Na: Albert Sanga,
Iringa.
|
Nianze kwa kuwasalimu
wasomaji wa safu hii ya Anga za Uchumi na Biashara, ambayo haikuwa hewani kwa
takribani wiki saba. Sababu kubwa iliyonifanya nikatoweka safuni ni msiba
niliokuwa nao baada ya kufiwa na binti yangu wa kwanza na wa pekee, Faith,
aliyekuwa na umri wa takribani mwaka mmoja.
Katika juhudi na
mahangaiko ya kuokoa uhai wake, binti yetu alifariki katika hospitali ya
Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi wilayani Kilosa. Msiba huu uliniachia uchungu
na majonzi makubwa mno kiasi ambacho akili, moyo na morali vilitoweka kabisa na
isingekuwa rahisi kumudu tafakari pana zinazoijaza safu hii.
Nimekuwa na uzoefu
(kiasi Fulani) wa kumudu majanga, mitikisiko na mikasa ya kibiashara; lakini
lilipokuja suala la kupoteza mtu muhimu kama mwanangu, hakika nilijikuta ni
mgeni kabisa wa kuhimili mtikisiko wa msiba huu.
Matakwa yetu na maombi
yetu yalikuwa ni kupona kwa binti yetu, lakini Mungu aliamua kuutwaa uhai wake.
Tunamshukuru na kumtukuza Mungu kwa yote tuliyopitia nasi tunajua Mungu anabaki
kuwa Mungu hata kama hakujibu tulivyotaka.
Kipekee kabisa
ninatumia fursa hii kuwashukuru makumi ya wasomaji wa safu hii kutoka maeneo
mbalimbali nchini ambao, baada ya kuona sionekani walinitafuta na kutaka kujua
kulikoni? Mbarikiwe sana mliotutumia rambi rambi za fedha na salamu za faraja.
Ijapokuwa sikuaga
wakati napotea safauni lakini sisiti kupiga mbiu inayoashiria kuwa nimerejea.
Yapo mambo mengi ambayo tutaendelea kushirikishana yahusianayo na ustawi wetu
kiuchumi, kiujasiriamali na kibiashara. Kwa kuwa leo ndio kwanza ninarejea,
nitachambua kiunaga ubaga namna utamaduni wa watu kupenda fedha kuliko thamani
ya walivyonavyo; jinsi unavyourubuni uchumi wetu.
Ni vema tukajikumbusha
historia ya namna fedha zilivyoanza kutumika katika maisha ya wanadamu. Hapo
zamani kulikuwa kukifanyika biashara ya ubadilishanaji wa vitu kwa vitu (barter
trade). Ilikuwa kwamba mtu awapo na ng’ombe basi atabadilishana na mwenye
chumvi, vivyo hivyo kwa mwenye mahindi anaweza kubadilishana na mwenye nguo.
Kadiri mfumo huu
ulivyoendelea ikaonekana suala la kubeba vitu na kuzunguka navyo ili kutafuta
wa kubadilishana nae ni usumbufu na lina ugumu mkubwa wa kuoanisha hayo
mahitaji. Wakati mwingine mwenye ng’ombe anapohitaji chumvi halafu mwenye
chumvi akawa hayupo tayari kupokea ng’ombe; basi hakuna biashara itakayofanyika
na hivyo mwenye ng’ombe anakwama kupata chumvi.
Katikati ya mfumo huu
kukaja kuibuka matumizi ya vito vya thamani (mfano dhahabu, pembe za thamani,
chuma na madini mengine); kama viambata vya kubadilishia bidhaa (media for
exchange). Hapa ilikuwa kwamba, mkulima anapovuna mahindi yake, pengine gunia
kumi, anayachukua mahindi hayo na kuyapeleka kwa hao wanaotengeneza vito vya
thamani, kasha anapewa idadi ya vito vya thamani vinavyolingana na thamani ya
mahindi yake. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa hiki tunachokiita fedha.
Hata hivyo baada ya
muda kupita ikaonekana kuna upungufu katika uthamanishaji wa vito vya thamani
na bidhaa wanazozalisha watu. Ndipo kukatokea watu ambao walikuwa kama wahakiki
wa thamani ya vitu, mali ama bidhaa alizonazo mtu.
Hapa ilikuwa hivi;
mkulima anapolima na kupata mahindi yake, pengine tuseme gunia kumi, alikuwa
anayapeleka mahindi hayo eneo maalumu ambapo wanamtunzia. Wale wenye ile stoo
(eneo alipotunzia), walikuwa wanaandika karatasi (kibali) linaloonesha kuwa
mkulima A anamiliki magunia kumi ya mahindi yaliyopo stoo B.
Kwa hiyo mkulima
alikuwa hana tena sababu ya kutembea na magunia ya mahindi kumtafuta mwenye
chumvi; badala yake alitembea na lile karatasi kiasi kwamba anapofika kwa
mwenye chumvi anampa lile karatasi na kupewa chumvi.
Yule aliyempa mkulima
chumvi ataenda kule kwenye stoo (iliyotunza mahindi) na kuchukua mahindi
yanayolingana na thamani ya chumvi aliyompa mkulima; kasha lile karatasi
analiacha pale stoo. Hizi stoo zilikuwa ndio chimbuko la benki tunazoziona hadi
sasa nay ale makaratasi yaliyokuwa yanaandikwa na wenye stoo ndio chimbuko la
hizi noti tulizonazo hadi leo.
Hii ina maana mfumo wa
mabenki na fedha ulitokea ili kuwe na haki, usawa na ukweli. Mkulima mwenye
magunia kumi ya mahindi ni lazima apewe karatasi (fedha) inayoonesha kweli
anamiliki hayo magunia kumi na si vinginevyo. Kama huyu mkulima akipewa
karatasi inayoonesha anamiliki magunia kumi ya mahindi wakati hajapeleka
chochote kule stoo ingekuwa ni kumrubuni, kumdhulumu na kumlaghai Yule mwenye
chumvi.
Hii ni kwa sababu
mwenye chumvi atakapoletewa lile karatasi na mkulima (aliyedanganya) ataitoa
chumvi yake; lakini atakapoenda kule stoo ataambiwa hapa hakuna magunia ya hayo
mahindi yanayoonekana kwenye karatasi uliyotuletea!
Baadae sana jukumu hili
la kuandika (kuchapisha) haya makaratasi (fedha) yanayoonesha fulani kazalisha
nini kilichopo wapi, likachukuliwa na mamlaka za kiserikali zilizokuwa
zinasimamia jamii mbalimbali. Hivyo ikawa mkulima akizalisha mahindi yake
anapewa karatasi lake (fedha), vivyo hivyo kwa mfugaji anapofuga na kuongeza
mifugo na mjenzi anapojenga jengo. Kila mtu katika jamii alikuwa anashika fedha
inayoonesha thamani halisi ya kile alichozalisha katika uchumi.
Kwa jinsi hii, tunaona
kuwa, fedha katika uhalisia wake ni matokeo ya uzalishaji anaoufanya mtu katika
uchumi. Fedha sio mafanikio, isipokuwa
ni utambulisho wa mafanikio. Utajiri wa mkulima hauwi katika yale makaratasi
aliyoyashika (fedha) isipokuwa utajiri wake unakuwa kwenye yale magunia
aliyoyazalisha. Thamani ya mwalimu haitakiwi kupimwa kwa kiwango anacholipwa
isipokuwa kwa maarifa aliyoyazalisha kwa wale anaowafundisha.
Lakini katika jamii na
nchi yetu sasa, watu wamekuwa wanathamini fedha kuliko uzalishaji. Watu wanapenda
kupata fedha hewa! Ndio maana wanataka kuonekana ni matajiri wakati hakuna
lolote walilozalisha katika mfumo wetu wa uchumi. Tunapokuwa na jamii
inayothamini fedha kuliko uzalishaji; maana yake ni kuwa tuna jamii inayopenda
kurubuni, inayopenda mikato-mikato, uwongo-uwongo na unyonyaji kwa wengine.
Kwa mizania ya uchumi
ni kuwa moja ya sababu za mfumuko wa bei ni uwepo wa ujazo mkubwa wa fedha
katika uchumi usiolingana na uzalishaji (uzalishaji mdogo). Kinachotokea ni
kuwa fedha zinakuwa nyingi na bidhaa ni chache.
Wale walioshika fedha
wanaanza kugombania zile bidhaa chache zilizopo; kinachotokea? Watu
wanapandishiana “dau”, mwenye nguvu ananunua na mnyonge anabaki kulalamika.
Matokeo? Ndio tunasikia vitu vinapanda bei kwa kasi kubwa.
Unapoona madalalai
wamejaa mtaani, ambapo kila unachotaka kununua wapo katikati, ujue kuna ulaghai
unafanyika kiuchumi. Ikiwa ninataka kununua nyumba na mwenye nyumba anaeuza
namfahamu, dalali wa nini hapo katikati? Kwa kuwa tumeshauzoea mfumo wa
udalali, ninaenunua nyumba ya milioni 25 ninalazimika kulipa milioni 30 ili
dalali apewe milioni 5 yake.
Kiuchumi ni kwamba
tunakuwa tumempa dalali milioni 5 za uwongo kwa sababu hakuna uzalishaji wowote
alioufanya; ingawa “kijamii” tutamuona anamiliki utajiri wa milioni tano!
Dalali anapoichukua ile milioni 5 na kwenda kwa mkulima kununua mahindi,
unakuwa ni ulaghai kiuchumi.
Ni ulaghai kwa sababu
hela ile (milioni 5) imechapishwa wakati hakuna uzalishaji katika uchumi. Kesho
na keshokutwa mkulima anapotaka kuitumia ile milioni 5 kununua pembejeo
anajikuta haitoshi tena (imeshuka ama kupoteza thamani) kwa sababu ni ya
uwongo!
Sina ugomvi na madalali
na wala siwachukii; isipokuwa tunatakiwa tuwatumie madalali pale tu panapokuwa
na ulazima na ikiwa kweli uwepo wao unazalisha thamani “halisi” ya gharama
wanazotaka. Madalali ni mfano mmoja tu lakini ulaghai wa kupata fedha pasipo
uzalishaji upo katika mazoea mengi mno.
Kahaba anapodai malipo
ya elfu 50, ni nani anaekuwa amethibitisha kiuchumi ya kuwa huduma yake ina
thamani hiyo? Mfanyakazi wa serikali anapotaka asilimia kumi (10%) ili kutoa
tenda kwa upendeleo, ni uzalishaji gani ameufanya kiuchumi? Mfanyakazi
anapolilia mshahara mkubwa pasipo kuongeza tija kiuzalishaji, anatutakia nini
kiuchumi kama sio balaa?
Uchumi wetu hauwezi
kusonga mbele kwa kiwango kizuri ikiwa tunaendekeza kupata fedha na utajiri
usiolingana na uzalishaji tunaoufanya katika uchumi. Hakuna fahari ya mtu
kujiridhisha na utajiri ama mafanikio ya fedha yaliyopatikana kiujanja-ujanja,
kimteremko-teremko na kiusanii-sanii.
stepwiseexpert@gmail.com
Pole sana kwa msiba.
ReplyDelete