Na Markus Mpangala, Nyasa
Mchungaji Harold Camping wa Family Radio alisema kuwa mwisho
wa dunia ungelikuwa ni Mei 21/2011. Akaongeza kwa kusema siku hiyo Watakatifu watakwenda
mbinguni na hapo ndipo mwisho wa dunia utatokea. Katika mahubiri wa Mchungaji Harold Camping moja kwa moja
yanashabihiana na yale ya Mchungaji Benny Hinn, naye mwenyeji wa Marekani.
Mchungaji Benn Hinn naye akafuata mkondo wa Harold Camping
kwa kubashiri mambo mbalimbali, kwamba yatatokea, lakini hakuna lililojiri hata
moja. Ubashiri wa Mchungaji Harold Camping ameweka kwenye kitabu
chake cha Time has an end. Na
amehubiri kuwa Mei 21, 2011 ndiyo mwisho wa dunia.
Lakini naomba niwaambie neno hili; “Watu huniheshimu kwa
midomo yao, ila mioyo yao iko mbali nami. Nao huniabudu bure wakifurahisha
mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu” (Mathayo 15;8).
Tunaishi nyakati hizi lakini hatujui tushike kitu gani kumuabudu
Mwenyezi Mungu. Tumekuwa watu wa kutangatanga kwa kila aina ya mahubiri. Lakini haigombi kuyasikiliza ila mwana mwema husikiliza na
kufanya tafakuri juu ya yale maagizo ya Baba wa Mbinguni. Pia niharakishe kusema sikupendelea kujikita katika dini
hivi kwani wasomaji wetu wengine ni waumini wa dini zingine. Kwakuwa tunavunja
mlango ili tujenge nyumba basi leo waniwie radhi nitasema machache.
Je, Biblia anayosoma Mchungaji Harold Camping ni ile ambayo
sote tuisomayo? Hilo la kwanza, na kama jawabu ni ndiyo ni kwanini anataka
kupingana na Biblia anayohubiri na kuwafundisha watu wake?
Je, tujiulize alifanya hivyo kwa Nasibu kwamba Mei 21, 2011
kuwa mwisho wa dunia? Ni muujiza ama neema gani aliyoshushiwa hata akasema kuwa
siku hiyo ndiyo ile ambayo Mwana wa Adamu alisema kuwa ni Baba wa Mbinguni
pekee aijuaye siku hiyo?
Iliandikwa hivi; “Walakini habari ya siku ile hakuna
aijuaye, hata Malaika walio Mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake” (Mathayo
24:36). Kwa vyovyote itakavyokuwa na kwa namna yoyote yanavyokujia
mahubiri ya namna hii, kitu cha kwanza yanakupa hofu. Kwahiyo matokeo yake ni
kuchanganyikiwa kwamba unabii unakuja tarehe hiyo ya Harold Camping?
Lakini tutumia Biblia hiyo kuangalia unabii unaohubiriwa,
kama ambavyo tulivyoona Injili ya Mathayo kwamba ‘WALAKINI’ hakuna aijuaye siku
ile, bali Baba peke yake. Hivyo angalia neno la Mungu linasema; “Wakati ule watu
wawili watakuwako kondeni, mmoja atwaliwa, mmoja aachwa, wanawake wawili
watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa”, (Mathayo 24; 40-41).
Kuna mambo mengi ynasemwa kuwa ni mwisho wa dunia, lakini
mara zote hakuna ukweli wowote kwani hakuna ajuaye siku ile. Mwaka 1999 lilitokea shirika fulani la Bima huko Marekani,
ambalo likuwa linachukua mali za watu waliosadiki kuwa mwisho wa dunia ni mwaka
2000.
Sijui ni kitu gani kilichowafanya waamini hivyo lakini
ukweli haikutokea, ni Mungu pekee ajuaye. Wakaishia kuendelea kuishi kwa
kubashiriwa, hata hivyo ilisemwa na mwana wa Adamu kuwa angalieni mtu
asiwadanganye. Kwasababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni
Kristo; nao watadanganya wengi.
Kwa mambo yanavyotokea na kwa jinsi tunavyojipa hangaiko
ndivyo tunavyozidi kuona akina Harold Camping ndiyo tumaini letu. Waandishi wa
Biblia hawakuwa magwiji wa Theolojia, hawakuwa Maprofesa wala madaktari walau
wasanifu wa habari bali walielewa mafunzo ya Kristo wakayaandika na
kuyafundisha kwa uhuru ili watu wajue na kurudisha waliopotea.
Na wakasisitiza kuwa
mkisikia yuko Jangwani asilani msitoke, wala mkisikia yumo ndani ya
nyumba fulani, msihangaike kutoka. Sikiliza ndugu msomaji; ilisemwa kwamba
desemba 31, 1999 utakuwa mwisho wa dunia, lakini haukutokea hivyo.
Ikasemwa Desemba 31, 2000 utakuwa mwisho wa dunia, lakini
haikutokea hivyo. Sisiti kusema haya ni mafunzo ya akina Kibwetere wa Uganda na
miungu bubu ya wahuni inayopigiwa kelele.
Mfano wa pili ni waumini wa UFO, ambao walikufa kwenye mji
wa San Diego, Marekani mnamo Mei 26, 1997 kwa madai kuwa walikuwa wakisubiri
kwenda mbinguni kwa dhehebu lao la ‘Lango la Mbinguni’.
UFO ni itikadi juu ya vitu vya anga visivyotambuliwa,
wanaamini kuliko imani yenyewe, inatisha kweli kweli! Neno hili UFO ni kirefu
cha Unidentified Flying Objects. Mwisho wa waumini hawa wa UFO wakawa ni kama akina Harold
Camping wanaohubiri mwisho wa dunia ungelikuwa ni Mei 21, 2011.
Mfano wa tatu; Mchungaji Jim Jones wa nchini Marekani katika
dhehebu lake walikufa watu 914 mwaka 1978 kutokana na imani hizo za mwisho wa
dunia kuwa ni siku fulani. Dhehebu jingine lilijiita ‘Tawi la Daudi’, ambalo ilikuwa
mjini Waco jijini Texas, yapata April 19, 1993 nchini Marekani lilikuwa katika
mashambuliano ya risasi dhidi ya jeshi la Polisi na wengi wakauawa.
Sababu kubwa ilikuwa kuamini siku ya mwisho ni hii hapa, au
ile kule na zaidi ipo pale. Hivyo hata kutii sheria za nchi tabu! Mahubiri ya
Harold Camping siyo mageni, kwani Yuda alikwisha kuwavuta watu siku ile
wakamsadiki kisha akawahadaa.
“Hata kabla ya hapo alipoondoka Theudia, akajidai kuwa yeye
ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote
waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu” (Matendo 5; 36-37).
Hivyo ukitazama wafuasi wa wachungaji hao waliangamizwa
kabisa hawakusalia hata chembe. Na imeandikwa “Msimwamini rafiki, msimwekee
kiongozi tumaini” (Mika 7:5). Ni upendo wa mwenyezi Mungu.
Lakini wafuasi wanaoamini kwamba siku hiyo ni ile aliyoitaja
mhubiri Harold Camping, angalieni kwamba watambaratika hakuna akayesalia. Wengi hawajui kwamba wanadanganywa, wameweka kila kitu
mikononi mwa Harold Camping wala hawajisumbui kujua ukweli. Na hao wengi
‘watakuwa siyo kitu.’
Ni dhahiri kwamba siku ya mwisho itawadia katika ulimwengu
huu na hakuna atakayesalia. Bibilia inasema hivi; ‘Halitasalia jiwe juu ya jiwe
ambalo halitabomoshwa’. Na hakuna kiumbe hai atakayesalia kati yetu tuliomo.
Imeandikwa “Basi alikaribia mahali niliposimama; nami niliogopa
alipokaribia nikaanguka kifudifudi; lakini aliniambia fahamu, Ee mwanadamu, kwa
maana maono haya ni ya wakati wa mwisho” (Daniel 8:17).
Wakati watu wakiwa katika mshangao huo wa siku ile (nasema
ile maana haikutajwa siku rasmi katika Biblia) viumbe wote wataondolewa katika
ulimwengu huu na kupotezwa kabisa. “Basi yoyote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini
kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi” (Mathayo
24:3).
Vilevile imesemwa “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za
mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda
wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana,
wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,”(2 Timotheo 3:1-2).
“Lakini siku ya bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo
mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na
kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa kuwa
vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani
katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na
kuhimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili
vitateketea na kuyeyuka? (2 Petro 3:10-12).
Na imeandikwa kwamba; “Mkijua kwanza neno hili ya kwamba
katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao
tamaa zao wenyewe, na kusema iko
wapi ahadi ya kuja kwake? Kwa maana tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote
vinakaa hali hiyo tangu mwanzo wa kuumbwa” (2 Petro 3:3-4).
Sasa kwakuwa mahubiri ya Harold Camping yalida kuwa siku ya
mwisho kuwa ni Mei 21, 2011 basi tutafakari mwenendo hu unaashiria nini. Kwa imani ya mwenyezi mungu na kwa mwongozo wa Biblia
tumwachie Mungu aamue. Imeandikwa “Mbingu na nchi zitapita Kamwe; lakini maneno
yangu hayatapita kamwe,” (Mathayo 24:35).
“Mungu si mtu, aseme uwongo; wala si mwanadamu, ajute; iwapo
amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? (Hesabu 23:19).
Je, ni Yesu yupi na Mungu yupi aliyetaja siku hiyo hata
Harold Camping akatubashiria kuwa ilikuwa ni Mei 21, 2011 na kwanini
haijatokea? Na hata kama tutajiuliza siku hiyo ni lini, hakuna anayejua. Tumeonywa kwamba dai la kujua siku ile lipo tangu zamani za
wanafunzi wa Yesu, lakini hawakupata kuijua, na hakuna aliyeijua baadaye hata
ufufuko wa Yesu.
“Si juu yenu kupata ujuzi wa nyakati au majira ambayo Baba
ameweka katika mamlaka yake mwenyewe” (Matendo 1:7). “Nani ni mshauri wa Bwana? “Jinsi zilivyo kuu utajiri na
hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake
hazitafutikani,” (Warumi 11:33-34).
“shauri la Bwana lasimama milele, makusudi ya moyo wake
vizazi na vizazi” (Zaburi 33:11). Imesemwa kwamba mawazo ya bwana siyo mawazo yetu, na kamwe
siyo mawazo ya Harold Camping yatafikisha ulimwengu mwisho. Soma Isaya 55:8-11.
Na tumefundishwa katika; 2 Timotheo 3:1-5). Watu wamepoteza maisha yao, kwakuwa
wanasadiki kuwa siku hiyo ni ile aliyotaja Mchungaji Harold Camping.
Amri ya Bwana haina mshauri, yeye hutenda awezavyo na
apendavyo ndiyo maana hakuna binadamu aliyetajiwa siku ile. Na ‘WALAKINI’ hakuna aijuaye wala Malaika wa Mbinguni, wala
Mwana wa Adamu, bali ni Baba peke yake.
hakuna anayeweza kutabiri mwisho wa dunia zaidi ya baba Mwenyezi Mungu....
ReplyDelete