Na: Albert Sanga, Iringa
Nafahamu kuwa wengi kama sio wote tunakubaliana kuwa fedha zina umuhimu
mkubwa sana katika maisha ya mtu, tunachotofautiana ni imani kuhusu fedha.
Mitazamo kuhusu fedha ndio inayoamua kiwango cha fedha alichonacho kila mmoja.
Hii ina maana kuwa kila mtu anamiliki kiwango cha pesa sawa sawa na imani ama
mtazamo wake kuhusu fedha.
Kimsingi ni kwamba zipo imani zinazosapoti watu kuwa na fedha za kutosha na
zipo imani na mitazamo inayozuia watu kuwa na fedha ama inawafanya waishi
maisha ya kupungukiwa nyakati zote! Imani na mitazamo hii kimsingi huzalishwa
kutokana na malezi, utamaduni na
mazingira. Mtazamo wa mtu kuhusu fedha tunaita, “Money blue print” (Kila
nitakapotumia neno hili la kimombo litakua limebeba maana hii)
Mathalani, ukiwa mikoa ya Nyanda za juu kusini kuna mivumo, ‘myths’ kuhusu
kabila la Wakinga (bahati nzuri na mimi ni Mkinga). Watu wengi kutoka kabila
hili wanasifika sana kwa kufanya biashara na matajiri wengi katika mikoa hii ni
Wakinga. Pamoja na sifa hii, Wakinga wanatajwa kuwa ni mabingwa wa kutumia
ushirikina katika biashara zao.
Hivyo utabaini kuwa kwa mtu anaewatazama wakinga na utajiri wao, akiamua
kuchukua ‘myth’ hii; basi ataunganisha fedha na uchawi. Hii itakuwa kichwani
kwake kwamba, ili uwe na fedha nyingi (tajiri) ni lazima uwe mchawi na hii ndio
itakuwa, ‘Money blueprint’ yake.
Mfano mwingine unawahusu rafiki zangu Wachaga. Wapo watanzania wengi ambao
wanaamini mchaga yeyote anayetajirika ni lazima awe ametumia wizi ama
udhulumaji. Kwa watanzania wenye mtazamo
kama huu, ni wazi kuwa wanapoitazama fedha wanaiunganisha na wizi ama
udhulumaji. Kwao hawa hii ni ‘blue print’ yao.
Ukiiangalia mifano hiyo yote miwili utabaini kuwa ni mitazamo inayozuia mtu kuwa na fedha
nyingi (hata kama mwenye mtazamo huo akiwa hajijui). Na hii ni kwa sababu watu
wengi hawapendi uchawi, hawapendi wizi na wanauchukia ujambazi. Kwa kuwa
wameunganisha fedha na uchawi, wizi na ujambazi, ‘automatically’ wataichukia
fedha bila hata kujijua ikiwa wanaichukia fedha! Matokeo ya chuki zao dhidi ya
fedha yanadhihirika katika kiwango cha fedha wanazomiliki. (Nakuthibitishia
eidha wanakuwa ni masikini ama ni watu wenye kuhangaika milele kwa kupata fedha
isiyowatosha-hata kama wawe ni wenye vyeo vikubwa!).
Ingawa mtu kuwa na fedha nyingi sio kipimo cha utajiri lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu aweza
kusema ni tajiri ikiwa hana fedha (hata kama iwe katika maumbo mengine). Kwa
maana hii tukiongelea fedha kwa namna moja ama nyingine tunakuwa tukiiunganisha
na utajiri (ingawa kuna watu hawataki kabisa kuwa matajiri-hawa nao blueprint
zao ndivyo zinavyowaelekeza!).
Kiuhalisia ni kuwa utajiri ama umasikini wa mtu haupo katika wingi ama
uchache wa mali au fedha anayomiliki. Tofauti kubwa iliyopo kati ya masikini na
matajiri ni ile ya kifikra. Masikini
huwaza kimasikini, tajiri huwaza kitajiri. Utajiri ama umasikini wa mtu huanzia
katika fikra na mitazamo yake.
Kwa mfano, fikra za kitajiri huamini
kuwa ukiwa na fedha ya kutosha utaishi kwa furaha, amani na upendo kwa wengine
hivyo utatimiza agizo la Mungu kuwa mpende jirani yako kabla ya kumpenda Mungu.
Fikra za kimasikini zitajinenea hivi, “sio vizuri kuwa na fedha nyingi, kwa
sababu hautampendeza Mungu”
Kama alivyosema, Mchungaji Pepe Minambo kutoka Kenya ndivyo na mimi
ninavyoamini kuwa ni vigumu kwa masikini kuingia mbinguni. Sababu za uwezekano
wa masikini kuikosa Mbingu zipo wazi; kwanza masikini ni mlalamikaji na
mnung’unikaji (na Mungu hapendi walalamishi na wanung’unikaji), masikini ana
wivu na masikini hajiamini.
Msomaji usisahau kuwa hapa siongelea masikini wa roho aliowasema Yesu
Kristo, ila naongelea masikini wa fikra chanya. Ni vema tukafahamu kwamba,
tajiri huwa tajiri kabla hajamiliki kitu na masikini huwa masikini kabla ya
kudhihirika kwa hali yake; kwa vile umasikini na utajiri vyote ni matokeo ya
kuwaza.
Vile vile nigusie kundi maarufu sana la uchumi wa kati “middle class”. Hawa
ni watu ambao hawana fedha nyingi na wala sio masikini kabisa. Kundi hili ni
sumbufu sana kifikra na ndilo ambalo husambaza fikra hasi kuhusu fedha. Kundi
hili, hupenda kuridhika mapema na hupendelea sana usalama “comfort zone”.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba
kuna wanasiasa wanadai kupigania uwepo wa watanzania wengi katika kada hii ya
watu wa kati; wakati mfumo na uchumi wa dunia unawafuta kwa kasi kubwa. Mfumo
wa uchumi wa dunia uliopo (na utakaoendelea kuwepo kwa mamia ya miaka ijayo) unawabeba watu wa aina
mbili tu, masikini na matajiri.
Ni ama uchague kuwa masikini au uchague kuwa tajiri. Kazi ni kwako msomaji
kama unaamini na kutamani kuwa mtu wa kada ya kati. Kwa wanaofuatilia duru za
kiuchumi kwa umakini hawashangazwi na hali iliyopo ya matajiri kuendelea kuwa
matajiri na masikini kuzidi kuwa mafukara, sio Tanzania tu lakini ni katika
dunia nzima.
Kwa kuwa ninaongelea kuhusu imani
kuhusu fedha ni vema nikagusia imani iliyochimbika miongoni mwa baadhi ya
wakristo. Katika Biblia kumekuwa na maandiko ambayo, tafsiri (nasisitiza kuwa
ni tafsiri kwa sababu Biblia ipo ‘perfect’) zake zimekuwa na ‘Money blue print’
ambazo hazisapoti mtu kutafuta na kunia kumiliki fedha. Nitataja maandiko
mawili; la kwanza ni lile lisemalo, “Huwezi kumtumikia Mungu na mali” na la
pili ni lile lisemalo, “Kupenda fedha ni shina la maovu yote duniani”.
Si kusudio langu kuhubiri (ingawa nina karama ya kuhubiri pia) lakini
nifafanue kidogo kuhusu maandiko hayo. Neno mali (ama Biblia zingine zimeandika
fedha) limetafsiriwa kutoka katika neno ‘Mamos’ linalomaanisha ‘roho
inayotawala mali’. Kwa maana hii, kimantiki ilitakiwa kueleweka kuwa, “Huwezi
kumtumikia Mungu na roho inayotawala mali”.
Kuhusu fedha na maovu ninachoamini ni kuwa ikiwa pesa itatumika vibaya
itazalisha maovu na ikiwa itatumika vema inaleta tija. Ni kama kisu kilichopo
jikoni, kinaweza kukata mboga na kinaweza kutumika kuua ama kumdhuru mtu.
Kusema kisu ni chanzo cha ‘mauji yote ya jikoni’ itategemea umeangalia upande
upi wa matumizi!
Kwa upande wa malezi na utamaduni wetu nako kumezalisha imani na mitazamo
mingi iliyo hasi kuhusu fedha. Kwa mfano; jamii zetu zinaamini kuwa wanaume
ndio wanastahili kuwa na fedha kuliko wanawake. Ndio maana mwanamke
anapotajirika migogoro hutokea ikilinganisha na mwanaume anapotajirika.
Wanawake wengi waliomatajiri utasikia habari kuwa ama hajapata kuolewa, ama aliolewa akaachika
ama ndoa aliyonayo ina mgogoro mkubwa. Unajua tatizo linapoanzia? Nitaeleza
hapa chini, lakini kabla nataka niseme jambo hili; imani ya jamii kuhusu fedha ndio husababisha
wanawake wanaotajirika kuonekana kuwa hawapo sawa.
Katika familia nyingi watoto wanapokua, huwa kuna mazoea ya kuomba fedha
kwa mama. Mama zetu mara nyingi tukiwaomba fedha huwa wanasema kauli kama hii,
“Msubiri baba yako, akija ndio atakupa fedha”. Kinachojengeka katika akili ya
mtoto ni kuamini kuwa, wanawake hawana na hawastahili kuwa na fedha! Hii ni
‘Money blueprint’ hatari sana na imechangia sana wanawake wengi kuwa nyuma
kujitafutia fedha na pengine kutajirika.
Kutoakana na ‘blueprint’ hii ndio maana huwa sishangai ninapoona mabinti
wakijiorodheshea vigezo vya wanaume wanaowataka; katika vigezo hivyo hawaachi
kuweka, ‘mwenye kazi nzuri (moja kwa moja atakuwa na fedha)’, ‘mwenye fedha za
kutosha’, ‘aliye maarufu (umaarufu kwa kiasi fulani huleta fedha)’ na vigezo
vya kufanana na hivyo.
Zipo imani na mitazamo mingine mingi ambayo imewaathiri watu wengi bila
kujijua na imesababisha kuishi katika maisha ya uchache badala ya utele wa
kifedha. Kwa mfano wapo watu ambao wanaamini kuwa haiwezekani watu wote tukawa
matajiri. Wanachosahau kujiuliza ni hiki, “Ni wapi imeandikwa kwamba wewe
fulani, bin fulani utakua masikini?” Kama dunia inaendelea kuzalisha matajiri,
kwa nini usiwe mmoja wao na badala yake unajivisha haki ya umasikini?
Wapo watu wengine ambao wanaamini kuwa matajiri ni mabahiri; kwao hawa
utajiri ni ubahili na wengine wanajiridhisha kuwa fedha haiwezi kununua furaha.
Ukweli ni kwamba matajiri wengi wana nidhamu ya matumizi ya fedha (ndio maana
wanazidi kutajirika) na uhalisia ni kwamba ingawa fedha sio kigezo pekee cha
mtu kuwa na furaha lakini siku za masikini hutawaliwa na huzuni kutokana na
kutopata anavyovitaka. Kupata unachokitaka ni moja ya mihimili ya furaha. Na
mtu una uwezekano wa kupata unachokitaka kwa sehemu kubwa ikiwa utakuwa na fedha
Msingi mwingine wa kupata fedha (na mafanikio mengine yeyote) ni kuzingatia
kile unachokipenda na sio kile usichokipenda (focus on what you want and not on
what you don’t want). Hii inatokana na kanuni mbili za kiubongo na kiasili;
ambazo ni hizi(Nitatumia kiombo kidogo).
Kanuni ya kwanza inasema“What you focus expands-yaani unachozingatia hukua”
na ya pili inasema “Your eyes will see what your mind has prepared to see-macho
yako yataona kile ambacho fikra zake zimejiandaa kukiona”. Iko hivi, ukitaka
fedha zingatia utele (namna ya kuongeza fedha) na usizingatie uchache (kuishiwa,
kufilisika)!
Nihitimishe makala haya kwa kudurufu mambo machache. Mosi ni kuwa kila mtu anayo nafasi sawa (equal channce) ya kuwa na fedha za
kutosha kumpa uhuru wa kiuchumi. Pili hakuna raha wala sifa ya kuendelea kuwa
masikini, kwa sababu masikini ni mzigo kwa dunia. Masikini na umasikini wake
hata awe ni mtakatifu na mwema kiasi gani ni kwamba anaitesa dunia (kwa sababu
anahitaji kusaidiwa). Tajiri (ama niseme mwenye fedha za kutosha) hata kama ni
mchoyo ama bahiri bado ni msaada kwa dunia (kwa sababu anajisaidia).
Pamoja na haya yote, sio kusudio langu kuwabeza masikini na tena sio
kusudio langu kuwataka watanzania wote wawe matajiri (japo ikiwa hivyo
nitafurahi pia-manake nami nitakuwa mmoja wa matajiri); lakini ninataka kila
mmoja apokee changamoto ya kutamani kuwa
na uhuru wa kifedha na kiuchumi. Na hili linawezekana ikiwa mitazamo na imani
za wengi kuhusu fedha zitabadilika na kuwa zinazosapoti badala ya kuvuruga
nafasi ya mtu kupata fedha.
Kila mtanzania anastahili ushindi wa kifedha!
0719 127 901,
stepwiseexpert@gmail.com
No comments:
Post a Comment
Maoni yako