Na
Markus Mpangala, Dar es salaam
Wanafunzi
ambao walianza Darasa la kwanza mwaka 2002, walipoanza shule ada ikafutwa, na walipofika
Darasa la 4 mitihani ikafutwa na hatimaye wakaibuki kidato cha kwanza mwaka 2009. Walipofika
kidato cha pili mitihani ikafutwa mwaka 2010, pia matokeo yao ya mtihani wa kidato
cha nne mwaka 2012 yakafutwa baada ya kufeli sana.
SWALI: Ndugu
Zotto, hii ni mara ya pili tunafanya mazungumzo kuhusu sekta ya elimu. Unachukuliaje
matokeo mapya ya kidato cha nne baada ya kufutwa yale ya awali?
ZOTTO: Ningepata hata Daraja la Tatu wakati ule
nikiwa sekondari, hakika leo ningejivunia sana kuliko hizi madaraja ya kwanza ya matokeo haya.
Kipindi tunasoma Sekondari ya Ilboru,
tulitaka kugomea mtihani wa Mock ya Mkoa baada ya kusikia tetesi kuwa imevuja. Tuliposikia mtihani wa Taifa, nayo imevuja
na hivyo maswali yamekuja kwa fax, nakumbuka nilimwambia mwenzangu Frank
Mirindo afadhali tukalale kuliko kuona maswali hayo. Leo hii serikali
imewafanyia wanafunzi NECTA. Sitashangaa hata wakifanyiwa wanafunzi wa kidato
cha sita.
SWALI; Tukichambua matokeo ya
haya ya pili unadhani ni suluhisho kwa uamuzi uliochukuliwa na serikali?
ZOTTO; Hapa naona imekuwa kama suluhu ya mchezo wa mpira hapa nchini, ambapo
timu zilikuwa zinapewa ushindi wa mezani, lakini hawa wadogo zetu wameiumbua
serikali kwa kuiambia mazingira ya elimu ni mabovu. Hata hivyo, si unajua
serikali yenu ni sikivu? Haya liwalo na liwe!
SWALI; Inaelekea hujaridhishwa na matokeo mapya. Huoni kuwa kuna sababu za msingi kufutwa
matokeo?
ZOTTO; Sioni sababu mpya hata kidogo hapo, maana
siku hizi visingizio vingi;- Walimu hawafundishi, Walimu hawana sifa, hakuna
Maabara, hakuna Maktaba, kuna twisheni, shule fulani wanafundisha vizuri, serikali
isaidie kufaulisha. Ndugu yangu ninajua fika mwisho wa hayo matokeo na
visingizio, ila wenyewe walioamua kufuata, watakuwa ndio wanaondoka madarakani,
lakini ukweli utabaki ukweli kwamba elimu yetu ni bomu.
SWALI; Unaamini kuna siku vyuoni
wanafunzi wataandamana kupinga matokeo, na mtakuwa tayari kuyafuta?
ZOTTO; Mimi naeleweka kwa
msimamo wangu, haitatokea huo upuuzi kwangu. Kuna chuo waliniletea mizengwe
kisa niliwaambia sina marks (alama) za mezani. Ila walijua uwezo wangu na wanalitambua
hilo. Niliwaambia, mimi nitabaki kusimamia taaluma na sipendi fedheha. Hawa wanafunzi wakiwa chuoni wanataka
wapite tu hata kama hawastahili, lakini wakimaliza wanajua mwalimu gani mbabaishaji.
Katika taaluma, tuna evaluation za aina mbili, formative na summative
evaluations.
SWALI;
Takwimu zipo wapi na zinazonyesha mabadiliko ya matokeo. Je, unadhani takwimu
zitasaidia kuboresha ufaulu wa wanafunzi wetu?
ZOTTO; Mimi si muumini wa takwimu japo nilifaulu vizuri.
Udhaifu wa takwimu ni kukosa maelezo na hivyo watu kufikiri namba ni ukweli. Ina
maana gani ufaulu umeongezeka kwa desimali, maelezo yapoje?
Shule zimepata daraja la kwanza wanafunzi
6, darja la tatu ndo lukuki na la nne. Kipimo cha ufaulu ni daraja la 4 ambao
hawastahili kwenda vyuoni na tumefuta vyuo vya ufundi? Kwa sababu hiyo, naamini
kuwa wanafunzi wamefeli na matokeo ni hovyo. Ingekuwa zama zetu ambapo vyuo ni viduchu, hawa
watu wengi wasingeenda vyuo vikuu. Hata hivyo, wengi hawastahili kwenda vyuo
vikuu.
Hizi division one zimekuwa adimu kwa nini? Mwaka
wetu kati ya wanafunzi 100, zaidi ya sitini ilikuwa division one. Sasa
tunajipongeza ufaulu wa desimali na daraja la tatu na la nne? Tumeua Polytechnics,
sasa hawa daraja la nne wataenda wapi?
Kwanini sisi tunawaza kuwa maana ya elimu
ni kufika chuo kikuu tu? Plato alikuwa sahihi kutoa mgawanyiko wa elimu japo
watu wamesema kuwa ni matabaka, akatoa makundi yao Golden Boys, Silver boys na
Iron boys.Tusio na uwezo wa kuingia chuoni basi
twendeni sehemu zinazostahili. Lakini je, hivyo vyuo vipo? Hatma ya hawa laki mbili walofeli ipoje,
hii itasaidia kuleta mapinduzi.
SWALI:
Kuna vyuo vingi vimeanzishwa hapa nchini. Karibu kila mwaka utasikia chuo kikuu
kimeanzishwa. Una mtazamo gani katika suala hili?
ZOTTO: Hapana hapata shida, najiuliza mengi. Hivi
vyuo vyetu vilivyoota kama uyoga vinakidhi mahitaji ya elimu tunayoyahitaji? Kila
chuo kipya hasa binafsi vinatoa shahada ya elimu hata kama kuna upuuzi mkubwa! Mmeamua kufanya elimu kuwa biashara. Hawa
walimu wakitosha, hivi vyuo vitatoa shahada gani? Na je tuko washindani kuuza
wahitimi wetu nje ya nchi? Na hizi kozi zetu zina tija? Mitaala yetu haina
mashiko.
SWALI;
Kuna tofauti gani ya elimu ya zamani ambayo ilikuwa inafundishwa na walimu wa
UPE na waliopo sasa baadhi yao ni zao la mafunzo ya muda mfupi. Unadhani nini
hasa kinasababisha kuwa na tofauti yoyote kuzalisha wanafunzi bora kutoka makundi
haya mawili ya Walimu?
ZOTTO; Ni kweli kuna kipindi tuliambiwa kulikuwa
na walimu wa UPE na wasio na adabu wakawaita walimu weupe, hebu angalia waliopo
madarakani nani hakufundishwa na hao walimu? Leo hii hali ikoje? Sitaki turudi nyuma, lakini tujifunze kwanini
wale walifundisha na tukaandika mwandiko mzuri lakini leo hii wanafunzi
wanaingia kidato cha kwanza hawajui kuandika majina yao.
SWALI:
Katika mahojiano yetu ya kwanza ulisema wanafunzi ni wazembe kupindukia. Ni
kwanini una mtazamo huo?
ZOTTO: Wanafunzi wanapenda sana mteremko hasa huku vyuoni na haya ni matokeo
ya kubomoka ngazi za chini, wakiambiwa wakafanye citation, wao wanataka
kuandika essay kama barua iendayo kwa wapenzi wao. Yaani
ile morali ya kazi haipo tena, unaweza kuona wanafunzi wanasoma kozi fulani na
wanaiona ngumu bila sababu yoyote.
SWALI: Je wanafunzi wetu wanajibidisha kupanua uelewa
na ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi pamoja na sifa
zinazostahili?
ZOTTO: Lazima tuwe na maswali ya msingi tupate muongozo. Mitaala yetu ya elimu
inatoa fursa kwa wahitimu kuajiriwa nje ya nchi? Wanafunzi wetu wanaandaliwa
kwa masoko ya nje na wanajiamini ipasavyo?Ukimchukua
mhitimu wa chuo X atalinganishwa na mhitimu wa chuo Y ambao wote wamesoma
masomo hayohayo? Napata wasiwasi napoona baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu
hawawezi kuandika CV.
Kwenye
elimu tumekoroma maana huwezi ukajieleza kwenye usaili kwa kuwa eti CV sio
muhimu. Kitu cha kwanza kwenye usaili watahitaji kujua wewe ni nani, kwahiyo CV
mbovu itakuwezeshaje usaili. Huanzi
kuomba kazi kwa usaili bali kwa CV. Watu wanatumia vyeti vya marehemu, wengine
vya walioenda high school wakaenda kusomea ualimu.
Tukianza
kufuatilia cheti cha kila mtu makazini humu jamani sijui wangapi watapona.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako