NA
ZITTO KABWE
MIAKA
50 imetimia tangu Komredi Che Guevara auwawe huko Bolivia mnamo tarehe
9/10/1967. Che, mwanamapinduzi mzaliwa wa Argentina na mkombozi wa Cuba ni
mmoja wa wanadamu waliojitoa mhanga kupambana dhidi ya ubeberu kote duniani.
Katika maisha yake aliwahi kupita Tanzania na kushiriki kwenye vikao na vyama
vya ukombozi kusini Mwa Afrika.
Tanzania
iliunganishwa na Che kupitia Zanzibar. Vijana wa Zanzibar walipelekwa mafunzoni
Cuba Kwa ajili ya ukombozi. Mwaka 1962 wakati wa
mgogoro wa Oktoba 1962, vijana wa kizanzibari waliokuwa mafunzoni Cuba
walijitolea kupigana bega Kwa bega na waCuba dhidi ya Marekani. Jambo hili
liliwafungua macho wacuba kuhusu Afrika na Kwa hakika Afrika yao ilikuwa
Zanzibar.
Vijana hao baadhi yao
wapo hai wakiwa ni wazee Sasa. Mmoja ni Mzee Ali Sultan Issa na Komred Shaaban
( pichani nikiwa naye nyumbani Kwa balozi wa Cuba ). Pia Dkt. Salim Ahmed Salim
akiwa Mkuu wa Ofisi ya Zanzibar kule Havana, Cuba. Mzee Ali Sultan Issa ndiye
alikuwa mwenyeji wa Che huko Zanzibar mwaka 1965. Prof. AbdulRahman Mohamed
Babu, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Zanzibar na baadaye Waziri wa zamani
wa Uchumi wa Tanzania alikuwa mtu wa karibu wa Che Guevara. Pichani walipokuwa
kwenye mkutano huko Geneva, Uswiss.
Kwa
sisi watu wa Kigoma Ujiji Che Guevara ana historia kubwa. Che alikwenda Congo
mwaka 1965 kupigana dhidi ya mabeberu waliomwua Patrice Lumumba. Alikaa huko
miezi 7. Alipokwenda Congo alipitia Kigoma na kulala nyumbani Kwa Mkuu wa Mkoa
wakati huo akiitwa Semvua Msangi ( mtoto wa Semvua alikuwa Mwalimu wangu Shule
ya Sekondari Kibohehe Moshi, akiitwa Zidikheri Semvua Msangi).
Che
alipanda Boti kutokea kijiji cha Bangwe kwenda Congo. Hata alipokuwa akifanya
mikutano walifanyia Kigoma mjini akiwa pamoja na kina Mzee Laurent Kabila
ambaye baadaye alikuja kuwa Rais wa DRC.
Che Guevara katika nyakati hizi aliitwa Tatu huku mwenzake Dreke akiitwa Moja ili kuficha majina yao ya asili.
Che Guevara katika nyakati hizi aliitwa Tatu huku mwenzake Dreke akiitwa Moja ili kuficha majina yao ya asili.
Moja
bado yupo hai na Kwa kushirikiana na ubalozi wa Cuba tumemwalika kuja nchini na
yeye pamoja na aliyekuwa Myeka wa Che wataambatana na baadhi ya Watanzania
kwenda Kigoma Kwa kufuata njia aliyopita Che.
Manispaa
ya Kigoma Ujiji imeamua kutunza historia Hii Kwa kuiita Che Guevara Barabara
inayoanzia Stesheni ya Reli mpaka mji wa Bangwe. Pia mazungumzo yanaendelea na
Meya wa Mji wa Cadiz katika Nchi ya Spain ili kujenga jengo la makumbusho mjini
Kigoma Kwa ajili ya kuenzi nafasi ya Kigoma katika juhudi za ukombozi dhidi ya
ubeberu barani Afrika.
Che
Guevara ni alama halisi ya mwanamapinduzi wa kimataifa aliyepinga dhuluma
kokote duniani. Maneno yake ya mwisho Kwa mkewe na wanawe yalidhihirisha hilo.
Aliwaambia uzuri wa uanamapinduzi ni kuchukia dhuluma inayofanyika dhidi ya
yeyote popote duniani. Kwa kimombo alisema;
"Above
all, always be capable of feeling deeply any injustice committed against
anyone, anywhere in the world. This is the most beautiful quality in a
revolutionary.”
Che
bado anaishi.
Zitto Kabwe Ni mbunge wa Kigoma Mjini
No comments:
Post a Comment
Maoni yako