Na John Chitanya, Nyasa
Wilaya ya Nyasa ni miongoni mwa wilaya mpya zilizoanzishwa
mwaka huu kwa mujibu wa sheria za TAMISEMI chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Juhudi za kuanzishwa kwa wilaya mpya, sote tunajua linalenga kusogeza huduma
kwa wananchi ili kukabiliana na matatizo mbalimbali na kuweza kujiletea
maendeleo.. Wakala wa Nishati Vijijini kwa mujibu wa sheria Na.8 ya
Bunge ya mwaka 2005 inaeleza kuhamisha, kusimamia na kuruzuku miradi ya Nishati
vijijini ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa nishati bora vijijini kwa ajili ya
shughuli za uzalishaji, mali na
kijamii.
Wakala wa Umeme vijijini umeandaa mpango wa kusambaza umeme
uitwao Underline Transformers na unatarajiwa kuunganisha vijiji zaidi ya 726
katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Kwahiyo jukumu la wakala wa umeme katika
maeneo ya vijiji kwa maana ya kujenga ‘Backbone Transmission Line’ inatakiwa
wananchi kulipigia gharama za kuunganishwa kwenye ofisi za TANESCO zilizopo
karibu na eneo la kijiji chao.
Wanafunzi wakienda shuleni katika shule ya Kata wilayani Nyasa.
Picha kwa hisani ya jaizmelaleo blog.
Miongoni mwa vijiji vitakavyopitishwa nyaya za umeme ni
vijiji vya wilaya Nyasa. Kutokana na hali hiyo, nikiangalia hali ya uchumi ya
watu wa vijiji vya Nyasa hakika najikuta nabaki na swali, ni namna gani
wataweza kumudu gharama za kuunganishiwa umeme katikati yamiundombinu mibovu iliyopo
wilaya hiyo?
Kwa sasa harakati za kutengeneza miundombinu inafanyika.
Ujenzi wa Barabara kutoka Mbamba Bay hadi Liuli, kisha kutoka Liuli hadi
Lituhi, ikiwa na lengo la kurahisisha usafiri kwa wakazi wake. Mpango wa
serikali ni mzuri, lakini ni vema tukaangalia namna ya kuhakikisha gharama za
kuunganishiwa umeme zinatozwa kulingana na eneo husika.
Kusema hivi sina maana kwamba wakazi wa wilaya ya Nyasa
wapate upendeleo, la hasha ila kwa hali ya uchumi wa wilaya hiyo naelewa ugumu
wao kuweza kulipigia gharama za kuunganishiwa umeme. Wilaya Nyasa ni changa, na
wakazi wake wanategemea shughuli za kilimo na uvuvi.
Kilimo cha mpunga, kahawa, mahindi, mtama, uwele, ulezi,
zinaweza kuwakwamua ikiwa watajengewa miundombinu mizuri. Lakini suala la
nishati ya umeme licha ya kuwa muhimu katika maisha yao, bado naona taswira
ngumu kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Miji muhimu kama Lituhi, Lundu, Kihagara/Njambe, Liuli,
Mkali, Lundo, Mbamba Bay,na Kilosa inaweza kujipatia huduma za umeme kwa baadhi
ya wananchi. 855 ya wakazi wa wilaya Nyasa hawatakuwa na uwezo wa kulipigia
gharama za kuunganishiwa umeme.
Hiki ndicho kitendawili ninachoona hapa. Wakala wa umeme kwa
kushirikiana na TANESCO wanatakiwa kufanya tathmini juu ya mazingira ya wakazi
wa vijijini kuunganishiwa umeme.
Ni rahisi kuunganisha umeme katika mji wa Mbinga ambapo
shughuli za kiuchumi ni kubwa na zimekuwa zikifanyika kwa muda mrefu. Lakini
kwa wakazi wa wilaya mpya kama Nyasa, hakika ni mtihani mkubwa kwa wakazi wake.
Nadhani tunao wajibu sio wa kuwaelimisha juu ya matumizi ya
nishati ya umeme, bali umuhimu wa kuwawekea mazingira mazuri ya kufanikisha
upatikanaji nwa umeme. Ni vyema kabisa wahusika wakaelewa hili kuwa suala la
wakazi wa wilaya ya Nyasa kulipia kuunganishiwa umeme ni kitendawili.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako