ALBERT SANGA; NATAKA
KUOKOA MAZINGIRA NA KUWATAJIRISHA WATANZANIA
Albert Sanga(katikati) akiwa na mgeni wake kutoka Chuo Kikuu cha Moshi alipotembelea Mradi wa kampuni ya Fresh Farms(T) katika mashamba yake yaliyoko eneo la Mapanda, huko mufindi mkoa wa Iringa.
SWALI: Habari
za kazi ndugu Sanga. Watanzania wangependa kufahamu zaidi, nini hasa
uanchomaanisha kuokoa mazingira na kutatajirisha watanzania?
SANGA: Nashukuru ndugu yangu,
kazi zinakwenda vizuri na hakika hii ya kuokoa mazingira imenipa wasaa wa kujadiliana
na wadau mbalimbali nchini. Lakini dhumuni langu ni kuwatajirisha watanzania.
SWALI: Bado
hujatoa jibu, ni kwa vipi unaweza kuokoa mazingira na kuwatajirisha watanzania
kwa wakati mmoja?
SANGA: Kwa muda mrefu sana
nimekuwa nikinuia kuzikomboa fikra za watu kutoka kuitazama serikali kwa kila
kitu kuja katika kutekeleza wajibu wao ipasavyo. Nalenga hasa kuanzia uhaba wa
kifedha kwenda katika utele wa kifedha na kuwa na mfumo chanya wa kufikiria.
SWALI: Ni
hilo tu ndio linakusukuma uokoe mazingira, ama njia nyingine ya kutunza
mazingira kwa kuhimiza utajiri?
SANGA: Ndio maana nimesema
kukomboa fikra za wengi. Mkondo huu ni kuingia katika utekelezaji/matumizi ya
fikra chanya. kwahiyo kuna mradi wa kibiashara ambao napenda watanzania
washiriki kujitajirisha katika biashara ya miti. Nitakueleza kila kitu ikiwemo,
hali ya biashara hiyo kwa sasa na miaka ijayo, gharama na hatua za kuanzisha
biashara hiyo, usimamizi wa biashara hii, nadhani miti itaokoa mazingira pia.
SWALI:
umezungumzia biashara ya miti ambayo ndio msingi wa kuwatajirisha watanzania,
halafu unasema unaokoa mazingira. Je unaweza kueleza namna ya biashara ya miti
ilivyo na jinsi ya kuokoa mazingira?
SANGA: Lazima nikiri kilimo
cha miti kimepata umaarufu kwa miaka ya karibuni kutokana na ongezeko la
mahitaji ya mazao ya miti na changamoto ya mazingira.
Hapa Iringa tunaongoza kwa misitu mikubwa ya
kupandwa. Sasa hii, miti inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea
pamoja na utengenezeaji wa karatasi.
Hapa najua wengi tumezoea kuona mashirika ya
kimazingira kutoka Ulaya yananunua hewa ukaa.
Kwa maana hiyo unaweza kupanda shamba la miti
halafu ukawa unakusanya dola kwa kuuza hewa ukaa wakati ukisubiri miti ikomae
uvune mbao, nguzo ama miti ghafi ya kutengenezea karatasi. Utakuwa umeokoa
mazingira pia.
Albert Sanga akiwa na mgeni wake Emmanuel Lulandala kutoka Chuo Kikuu cha Biashara na Ushirika cha Moshi
SWALI: Umeeleza
kuwa kuna mashirika kutoka nchi za Ulaya yananunua hewa ya Ukaa, kisha
unazungumzia pia biashara ya miti, hivi unatenganisha vipi haya mambo matatu?
SANGA: Binafsi
niliichangamkia biashara hii miaka minne iliyopita. Nimejiwekea lengo la
kupanda miti ekari ishirini kila mwaka.
Kilimo hiki cha miti ni uwekezaji wa muda wa
kati na mrefu. Unajua tena, Watanzania wengi huwa hawavutiwi na uwekezaji wa muda
mrefu.
Lakini kama una mpango kuimarika kiuchumi
usikwepe kufikiria uwekezaji wa muda mrefu. Waingereza husema “Information is
power”.
Wengi hawajachangamkia fursa hii kwa kukosa
taarifa tu. Ndio maana nasema wenzetu Ulaya na Amerika wananunua hewa ya Ukaa,
sisi tusizubae kwa hilo. Kilimo cha miti ndio suluhisho.
SWALI: Sawa,
kwahiyo unataka kusema kuna ekari ambazo zinauzwa kwa wateja ama watanzania
wanaotaka kuanzisha kilimo cha Miti hapa Iringa na gharama zake zipoje kwa
manufaa yao?
SANGA: ndiyo, zipo ekari
zinauzwa, kwa utaratibu rasmi na kwa mujibu wa sheria ya ardhi. Kwa mfano ekari
moja ya shamba inachukua wastani wa miti mia sita (600).
Wastani wa chini wa mti mmoja kwa sasa
uliokomaa ni shilingi elfu ishirini (20,000). Ina maana katika ekari moja ukiwa
na miti iliyokomaa unakusanya jumla ya shilingi milioni kumi na mbili (12,000,000).
Hiyo fedha ni kadirio la chini sana, utaipata
ikiwa unaamua kuuza kwa bei ya jumla miti ikiwa shambani.
Lakini kama ukiamua kupasua mbao mwenyewe
unaweza kuvuna mbao hadi za milioni ishirini na tano (25,000,000) kwa ekari
moja.
maeneo ya Mufindi yanafaa pia wka kilimo cha Chai. Ni mji wenye uoto wa asili na udongo unafaa kwa Kilimo cha Miti na Chai
SWALI:
Hivyo kilimo hicho cha miti kinalenga kupasua mbao na kuziuza. Huoni kuwa hilo
la miaka minne na gharama za upasuaji mbao zipo juu, unadhani mteja atamudu
namna gani kwa hilo?
SANGA: Hapana, hakuna gharama
za moja kwa moja hapa, kumbuka Iringa ni mkoa wenye miundombinu nafuu. Kwa
mfano gharama za kununua shamba tupu ni shilingi laki mbili hadi milioni moja,
kutegemea na maeneo unayotaka.
Gharama za kuandaa shamba, kununua miche na
kupanda ni kati ya shilingi laki nne hadi laki sita. Hii ina maana unaweza
kumiliki ekari moja ya msitu wa miti kwa shilingi laki sita tu!
SWALI:
Je,suala la ulinzi na usalama wa miti hiyo linakuwa mikononi mwa mteja au
muuzaji, na kuna utaratibu gani katika suala hilo?
SANGA: Kwanza elewa kilimo
cha miti ni rahisi sana kwa sababu ukishapanda hakihitaji uangalizi mkubwa na
wala huhitajiki kuwa karibu na shamba/mradi muda wote.
Kuna kazi chache ambazo zinahitajika
ukishapanda shamba lako. Mvua inyeshe ama isinyeshe mti wa mbao, nguzo ama
karatasi ukishachipua huwa haufi kwani huendelea kutumia unyevu wa ardhini.
Kazi namba moja unapokuwa umeshakamilisha
upandaji wa miti kwenye shamba; ni kutengeneza njia za kuzuia moto walau mara
moja kwa mwaka, kazi ya pili ni kufyekea miti inapokua walau kwa mwaka mara moja
(prooning). Gharama zote hazizidi laki mbili kwa mwaka mzima.
SWALI: Kwahiyo
unataka kusema kilimo hicho kina muda wake kama kingine. Na, je miti hiyo
inachukua muda gani hadi kukomaa kisha mteja akavuna faida?
SANGA: Ndio maana nasema
nataka kuwatajirisha watanzania. Hii miti hukomaa kuanzia miaka sita hadi kumi,
lakini inategemea na utunzaji wako.
Kwa mfano ukichukua shilingi laki mbili kugharimia
shamba kila mwaka ukazidisha mara sita unapata shilingi milioni moja na laki
mbili (1,200,000/=) na ukizidisha mara kumi unapata shilingi milioni mbili
(2,000,000/=).
Gharama za kuhudumia shamba la miti ekari moja
kutoka kupandwa hadi kuvunwa ni kati
ya shilingi milioni moja na laki mbili na milioni mbili.
Ukichanganya na gharama ya kupata ardhi na kupanda
miti yenyewe unapata kuwa gharama nzima hadi unavuna ni kati ya shilingi
milioni milioni mbili (2,000,000/=) kwa kadirio la chini sana.
SWALI:
Suala hilo la kilimo cha miti bila shaka inakusudia kuwa biashara yenye tija
kwa mmiliki. Lakini wewe umesema mwanzoni kuwa unakusudia kutunza mazingira. Je
utafanya hivyo kwa namna gani?
SANGA: Nadhani unafahamu kuwa
ardhi ni rasilimali inayopanda thamani kila siku. Vile vile tunatambua kuwa
suala la mazingira ni tete kwa sasa na katika karne zijazo kama wataalamu
wanavyosema.
Kwahiyo sisi Fresh Farm(T) ukiwa na shamba la
miti leo; thamani ya ardhi hiyo inazidi kupanda kila siku na miti uliyopanda
inazidi kupanda thamani kila kukicha.
Jambo la uhakika ni kuwa hata kama bei ya miti,
mbao, nguzo itayumba hutaweza kupoteza mtaji uliotumia na wala hutakosa
kuzalisha faida kwa shamba utakalokuwa umemiliki, iwe ni ekari moja, kumi, mia
ama elfu moja.
Mbali na hivyo unaweza kudhani miaka sita hadi kumi ni mingi mno; bado
una nafasi ya kupata faida hata ndani ya mwaka mmoja, miwili n.k.
Ukishapanda shamba la miti ekari moja kisha
baada ya mwaka mmoja ukaamua uuze utauza si chini ya milioni mbili hadi nne.
Kukusanya milioni nne kwa mtaji wa laki sita,
pasipo kutumia muda mwingi ama usumbufu wa kusimamia; hakika ni faida nono. Na
utakuwa umechangia kutunza mazingiara, hiyo ndio maana yangu ndugu.
SWALI:
Sanga, watu wengine wanaishi Moshi (Kilimanjaro), Musoma (Mara) au Ilemela
(Mwanza), wangependa wawe wakulima wa miti. Lakini hawapafahamu Iringa na hata
kama wanafahamu wataanzia wapi kupata hayo maeneo, wengine wako mbali hawawezi
kuhudumia shamba lao Iringa, watafanyaje?
SANGA: Ni kweli kwa wengine
imekuwa changamoto. Lakini majibu hayakosekani. Kiukweli msimu wa kutafuta na kuandaa mashamba sisi Fresh Farm
(T) tunaanza Agosti na Oktoba na upandaji ni Novemba, Desemba na Januari.
Katika kuwasaidia wengine ili wawekeze katika
biashara hii ya mashamba ya miti mimi na wewe tuungane na serikali na dunia
nzima katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupanda miti mingi.
SWALI:
umekuwa ukitaja suala la Fresh Farm (T). Ni nini hicho ambacho kinaweza
kuwaelewesha watanzania?
SANGA: ndugu yangu, siku zote
napenda kuendeleza wafanyabiashara na wawekezaji wapya, kupitia mfumo wa
biashara zetu. Hivyo tumeanzisha kitengo maalumu cha Fresh Farms (T).
Kazi yetu kupitia kitengo hiki itakuwa ni kutoa
ushauri wa kibiashara, kutafuta maeneo ya kilimo cha miti hapa Iringa, na kiasi
cha ekari anazohitaji mteja.
Kazi nyingine ni kuandaa hayo mashamba, kupanda
miti na kusimamia utunzaji wa shamba katika hatua za awali.
SWALI:
Ndugu Sanga, kwa kumalizia naona bado hujafafanua suala la umilikaji ardhi,
yaani ekari zinazonunuliwa na mteja. Kuna utaratibu gani?
SANGA: sisi Fresh Farm (T) tunatumia
sheria ya ardhi ya mwaka 1999, pia taratibu na tamaduni zote za wenyeji zinazohusiana
na umilikaji ardhi. Tuna uhakika wa kutunza mazingira na kuwatajirisha
watanzania. Nawakaribisha sana hapa Mufindi.
nawatakieni kila la kheri pia mafanikio mema na kazi iende ikiwa imenyooka.
ReplyDeleteNashukuru kwa maelezo yako mazuri sana.Ningependa kufahamu kama kuna mbolea yoyote inayohitajika wakati wote wa kutunza miti tya mbao.Kama ipo ni aina gani?
ReplyDelete