October 05, 2017

NINAONDOKA

Ndugu zangu sikieni, mimi hapa naondoka,
Ninahitaji amani, mirindimo nimechoka,
Ninakwenda kwa jirani, hata kama akifoka,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Mitaani kuna mambo, twakimbizana daima,
Yapo mengi machafuko, yananitisha daima,
Yatokea milipuko, inanipatia homa,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Risasi zinasambaa, mirindimo inazidi,
Naishia kutambaa, ninapigwa na baridi,
Ninawasha mishumaa, kufukuza ukaidi,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.


Waasi nao watisha, siwezi kuvumilia,
Mikutano waitisha, mapigano kutulia,
Wakirudi wanawasha, bomu kutufyatulia,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Jirani niwie radhi, hali yangu waiona,
Unigawie ardhi, na wanangu nitapona,
Yaone yangu maradhi, nisaidie kupona,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Siwezi kuishi hapa, na milio ya risasi,
Mabomu yanalipuka, jirani kabisa nasi,
Wanangu hawana raha, wanalala kwenye nyasi,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Ndoto yangu kuwa hai, kila siku nilalapo,
Ninahitaji uhai, na wanangu waliopo,
Hatupuganii chai, amani hapa tulipo,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Ninataka hewa safi, siyo kama iliyopo,
Inanuka tu baruti, inakuwa na uvundo,
Vumbi limetamalaki, mchakato wa mapigano,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Ninataka maji safi, si haya niliyonayo,
Yamechafuliwa maji, ninaumia kwa moyo,
Maji kweli ni uhai, hapa kwetu ni uchoyo,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Nitakuwa mkimbizi, niipate tu amani,
Sihitaji kuwa mwizi, kuna nini duniani,
Hatuna pia mavazi, ni haya tu ya mwilini,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Ninakwenda kwa jirani, nikaipate hifadhi,
Kuitafuta amani, na kipande cha ardhi,
Nipokeeni jamani, niyaondoe maradhi,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Mashamba yangu hakika, yana hali mbaya sana,
Yamegeuzwa uwanja, wa vita kupigana,
Na mimi sina hatia, moyoni ninaumia,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Siasa za kupigana, hazitazaa matunda,
Waasi wanazaliwa, watazidisha ununda,
Mimi sitaishi hapa, moyo wangu unadunda,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Vikao vingi vyafanywa, kukomesha mapigano,
Haionekani dawa, kuponyesha mirindimo,
Nabaki nimeduwaa, naumia kwenye moyo,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Bunduki zinarindima, zimekuwa kama bao,
Siwezi kuishi hapa, penye sauti za ndumo,
Uhai ninautaka, sipendi kuwa na ndweo,
Nianondoka jamani, amani naitafuta.

Kwa herini waungwana, mimi sasa mkimbizi,
Tutakuja kuonana, hadi iachwe bunduki,
Ninahitaji kupona, makovu haya kichwani,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Wasalamu natamka, ninakwenda kwa jirani,
Hapa mimi nimechoka, nianatafuta amani,
Nalazimika kutoka, nikaishi ugenini,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.


Na Kizito Mpanagala

No comments:

Post a Comment

Maoni yako