January 19, 2018

TAITU BETUL: MALKIA JASIRI ALIYEASISI MJI MKUU WA ETHIOPIA, ADDIS ABABA.

Na Kizito Mpangala

Taitu Betul alizaliwa mwaka 1851 nchini Ethiopia ambayo wakati huo ilikuwa ni Milki ya Ethiopia kabla ya kuwa Jamhuri. Neno Taitu kwao lilimaanisha “mng’ao wa jua au jua”, hilo ndilo lilikuwa jina lake la asili.
Baada ya kubatizwa katika kanisa la dhehebu la Orthodox aliitwa Walatta Mikael, lakini baadae alilirudia jina lake la asili yaani Taitu Betul. Baba yake alikuwa aliitwa Betul Haile Maryam ambaye alikuwa na uhusiano na ukoo wa Mfalme Sulemani. Lakini baba yake huyo hakufahamika sana kama alivyofahamika mjomba wake  aliyeitwa Dejazmach Wube Haile Maryam, ambaye alikuwa mtawala wa Ethiopia Kaskazini miaka ya 1840.
Familia ya baba yake Taitu ilikuwa imeweka makazi yake katika mkoa wa Semien ambao ulikuwa ukitawaliwa na Mfalme Susenyos I. Baba yake alikuwa ni mjukuu wa Ras Gugsa ambaye alikuwa mshirika wa familia iliyotawala eneo la Yejju iliyokuwa na asili ya kabila la Oromo. Baba yake huyo alikuwa Muislamu na baadae akabadili dhehebu akajiunga na Ukristo.

Taitu Betul alikuwa na nafasi kubwa ya kuwepo katika ngazi za juu katika maeneo hayo kutokana na ndugu zake wengi kuwa katika nafasi za milki mbalimbali hasa katika ngazi za mikoa. 

Taitu Betul aliolewa mara nne na kuachwa kabla ya kukutana na Mfalme Menelik wa Shewa kama mke wa tatu. Muda mfupi baadae, baada ya kuolewa na Mfalme Menelik wa Shewa, Mfalme huyo akatawazwa kuwa Mfalme wa Milki ya Ethiopia (Ethiopian Empire). Taitu Betul akiwa kama Malkia pamoja na mumewe Mfalme Menelik II walikuwa wanamiliki watumwa elfu sabini (70,000).
Anafikiriwa kuwa na nguvu kubwa kisiasa katika Milki ya Ethiopia, kabla na baada ya kuwa Malkia baada ya kutawazwa mumewe Menelik kuwa Mfalme wa Milki ya Ethiopia mwaka 1889. Aliongoza kikundi cha upinzani mahakamani, kindundi hicho kilikuwa kikiwapinga wale waliokuwa wakijiita “watu wa kisasa” ambao walitaka kuingiza mtindo wa maisha wa Magharibi katika Milki ya Ethiopia. Aliupinga Mkataba wa Wuchale uliopendekezwa na Wazungu wa Italia, mkataba huo ulikuwa unahitaji kuifanya Ethiopia na watu wake wajihisi kuwa ni Waitaliano na wafuate tamaduni za Italia, wakati huo mkataba huo uliinyima nafasi jamii ya Ethiopia kufuata tamaduni zake za asili ziliyofuata misingi ta Amhara. Taitu Betul aliwapinga Waitaliano kwa nguvu sana.

Waitaliano walipovamia Milki ya Ethiopia kijeshi wakitokea katika koloni la Eritrea, Malkia Taitu Betul aliambatana na mumewe pamoja na askari wa Milki ya Ethiopia ili kuwashambulia Waitaliano upande wa Kaskazini mwa Ethiopia na ilifahamika kama Pambano la Adwa kwa kuwa mapigano yalifanyika katika mji wa Adwa nchini Ethiopia na kuwashinda Waitaliano mnamo mwezi Machi, 1896. Lakini mwaka 1935, Ethiopia ilivamiwa tena na Italia iliyokuwa chini ya Benito Mussolini na kuwashinda Waethiopia. Baadaye Ethiopia ilitawaliwa na Italia kwa muda wa miaka mitano yaani 1936 hadi 1941.

Taitu Betul alijiamini sana kuitetea Ethiopia isisumbuliwe ma Waitaliano. Alimpinga mumewe Mfalme Menelik II kwa tabia yake ya kuahirisha mambao bila sababu ya msingi. Mfalme Menelik II alikuwa anapenda kuahirisha mambo hata yale yaliyokuwa yanaweza kuhatarisha usalama wa Milki ya Ethiopia, alikuwa akisema “Ishi, nega” (kwa lugha ya Amhari) akimaanisha “Ndiyo, kesho” (kwa Kiswahili). Alikuwa akisema hivyo mara kwa mara hali ambayo ilimfanya Malkia Taitu Betul kuwa na sauti zaidi katika usalama wa Milki ya Ethiopia. Taitu Betul alikuwa akimjibu mumwewe akisema “Imbi” (kwa lugha ya Amhari) akimaanisha “Hapana” (kwa Kiswahili).
Eneo la Adwa katika Mji wa Tigray kaskazini mwa Ethiopia. Mahali hapa ndipo kikosi cha jeshi la Mfalme Menelik II kiliweka kambi kama walivyoshauriwa na Malkia Taitu Betul.
Taitu Betul alikuwa mpiganaji pamoja na askari wa Milki ya Ethiopia, alikuwa pia akiwapa huduma ya kwanza askari walioumizwa katika uwanja wa medani. Taitu Betul alikuwa pia mchambuzi wa taarifa za intelijnsia zilizoletwa na makachero wa Milki ya Ethiopia. Uchambuzi wa taarifa hizo ulimsaidia Mfalme Menelik II kutoa uamuzi wa uwanja wa medani kukutana na Waitaliano jambo ambalo alifanikisha. Waitaliano walitumaini kwamba Mfalme menelik II angefika eneo la Adigrat jirani na mpaka wa Ethiopia na Eritrea, lakini Mfalme Menelik II alizutmia taarifa za makachero wake na kwenda katika eneo la Adwa. Ushauri wake na matendo yake vilisaidia kuwashinda Waitaliano. Ushauri wa kwanza kufanyiwa kazi ni ule wa kukata mabomba yoye ya maji yaliyokuwa ynapeleka maji katika ngome ya Waitaliano. Jambo hili liliwashtua Waitaliano.
Mwaka 1906 afya ya Mfalme Menelik II ilipoanza kudhoofika, Malkia Taitu Betul alikuwa akifanya maamuzi mbalimbali katika utawala wa Milki ya Ethiopia kwa niaba ya mumewe. Alikuwa akiwapa madaraka wale aliowapenda yeye na vilevile ndugu zake. 

Taitu Betul aliiongoza Ethiopia katika hali mbalimbali, hali ya taabu na raha bila kunung’unika. Alianzisha benki ambayo iliweza kuwapa mikopo wafanyabiashara wengi wadogowadogo huko Ethiopia. Sababu ya kuanzisha benki hiyo ni kupinga kuanzishwa kwa benki ya Abyssiania ambayo ilikuwa ni ya kigeni yenye lengo la kuutawala uchumi wa Ethiopia.

Taitu Betul aliwakaribisha wawekezaji kutoka Uturuki na India ambapo kwa ushirika wao walijenga kiwanda cha nguo. Pia, alijishughulisha na utengenezaji wa mishumaa na kuigawa makanisani.
Taitu Betul aliweka mbele masilahi ya taifa. Alikuwa makao makuu ya Milki ya Ethiopia, eneo la ADDIS ALEM likimaanisha “ULIMWENGU MPYA”. Baadaye akahamia katika mji wa Entoto, huko hakukaa sana, akahamishia makazi ya uongozi wake katika eneo lililoko Magharibi mwa mji wa Addis Alem. Alianzisha eneo hilo jipya la kiutawala nchini Ethiopia. Eneo hilo alilifanya kuwa makao makuu ya serikali kuu ya Ethiopia mapaka sasa. Eneo hilo aliliita ADDIS ABABA likimaanisha “UA JIPYA”. Alijenga nyumba na kuizungushia uzio uliokuwa na alama maalumu iliyotambulisha kuwa ilikuwa nyumba ya Mfalme wa kabila la Shoan, Negus Sahle Selassie, ambaye alikuwa ni babu yake Mfalme Menelik II.

Alijenga hoteli ya kisasa jijini Addis Ababa ambayo sasa inajulikana kwa jina la “Hoteli ya Itege” na yeye mwenyewe alikuwa meneja wa kwanza katika hoteli hiyo na kuhamasisha utalii wa ndani na wa nje.
Mwaka 1910 alitimuliwa madarakani kwa lazima na Ras Tessema Nadew alichukua nafasi ya hiyo kuiongoza Milki ya Ethiopia. Taytu Betul aliamua kmtunza mumewe. Taitu Betul na Mfalme Menelik II hawakupata mtoto hata mmoja katika kipindi chote walichoishi kama mume na mke. Sababu ya kutopata mtoto ni kutokana na tohara aliyofanyiwa Taitu betul alipokuwa na umri wa miezi mitatu tangu alipozaliwa. Tohara hiyo ilimsababishia matatizo ya uzazi. Mumewe alifariki mwaka 1917. Ras Tessema Nadew naye alinyang’anywa madaraka na Lij Iyasu ambaye haukupenda kuwa karibu na Taitu Betul. Lij Iyasu naye alinyang’anywa madaraka miaka mitatu baadae.

Madaraka hayo alikabidhiwa Malkia Zewditu ambaye alikuwa na uhusiano mzuri na Taitu Betul, lakini baadae madaraka hayo akahamishiwa kwa Ras Tafari ambaye baadae alijulikana kwa jina la Haile Selassie.   
Ras Tafari (Haile Selassie)
Baada ya kufariki mumewe, Taitu Betul alitimuliwa pia katika makao makuu ya Milki ya Ethiopia, mjini Entoto. Lakini anaheshimika sana katika historia ya Ethiopia. Taitu Betul alikuwa mfadhili mkubwa katika kanisa la Orthodox katika Milki ya Ethiopia. Alipenda kujifunza fasihi ya jamii ya Ce’ez. Alitoa ardhi na vifaa vya ujenzi wa makanisa mbalimbali ya dhehebu la Orthodox nchini Ethiopia, na pia alitoa misaada mbalimbali katika kanisa la Kiethiopia lililoko jijini Jerusalem nchini Israel.

© Kizito Mpangala. (0692 555 874)

No comments:

Post a Comment

Maoni yako