Na KIZITO MPANGALA
Mafundisho ni moja kati ya
elimu ambayo haina mpinzani katika maisha yetu ya kila siku. Mafundisho hayo
yapo kwa namna mbalimbali, kuna mafundisho ya jumla, kuna mfundisho ya kipekee
ambayo hugusia katika uga husika kama vile mafundisho ya dini, mafundisho ya
stadi za kazi, mafundisho ya maadili, mafundisho ya rika na kadhalika. Hayo yote
husaidia kujenga jamii na kuiweka katika mwenendo unaokunalika na wengi na
ambao una manufaa mazuri kawa jamii hiyo na pengine hata kuakisi kwa jamii
nyingine mahali popote duniani.
Mafundisho ya kijinsia yana
umuhimu mkubwa sana katika maisha yetu. Jinsia fulani ifundwe yale yanayopaswa
kufanyika nayo ili kuendeleza maadili au jeme lipatikanalo kutoka katika
mafundisho hayo. Ikiwa mtu wa jinsia tofauti ataifunda jinsia nyingine fundisho
fulani, kinachotakiwa ni kufikiri kilichosemwa ili kubaini kama kina manufaa ya
kurekebisha kitu fulani kwa jinsia iliyofundwa au kama kina maudhui mabaya
dhidi ya jinsia iliyofundwa kishapo hukumu itolewe, iwe hukumu chanya au hukumu
hasi.
Kitendo cha kutoa mafundisho
kinaweza kuwa cha namna mbili. Huenda mafundisho yakatolewa kinagaubaga au kwa
kutumia mifano ambayo inalenga kurekebisha jambo fulani katika jamii. Ikiwa hilo
linafanyika, si vema kulalamika ghafla bila kufikiri lengo au dhamira ya
mafundisho hayo. Na kwa sasa jinsi ilivyo rahisi kusambaza taarifa katika
mitandao basi ndani ya dakika kadhaa dunia yote huenda ikajua kinachojiri na
kisha kila aliyepata taarifa anatoa maelezo yake kadiri ya taarifa
ilivyomfikia. Watasifu, watalaani, watahamasisha watu kuwa watulivu,
watamshutumu mnenaji, watamtetea mnenaji na kadhalika.
Katika suala hili la kuishi
katika mafundisho yanayotolewa kwa mifano, inawezekana mfundaji anakuwa na nia
ya kuonya au kurekebisha jambo fulani lakini huenda akaeleweka tofauti na lengo
la fundisho lake. Hii inatokea mara nyingi na pengine husababisha maandamano
ambayo yanaweza kuzua madhara kwa waandamanaji wakiwa wanakemea fundisho
wasilolikubali au kama limefikirirwa kuwa ni la kejeli kawa kundi fulani katika
jamii.
Nchini India, profesa mmoja
katika chuo cha taasisi cha Farook katika jimbo la Kerala kusini mwa nchi hiyo
amekuwa katika wakati mgumu baada ya kuwakanya wasichana wa chuo hicho. Profesa
Jouhar Munavvir T, aliwakanya wasichana hao kuhusu uvaaji wa mavazi ambayo
huacha wazi sehemu za kifua na kusababisha mwonekano wa matiti yao huku
vichwani wakiwa wavalia hijabu. Profesa Jouhar aliwaambia wanafunzi kwamba
sehemu hiyo huwavutia wanaume na ndipo hutambua kuwa mnavutia vema na kisha
kuwanyanyasa. Katika mafundisho yake hayo kuhusu mavazi alifananisha matiti
hayo na tikitimaji huku akisema: “ni kama kipande cha tikitimaji kilichokatwa
kuonyesha jinsi tunda hilo lilivyoiva vizuri,” kauli hii ambayo aliitoa kwa
lengo la kuhimiza wasichana hao kujisitiri kikamilifu, imeeleweka vibaya kwa
watu wengi nchini India.
Kueleweka vibaya kwa kauli hii
ni kutokana na profesa Jouhar kusema kwa msisitizo huku aliwa na lengo la
kuwataka wasichana hao wawe wanajisitiri vema na siyo kujisitiri kichwani tu
kwa kuvalia hijabu kikamilifu huku sehemu zingine za miili yao huziacha wazi. Wanawake
wengi wamemshutumu profesa Jouhar na kufanya maandamano sehemu kadhaa nchini
India kwa lengo la kumkemea profesa huyo kwamba ametoa kauli ya kuwavunjia
heshima wanawake kwa kufananisha matiti yao na vipande vya tikitimaji
liliokatwa. Wanawake kadhaa nchini India walitumua picha zao katika mitandao ya
kijamii huku wakiwa bila nguo kuanzia kiunoni kwenda juu, yaani sehemu za kifua
ziliachwa wazi, wakiwa na lengo la kuiambia jamii kwamba profesa Jouhara
amewadharau na hivyo wameamua kuiacha wazi sehemu hiyo watu waione na
waichukulie kuwa ni ya kawaida tu. Wanawake hao walioachia sehemu hizo wazi nao
walishutumiwa vikali huku wakiitwa ‘malaya’ na kwamba walikuwa wakitafuta
wateja, lakini hilo halikuwarudisha nyuma.
Kwa ujumla kauli ya profesa
Jouhar haikuwa ya kuvaliwa njuga kiasi hiki. Hii inaonyesha wazi kwamba jimii
zetu nyingi duniani zimechoka kuishi na mafundisho yanayotolewa kwa mifano na
watu mbalimbali. Na kwa upande wa wanawake uchovu huu umekuwa mkubwa sana kiasi
kwamba mzigo wa kilogramu moja tu unaweza kubadili taswira ya uchovu huu
duniani kote.
Wasichana na wanawake wengi
sasa wanaishi mazingira kama ya wasichana wa chuo cha taasisi cha Farook na
hasa huko vyuoni. Katika hali ya kawaida mwanamke fulani anaweza kuvaa mavazi
ambayo yanaweka wazi sehemu fulani ua kifua chake na hivyo mgawanyika wa matiti
yake ukaonekana barabara, lakini akiwa ananyonyesha ataona aibu kutoa titi moja
na kumnyonyesha mtoto sehemu zenye watu wengi au sehemu za mikusnayiko
mbalimbali. Sasa nani bora hapa, mtoto au fasheni?
Kauli aliyoitoa profesa Jouhar
ilipaswa kutafakariwa sana na kuwa ni mafundisho kwa wasichana na wanawake wa
namna hiyo lakini pia hata kwa wavulana na wanaume, utaona aibu kuchomekea vema
shati lako lakini mazingira mengine unaona fahari kuvalia mlegezeo, hivyo basi,
jamii inaonekana kuchoka kuishi kwa mafundisho yanayotolewa kwa mifano ili mtu
arekebike. Badala yake, wanajamii wengi husukumwa na matangazo mbalimbali
kuhusu mitindo ya maisha katika mitandao ya kijamii.
Rai ya profesa Jouhar si
kukejeli wanawake, bali ni kurekebisha mwenendo aliouna kuwa haufai, ndiyo
maana aliamua kutoa fundisho lake kwa mfano. Na mfano alioutumia ni kipande cha
tikitimaji kilichokatwa kuonyesha tunda hilo lilivyoiva vizuri ili kuwavutia
wateja.
© KIZITO MPANGALA
No comments:
Post a Comment
Maoni yako