October 05, 2017

SHAIRI: PAMBO LA NDOA

NA KIZITO MPANGALA,0692 555 874

Ndoa ni kitu johari, thamani yake nyumbani,
Ndoa usiikahiri, utakuwa matatani,
Ndoa yahitaji siri, zihifadhiwe chumbani,
Pambo la ndoa mapenzi, yenye afya na nidhamu.

Kuvumiliana nako, ni muhimu kwenye ndoa,
Usiupende unoko, utakutia madoa,
Nawirisha ndoa yako, isinuke fondogoa,
Pambo la ndoa mapenzi, yenye afya na nidhamu.

Pambo la ndoa si pesa, ni mapenzi nakwambia,
Hata pesa ukikosa, mapenzi yatafidia,
Ninakuambia sasa, kwa masikio sikia,
Pambo la ndoa mapenzi, yenye afya na nidhamu.

Penzi halina mwalimu, wanandoa mfahamu,
Mlidumishe lidumu, sizungumzi fonimu,
Nisikilize ghulamu, lisikufikie ghamu,
Pambo la ndoa mapenzi, yenye afya na nidhamu.

Mapenzi pambo la ndoa, wanandoa nawambia,
Yaepukeni madoa, ndoa kuwaharibia,
Hamwezi kukokotoa, kwa hisabati na bia,
Pambo la ndoa mapenzi, yenye afya na nidhamu.

Msikilizane vema, jeuri ya fedha noma,
Zungumzeni daima, kwa wema nayo hekima,
Mapenzi yape heshima, mnapoishi daima,
Pambo la ndoa mapenzi, yenye afya na nidhamu.

Migogoro itupeni, mbali isionekane,
Yadumisheni mapenzi, tena mvumiliane,
Msifanye unajisi, na wala msizozane,
Pambo la ndoa mapenzi, yenye afya na nidhamu.

Wasalamu kutamka, sio kauli kukata,
Sasa muda wa uraka, na ulimi unanata,
Ndoa kuwa na viraka, inaongeza utata,
Pambo la ndoa mapenzi, yenye afya na nidhamu.

Na Kizito Mpangala

No comments:

Post a Comment

Maoni yako