March 23, 2018

LAURA BASSI: PROFESA WA KWANZA MWANAMKE BARANI ULAYA.

Na Kizito Mpangala

Wanawake wanayo nafasi ya kufikia malengo ambayo wanakusudia, ni kwa juhudi na maarifa wataweza kufikia malengo hayo. Suala la kipaumbele kwa wanawake duniani kote limepitia hatua kadhaa za ushawishi na changamoto kadhaa ambazo hasa huwakabili wanawake wenyewe. Katika uga wa sayansi na teknolojia, ni wanawake wachache ambao wamefikia malengo yao ugani humo. Hata sasa uhamasishaji bado unaendelea duniani kote.

Haikuwa kazi rahisi kwa mwanafizikia Laura Caterina Bassi kufikia kiwango cha profesa wa Fizikia katika chuo kikuu cha Bologna nchini Italia.
Laura Bassi alizaliwa mwaka 1711 mjini Bologna nchini Italia ambapo baba yake alikuwa mwanasheria. Laura Bassi alifundishwa nyumbani na mwalimu aliyeajiriwa na familia yake kwa muda wa miaka saba. Alianza kufundishwa akiwa na umri wa miaka 13. Mwalimu wake, Gaetano Tacconi, alimwelekeza zaidi katika sayansi na hisabati ndipo Laura alipoingiwa na hamu ya kutaka kujua zaidi yaliyomo katika sayansi.

Kutokana na msukumo aliokuwa nao katika sayansi, Laura alivutiwa zaidi na somo la Fizikia ambapo alijifunza zaidi kuhusu Sayansi ya Newton (Newtonian Science) ingawa mwalimu wake alitarajia kwamba Laura atajikita zaodi katika hisabati, lakini haikuwa hivyo.
Laura Bassi, katika juhudi zake za masomo alilazimika kusoma pia hisabati ili kujiimarisha katika Fizikia. Hapa Laura alimuomba binamu yake, Padre Lolenzo Stegani, amfundishe hisabati. Padre Lolenzo Stegani alikuwa akijua hisabati na lugha ya kilatini. Kwa kuwa vitabu vingi viliandikwa kwa lugha ya Kilatini, Laura alipaswa kujifunza sarufi ya lugha hiyo na baadae akafundishwa hisabati kwa lugha ya Kilatini.

Baada ya kuweka juhudi zaidi katika elimu hiyo ya sayansi, mwaka 1732 Laura aliandika kazi yake ya kwanza ambayo aliitetea mbele ya hadhira katika mihadhara mbalimbali katika ukumbi wa Pazzalo. Hiyo ilikuwa dira yake ya mafanikio ya elimu aliyokuwa akiitafuta zaidi.


Mwaka 1938, Laura Bassi aliolewa na dakitari wa falsafa na dawa, Giuseppe Veratti, ambaye pia alikuwa mhadhiri msaidizi wa Fizikia katika chuo kikuu cha Bologna. Walifanya kazi za kisayansi pamoja na hapo Laura Bassi alianza kusoma Fizikia ya Majaribio yaani Experimental Physics. Laura na Giuseppe walifanikiwa kuwa na watoto 12 ambapo kati yao ni watoto 7 walifariki katika umri mdogo.
Katika mwaka 1732, Laura Bass aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kitivo cha Fizikia katika chuo kikuu cha Bologna na wakati huo alikuwa ni mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa katika jopo la wanasayansi katika kitivo hicho cha Fizikia chuoni Bologna.

Baada ya kueleza na kuzitetea kazi zake (theses) za kisayansi ambazo zilikuwa ni 49 katika ukumbi wa Palazzo, Laura alitunukiwa shahada ya udakitari wa falsafa (PhD) mwaka huo huo 1732 mwezi Mei. Hapo Laura Bassi akawa mwanamke wa pili kutunukiwa shahada ya udakitari wa falsafa barani Ulaya baada ya Elena Piscopia kuwa wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo ya udakitari wa falsafa.
Kwa hakika, kipenda roho hula nyama mbichi. Mwezi uliofuata Laura Bassi alitoa tena kazi (theses) 12 mpya ambazo zilijadiliwa katika ukumbi mkuu wa Archiginnasio wa chuo kikuu cha Bologna nchini Italia. Hii ilikuwa fursa kubwa kwake kwa kuwa alipewa rasmi nafasi  ya kuwa mkufunzi wa kudumu katika kitivo cha Fizikia chuoni Bologna.

Haikuishia hapo tu. Pengine ndio ulikuwa mwaka wake wa mafanikio zaidi kitaaluma. Laura Bassi alitunukiwa nafasi ya kuwa profesa katika falsafa chuoni Bologna, nafasi hii ilimpa fursa ya kuwa profesa wa kwanza mwanamke barani Ulaya.
Katika kipindi kimojawapo darasani alisema (Kilatini): “De aqua corpore naturali elemento aliorum corporum parte universi” ambapo tafsiri yake katika lugha ya Kiswahili ni “maji ni dutu ya asili kwa vitu vingine.” Lakini pia, chuo cha Bologna bado kiliamini kwamba mwanamke anapaswa kuwa kiongozi wa maisha yake binafsi tu ila siyo kuwa kielelzo kwa maisha ya kitaaluma kwa wengi. Hali hii haikumpa kero yoyote profesa Laura! Aliendelea na kazi na tafiti mbalimbali katika Fizikia na kuandika kazi zingine zilizohusu kani ya graviti na umeme.

Kwa kuwa hakuwa na vipindi vya mara kwa mara chuoni hapo, profesa Laura aliamua kufanya majaribio katika maabara ndogo nyumbani kwake. Jambo hili lilimpa nafasi ya kuwa mbali na mawazo ya kufundisha chuoni Bologna kutokana na itikadi kali iliyokuwepo barani Ulaya kuhusu wanawake wakati huo. Pia, alikuwa akihudhuria mihadhara ya kisiasa kila mwaka iliyojulikana kama The Carnival Anatomy.
Laura Bassi alikuwa akilipwa ujira mkubwa sana chuoni Bologna fedha ambazo alizitumia zaidi katika kuboresha maktaba yake ndogo ya nyumbani. Alikuwa kiungo muhimu katika mikutano ya umma iliyohusisha chuo kikuu cha Bologna licha ya kuwepo kwa itikadi kali kuhusu wanawake wakati huo.

Baada ya kifo cha mhadhiri mkuu wa Fizikia kufariki chuoni hapo, Laura Bassi aliteuliwa kushika nafasi hiyo na mumewe alikuwa mhadhiri msaidizi katika kitivo hicho. Miaka miwili baade alifariki huku akiifanya sayansi kuwa sehemu ya maisha yake yote na kuboresha hadhi ya wanawake kitaaluma barani Ulaya.
Laura Bassi alifundisha Fizikia ya Newton (Newtonian Physics) kwa muda wa miaka 28 chuoni Bologna na kwa kushirikiana na mumewe alifanya tafiti mbalimbali kuhusu umeme jambo ambalo liliwavutia wanafunzi wengi kujiunga na fani ya umeme chuoni Bologna (Bolonya).

Katika maisha yake aliandika rasimu (miswada) 28 iliyohusu Fizikia na taaluma ya uhandisi wa maji (Hydraulics), kati ya rasimu hizo, ni rasimu 4 tu zilichapishwa kama vitabu na kutumika chuoni Bologna. Mwalimu wake mkubwa wa kiroho alikuwa ni Kardinali Prospero Lambertini (Papa Benedikti wa 14) ambaye alimhamasisha katika sayansi.
Kazi zake nyingi kuhusu umeme zilikuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wengi chuoni Bologna kwa muda mrefu. Mmoja kati ya waliofaidika na kazi za profesa Laura Bassi ni mwanafizikia nguli katika kitivo cha uhandisi wa umeme, huyo ni Alessandro Volta ambapo katika umeme kuna kizio cha “VOLT” kikiwa ni kiasi cha nguvu ya umeme kipitacho katika nyaya kimetokana na jina la ukoo wa Alessandro. Alessandro Volta wakati fulani baada ya kusoma kazi za Laura Bassi alisema; “hakuna Laura Bassi jijini London, na nitakuwa na furaha sana kusoma katika chuo hiki cha Bologna kuliko Uingereza ingawa imemzalisha Isaac Newton”. Naye Franscesco Algaroti alitunga mashairi memgi kumsifia Laura Bassi kwa kazi zake.

Laura Bassi alitunukiwa medani ya shaba kutoka kwa mchoraji Domenico Fratta kutokana na kazi yake iliyoitwa Pubblica Docente e Collegiate. Medani hiyo ilikuwa na picha ya Laura Bassi. Na pia, kreta mojawapo katika sayari ya Venus imepewa jina lake kwa hsehima ya kazi zake za kisayansi.

Huyu ndiye Laura Bassi. Juhudi na maarifa yake vimeisaidia dunia katika sayansi na teknolojia licha ya changamoto mablimbali za kiitikadi alizokutana nazo.
© KIZITO MPANGALA        0692 555 874

No comments:

Post a Comment

Maoni yako