).
Mkataba mwingine ulikuwa ni kati ya Ureno ambayo ikawekeana mipaka na British Nyasaland (Malawi), kwahiyo, kipindi cha Ujerumani, mipaka inasomeka 'it passes along the shore of the lake (Nyasa).”
Hata hivyo kuliwahi kutokea mabadiliko ya mipaka hiyo. Mabadiliko ya mipaka yalianza kipindi cha ukoloni, kabla ya Ujerumani kuondoka.
Kikwete na Banda
Marekebisho ya mipaka yalifanyika kati ya Ujerumani na Ureno kwa kusogeza mipaka mbele na kutamka, “0.5 KM from the original tripartite point” na vijisiwa vya mto Ruvuma vikagawanywa. Mipaka hiyo ipo hivyo hadi leo.
Na eneo lingine ni kati ya Uingereza na Ureno, ambapo, kisiwa kilichopo eneo la Malawi kinamilikiwa na Msumbiji mpaka leo na eneo la ardhi lililopo Msumbiji linakaliwa na Malawi.
Huo ulikuwa mkataba wa marekebisho na ipo hivyo mpaka leo. Kwahiyo, tulivyorithi mipaka, tumerithi na mabadiliko haya na hivyo hatuwezi kugombana na Msumbiji wala Msumbiji hawawezi kugombana na Malawi.
Mpaka wetu na Malawi haukurekebishwa popote pale mpaka Ujerumani ilipoondoka nchini. Nafikiri viongozi wajiandae pia kwa hili ili tuweze kuwashinda ndugu zetu wa Malawi.
Marekebisho ya mipaka kipindi cha Uingereza:- sote tunajua German East Africa, ni sisi(Tanzania) pamoja na Rwanda na Burundi tuligawanywa katika sehemu kuu mbili.
Mosi, tulipokuwa chini ya League of Nations tukiangaliwa na Uingereza. Kuna mambo nahitaji tuweke sawa ili kuongeza hoja kwa mheshimiwa waziri wa mambo ya nje, Bernad Membe.
Tulipokuwa chini ya League of Nations, tukaitwa ‘Mandated Territory’, na Uingereza ikawa ni ‘Mandatory Power’. Turudi katika Kamusi tutofautishe “a an annexed colony and a mandate.”
Mpaka ukawekwa kati ya Ubelgiji na Uingereza, uliitwa The Milner-Orts Agreement of 1922! Naam, katika mkataba huu, mto Kagera ulikatwa katikati , hivyo hadi naandika makala hii mipaka hiyo tumerithi hivyo.
Hapakuna mahali popote pale ambapo eneo la ziwa Nyasa kama palirekebishwa kwa njia ya mkataba baina ya Nyasaland State na Tanganyika State.
Isipokuwa tofauti na Mandates zote, Tanganyika pekee, ilikuwa na tofauti ndogo, ambapo mpaka wake wa ziwa Nyasa ukapewa wanachoita 'Wording'. Na hivyo, ramani ya Tanganyika na Official Records zikaonyesha kuwa mpaka umepita katikati ya ziwa Nyasa!
Hapa ndipo tatizo linapoanza na sisi tumeshindwa kusogea mbele kidogo. Ninachokisema hapa kipo pale National Archives Secretariat Files, Accession Numbere AB 8 na AB 30!
James Zotto akiwasilisha utafiti wake kuhusu mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa.
Nafikiri hotuba yote ya mhehimiwa Waziri Membe imetokana na Files hizo, ndizo walizopelekewa. Ndugu zangu watanzania, ni muhimu kujadili zaidi ya hapo.
Twende mbele kidogo, ni kweli kama mheshimiwa alivyosema katika hotuba yake, ramani nyingi kuanzia mwaka 1922 hadi mwaka 1939 zinaonyesha mpaka upo katikati ya ziwa Nyasa!
Je, ukweli huu utatutosha pekee mbeleni tukifikishana mbali? Hapana, tuendelee kusaidiana kwa hili, nafikiri ujumbe utawafikia tu.
Waziri Membe hakusema kuwa ramani zingine, japo chache muda huu na Official Reports hazionyeshi mpaka au zinaonyesha mpaka upo chini. Lakini ni chache! Kwanini hili?
Bado natafuta majibu, lakini kwa haraka, tunaweza kusema kuwa Uingereza ilitamani Tanganyika iwe koloni lake na si Mandate! Na pia ilishinikizwa na wawekezaji na hata jeshi ilisema afadhari waiteke ili liwe koloni na waachane na Mandate!
Nahitaji tuelewe maana ya mandate. Hii yote ilitokea baada ya gavana Donald Cameroon, wa Tanganyika kusema kuwa “Tanganyika is a part of the British empire and it will remain so”.
Hii ni siasa na si ukweli kama unaelewa maana ya kuwa wao hawakuwa wamepewa koloni kama mali yao, bali kuliangalia hadi wananchi wapate 'akili' ili wapewe uhuru!
Kwa hiyo na kimsingi, kwa maana ya sheria ya kimataifa, Tanganyika haikuwa Part ya British Empire kama yalivyo makoloni yaliyotekwa moja kwa moja na Uingereza yenyewe!
Hapa pakatokea mvutano mkubwa sana katika House of Lords na House of Commons! Na hivyo basi, mtafaruku huu wa mipaka ulianzia hapo, hivyo hata waingereza wenyewe walivutana kuhusu mipaka.
Kwa mfano, mwaka 1926, wajumbe wa mabaraza waliibana serikali iseme mipaka ya Tanganyika na ule wa ziwa Nyasa! Mabishano, kama haya yetu leo yalikuwa makubwa, ila si kwa kutishiana kwa kuwa walikuwa wenyewe na walitaka kuwekana sawa!
Rais Kikwete na Joyce Banda walipokutana katika kikao cha SADC mjini Maputo, Msumbiji.
Naam, ndipo Secretary of state for colonies alibanwa na mjadala ulikuwa wa kisheria zaidi ukihoji Status of the Mandate, British Empire n.k, na kama waingereza wana mamlaka ya kujipangia kuhusu koloni walilokabidhiwa kuliangalia(nieleweke na sio kulimiliki koloni).
Mwishowe wenye dhamana(Waingereza) walisema kwamba, hata wao wanashindwa kuelewa, 'What exactly is the sovereignty of Tanganyika lying', jamani mnamwelewa huyu mtu wa kiingereza?
Kwamaana hiyo, haelewi vizuri mipaka yetu, ambayo wenyewe ndo wameirekebisha au kuipa 'Wording'! hivyo, tatizo linaanzia hapa na si muda mwingine wowote!
Jambo kubwa ambalo Waziri Membe hakusema ni hili: kuanzia mwaka 1939, mambo yalibadilika na hawa hawa watu(Wakoloni) tunaochukua ushahidi kutoka kwao, wakafanya madudu!
Na ilipoisha vita ya pili ya dunia, jamani oneni haya, hawa waingereza katika ramani zao, tena nyingi mno, tuangalie East Africana Section ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, katika sehemu ya Thesis, kuna Cabins 3 zimejaa ramani na bado ni mpya sana kutokana na kutunzwa na pia kutotumika sana.
Zinaonyesha, bila shaka yoyote, kuwa mpaka wa Tanganyika na Nyasaland unapita pembeni mwa ziwa na sio katikati! Nieleweke naonyesha tu mambo yalivyo ili tuweze kuchukua hatua zaidi.
Hotuba ya Waziri Membe, iliishia nyaraka za mwaka 1939! Kumbe hawa jamaa walichora tena ramani zote zikionyesha mpaka upo pembeni mwa ziwa! Kwanini hili? Natafuta majibu.
Lakini kwa haraka naweza nikakisia mambo mawili. Mosi, karibu na vita vya pili vya dunia, ilisikika tetesi kule duniani(ughaibuni) kuwa, Ujerumani inarudi na inakuja kuchukua makoloni yake.
Tukitaka kuhakikisha jambo hili, tusome National Archives of Tanzania, Secretariat Files zote zenye kichwa cha habari, 'The future of Tanganyika in British Empire'.
Kwa hiyo, waingereza walihofia kutimuliwa na kurudi kwa wajerumani, na hivyo, wakarudisha ule mpaka wa awali wa mwaka 1890 unaotumiwa tena na Malawi kwa sasa!
Na pia, katika kipindi hicho, baada ya kumalizika vita hivyo, Tanganyika ikawa chini ya Umoja wa Mataifa(United Nation Organisation), ambapo ilipewa Trusteeship Status!
RAMANI YA ZIWA NYASA.
Maana ya hii ni rahisi kuliko Mandate! Kwanini? Hii ilimaanisha ‘to be granted immediate independence’! maana ya neno ‘immediate’ hapa ni kwamba, kwa tafsiri yangu, waingereza walifahamu wanatimka mapema mno kwani mkataba unasema hivyo.
Nafikiri, wakarudisha ramani zikionyesha mpaka upo pembeni mwa ziwa na kitabu cha ‘Nyasaland’ cha mwaka 1958, kinaonyesha mipaka ya Nyasaland na ziwa lote likiwa kwao!
SASA TUFANYE NINI WATANZANIA?
Tukitaka kuwashinda watu wa serikali ya Malawi, lazima tukisome vizuri kipindi hiki na tuelewe ukweli, hoja zipi zinawapa kiburi. Na hoja zipi sisi tuzitumie kupambana nao, tunaweza!
Kwahiyo hatima ya nchi yetu haikujulikani itakuwaje. Kipindi hiki, pamoja na mipaka yake pia, tujiulize, kwa maana ya Mandate, waingereza walikuwa na ‘Legal Authority 'kurekebisha' mpaka wa ziwa nyasa?
Na je makosa waliyofanya waingereza, ndio Legal backing yetu sisi Watanzania? Hebu tuzame tena tutafute ukweli zaidi ili tuwashinde hawa jamaa wa Malawi!
Tulishindwana na Uingereza kurekebisha mipaka. Mwalimu Nyerere, alisubiri hadi Malawi ipate uhuru, ndipo akatoa miaka mitatu tu na asingetambua mipaka ya kikoloni(Soma Hansard, 1962).
Malawi walipopata uhuru, kukawa na matatizo ambayo Waziri Membe aliweza kuyaeleza. Nampongeza kwa hilo, ni dhahiri mwaka 1964 wakati wa mgogoro wa baraza la mawaziri la Malawi, na baadhi ya mawaziri kutorokea nchini kwetu kupitia ziwa Nyasa, Rais Kamuzu Banda akaona ziwa ni infiltration route!
WAZIRI MEMBE akinawa maji ya ziwa Nyasa mjini Mbamba Bay.
Sera zetu za mambo ya nje za Tanzania zilikuwa tofauti na Malawi. Tanzania ilikuwa nchi iliyoongoza ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, wakati wenzetu Malawi wakaunga mkono Makaburu na Wareno na wakawa na balozi sehemu hizo
Rais Banda akagombana na Mwalimu Nyerere, na matukio ya kutishiana kijeshi yalijitokeza kati ya miaka ya 1967-8; matusi na kejeli zikatawala kati yetu na wao.
Tunakumbuka tuliimba, .....kipara cha Kamuzu Banda kina magamba”, tuliimba tukiwa jeshini hayo. Mwalimu Nyerere akasema suala mipaka ni hadi Malawi itakapota Sensible Leader akitokea Malawi ndipo tutajadili tena, sio utawala ule wa Kamuzu Banda!
Kipindi chote hicho tulikuwa kimya, na kuanzia mwaka 1975, hatukuwa na tatizo, lakini sio kusema kuwa tulitatua tatizo la mipaka yetu na Malawi!
Tulikaa kimya! Mipaka haina tatizo isipokuwa ni time bomb ambapo ikitokea rais mwendawazi akamwaga petroli tu, basi ni vurugu kubwa!
Tuliirithi kupitia Article III ya Azimio la Umoja wa Afrika la mwaka 1964(OAU Charter, 1964), baadaya ya majadiliano makubwa na wengi wakaridhia “uti possidetis, ita possidetis principle” (so as you exist, so may you exist).
Kama kawaida yetu tulinakili kanuni za mipaka za kibeberu za Westphalia(Westphalia border inviolability)! Hatukupata muda mwingi wa kutafakari na kuangalia kila mpaka na matatizo yake....tulirithi na matatizo na yanatutatiza leo!!!
UTATUZI WA MGOGORO: Tusonge mbele! Nakiri tuna namna tatu ya kulimaliza;- moja ni kwa majadiliano ya kawaida(Diplomacy) kama Waziri Membe alivyosema katika hotuba yake.
Pili ni kupigana vita (war is another means of diplomacy). Ndugu zangu watanzania nadhani mnataka kuniona kichaa kutamka hilo! Huo ndo ukweli, atakayeshindwa atasalimu kama ilivyokuwa kwa Uganda na sisi watanzania.
WAZIRI WA MAMBO YA NJE, BERNARD MEMBE.
Tatu; ni Mahakama ya Kimataifa(International Court of Justice) hapa nina wasiwasi. Kama nyaraka zenyewe ni zile za Waziri Membe tu, sijui kama tutafanikiwa kushinda kesi.
Tutulie, tuite wataalamu wetu wajikite ndani sana. Ni kweli kama alivyosema Waziri Membe kwenye hotuba yake kwa kunukuu kesi nyingi na zilizoshinda, na kwa kusema kuwa, tukienda mahakama ile sisi ndo tutashinda.
Nina shaka, tumejipa favour ya verdict, kabla ya kesi. Sijui, ila nina shaka kubwa, kuna kushinda, kushindwa au suluhu! Ninashaka tena na tena!
Mimi ni mzalendo, nataka ukweli kwa njia ya mahojiano na kuumiza kichwa, tutetee mali zetu tukijua tunawashinda kwa hoja.
WASIWASI: Inasemekana kuna mafuta ziwani, kwahiyo tujue Marekani na washirika wake hawako mbali! Kampuni ya Surestream ya Uingereza ndio ilipewa leseni ya kutafiti mafuta na utawalawa Bingu wa Mutharika.
Lakini, tujue operesheni ya majeshi ya kibeberu na huyu mama Joyce Banda, ambaye ni mpwa wa Kamuzu Banda, anapata wapi hiki kiburi? Nyuma yake kuna nini na nani? Tuangalie haya pia.
HITIMISHO: Tusiwe na hoja moja tu mkononi kama ndio water-tight evidence yetu kwa serikali na wananchi kwa ujumla. Tujaribu kuzibishanisha hoja zetu. Na hoja nzuri ni zile zinazopingana nasi na tusizozipenda, tukizielewa na kuzikubali ndipo tutajipanga namna ya kuzigalagaza. Tumwelewe vizuri adui yetu. Mungu ibaraki Tanzania, ziwa Nyasa, wanyasa, na watanzania! Tusing'ang'anie tu Reparian Law.
James Zotto ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM).
No comments:
Post a Comment
Maoni yako