Markus Mpangala |
Na Markus Mpangala
Usinitazame kwa huzuni.
Nitazame kwa furaha kwakuwa sijui namna ya kufirikia matatizo. Sijui namna ya
kuwaza kwamba vikwazo vitaniandama. Bali nawaza namna bora na
namna ninavyoweza kuishi kwa njia bora. Huwa siwezi kufikiria vikwazo kwakuwa
najua vitanirejesha nyuma ili nitaabike. Ninasonga mbele. Usikae ukajuta. Fikiria
njia zako. Tafakari kile unachokifanya ili kufanye jambo moja tu la kuamua
maisha yako.
Amua leo usisubirie kesho.
Amua kitu kimoja tu ili uweke misingi maishani au kutoweka misingi. Amua moja kama unadhani
kkimbia matatizo ni suluhisho. Amua tu kama unadhani mapenzi bora anapatikana
nyumba ndogo kuliko kwa njiwa wako ulimwahidi kuimba naye nyimbo zenye marashi
ya huba milele.
Iko wapi ile ahadi ulimwahidi mwenzio kuwa mtaimba nyote nyimbo tamu
za mapenzi yaliyojaa huba. Iko wapi ahadi ulimwahidi
binti wa wenzio kwamba utamvika pete ya ndoa. Kwani umgeuze mtoto wa wenzio
kuwa kitoweo kisha ukishiba unatanga na njia?
Kwanini iwe hivi kwake na
si wewe kutendewa. Ni vizuri kufanya uamuzi mapema kuliko kumwingiza kwenye
matatizo huku ukijua unaweza kuyakwepa. Amua sasa maana siku
utakayoamua utakuwa umechelewa, basi nakuhimiza sasa.
Endapo njia zako hazina
misingi basi unakaribisha tatizo kubwa. Endapo huna falsafa basi nakaribisha kasoro maishani mwako. Acha kuwarubuni watoto wa wenzio, acha
kuwafanya wao ni kitoweo chako pale udhaniapo unahitaji kula daima. Nakutaka uamue leo na si
kesho ambayo hujui itakuwa na sura gani siku hiyo.
Amua sasa kama unaona hakuna haja ya kusoma au kufanya kazi. Maana wapo watu wanadhani wanaakili kuliko akili zao zilivyo.
Amua sasa kama unaona hakuna haja ya kusoma au kufanya kazi. Maana wapo watu wanadhani wanaakili kuliko akili zao zilivyo.
Amua sasa kwamba hutawasumbua watoto wa wenzio.
Amua sasa kwamba unahitaji
kufanya kazi kwa bidii.
Amua sasa kwamba ofisi yako inahitaji uwajibikaji wa
pamoja.
Taswira ya Mungu |
Kuna mambo maishani ni
lazima yafanyiwe uamuzi.
Ni muhimu kuyaangalia kila leo maana ya kesho huwezi
kuyaona kwakuwa mshale wa saa unakuwa na mambo mengine zaidi ya hayo. Najua wapo wengine wenye
matatizo ya kiafya,mali na mengineyo. Lakini hakuna jambo zuri kwenye maisha
kama kufanya uamuzi juu ya hali uliyonayo.
Endapo wewe huna kazi, amua
kuwa unahitaji kazi inayoweza kukufanya ukafanya mambo mazuri zaidi. Au unaweza kuamua kwa kuwa
mchuuzi maana kushindwa yule si kushindwa kwa wewe.
Jukumu lako ni kuamua namna
ya kuishi kwenye hii sayari yetu ya dunia. Ni muhimu kuyafanya maisha yako kuwa
bora kwakuwa hakuna kizuizi chochote.
Hakuna awezaye kukuzuia
ikiwa unafuata taratibu halali za maisha yako. Ni mwenyezi Mungu pekee anaweza
kukuzuia lakini mafanikio yako yapo mikononi mwako. Juhudi zako ndizo
zitakufanya uwe bora kila siku.
Amua moja kusuka ama kunyoa, kufunga pingu za
maisha au kukaa kuoa. Kuishi vizuri au kuishi kipuuzi. Ni wewe unaweza kuamua
namna ya kuishi kwenye hii dunia. Amua moja tu ndugu yangu. Amua ukijua kuwa
uamuzi wako unastahili kuheshimiwa na watu wote.
Usifanye jambo ambalo
linaumiza nafsi yako. Amini uamuzi wako unastahili kukufanya uishi vizuri zaidi
ya leo. Ni wakati wako wa kufanya
uamuzi ili uweze kujua unakokwenda na namna gani unaweza kuishi kwa amani. Amua
sasa.
Misingi ambayo itakufanya uwe na nyumba bora,
familia bora na yenye amani ila siku. Familia yenye heshima na
wingi wa upendo. Lakini muhimu ni kuamua namna ya kuwa familia hiyo. Huwezi kupanga kuwa na familia yenye upendo
ikiwa hujawa sehemu ya upendo huo.
Huwezi kuota kuwa na mke mwema/mume ikiwa
matendo yako hayaambatani na wema/upendo. Unatakiwa kujiuliza sana
kila unavyoishi. Jaribu kujenga picha ambayo mbele yako unajiona na kujisemea
kuwa unajipenda.
Basi vivyo hivyo unatakiwa kuwapenda wengine ama famili yako. Yote haya yanakujia ikiwa
tu umeamua kupenda na kutazama njia zenye mustakabali mwema maishani. Hebu jiulize kwanini wewe huwi mfano wa kuigwa
bali unabaki kusema kwamba unataka kumuiga fulani? Kwanini usiamue kuwa wewe
unayeigwa badala ya kuwatazama wengine?
Amua sasa kuwa maisha yako yatakuwa
mfano wa kuigwa zaidi kadiri unavyokwenda maana ni wewe tu uwezaye kusuka
taswira ya maisha yako. Uwe mfano zaidi kila siku ili utambue thamani ya kuigwa. Sasa ili kuweza kuamua
maisha yako basi ni lazima utambue kuna kanuni zinazoongoza maisha ya wale
unaowaiga kwa maisha yao mazuri na mema.
Ni misingi 6 tu ya kuamua namna ya
kuishi kutenda mema ama mabaya. Bila shaka utanielewa vema. Na uichunge misingi
6 hii iwe dira yako maishani mwako ili ufanikiwe.
1.Usimchukie yeyote hata
kama atakukosea vipi.
2.Ishi maisha ya kawaiada
hata kama upo juu kwa kiasi kikubwa.
3. Tarajia heri hata kama
mitihani inakusakama.
4. Toa kwa wingi hata kama
wewe umenyimwa.
5. Onesha tabasamu hata
kama moyo unavuja damu
6. Usiache kumuabudu mungu.
Nakutakia
siku njema na afya nje. Usisahau kuwa yaliyotokea jana yanakufahamisha kwamba
aidha ujirekebishe au unapaswa kusonga mbele kutokana na hali ilivyo sasa.
Ichunge misingi hiyo muhimu maishani. AMUA SASA.
KUAMUA, KUWA NA MSIMAMO NDIO MSINGI WA MAISHA ..NIMEPENDA SOMO LA LEO....
ReplyDeleteAsante kwa somo lako linatufundisha mambo mengi linatutia moyo tuwaze mafanikio mbele katika maisha na pia Kamwe tusikumbuke matatizo yaliyopita sababu yanaumiza na tusiwaze yajayo sababu yanatia hofu,ila maisha ni hapo ulipo maamuzi ni kielelezo cha maisha bora yajayo. unatazama mbele kwa kujiamini nyuma kwa taadhari na ulipo kwa matumaini hapo tutajenga maisha bora na si bora maisha...
ReplyDelete