Na,
Albert Sanga, Iringa.
Rais wa Marekani Barack
Obama alipofanya ziara ya kiserikali nchini kuna mengi tumesikia. Ujio wa Obama
umekuwa na shamrashamra nyingi sit u Dar es Salaam bali macho na masikio ya
watanzania wote yameelekezwa katika safari hii. Ni ziara ambayo pamoja na mambo
mengine mengi pia imekusudia kuimarisha uhusiano mwema baina ya Tanzania na
Maekani.
Kwa miongo mingi huko
nyuma, Marekani imekuwa na historia ya kuzisaidia na kushirikiana na nchi
mbalimbali za Kiafrika. Maeneo ambayo Marekani imeng’aa kuisaidia Afrika ni
katika mapambano dhidi magonjwa ya malaria na Ukimwi. Pia Marekani imekuwa
mstari wa mbele katika kuzisaidia nchi za Afrika kibajeti, kiulinzi, haki za
binadamu na utawala bora. Eneo jingine muhimu ambalo Marekani imeelekeza macho
yake Afrika ni katika ushirikiano wa kibiashara. Ni Katika ushirikiano huu wa
kibiashara ndipo ambapo Marekani iliamua kuanzisha mpango na sheria maalumu
iitwayo Africa Growth Opportunities Act (AGOA).
Kupitia mpango na sheria
hii, Marekani imekusudia kuimarisha ushirikiano wa kibiashara wenye usawa baina
ya Africa na wao. Kabla ya AGOA ilionekana kuwa nchi nyingi za Afrika hazikuwa
na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye kukidhi vigezo vya kiviwango vilivyoko
katika masoko ya Marekani. Mojawapo ya zana muhimu
sana kupambana na umasikini ni biashara. Afrika inahitaji sana kuongeza uwezo
wake wa kusafirisha bidhaa inazozizalisha kwenda nje ili iweze kugharimia
maendeleo yake. Mbali na changamoto za ruzuku katika sekta mbalimbali ikiwemo
kilimo, fursa ya Afrika kusafirisha bidhaa zake katika nchi zilizoendelea ni
finyu mno.
Ukomo wa ujazo (quotas)
unazuia kiwango cha bidhaa zinazoweza kuingia katika soko Fulani; na wakati huo
huo ushuru unaotozwa kwa bidhaa hizo unazifanya bidhaa hizo kuwa gharama na
zinashindwa kushindana katika masoko hayo ya kimataifa. Wakati mwingine viwango
vya ushuru vinakuwa vikubwa mno kiasi kwamba Afrika inakwama kuendelea
kuzalisha bidhaa hizo kwa kokosa masoko na ushindani.
AGOA ni njia mojawapo ambayo Marekani imeamua
kuitumia ili kufungua masoko yake kwa Afrika. AGOA ilianzishwa mwaka 2000 kama
sheria ya kibiashara inayokusudia kuongeza na kuhamasisha biashara baina ya
nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na Marekani. Katika sheria hii Marekani
inaruhusu bidhaa kutoka katika nchi hizi kuingia nchini humo pasipo kulipiwa
kodi. Tangu kuanza kwa mpango huu wa AGOA nchi nyingi zimeendelea kunufaika mno
kibiashara.
Zaidi ya bidhaa 6,000 zimeorodheshwa kunufaika na
mpango huu wa AGOA. Kimsingi ili nchi ipate fursa ya kuingizwa katika mpango wa
AGOA inatakiwa iwe imetimiza masharti kadhaa ikiwemo kuboresha utawala wa
sheria, haki za binadamu na kuheshimu haki na viwango vya wafanyakazi. Tanzania
imekuwa ni moja ya nchi takribani 40 zilizokidhi vigezo, hivyo na hadi sasa imo
ndani ya AGOA.
Baadhi ya bidhaa zilizomo kwenye orodha ya mpango
wa AGOA ni pamoja na madini, mafuta, bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo,
bidhaa zilizoongezwa thamani ikiwemo nguo, viatu, vinywaji, Hii ina maana
wakulima wa maua, wafugaji wa nyuki, ng’ombe na bidhaa zingine wote kwa pamoja
wananafsi ya kunufaika na AGOA.
Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha bidhaa
zinazoingia Marekani kutoka katika nchi za AGOA kimekuwa kikiongezeka kila
mwaka tangu kuanzishwa kwa AGOA.
Inatajwa kuwa kiwango hicho kimekuwa kikiongezeka kwa wastani wa
asilimia 30. Vile vile biashara baina ya pande hizi mbili imeongezeka mara tatu
zaidi ya ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwa sheria hii ya AGOA. Wajasiriamali wa Tanzania hatujachangamkia vya
kutosha fursa AGOA kwa sababu taarifa zinaonesha kuwa nchi zinazooongoza
kuitumia fursa ya AGOA ni zile za Magharibi mwa Afrika. Katika jumla ya thamani
ya bidhaa zilizopelekwa Marekani za takribani dola bilioni 100, mafuta
yanaonekana kuongoza. Ingawa nchi zinazozalisha bidhaa za kilimo, nguo na
mashine za kimakenika zimenufaika pia.
Ingawa, AGOA ilipangwa kukoma mwaka 2008, lakini
Marekani iliamua kupitisha marekebisho ya sheria ya AGOA na kurefusha mpango wa
AGOA hadi mwaka 2015. Katika mpango na marekebisho haya inaruhusu nchi masikini
kutumia malighafi za bei nafuu kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya
kutengeneza nguo na kuzipeleka Marekani.
Kila mwaka huwa kunaitishwa jukwaa la AGOA ambapo
huwaleta pamoja viongozi wa kiserikali na sekta binafsi kutoka Afrika na Marekani.
Jukwaa hili hufanyika jijini Wshngton kila mwaka na pia jukwaa hili hitishwa
katika moja wapo wa nchi zilizokidhi vigezo kuwemo katika AGOA. Hadi sasa
majukwaa ya AGOA yamefanyika mara nne jijini Washington, na mara moja moja
katika nchi za Senegal, Ghana, Kenya na Zambia.
Kimsingi mpango wa AGOA
umelenga kuwanufaisha wajasiriamali ambao ndio wanaotakiwa kuchangamkia fursa
ya kuzalisha bidhaa na kuzisafirisha Marekani ambako licha ya kusamehewa ushuru
lakini pia kuna masoko ya uhakika. Ni katika njia hii ndipo ambapo nchi yetu
inaongeza thamani yake kwa kupata fedha nyingi za kigeni na kukuza uchumi.
Wajasiriamali na
makampuni yote yanayotaka kusafirisha bidhaa zake kupitia mpango wa AGOA, ni
sharti wafikie vigezo kadhaa vya biashara za kimataifa ikiwemo kuwa na maelezo
sawia na ya kina kuhusu asili (zinakotoka), ya bidhaa zenyewe.
Msafirishaji husika
(kampuni, mjasiriamali) anatakiwa kujisajiri katika wizara husika katika nchi
anakotoka. Kwa hapa msafirishaji atatakiwa kujisajiri katika wizara ya viwanda
na biashara. Vile vile kunakuwa na hatua kadhaa za kufuata ili kupatiwa vibali
vya kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi.
Vitengo katika serikali
na ndani ya wizara zinazohusika na ufanikishaji wa mpango wa AGOA, kwa pamoja
wanahitaji taarifa za wajasiriamali na haya makampuni kwa ajili ya takwimu,
kudhibiti ubora na viwango vya bidhaa zinazopelekwa huko nje pale inapohitajika.
Nimebainisha hapo juu
ya kwamba wajasiriamali na makampuni yana fursa za kusajiliwa na kunufaika na
AGOA, hata hivyo pia niseme kuwa anayesajiliwa anaweza kuwa mzalishaji,
mtengenezaji ama msambazaji wa bidhaa zilizopo kwenye orodha ya AGOA.
Kwa upande wa Tanzania
yeyote anayetaka kusajiliwa kwa ajili ya AGOA anashauriwa kuwa amejiunga ama
kusajiliwa na mpango wa EPZ (Export Proccessing Zone). EPZ ni maeneo maalumu ya
kiuchumi na kiuzalishaji yenye lengo la kuwasaidia wazalishaji kuongeza ubora
wa bidhaa zao na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa katika maeneo hayo zinakadhi
vigezo vyote vya kimataifa.
Vigezo rahisi
vinahitajika katika kwa msafirishaji kujiunga na AGOA ikiwemo jina la biashara,
majina ya wakurugenzi, orodha ya bidhaa zinazokusudiwa kusafirishwa kwenda nje,
orodha ya malighafi zinazotumika na rejea zake za ushuru, ufafanuzi kuhusu
bidhaa, mchanganuo gharama. Sio lazima mzalishaji, msambazaji ama mtengenezaji
kuhangaika na kila kitu, isipokuwa inawezekana kuwatumia mawakala wa
usafirishaji na uingizaji.
Serikali kupitia vyombo
vyake vinavyohusika na biashara ikiwemo TRA vinatoa usaidizi na maelekezo ya
kutosha sana kuwawezesha wajasiriamali wanaochangamkia AGOA. Katika vitengo
hivi mjasiriamali anaechangamkia fursa ya AGOA atapewa nyaraka zote
zinazohitajika ambazo zitamsaidia kupokelewa kwa bidhaa zake huko Marekani.
Serikali kupitia vyombo
vyake vya kibiashara vitakagua na kujiridhisha katika maeneo yafutayo kabla ya
kutoa nyaraka na ruhusa. Watakagua maghala ya kuhifadhia, watasaidia
kuidhinisha malighafi za bidhaa husika, watapitia takwimu za usafirishaji kwa
mujibu wa taratibu za AGOA, watakabidhi vyeti na nyaraka kwa mjasiriamali.
Wajasiriamali wa
Tanzania tunatakiwa tujiamini kwa kuchangamkia fursa za kimataifa ikiwemo AGOA.
Hakuna sababu ya kujiweka kando na kudhani kuwa AGOA ni ya watu Fulani Fulani
ama kudhani ni kwa ajili ya makampuni makubwa. Kila mjasiriamali ana haki ya
kunufaika na AGOA mradi tu akidhi vigezo vilivyoainishwa.
Tujenge mazoea ya
kutembelea vitengo mbalimbali serikalini ikiwemo wizara ya viwanda na biashara
ili kujifunza na kupewa maelekezo ya namna ya kunufaika na mpango wa AGOA.
Mbali na kutembelea wizarani vile vile wajasiriamali wanaweza kutembelea kituo
cha uwekezaji (TIC) pamoja na chemba ya TCCIA.
0719
127 901, stepwiseexpert@gmail.com
No comments:
Post a Comment
Maoni yako