March 16, 2018

FURAHA, EASTERLIN PARADOX NA MARIANO ROJAS

NA EZEKIEL KAMWAGA
 
JANA, ripoti kuhusu utafiti wa kimataifa ulioonyesha kwamba nchi yetu ina hali mbaya kwenye kigezo cha furaha kwa watu wake ilizua mjadala wa aina yake. Kuna walioupinga utafiti huo moja kwa moja kwa hoja kwamba ziko nchi zina vita wakati huu na haiwezekani wananchi wake wakawa na furaha kuliko sisi. Wengine wakapinga tu kwa sababu huwa wanapinga. Wengine wakaunga mkono kwa sababu za kisiasa tu.

Kitu kikubwa ambacho nilikiona jana ni kwamba wengi wetu tulitoa maoni kabla hata ya kuisoma ripoti yenyewe. Na hili ndilo tatizo kubwa ambalo wengi wetu tunalo. Tunapenda kutoa maoni katika mambo ambayo ufahamu wetu ni mdogo sana. Nafurahi kwamba nilijipa muda kuisoma ile ripoti jana. Hapa chini ni mawazo yangu baada ya kuisoma. Nimeyagawa mawazo yangu katika pande mbili tofauti; kabla ya kuisoma ripoti hiyo na baada ya kuisoma.

KABLA YA KUISOMA
Mimi ni muumini wa dhana kwamba furaha ni jambo gumu sana kulipima kwa mwanadamu. Nimewahi kuandika humu mitandaoni kwamba kuwa na furaha si jambo unaloweza kulipima kwa sababu ya wingi wa mali au marafiki.
Ninafahamu wapo watu masikini wanaokula mara mbili kwa siku – na hili sijasimuliwa maana nimeishi Dar es Salaam kwa maisha yangu yote, lakini nyumba zao haziishi kicheko. Ninafahamu pia watu wenye uwezo wa kuamua wale nini na mara ngapi kwa siku ambao hawana furaha na wengine wamefikia hatua ya kukatisha maisha yao.Hivyo, kuwa na furaha au kutokuwa na furaha ni jambo lenye mambo mengi ndani yake.

Katika mojawapo ya kauli za kukumbukwa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwenye miaka ya 1960, aliwahi kuzungumzia kuhusu furaha ya watu wake. Alisema katika urais wake, hatajihangaisha na jambo la kuwafanya wananchi wake wawe na furaha. Kwa mtazamo wake, si kazi ya Rais kuwafanya watu wawe na furaha.

Alisema atakachohangaika nacho ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote muhimu. Wamasai wapate maji ya kulishia mifugo yao, Watanzania watoke katika lindi la ujinga na umasikini, shule zifunguliwe kila kona ya nchi na mambo mengine. Nakumbuka aligusia kwamba wakati mwingine, yeye akiwa katika jumba la Ikulu hakuwa na imani kwamba alikuwa na furaha kuliko Mmasai aliye porini akichunga ng’ombe wakwe.

Alimuuliza mwandishi mmoja wa Marekani aliyekuwa akimhoji;
“ Unadhani mimi nina furaha hapa Ikulu kuliko Mmasai ambaye ng’ombe wake wana afya na wanapata kila wanachohitaji?”. Kusema ukweli, tafsiri yangu ya furaha inafanana na ya Mwalimu. Ukitaka kuwafurahisha watu, utakuwa na kazi kubwa zaidi. Na hii ni kwa sababu, kuwa na furaha si jambo lenye kanuni moja. Huo ndiyo mtazamo wangu kuhusu furaha kabla hata utafiti ule haujaanza kutolewa (hii ni mara ya sita kutolewa kwa utafiti wa namna hii).

BAADA YA RIPOTI YA JANA
Wakati unasoma ripoti hii, kuna wakati unasisimkwa, kuna wakati unasema mmmh na kuna wakati unacheka. Hii ni kwa sababu walioandika ripoti hii wamegusia maeneo tofauti na kwenye muktadha tofauti.

LABDA TUMCHUKULIE PROFESA JEFFREY SACHS.
Katika utafiti huu, huyu bwana amejikita zaidi katika eneo la afya. Mojawapo ya mambo yaliyoangaliwa na watafiti kwenye kuamua wapi kuna furaha na wapi hakuna ni eneo la umri wa kuishi. Nchi ambazo wastani wa kuishi wa mtu wakati unazaliwa, zina faida kuliko zile ambazo wastani wake ni mdogo.

Sachs amedadavua nchi yake ya Marekani. Utafiti unaonyesha sehemu ambako watu wana kipato kikubwa kuna furaha zaidi kuliko kwenye umasikini. Sasa amechambua kwamba kipato Marekani kimekua sana kwenye miaka ya karibuni lakini cha ajabu furaha imepungua.

Ndipo akaja na dhana inaitwa Easterlin Paradox . Jina la Easterlin linatokana na mtafiti Richard Easterlin aliyegundua dhana hiyo. Kwamba vije nchi watu wana hela lakini hawana furaha?

Akasema ni kwa sababu fedha inatakiwa iendane na vigezo vingine ambavyo havihitaji fedha. Una kampani kiasi gani, unaishi vipi na ndugu na jamaa zako, nani anakuhudumia ukiwa na shida au adha na mambo mengine. Kwa Marekani, anasema Sachs, upande huu wa pili umeporomoka sana nchini Marekani. Watu wana hela lakini wanakula vyakula vinavyowaongezea magonjwa, huduma za afya ni bei ghali na uhusiano wa mtu na mtu umefifia na matokeo yake watu wanapata sononi (depression). Mtu mwenye sononi, hata awe na mabilioni kwenye akaunti yake, hawezi kuwa na furaha.

Kwangu mimi, kitu kikubwa kuliko vyote katika ripoti hii ni kumhusisha Profesa Mariano Rojas kutoka Mexico katika utafiti wa mwaka huu. Yeye amezama katika eneo la Amerika. Amedadavua kwelikweli kuhusu muktadha na mazingira ya bara hilo.

Akaeleza kuhusu kwanini nchi ambazo kuna vita visivyoisha vya magwangwe wa dawa za kulevya, uchumi wa kati, jinai na bangi na cocaine ya kutosha mtaani, ziwe na furaha kama inavyoonekana kwenye utafiti huu. Akasema jambo kubwa la Amerika Kusini ni utamaduni wao. Unakuta kwenye nyumba moja wanaishi babu, baba na wajukuu. Watu wana majirani ambao wameishi kwa pamoja kwa vizazi na vizazi na ule utaratibu wa kufanya kazi na kupumzika na kutenga muda kwa ajili kukaa pamoja na kucheka.

Maneno haya yalinikumbusha wakati mmoja mwaka 2004. Nilikwenda Japan kwa mwezi mmoja kwa ziara ya kikazi na kulikuwa na makundi mengi ya watu kutoka pande tofauti za dunia. Kundi lililokuwa bomba sana lilikuwa la watu wa Amerika Kusini. Walikuwa wanatembea pamoja, wanacheka, wanaimba kwenye Karaoke usiku na walikuwa wanajua kucheza muziki. Mara nyingi nilikuwa najichomeka kwenye kampani yao ingawa sikuwa naijua lugha yao ya Kihispania. Vile vicheko na swaga zao tu vilikuwa vinanikosha.

Kuna nchi kama Costa Rica, zimeamua kutokuwa na Jeshi tangu mwaka 1949. Badala yake, wao wameamua kutoka elimu bure kuanzia msingi hadi sekondari. Ukienda hospitali, dawa zinapatikana bure. Hata kama mzazi hana fedha, wanaye watasoma na wakienda hospitali watatibiwa. Wakati huohuo, akirudi nyumbani atakutana na bibi yake kabla wazazi hawajarudi kutoka kazini. Matokeo yake, jamaa wana furaha sana.

Niliposoma maelezo ya Profesa Rojas, moja kwa moja nikaunganisha na hali ya kwetu Afrika. Pamoja na matatizo ya kipato yaliyopo, bado Watanzania (Waafrika), tunaishi kwa undugu. Mimi nawafahamu watu ambao hawana kazi ya kuajiriwa wala kipato cha uhakika lakini wanakula kila siku – na wengine wanalewa, kwa sababu ya ndugu, jamaa na rafiki zao. Na hapa ndipo ninapofanya ukosoaji wa ripoti hii.

Ripoti imejikita sana kwa Marekani, Ulaya, Amerika na Asia kwa kiasi fulani. Ripoti hii haikuwa na mtu kama Rojas ambaye angeeleza kuhusu furaha, utajiri na umasikini katika muktadha wa Mwafrika. Kama kungekuwa na Mwafrika wa kueleza undani wetu, bila shaka kuna mambo kwenye ripoti ile yangeweza kubadilika. Kwa mfano, kigezo cha kipato na furaha hakina maana sana huku kwetu.

Mfano wa pili ni kigezo cha ukarimu. Swali lililoulizwa na watafiti kwenye utafiti ule lilisema; “ Je, umewahi kuchangia mfuko wowote wa kusaidia ubinadamu?”. Hili swali kwa Afrika ni tata. Ni kweli kwamba Afrika haina mifuko ya kusaidia ubinadamu kama wenzetu walivyo na vitu kama Oxfam nk. Lakini hilo halimaanishi kwamba sisi si wakarimu.

Ni kawaida kwa Mtanzania mmoja kuhudumia familia tatu; ya kwake na mkewe, ya wazazi wake na ya mwenza wake kama yuko kwenye ndoa.
Labda nitoa mfano wa Mwalimu Nyerere. Kwenye kitabu cha
“Tukimbie wakati wengine wakitembea”, ilielezwa kwamba kuna wakati nyumbani kwa Nyerere kulikuwa na watu takribani 34. Mtu mmoja, Nyerere alikuwa na jukumu la kuwalisha na kuwahudumia watu wote hao!

Huyu, angeulizwa kwenye utafiti huu, swali ambalo limeulizwa, angeonekana hana ukarimu kwa sababu hajachangia mfuko wa kusaidia ubinadamu.Na hii yote ni kwa sababu kwenye utamaduni wa Mwafrika, jukumu la kulea ni la jamii nzima na si la mtu mmoja tu. Wenzetu wa Finland hawana majukumu ya namna hii na ndiyo maana wanachangia kwenye mifuko ya kusaidia na kuonekana ni wakarimu.

Lakini, haya mambo yangeweza kuelezwa vizuri zaidi kama utafiti huu ungemhusisha ‘Mariano Rojas’ kutoka Afrika. Kwa bahati mbaya, Afrika haikuangaliwa kwa jicho linalofaa katika utafiti huu. Ndiyo maana nasema, ni muhimu sana kwa bara letu kuwa na vyombo vyake vyenyewe vya kufanya utafiti. Hatuwezi kupiga hatua kutoka hapa tulipo kwa kufanyia kazi tafiti ambazo zimefanywa kwa kuzingatia muktadha wa waliolipia zifanywe.
Kama hatukulipia utafiti wenyewe, yanini wahangaike nasi?

Ezekiel Kamwaga
Dar es Salaam
16/03/2018

No comments:

Post a Comment

Maoni yako