Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Siku kama ya Jana (Tarehe 16 Mwezi wa 12) miaka 49 iliyopita
(mwaka 1963) Bendera ya lililokuwa Taifa la Zanzibar (sasa ni sehemu ya Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania) na Bendera ya Jamhuri ya Kenya zilipandishwa Hewani
katika Viwanja vya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani ikiwa ni ishara ya
kutambulika Rasmi kwa Mataifa hayo kama Wanachama wapya wa Umoja wa Mataifa.
Zanzibar ilipata Uhuru wake Disemba 10, mwaka 1963 chini ya
Utawala wa Sultan kama Mkuu wa Nchi na Uongozi wa Shughuli za Serikali wa
Waziri Mkuu Sheikh Mohammed Hamad Shamte wa Ushirikiano wa Vyama vya Zanzibar
& Pemba Peoples Party (ZPPP) na Zanzibar Natiolist Party (ZNP) au
"Hizbu" cha aliyekuwa Waziri wa Kwanza Mambo ya Nje wa Zanzibar
Sheikh Ali Muhsin Barwany.
Balozi Hilal Mohammed Hilal Al-barwan aliteuliwa kuwa Balozi
wa Kwanza wa Zanzibar katika Umoja wa Mataifa ambapo Disemba 16, 1993 Waziri
Mkuu Mohammed Hamad Shamte alilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
katika Hotuba yake ya kuitambulisha Zanzibar kama Mwanachama Mpya wa Umoja wa
Mataifa.
Tarehe 17 Disemba, 1963 Balozi Hilal Mohammed Hilal
Al-Barwan aliwasilisha Hati zake za Utambulisho kama Balozi wa Kudumu wa
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana U Thant.
Serikali husika (iliyokabidhiwa Uhuru) ilidumu kukaa
Madarakani kwa muda Mchache tu kabla ya kufanyika Mapinduzi yaliyoongozwa na
Makomredi wa ASP na wale wa Chama cha Ummah Party kwa Msaada Mkubwa wa Serikali
ya Chama cha Tanu ya iliyokuwa Nchi ya Tanganyika (sasa Tanzania Bara, ikiwa ni
sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).
Mapinduzi hayo yalimleta Madarakani Sheikh Abedi Amani
Karume kama Rais Mpya wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuwa Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi katika Serikali iliyoundwa kwa ubia wa Wanachama wa Chama
cha ASP na wale wa Ummah Party cha Komredi Abdulrahman Mohammed Babu.
MCHAKATO ULIPOANZIA.
Mchakato wa Zanzibar kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa
ulianza Mwaka 1960 ambapo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Dag
Hamaskold aliitembelea Zanzibar Tarehe 6, Januari, mwaka 1960 wakati akielekea
katika Ziara yake Maalum ya Kikazi Nchini Zaire (Sasa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo).
Pichani ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Dag
Hamaskold akiwa pamoja na Viongozi Mbalimbali pamoja na Wajumbe wa Baraza la
kutunga Sheria la Zanzibar (Legco) katika Viwanja vya Bustani ya Victoria huko
Zanzibar wakati wa Ziara yake hiyo, ambapo Picha hii hutajwa kama Picha ya
Mwisho ya Bwana Darg na jopo lake kabla ya Ndege yake kuanguka huko Rhodesia ya
Kusini (sasa Zambia) wakati akielekea Zaire.
Wengine kwenye Picha waliosimama kutoka kushoto kwenda kulia
ni Sheikh Dahman (Mjumbe Baraza la kutunga sheria, LEGCO kupitia chama cha
ZNP), Sheikh Ali Sharif (Mjumbe Baraza la kutunga sheria, LEGCO kupitia Chama
cha ASP), Bwana N.V.Patel (Mjumbe Baraza la kutunga sheria, LEGCO kupitia ASP),
Bwana Master (Mjumbe katika Msafara wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa), Sheikh
Rashid Al-Ghaithy (Mjumbe Baraza la kutunga sheria, LEGCO kupitia ZNP) na
Sheikh Juma S. Al-Mugheiry (Karani wa Baraza la kutunga sheria, LEGCO).
Waliokaa kutoka Kushoto kwenda kulia ni Sheikh Juma Aley
(Waziri kupitia Chama cha ZNP), Sheikh Abeid Amani Karume (Waziri kupitia ASP)
Bwana Dag Hamaskold (Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa), Bwana Smithson (Waziri
katika Serikali ya Uingereza), Bwana Kirk Madan (Katibu Mkuu Kiongozi), Bwana
Hilal Mohammed Hilal Al-Barwani (Waziri, ZNP na Pia Balozi wa Kwanza wa
Zanzibar Umoja wa Mataifa) na Sheikh Ameir Tajo (Waziri, ASP).
ZANZIBAR NA TANGANYIKA ZAPOTEZA UANACHAMA WAKE KATIKA UMOJA
WA MATAIFA.
Tanganyika imekuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa tokea
Disemba 14, mwaka 1961 mara baada ya kupata Uhuru wake tarehe 9 Disemba, mwaka
1961 kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza ambapo Dr. Vedastus Kyaruzi alikuwa
Balozi wa Kwanza wa Tanganyika katika Umoja wa Mataifa akifuatiwa na Balozi A.
Z. Nsilo Swai na kisha Chifu Erasto A. M. Mang'enya kuwa Balozi wa Mwisho wa
Tanganyika katika Umoja wa Mataifa.
Mara baada ya Muungano wa Nchi za Tanganyika na Zanzibar
Mwaka 1964 na kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nchi ya Zanzibar
pamoja na Nchi ya Tanganyika zilipoteza Viti vyake katika Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa ambapo kilitengwa kiti kipya kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, kiti ambacho kimeendelea kuwepo mpaka leo kikiiwakilisha Tanzania
huko Umoja wa Mataifa.
Tarehe 19 Mwezi Novemba Mwaka 1964 Bwana John Samuel
Cigwensisi Malecela aliteuliwa Kuwa Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja
wa Tanzania. Mabalozi wengine waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika Umoja wa
Mataifa ni Balozi Akil B.C. Daniel, Balozi Salim Ahmed Salim, Balozi Paul M.
Rupia, Balozi Mohamed Ali Foum, Balozi Dr.Wilbert K. Chagula, Balozi Anthony B.
Nyaki, Balozi Daudi N. Mwakawago, Balozi Dr.Augustine P. Mahiga, Balozi Ombeni
Y. Sefue na huyu Mpya Balozi Tuvako Manongi.
CHANGAMOTO ZA MUUNGANO.
Miongoni mwa mambo ambaye yamekuwa yakiibuliwa kama moja ya
malalamiko ya baadhi ya Wazanibari juu ya kero za Muungano ni ukweli kuwa
Ushirikiano wa Kimataifa halikuwa katika moja ya Mambo yaliyokubalianwa katika
Mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar (Kimsingi Mambo ya Nje ndio
moja ya yaliyokubalianwa katika Mkataba wa Muungano).
Hivyo basi kuingizwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa katika
Mambo ya Muungano kinyume na Makubaliano ya Muungano huonekana kama ni batili
na sehemu ya kuiminya Zanzibar katika Muundo wa Muungano (ukitolewa Mfano kuwa
katika Mabalozi wote waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Mataifa
tokea Muungano Wawili tu ndo Wazanzibari na waliobaki wote ni Watanganyika).
Kwa kiasi flani hali hii (ya kuingizwa kinyemela kwa
Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Mambo ya Muungano na kutokuwepo kwa uwiano wa
kuridhisha wa Uteuzi wa Mabalozi wa Kudumu katika Chombo hiki kikuu cha
Ushirikiano wa Kimataifa Duniani) inatumika kama moja ya sababu kuu za Msingi
za wanaodai Zanzibar huru na kuvunja Muungano, lakini pia imekuwa Moja ya madai
makuu ya wanaotaka kuendelea kwa Mashirikiano na Muungano wenye Utu na Heshima
kati ya Tanganyika na Zanzibar kwa Kuboresha Muundo na kuondoa zile ambazo
zinaonekana kuwa ni kero za Muungano.
Jambo hili ni zito na lina Mantiki makubwa katika
mustakabali wetu kama Nchi, Kwa nafasi yetu kila mmoja ana wajibu wa
kulitafakari hili na kuja na majibu ya msingi kulingana na uelewa wake, mifano
kuntu na uzoefu juu ya hali hii kutoka katika Mataifa mbalimbali yenye
Mashirikiano kama yetu.
Naamini Tutafanikiwa, Mungu Ibariki Tanzania.
Picha ni kwa Hisani kubwa ya Bwana Shafiq Sanya na Maelezo
ni Kwa Hisani Kubwa ya Seif Abalhassan wa Watanzania Mashuhuri.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako