February 04, 2013

TOFAUTI ZETU ZA DINI, ZISITUFIKISHE KWENYE UHASAMA


Na Markus Mpangala, Dar es salaam

Niwe mkweli, nasikitishwa sana na baadhi ya watanzania wenzetu wanavyochukulia mambo kwa njia HASI. Huwa sichelewi kabisa kupambana nao ili kuokoa hali mbaya inayoweza kujitokeza. Kuna wakati baadhi ya wananchi katika mkoa fulani(sitataja) waliwahi kutoa maoni yao kwa tume ya Kukusanyasa Maoni ya Katiba kwamba katiba iangalie pia suala la Machinjio kwanini kuna Waislamu pekee. 
Hawa ni rafiki zangu nilipokuwa UDSM. Hapa wapo waumini wa dini tofauti, lakini wameishi kwa upendo na amani bila kuulizana masuala ya DINI zao kuwa tofauti. Wanaishi kwa raha
Sijui mwananchi yule alipata wapi utafiti na kuhimisha kiasi kile, lakini ni wazi kuwa tupo katika kipindi kibaya au mwanzo wa kipindi kibaya kabisa. Natambua kuwa nyakati mbaya huwa haziishi ila watu wabaya huisha, lakini hakuna ubaya zaidi kama kufikiria mabaya na kuilisha jamii ubaya. Ni wazi kuwa kila mwananchi anao mtazamo wake kuhusu DINI, lakini mitizamo hii isitufanye tugawane mbao za nchi yetu eti wewe MKRISTO au wewe MWISLAMU. 
Nchi hii sio ya Waislamu na Wakristo pekee, bali kuna wapagani, wahindu na wabuddha pia. Kuna watu wa dini mbalimbali, hivyo haipendezi kuonyesha kwamba waislamu na wakristo ndio wapiga filimbi ya kujidhania wao ndio Tanzania. Januari 14, 2013 nilitumiwa ujumbe kuwa niwe sehemu ya watu wanaopinga kuanzishwa Mahakama ya Kadhi. Nakiri niliudhika kwa ujumbe huo na mara moja nikauripoti sehemu zinazohusika. 

Mpaka sasa natambua ujumbe ule ulishaandikiwa ripoti na uchunguzi unaendelea hadi sasa. Sina shaka kuwa hatua iliyofikiwa ni nzuri na siku sio nyingi tutabainishwa kuwa wahusika ni akina nani wanaosambaza ujumbe huo ili kuwahamasisha wakristo etu wapinge Mahakama ya Kadhi ambayo kimsingi utaratibu wake uko wazi kabisa. 

Lakini leo hii Ferbruari 04, 2013 niliambiwa kuwa niwe sehemu ya wanaponga suala la MACHINJIO kwa kuandika na kuchambua zaidi. Mtu aliyeniambia hilo natambua anafahamu kuwa anasoma magazeti na ananisoma mada zangu nyingi ninazoandika. Yeye anataka niandike mada juu ya Machinjio na anadai kuwa kuna KITU KIMEJIFICHA.

 Hakika hili ni jambo la ajabu na nimeshangaa sana. Inakuwaje mtanzania amefika mahali kuona watanzania wenzake wa dini nyingine kuwa kero. Pai ni kitu gani kinachomshukuma mtu huyu kusema kuwa kuna jambo limejificha katika madai ya uchinjwaji wa nyama unapofanywa na waislamu huku walaji wengine wakiwa Wakristo, au Waislamu wanavyokataa kula nyama iliyochinjwa na mkristo ama mwenye imani tofauti na wao.

 Wengi wanatumia kigezo hiki kwamba mnyama anapochinjwa na mwislamu ni halali na pale anapochinjwa na asiyekuwa mwislamu ni haramu. Kimsingi haya ni mawazo yenye uozo mkubwa. Ni aibu, ni mafunzo ya kishetani kudai kuwa mnyama anapochinjwa na mwislamu ni nongwa hivyo nasi wakristo tuanze kupinga kwa kuingiza hoja hizi. 

Ndugu zangu, dini zililetwa kwaajili ya amani na upendo sio kugombana na uhasama. Ni umasikini na upumbavu mkubwa kudai kuwa eti mnyama aliyechinjwa na mwislahu anatakiwa kupingwa na mkristo sababu tu waislamu wanaona haramu. 

Kama waislamu wanaona haramu ni wao, na hakuna sababu ya kuchukulia kama nyenzo ya uhasama.  Ndugu zangu, sijui nini kinamfikisha mtu kufikiria hilo. ...NAWAULIZA MASWALI HAYA ..........Unataka Nyama au Mchinja Nyama? .... Ndio, nasikia mmeanza kuhoji kwanini wanaochinja Wanyama kwenye machinjio ni Waislamu na kwanini wenye Mabucha ya Nyama ni Waislamu......... naendelea kuwasikiliza ..... Hivi Ng'ombe ana DINI?

 Mbuzi ana DINI? Unakula DINI au Nyama? Kisu kina DINI? Supu ina DINI? Kuku ana DINI? ... Kama wewe huli mnyama aliyechinjwa na Mkristo unadhani itabadilika na kutokuwa Nyama? Kwanini mnyama aliyechinjwa na Mwislamu itabadilika kutokuwa Nyama? ... SIRI iko wapi hapo? Umelazimishwa kula? Kitu kimoja rahisi ni kujiuliza tatizo hapo ni nyama ama mchinjaji? Na kama unaona mchinjaji ni tatizo kwanini usianzishe bucha lako ambalo litakuondolea kwenye ukakasi eti waislamu ndio wachinjaji? 

Kwanini usinunue ng'ombe wako au mnyama wako ukamchinja mwenyewe kwa raha zako ili kuepusha uhasama huu? Ndugu zangu hakuna kitu kibaya kama hatua tuliyofikia. Inapofika watu wanaanza kuhoji mambo yenye uozo kama haya ni wazi kushiba kwao ni tumboni tu sio akilini. Ubongo wa wanafikiria haya haujashiba hata kidogo ndio maana wanaona hilo la mchinja wanyama ni kero kama zilivyo kero za kukosa pesa, kukosa chakula, kukosa mahitaji muhimu au la. Hakuna mwanadamu atakayekufa kwa kutokula nyama. Hakuna mtanzania ambaye atapoteza uhai kwa kukosa nyama. 

Matatizo haya tutafika mahali hata wakristo wenyewe wataanza kusema, hawali nyama yoyote iliyochinjwa na mpetekoste, mkatoliki, mlokole, mlutheri na wengineo, vivyo hivyo tutafika mahali tunanyoosheana vidole mbona hawa wanacheka na wale wamenuna. Upuuzi huu hakika unapaswa kukemewa, na wala haifai kabisa kuwa endapo mtu amenunua nyama kisha akagundua mchinjaji ni mwislamu, basi aitupilie mbali. Huu ni uozo wa akili zetu, na ukosefu wa kushiba kifikra. Tatizo hili lisipokemewa mwishowe tutakuwa tunaishi kwa kumwaga damu kila siku.  

No comments:

Post a Comment

Maoni yako