Na: Albert Sanga, Iringa |
Wakati fulani nilikuwa
nikisikiliza wimbo mmoja ulioimbwa na mwanamuziki nguli hayati Luck Dube, na
ukatokea kunivutia sana kutokana na maudhui yake. Ndani ya kibao hicho, Dube
anaeleza namna wanawake wanavyopambana na maisha kupitia kujituma ili kuhakikisha
kuwa familia zao zinakuwa na ustawi mzuri. Hata hivyo Dube anaulaumu ulimwengu
kwa kumsahau kumtangaza mwanamke kama shujaa
na kutompa usaidizi unaotakiwa.
Katika ghani za shairi mojawapo, Dube
anasema maneno yafuatayo, “…kila siku tunawasifu mashujaa, lakini wapo
tunaowasahau; nao ni wanawake wa ulimwengu huu. Wanawajibika na kusimama imara
katika majukumu yao.
Mungu wabariki wanawake!”.
Katika zama hizi za ujasiriamali
tunazoishi sasa kwa hakika hatuwezi kabisa kumuweka kando mwanamke kutokana na
nafasi yake katika jamii. Hili linatokana na vuguvugu la ukombozi wa mwanamke
linaloendelea duniani pote, ambapo mwanamke anahitaji kuwa huru katika nyanja
zote ikiwemo, kiuchumi, kijamii na kisiasa. Katika kuelekea ukombozi kamili wa
kiuchumi, mazingira na hali zinamlazimisha mwanamke kuwajibika kikamilifu
katika harakati za ujasiriamali.
Iwe mwanamke ameolewa ama
hajaolewa ni lazima kutambua kuwa ni vigumu kuwa huru katika maeneo mengine ikiwa
hatakuwa huru kiuchumi. Na ifahamike kuwa uhuru wa mtu haushikwi na mwingine.
Maana yake ni kuwa wanawake wasitegemee kuwa huru kiuchumi kama
hawatajishughulisha kikamilifu ama kama
watategemea uhuru wao uwe mikononi mwa waume zao.
Na kwa wale wasioolewa bado (iwe
ni wasomi ama wasio wasomi), nao wanatakiwa kuzichanga vema karata zao na
kuhakikisha wanakuwa na mipango madhubuti ya kujikomboa kiuchumi ikibidi hata
kabla hawajaingia katika ndoa zao. Kwa sababu huko kwenye ndoa ni wanaume
wachache wanaoruhusu wake zao kufanya ujasiriamali!
Mara zote nimekuwa mstari wa
mbele kuhamasisha wanawake kutopuuza nafasi yao ya utii kwa waume zao, kwa namna na
katika mazingira yeyote yale. Pamoja na hilo,
mwanamke kamwe hatakiwi kufyata mkia na kuruhusu ndoto zake kufutwa na kile
kiitwacho ‘ndoa’.
Kama
mwanamke ana ndoto ya kujiendeleza kimasomo, kuwa majsiriamali ama kupata
mafanikio mengine yeyote yale hana budi kushikilia na kushughulikia ndoto yake
mpaka aone ikitokea bila kukwama kutokana na vikwazo vya mazingira ya ndoa ama
mwanaume aliyemuoa.
Ninapoongelea ujasiriamali kwa
wanawake ninafahamu kuwa kutakuwa na ukinzani mkubwa kama
sitatengenisha wanawake kwa makundi. Kwa uthubutu, kundi la kwanza ninawaweka
wanawake ambao hawajaolewa na lile la pili ninaweka kundi la wanawake
walioolewa.
Ninasukumwa kufanya hivi kwa
sababu ninafahamu kuwa kundi la wanawake walioolewa maamuzi yao yanafungwa na matakwa ya waume zao wakati
kundi la wanawake ambao hawajaolewa lenyewe lipo huru zaidi.
Nimesema wanawake wenye ndoa
maamuzi yao yanadhibitiwa sana na wanaume, kwa kuwa kuna wanaume ambao
wanawaunga mkono wake zao kufanya ujasiriamali lakini wapo wanaume ambao hawapo
tayari kuruhusu wake zao kujishughulisha na ujasiriamali. Kwa hawa mbali na
changamoto nyingi za kijasiriamali pia wanakumbana na dubwasha jingine, liitwalo
‘kunyanyaswa na waume zao’.
Kiukweli asilimia kubwa ya
wanaume wengi wana matatizo katika fikra zao, kutokana na namna
wanavyouchukulia uwezo wa wanawake katika ujasiriamali. Wengi wanaona mwanamke
kuwa mjasiriamali, atakuwa na kiburi, wanahisi atachukua nafasi yao katika familia na
kubwa linalowaogopesha ni kudhani kuwa mwanamke mjasiriamali ni muhuni.
Ujinga wa baadhi ya wanaume ni
kudhani kuwa hulka hasi wanazokuwa nazo wao katika ujasiriamali, zipo pia kwa
wanawake wajasiriamali. Upo ukweli kuwa baadhi ya wanaume wanapofanikiwa
kiujasiriamali (na hata katika maeneo mengine) huwa na mtindo wa kuanza kiburi
kwa wake zao, kusaliti ndoa zao na kusahau michango ya wake zao kwa hatua
wanayokuwa wamefikia. Kutokana na hili, wanaume ni kama
wanaogopa vivuli vyao wenyewe, katika kuwapa uhuru wake zao kujishughulisha
kikamilifu na ujasiriamali.
Dhana hii imepelekea wanaume
wengi kuwanyanyasa wake zao wanaojishughulisha na ujasiriamali na hata
kuwakatisha tamaa. Na hili linatokea sana
pale ambapo, eidha mwanaume sio mjasiriamali ama ikiwa wote ni wajasiriamali
lakini wanafanya biashara tofauti. Inamhitaji mwanamke kujifunga kibwebwe ili
kuendelea mbele.
Mara nyingi sana inapofika hapo (manyanyaso kuzidi) wanawake
wengi husalimu amri na kuuacha ujasiriamali. Ni wachache tu ambao huamua
kujitoa katika ndoa na kujikita katika ujasiriamali. Ndio maana takwimu na
uzoefu unaonesha kuwa idadi kubwa ya wanawake waliofanikiwa kiujasiriamali
eidha hawakuolewa kabisa ama walitalikiana na waume zao ama wanavumilia kuishi
katika ndoa zenye migogoro mikubwa sana.
Kwa wale wanaume ambao wameoa na
wanafanya ujasiriamali pamoja na wake zao nao bado wameendelea kuwa wagumu sana katika kuwashirikisha
wake zao kikamilifu. Kama ni duka, mwanamke anabaki kuwa muuzaji tu, hajui ni
wapi mali
zinanunuliwa, hajui mfumo kamili wa mapato na matumizi tena hajui hata mipango
na mikakati ya biashara.
Wapo wanaume ambao huwa
wanadiriki hata kuchukua mikopo katika mabenki kwa kutumia rasilimali za
familia bila kuwashirikisha kabisa wake zao. Hili ni tatizo kubwa! Ndio maana
idadi kubwa ya wajane wa wajasiriamali huwa hawafiki mbali kibiashara mara
baada ya waume zao kufariki.
Kwa wale ambao wanaendesha
biashara katika mifumo rasmi, (kwa mfano makampuni) ni vema na tena ni njia
rahisi ya kutoa kiwango unachodhani kinafaa cha ushiriki wa mke wako katika
biashara zako. Kwa mfano, mke anaweza kuwa na asilimia fulani ya hisa katika
kampuni. Hili litamuwezesha kuingia katika vikao vya bodi ya wakurugenzi pamoja
na kushiriki katika mipango na maendeleo ya kampuni, hata kama
anaendelea na kazi yake nyingine.
Siku zote ninasukumwa kuamini kuwa suala la ukombozi wa mwanamke linahitaji sana kuhusisha ukombozi wa
fikra za mwanaume, ili aweze (mwanamume) kuachia haki na uhuru wa mwanamke;
alioushikilia kwa karne nenda rudi kupitia hiki kinachoitwa mfumo dume.
Hata hivyo naomba niweke sawa
msimamao wangu katika hili ya kuwa sikubaliani na “baadhi ya wanaharakati”
wanaotaka mwanamke abebe majukumu ya mwanaume. Tumkomboe mwanamke lakini
tusithubutu kubadilisha uumbaji wa Mungu.
Ipo haja ya kuwekana sawa katika
hili kwa sababu si busara kuona wanawake wakizikacha ndoa ama wakikataa kuingia
katika ndoa, kwa sababu ya ujasiriamali. Ujasiriamali haupaswi kuwa kiwanda cha
talaka, haupaswi kutengeneza waseja (wanawake
wasiotaka kuolewa) na katu hautakiwi kuwa kapu linalotunza migogoro ya
ndoa.
Lakini tunapoongelea ujasiriamali
kwa wanawake ni lazima wao wanawake na jamii kwa ujumla, kuachana na mtindo wa kuwa
na mitizamo hafifu. Kuna fikra zimemea za kudhani kuwa wanawake wanatakiwa
kufanya biashara ndogo ndogo, kama kuuza
maandazi, kuuza mboga, kushona vitambaa na vibiashara vingine uchwara.
Hayumkini hili ni tatizo lililopo
hata katika fikra na mipango ya taasisi mbalimbali za fedha zinazotoa kile
kiitwacho mikopo midogo midogo kwa wanawake. Taasisi hizi zimejizoesha
kukopesha ‘vimikopo’ vya elfu hamsini, laki moja ikizidi sana laki tano! Ni vigumu wanawake kupiga
hatua kiujasiriamali kama hawataaminiwa na kupewa
mikopo zaidi ya hapo (mikubwa). Tukitaka mabadiliko hatuna budi kuwaamini
wanawake.
Wanawake wenyewe wanatakiwa kuachana
na mawazo hayo ya kujikunyata na unyonge, bali waanze kufikiria kiupana (thinking
in big picture). Ni wasaa wa wanawake kuibuka na mawazo makubwa ya kibiashara,
kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa, kuanzisha makampuni pamoja na kucheza na
fursa za biashara za kitaifa na kimataifa.
Wanawake sasa wawatazame wanawake
wenzao wachache waliofanikiwa kiujasiriamali duniani na katika mazingira ya Tanzania,
halafu wainuke na kuanza kutenda. Hakuna maana ya kuwa na visingizio, hakuna
maana ya kukata tamaa tena haina maana ya kudhani kuwa mwanaume ana asilimia
mia moja za uhuru wa mwanamke kiuchumi.
Kama
si kusimama peke yake kiujasiriamali basi mwanamke anatakiwa kushikana bega kwa
bega na mume wake, ili thamani na mafanikio ya familia kupitia ujasiriamali
yawe ni mchango wa nguvu, bidii na maarifa ya wanandoa wote kwa pamoja.
Faida iliyopo kwa wanawake ni
kuwa wana hulka ya uvumilivu na kujituma ambazo ni hulka muhimu sana katika ujasiriamali.
Kwa ‘added advantage’ hii kwa nini
wanawake wabaki nyuma?
Haina ubishi kuwa wanawake wapo
katika kipindi cha mpito katika kutokomeza mfumo wa kutoaminiwa. Kipindi hiki
ni kigumu na kinahitaji kukilipia gharama ili kupata mafanikio likiwemo eneo
hili la ujasiriamali. Ni kipindi cha mapambano, kutoka utumwa wa mwanamke kuwa,
‘mama wa nyumbani’, kuwa, ‘golikipa’ ‘kuwa tegemezi’ na kuwa ‘wa kuamuliwa hata
kama ana kazi yake’ kuelekea katika uhuru wa
kiuchumi.
Wanawake wasione taabu kukataliwa
na jamii zao, wasirudi nyuma kwa kuachwa ama kunyanyaswa na waume zao, na wavumile
kutukanwa na kusemwa vibaya na wanajamii ambao wanawaona wanawake wanaouendea
mstari wa mafanikio kupitia ujasiriamali, kana kwamba ni wahuni.
Ni lazima wanawake wajitahidi
kushinda changamoto za kuhudumia familia, kukabiliana na vishawishi, kubaki
wasafi kinidhamu, kimaadili na katika imani. Kwa kufanya hivyo, jamii
itaendelea kushuhudia na kuyaheshimu mafanikio ya wanawake katika ujasiriamali
nchini Tanzania
na duniani kwa ujumla.
Wanawake wajasiriamali
wanastahili ushindi
stepwiseexpert@gmail.com
No comments:
Post a Comment
Maoni yako