May 25, 2013

TUMETAYARISHA AJENDA GANI KWA OBAMA?

Markus Mpangala
Ziara ya Barrack Hussein Obama inaelekea kuwagusa wengi mno. Baadhi yetu tunaguswa na idadi ya watu watakaokuwepo kwenye ziara hiyo, ambao ni 700. Wengi wanajaribu kujiuliza ni kwanini Obama akae siku 4 nchini Tanzania. Lakini kwangu mimi muhimu sio siku zake atakazokuwepo hapa wala idadi ya watu atakaoambatana nao. Jambo muhimu kwangu ni Tanzania.
Naam, rais mstaafu George Bush alikaa hapa siku kama hizo hizo. Lakini wengi walidhani matokeo ya ziara yake ni siku chache ama zaidi. Sasa Obama anakuja, haendi Kenya, bali anakuja Tanzania. Hata hivyo tuendelee kufikiri zaidi kibiashara,uchumi na ushindani wa siasa za kimataifa baada ya ujio wa Xi Jinping.
Jambo muhimu kwetu ni kuangalia namna gani tutaweza kuzungumza na Obama katika masuala ya kibiashara na ushindani wa kimataifa kuhusu siasa na uwekezaji. Hatuwezi kuketi chini na kulalamika kuwa Obama anakuja na wageni wengi ambao hawana msaada kwetu. Lazima tutambue kuwa ujio huu unaitambulisha kwa namna nyingine nchi yetu ya Tanzania katika ulimwengu.
Wengi watakuwa wakijiulzia kwanini Rais huyo amekuja Tanzania na sio sehemu nyingine. Ni kweli kwamba Obama atakuwa na ziara katika maeneo mengine ambako anatarajiwa kuzungumza na viongozi mbalimbali. Katika mfumo wa siasa za kimataifa, ujio wa Barrack Obama ni mbinu ya kujaribu kufukuzana na China ambayo ilishamleta Rais wake Xi Jinping.

Rais huyo wa China aliihutubia dunia akiwa nchini Tanzania na alitumia lugha yao ya kichina. Sio hilo tu bali pia Rais huyo aliingia mkataba na nchi yetu ambayo mojawapo ni ujenzi wa bandari ya Bagamoyo ambapo China itakuwa msimamizi kwa kipindi cha miaka 50.
Kwa namna nyingine mkataba huu unaleta kizazi zaidi ya kioma kilichopo hapa nchini. Kwamba kizazi kijacho kitaachiwa urithi unaoonekana hivyo kuona manufaa ya uhusiano wa China na Tanzania. Kwa upande wa Obama, ziara yake lazima itakuwa na masuala ya sera za uchumi na kutengeneza njia ya maslahi yake kama ambavyo George Bush alifanya.

Kwahiyo ili kufanikisha yote haya lazima tukubaliane tunahitaji kushirikiana na wengi kote duniani hata kama washirika wetu wana desturi ya kuwa walaghai au kuwa na ksumba za kuwa nduli kama Idd Amin. Ili tuweze kuitangaza zaidi nchi yetu tunahitaji fursa kama hizi kujitokeza. Lazima tukubali tutaingaza nchi yetu mwaka huu kwa namna mbili kuu ambazo ni ujio wa Xi Jinping na Barrack Obama.
Lakini ujio huu sio kitu ambacho mwananchi anaweza kudhani sadaka bali anachojua ni wazi kuna maslahi yanafukuziwa hapa ambapo watanzania wana mali nyingi katika ardhi na mengineyo. Wananchi wanataka kujua ni ajenda gani ambazo tutaweza kuzungumza na Obama, au mwingine yeyote atakayekuja.

Tunafahamu ushindani uliopo kwa upande wa Mashariki ya Kati ambako mataifa haya ya China na Marekani yanajaribu kujenga misingi yao na kulinda maslahi yao. Sisi tunaonekana kuwa washirika wazuri wa mataifa haya. Lakini ingefaa zaidi nitoa angalizo kuwa katika ushirika huu lazima tukubaliane kuchukua hatua stahiki ili kuleta manufaa kwa wananchi wetu.

Sidhani kama tunahitaji kuelezwa mengi katika misingi yoyote iwe kijeshi, kiuchumi, kisiasa na kadhalika, yatupasa kuona kile ambacho tunatakiwa kukiona. Obama anakuja kulinda maslahi na kuendeleza misingi iliyoasisiwa na Bush. Obama anakuja kuwakilisha nchi yake, asilani tukaeti chini na kudhani tabasamu lake litakuwa la huruma kwetu.

Tunafahamu kuwa Marekani imejeruhiwa sana kiuchumi na inahitaji kujipanga na kuendeleza utawala wake kiuchumi. Kuna hali ya wazi kabisa afrika kuwa kitovu cha sera za nchi za mataifa mbalimbali kwahiyo hakuna njia ya mkato ambayo inatutweza kupata manufaa kama hii ya kuzungumza nao tukiwa na ajenda zenye maana mezani.

Lazima tujitarishe na kuamini kuwa ulinzi wa maslahi yetu ni jambo lenye maana sana hivyo hakuna sababu ya kuogopa kuweka sera zetu wazi mbele ya Obama na timu yake ya watu 700. Hakuna sababu yoyote ya kuhofia ujio huu kwanini kwa namna nyingine unaikumbusha dunia kuwa kuna taifa linaitwa Tanzania.
Ziara ya wkanza ya Obama akiwa Rais aliifanya nchini Ghana, ambako alizungumzia mengi sana. Sasa kwanino Obama ameichagua Tanzania? Lazima tukiri kuwa Ghana ni miongoni mwa nchi zenye ushawishi mkubwa sana kwa afrika magharibi ukiacha Nigeria hususani masuala ya uchumi na demokrasia. Kwa upande wetu Tanzania ni nchi yenye ushawishi mkubwa katika ukanda wa kusini mwa janwga la sahara.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinasimama mstari wa mbele kulinda maslahi ikiwemo kuendeleza misingi ya waasisi wa SADC. Tanzania ni nchi yenye ushawishi mkubwa sana katika ukanda huu na moja ya mambo yatakayojadiliwa sina shaka kabisa kuhusua hali ya Zimbabwe. Hali ya Zimbabwe sote tunaifahamu, na kwa eneo la kisiasa sina shaka kabisa itakwua moja ya ajenda za Obama katika ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara.

Ni wazi Jacob Zuma hana ushawishi wowote mbele ya Robert Mugabe ndiyo maana alisuswa alipotembelea Zimbabwe. Ni Tanzania ndiyo ilifanikisha uelewano chini ya Rais Kikwete ambaye akiwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika alifanikisha timu ya Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini kumaliza mzozo wa taifa hilo. Kwa maana hiyo watanzania lazima tukae chini na kuwahimiza watawala wetu wajipangie ajenda za msingi katika maongezi yao na Obama.

Lazima tukubali pia Obama anakuja kulinda maslahi ya nchi yake. Hakuna sababu zozote za kuficha hisia zetu, bali tuwahimize na kuwaambia twahitaji kuweka sera za wazi na zenye maslahi kwa taifa letu. Nafikiri yale yaliyoandaliwa na watawala wetu kuzungumza na Obama yanapaswa kuongezwa kwa kiwango chochote kile, ambacho iwe zaidi ya uwekezaji. Muhimu ni kusubiri ajenda yetu itakayowezeshwa na watawala wetu na kuinufaisha Tanzania.

1 comment:

  1. Anonymous27 May, 2013

    I am in fact grateful to the holder of this website who has
    shared this fantastic paragraph at here.

    Here is my homepage :: best cellulite treatment

    ReplyDelete

Maoni yako