Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
HIVI karibuni nilipata fursa
ya kumhoji mwandishi wa kitabu cha ‘Kumrudisha Mwafrika kwenye Asili yake:
Mradi mgumu kuliko yote,’ Mwinjilisti Kamara Kusupa.
Haya ndiyo mazungumzo yetu
ambayo bila shaka yatawanufaisha Watanzania kufahamu nini maana na asili ya
Afrika kwa ujumla wake na maisha halisi ya bara letu.
SWALI: Niliwahi kusoma vitabu
vyako viwili, “Maisha yangu Gerezani”, baadaye kile cha “Hii ndiyo Tanzania
tunayoitaka”. Kuna tofauti gani kati ya vitabu hivyo na hiki cha sasa?
KUSUPA: Tofauti ipo, sababu
kile cha kwanza niliongelea maisha ya gerezani na namna vijana wanyonge
wanavyoteseka. Wengine wanakosa utetezi na wengine hawana msaada wa kisheria na
wapo wanaogandamizwa.
Nikiwa na Mzee Kusupa |
Halafu kuna wale wanaosota
miaka mingi bila kesi zao kutatuliwa. Kitabu changu cha pili kimeongelea suala
la nchi yetu ya Tanzania,
kwamba tunataka iweje na iongozwe vipi katika kutafuta katiba mpya. Naizungumzia Tanzania
ya wakoloni, baada ya ukoloni, kipindi cha Nyerere na baada ya Nyerere. Halafu
nimeongelea hili suala la vyama vingi vya siasa. Lakini kitabu hiki kipya
namtazama Mwafrika na matatizo yake yanayomsonga kila kukicha bila ufumbuzi
huku akiwa tegemezi. Mwafrika ambaye hajachukua nafasi kuyachukua mazuri ya
mababu wa asili yake.
SWALI: Lakini maandiko ya
namna hii yako mengi hapa nchini na kote Afrika kwa ujumla kuhusiana na
Mwafrika. Wapo Watanzania ambao wameandika vitabu kuelezea matatizo ya Afrika,
mfano Dk. Malima Bundara aliandika, “Waafrika ndivyo Tulivyo”. Je, wewe
unazungumzia nini kwenye hiki kitabu kipya?
KUSUPA: Nakiri yapo maandiko
mengi kuhusiana na Waafrika. Yapo maandishi kama ya akina Cheikh Anta Diop
(Senegal), Dk. Elly Kamugisha (Tanzania), Franz Fanon (Algeria), Julius
Nyerere, Leopold Senghor (Senegal), Ali Mazrui, Marcus Garvey, Nelson Mandela
na wengineo.
Lakini jambo kubwa lililokuwa
likijadiliwa ni nani hasa huyu Mwafrika. Lakini wakasahau kuwa Mwafrika huyu
ana asili zake, hizo ndizo ninazoongelea kwenye kitabu hicho kipya.
SWALI: Unakubaliana na
mahitimisho mengi ya wasomi wa Afrika kuhusu Mwafrika ni nani na anaweza kurudi
kwenye asili yake kwa njia gani?
KUSUPA: Wengi wanakubaliana
kwamba Mwafrika ni mtu mweusi, hivyo kuwatenga Waarabu, Wahindi, Wazungu na Waberiberi
ambao kimsingi nao wamejikuta wakiwa wamezaliwa katika bara ya Afrika hivyo
hawawezi kutengwa.
Kwa mfano; msomi Dk. Harrith
Ghassany alipata kuandika nini asili ya Afrika. Kwa utafiti wake akaelezea kuwa
asili ya Afrika ni kutoka kule Tunisia.
Dk. Harrith alisema hayo
kwenye kitabu chake cha “Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni: Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia.” Yote haya
yanatuletea swali la msingi Mwafrika huyu ni nani?
Hata hivyo dunia imebadilika
na kila kona inatusaidia kujua nini hasa kinachopaswa kusemwa kwa dhati na moyo
safi kwa
nyakati za sasa na baadaye. Kuna Wazungu wamezaliwa Afrika Kusini, Tanzania
na wengine nchi nyingine za Afrika.
Je, hawa watakwenda wapi
ikiwa hawajui asili zao au mahali walikoanzia zaidi ya kujikuta wakiwa katika
nchi wanazoishi. Ni kama ambavyo Waafrika walioko Ulaya, Amerika na Asia wanavyojiuliza ni namna gani wataweza kurudi Afrika
ambako hawajui waanzie wapi.
Ni vigumu leo kumwelezea
Jesse Jackson, Mohamed Ali warudi Afrika kutoka Marekani. Ni vigumu vile vile
kumweleza Lennox Lewis wa Uingereza arudi barani Afrika.
Ni vigumu kumwambia Danny
Jordan wa Afrika Kusini kwamba uchotara wake sio kitu arudi kwenye asili ya
makaburu Uholanzi na kwingineko. Au ni vigumu kumwambia Hellen Zille,
mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance (D.A) pale Afrika
Kusini na gavana wa jimbo la Cape Town, kwamba arudi kwa wazungu wenzake.
SWALI: Unadhani hilo linatokana na
uhusiano wa Waafrika na wageni, ndio kiini cha Mwafrika kurudi kwenye asili
yake?
KUSUPA: Kwanza
niseme hii ni moja ya mabadiliko makubwa ya mipaka ya nchi ambayo imeshindwa
kuzuia uhusiano wa wanadamu kutoka nchi moja hadi nyingine au kutoka jamii ya
nchi moja kwenda jamii ya nchi nyingine.
Leo Mwafrika anaweza kuzaa na
Mchina au Mkorea hivyo ni vigumu mtoto atakayezaliwa kutotambuliwa kuwa Mwafrika,
na kuangalia asili. Lakini wapo watu wanaojaribu kujiuliza ni namna gani
wanaweza kuwakumbusha Waafrika wenzeo kuwa Mwafrika alikuwa na asili yake.
Hata kwenye dini, Waafrika
wanazo. Ukisema Waafrika hawana dini nitakuambia soma maandiko ya Mchungaji Blacid Temple
kwenye kitabu chake cha “Bantu Philosophy”, kwa hiyo ushahidi wa asili zetu upo
kidini, kisiasa na kiuchumi.
Propaganda iliyohubiriwa kwa
nguvu na pia kufundishwa na elimu ya kikoloni ni kwamba Mwafrika ameanza kuwa
na dini baada ya ujio wa Waarabu na Wazungu barani Afrika.
Baada ya kazi ni gumzo |
Kwa mfano; katika Afrika ya Mashariki,
Uislamu uliingizwa katika karne ya nane na wafanyabiashara kutoka Ghuba ya
Uajemi (leo tunaita Iran),
hao wafanyabiashara wa kiajemi ndio walioitia jina la Dar
es Salaam mji maarufu wa Tanzania lenye maana ya mbingu ya
amani.
SWALI: Je, ni kweli kwamba
kabla ya ujio wa wafanyabiashara wa kiajemi, Waafrika wa eneo hili hawakuwa
wakimwabudu Mungu?
JIBU: Narudi kama
nilivyoeleza mwanzoni, Waafrika walimjua Mungu wa kweli, walimwabudu na kuishi
kulingana na miongozo yake. Ushahidi wa kuonyesha Mwafrika aliabudu Mungu kabla
ya ujio wa Uislamu na Ukristo ni uwepo wa majina yanayoendana na masuala ya
kiroho na ibada.
Lakini tunapokuja kwenye eneo
linalohusu mambo ya kiroho, maneno kama ibada, Nnungu, Mungu, Mulungu, Ngai, Nkoyi, Kyala, Malaika
na Banzelu neno kutoka lugha ya Kilingala lenye maana ya viumbe weupe
wanaong’ara ni udhihirisho wa kwamba Mwafrika alimjua Mungu na alikuwa na mawasiliano naye.
Katika somo hili tunajadili
kwa ufupi juu ya Uislamu, Ukristo, Ubuntu na dini ya asili iitwayo Alabba ndani
ya kitabu nimeeleza sana
hili.
SWALI: Mwafrika haonekani
kutajwa kwamba mmoja wa watu waliowahi kuishi au kufika Marekani kabla ya
ukoloni. Labda tuseme Latini Amerika yote kusini na kaskazini. Lakini
tunashuhudia Waafrika wengi wakiwa huko na baadhi ya mila na desturi zao
zinalingana na Waafrika wa bara la Afrika. Kwa nini?
KUSUPA: Kwanza
niseme wanaoeneza kuwa Mwafrika hakuishi Marekani kabla ya biashara ya utumwa
hawako sahihi, au kule Latini Amerika. Kuna sababu nyingi, lakini kubwa
ilianzia kwa Columbus.
Mwafrika alikuwa wa kwanza
kuwasili Marekani kabla ya Christopher Columbus, hata ukisoma maandiko yenye ushahidi yaliandikwa na
Profesa Ivan Sertima kwenye kitabu chake "THEY CAME BEFORE COLUMBUS". Hizo 'voyage' mbalimbali za Christopher Columbus zimejaa
mengi ya kushangaza na kwa nini yanachukuliwa kuwa kama
yalivyo au ukweli wenyewe? Waafrika wanayo mengi hayakuandikwa vizuri.
SWALI: Kwa hiyo una maana
kwamba ndani ya Kumrudisha Mwafrika kwenye Asili yake: Mradi mgumu kuliko yote
umeelezea nyongeza yake na hali halisi ya Mwafrika na asili zake, ukizingatia
dhana ya uhai pia?
KUSUPA: Kwanza
tunaangalia sisi Waafrika ni nani na asili yetu ikoje, hicho ndio kiini. Dhana
ya uhai inakuwa kubwa na inachukua mkondo mkubwa pia, hivyo basi kitabu cha
KUMRUDISHA MWAFRIKA KWENYE ASILI YAKE; MRADI MGUMU KULIKO YOTE nimeleta baadhi
ya majibu ya maswali ambayo kila mara watu wanajiuliza.
Nimeelezea kuanzia kwenye
dini, siasa, utamaduni, na mengine mengi kuhusu Afrika, nimeelezea mengi kwamba
kuna makosa kadhaa yanafanyika ni vigumu kuizungumzia Afrika kama
wanazuoni Ali Mazrui wanaoitazama Afrika kichotara.
SWALI: Unazungumzia Afrika ya
kichotara, una maana gani hasa?
KUSUPA: Hakuna wakati wowote
katika historia ya dunia na maisha ya mwanadamu kiujumla, ambapo Afrika imeacha
kuhusiana na watu kutoka nje ya bara hili, hivyo nazungumzia Afrika na Wageni
kutoka Ulaya, Amerika na Asia. Tangu awali na
baada ya Kristo watu kutoka nje wamekuwa wakiingia Afrika kwa sababu moja au
nyingine.
Katika mada hii ya Afrika na
wageni, tunazungumzia wageni wa aina tatu kutoka nje ya bara la Afrika.
Tunajadili juu ya Afrika na wafanyabiashara kutoka mabara mengine ya Asia,
Ulaya na Arabuni, Afrika na waeneza dini kutoka nchi za ulaya magharibi na
Afrika na Wazungu wa magharibi waliojifanya
wavumbuzi yaani wale wachoraji wa ramani
za kuonyesha mito mikubwa, milima mirefu na maziwa.
Tunajadili juu ya Afrika na
tamaduni za kigeni, Afrika na dini za kigeni na mwisho tunajadili juu ya Afrika
na tawala za kigeni ikiwa ni pamoja na mifumo inayoendelea kutumika hadi sasa
kuongoza maisha ya Waafrika.
Kila jamii imekuwa kwenye
asili yake na inakuwa vigumu kurudi kwenye asili yake. Tujiulize je, dini za Waafrika
ni zipi? Mfumo wa utawala wa Waafrika ni upi?
Msingi wao na dhana ya uhai
vikoje? Uhusiano wao na jamii za nje ukoje? Je, Mwafrika ataepuka dhahama ya
mabadiliko ya kijamii duniani? Je, Mwafrika ataweza kurudi katika asili yake?
Nadhani ni moja ya mambo ya
kusisimua na hakika yatakuwa na hamasa kwa wasomi mbalimbali na wananchi wengine.
Kikubwa tuseme kama kweli tutaweza kurudi
kwenye asili yetu au ni mradi mgumu?
SWALI: Katika kitabu chako
umegusia suala la muungano wa bara Afrika?
KUSUPA: Hilo nimezungumzia kwa kina. Nimeanza toka
kwenye utumwa, ukafuatia ukoloni na baadaye utawala wa chama kimoja au udikteta
wa chama kimoja.
Hatimaye Afrika imeletewa
utandawazi unaoyafanya mataifa yenye nguvu yawe dikteta wa kudumu wa
kuzilazimisha nchi za Afrika kujiendesha sawa na watakavyo wao.
Afrika iligawanywa vipande
vipande na kuitwa majina mapya na wakoloni, lakini pia wakoloni hao wakati
wanachora na kuweka mipaka yao ya kufikirika, ndipo waafrika tulipogawanywa na
kutenganishwa na kupewa utambulisho mpya wa kuitwa Watanganyika, Wakenya,
Waganda, Wakongo, Wanyarwanda, Warundi, Warhodesia, Wamozambiki, Wanigeria,
Wakameruni, Waghana, Wasenegali, Wamali, Waliberia, Wasealeoni, Wanamibia,
Waangola, Wasudan, Wasomalia, Waethiopia n.k.
Wakati wakoloni wanaigawa
Afrika na kuweka mipaka yao
mipya tofauti na ile mipaka ya asili iliyokuwa inatambuliwa na wenyeji, pia
waafrika walitenganishwa na kuumbiwa hisia mpya. Mpaka wa kutenganisha nchi na
nchi nyingine uliweza kupita katikati ya eneo moja na kuwafanya watu wa kabila
moja au ukoo mmoja kuwa na uraia wa nchi mbili tofauti. Hivyo Afrika lazima
iungane.
SWALI: Nashukuru kwa
kushirikiana katika fursa hii. Naamini Watanzania watanufaika kutoka katika
maandiko yako mazuri ya kitabu chako.
KUSUPA: Karibu wakati
mwingine, ninyi vijana mnatakiwa kujua zoezi jipya la Afrika kuwa na mipaka
mipya lilimpa Mwafrika hisia mpya na utambulisho mpya. Nitafanya mhadhara UDOM
kuelezea hilo Mungu
atujalie. Kwa hiyo lazima tujirudishe kwenye asili zetu.
Baruapepe;
mwanazuoni27@gmail.com
I drop a leave a response when I especially enjoy a post on a website or if I have something to add
ReplyDeleteto the conversation. It's triggered by the passion displayed in the article I read. And after this article "KAMARA KUSUPA: MWAFRIKA ALIKUWA WA KWANZA KUWASILI MAREKANI KABLA YA CHRISTOPHER COLUMBUS". I was excited enough to write a thought ;) I do have some questions for you if you do not mind. Could it be just me or does it look as if like a few of the responses look as if they are coming from brain dead people? :-P And, if you are posting on additional places, I would like to keep up with anything new you have to post. Would you make a list all of your social sites like your twitter feed, Facebook page or linkedin profile?
Here is my blog :: magazine blackjack trade stimulator