Na Edgar Mwandemani, Dar es salaam
Inaelezwa kuwa matokeo ya haya yanayoendelea hivi sasa
katika siasa za Tanzania (kuzomeana, matusi na kukashfiana) ni, pamoja na mambo
mengine, ukosefu wa uvumilivu wa kisiasa. Sitaki kusema tafsiri hii ni kweli
ama si kweli. Pamoja na kwamba neno hili 'Uvumilivu wa Kisiasa' ni zuri
linapotamkwa na wakati mwingine humwenyesha aliyelitamka ni mstaarabu, mwenye
busara na asiyependa makuu.
Katika muktadha wa siasa za Kiafrika, Tanzania kwa upekee,
utamaduni huu umetumika kama silaha ya kuadhibiana miongoni mwa makundi hasimu
katika siasa. Kwa upande wa chama tawala kimekuwa kikiwashutumu mahasimu wake
kwamba ni kutokana na uchanga wao katika siasa ndio maana wanafanya hayo
wayafanyayo. Imefika hatua katika siasa za kibunge, spika wa bunge la Tanzania
amewahi kusema vurumai zilizotokea mwaka jana bungeni ni matokeo ya utoto wa
wabunge wa upinzani.
Kwa upande mwingine wale wa upinzani wameendelea kujitetea
kwamba wanayafanya wayafanyayo katika kutekeleza ile haki ya kimsingi ya
kikatiba ya 'uhuru wa maoni' na 'kusimamia maslahi ya umma'. Na kwamba juhudi
zozote za kuwanyamazisha ni kuminya uhuru huo. Ili mradi kila upande unajitetea
kwa namna yake!
Profesa S.S Mushi anatafsiri dhana hii kuwa ni
"...harmonization of diversity or the extent to which public authorities
accommodate divergent views in political governmental processes". Kwa
ujumla wake ni kuvumila mawazo ya tofauti bila kujali nani ameyatoa. Lakini
kuvimila mawazo/maoni tofauti si sawa na kumilia lugha chavu/matusi mbele ya
jamii; kwa hivyo kwa muktadha wa yanayotokea hivi sasa hapa nyumbani,
waheshimiwa hawa kwa maoni yangu hawatofautiani maoni/hoja bali tafsiri ya
maneno machafu/matusi.
Aidha, Mushi anaendelea kueleza kuwa dhana hii 'uvumilivu wa
kisiasa' chanzo chake ni mambo makuu mawili. Moja, ni kiwango cha mgawanyiko
kilicho katika jamii yenyewe. Mgawanyiko wa makundi mfano, makabila, dini,
rangi na kitaasisi unamchango mkubwa kujua kiwango cha 'uvumilivu wa kisiasa'.
Jambo la pili ni, Tabia na sera za asasi za umma; kwamba ziko zile zinazowaleta
pamoja raia na zingine huwagawa.
Tulipofikia jamii ya watazania imezama katika dimbwi la
mgawanyiko. Hivi sasa mgawanyiko wa kidini, kimakabila, kimaeneo, makundi rika,
jinsia na itikadi za vyama umeendelea kuliguguna taifa letu kiasi cha
kusababisha mafarakano, magomvi na vifo katika maeneo fulani. Watu wamevaa
tofauti zao kama silaha dhidi ya wenzao, hakuna tena umoja wa kitaifa. Bahati
mbaya ni kuwa mambo haya yamechochewa na fikra za kipumbavu miongoni mwa
makundi hayo; fikra za kujiona kila mmoja ni bora dhidi ya mwingine. Vyama
siasa kwa mfano, vimedhani kwa muda mrefu, rangi zao za bendera ndio utanzania:
kila chama kinataka kupuuza uwepo wa kingine!
Taasisi nazo si haba. Nyingi zake zimeendelea kuendeshwa kwa
tabia na sera zinazochochea migawanyiko katika jamii. Tukichukua mfano wa Bunge
letu hivi sasa; mijadala mingi inayoendeshwa humo imekuwa ikijikita katika
kuonyeshana ubabe na ununda wa vyama vya siasa. Kwa upande wa chama tawala
wamekuwa hawaheshimu wala kuzingatia maoni ya wale wengine kwa kisingizio cha
wingi dhidi ya uchache. Upinzani nao kwakisingizio cha 'kusimamia mabadiliko'
na 'uhuru wa maoni' wamekuwa wakijiona wao ndio kila kitu na kwa kuwa wamekuwa
wakipuuzwa basi ni vitimbi.
Bunge limebaki kuwa mahali pa vihoja badala ya hoja; na kwa
mwenye kihoja kikubwa ndio wa maana kuliko mwenzake. Katika mazingira haya
itakuwa si kweli kudai kuwa siasa za Tanzania zimekosa 'uvumilivu wa kisiasa'
kwani kilichopo hivi sasa ni vihoja uvumilivu utatoka wapi? Hakuna wa kuvumilia
vihoja!
Kama kweli tunataka kuwepo na 'uvumilivu wa kisiasa' lazima
tujitafakari juu utamaduni wa siasa zetu. Siasa ni matokeo ya utamaduni wa
maisha ya kila siku katika jamii. Tusipoujenga tutarajie vurumai zaidi katika
maeneo mbalimbali!
No comments:
Post a Comment
Maoni yako