July 16, 2013

IJUE RASIMU YA KATIBA 2013; MAPITIO NA MAPENDEKEZO


Na Edgar Mwandemani.


Ibara ya 78 na 79

Weredi na wasomi wengi wamekwisha kutoa maoni yao, wengi wakijielekeza katika suala la muundo wa muungano. Mimi kwa leo nitaanza na ibara tajwa ambazo haiyumkiniki zinaweza kusahaulika.

Ibara hizi kwa pamoja ni juu ya malalamiko kuhusu uhalali wa matokeo na Kiapo cha Rais!

Zinasema:

Ibara ya 78 (2) na ( 3)- Mlalamiko ya matokeo
(2.) Malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais yatawasilishwa Mahakama ya Juu ndani ya muda wa siku saba baada ya siku ya kutangazwa matokeo ya Uchaguzi wa Rais.

(3.) Mahakama ya juu itasikiliza na kutoa uamuzi wa shuari la kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Rais katika kipindi cha siku kumi na nne tangu kupokea malalamiko yaliyowasilishwa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (2) na uamuzi huo utakuwa wa mwisho.

Vipengele hivi vinafanana kimaudhui na Ibara ya 140 (1) na (2) ya Katiba ya Kenya kama ilivyopitishwa 2010. Tofauti zake ni lugha (kiingereza kwa kiswahili) na mpangilio wa namba- kimsingi tumechukua kama vilivyo!

Ibara ya 79- Kiapo cha Rais
(1) Rais Mteule ataapishwa na Jaji Mkuu na atashika nafasi ya madaraka ya Rais Mapema iwezekanavyo baada ya kutangazwa kwamba amechaguliwa kuwa Rais, lakini kwa hali yoyote, hatashika madaraka kabla ya kupita siku thelathini kutoka siku ya matokeo ya uchaguzi wa Rais yalipotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi au siku ya kuthibitishwa na Mahakama ya Juu.

Moani: Ibara hizi mbili zinatoa Haki kwa kunyang'anya haki- ni vipengere kinzani. Itakumbukwa kuwa vipengele hivi ni ingizo jipya mara baada ya malalamiko ya muda mrefu juu ya uwazi wa matokeo ya rais ikiwemo haki ya kuyapinga.

Nirejee tena Katiba ya Kenya; katika Ibara 141 (2) (a) na (b) juu ya kuchukua ofisi- Kiapo!

2) The president elect shall be sworn in in the first Tuesday following:-
(a) the fourteenth day after the date of the declaration of the result of the presidential election, if no petition has been filed under Article 140; or
(b) the seventh day following the date on which the court renders a decision declaring the election to be valid, if any petition has been filed under Article 140.

Maoni: Kimsingi vipengele hivyo katika Katiba ya Kenya vinatoa masharti kuwa hakutakuwa na kuapishwa kwa rais wala kukamata madaraka mpaka ile haki iliyotolewa katika ibara ya 140 itekelezwe pasipo shaka- uchaguzi wa uliomalizika mwezi Machi, 2013 umethibitisha hilo. Sisemi tuige kila kitu kutoka katika kipengele hiki lakini kwa kuwa lengo ni kuweka uwazi katika mchakato wa matokeo ya rais hatuna budi kuiga jambo hili.

Kwa upande wa Ibara tajwa katika rasimu yetu zimetoa na kunyang’anya haki hii. Ibara ya 79 (1) ndio imenyang’anya haki iliyotolewa na Ibara ya 178 (1) na (2) kwa kuruhusu kuapishwa kwa Rais mara baada ya matokeo kutangazwa. Kipengele hiki kimeyapa uhalali matokeo yatakayotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi mara baada ya kutangazwa hata bila ya kusikiliza pingamizi lolote na kwamba rais aliyeapishwa atasubiri siku 30 kabla ya kushika madaraka. Hapa tumedanganywa! Mtu haapishwi na kusubiri kushika madaraka; anaweza kusubiri kuapishwa ili ashike madaraka lakini si vinginevyo. Siku 30 zinazotajwa hapa ni kiini macho, kwani ni kwa namna gani mamlaka yoyote itaweza kutengua kiapo cha mtu eti kwa kuwa tu mahakama imesema sio halali. Hizi ni fujo!

Inawezekana tulitaka kuiga mfumo wa Marekani ambapo Rais Mteule husubiri siku 100 kabla ya kushika madaraka. Lakini kwa kuwa kiapo huenda na madaraka, Rais Mteule wa marekani huwa na siku 100 za mpito kabla ya kuapishwa na kushika madaraka- Hapishwe halafu akasubiri siku 100 kabla ya kushika madaraka. Kiapo ni kazi kiapo ni mamlaka hakiwezi kwenda kinyumenyume.

Aidha, tukirejea tena kwa wenzetu Kenya kwa mara nyingine, mara baada ya matokeo kutangazwa na Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi huku mpinzani wake Raila Odinga akiwasilisha malalamiko Mahakama ya Juu dhidi ya matokeo: ililazimu mamlaka husika kuwasihi Rais Mteule na Mwenza wake pamoja waache mara moja misafara na ziara kana kwamba wameshashika madaraka kwani kiapo bado na lolote linaweza kutokea. Shukrani kwamba mambo yalibaki kama yalivyotolewa na Tume.

Tuendelee na mjadala mimi nimeanza kwa Ibara hizo.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako