KOZI ya makocha wa ngazi ya pili (Intermediate)
inayosimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA),
inatarajiwa kufungwa Jumanne ijayo baada ya kudumu kwa wiki nne.
Kozi hiyo ilianza Juni 3 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Harbours
Club, uliopo Kurasini chini ya Mkufunzi Rogasin Kaijage, ambaye ni Kocha wa
timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ ambapo makocha mbalimbali pamoja na
wachezaji wa zamani wamejitokeza kushiriki.
Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo alisema kozi hiyo
imekuwa na mafanikio na wanatarajia makocha walioshiriki katika kozi hiyo
watakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza mpira wa miguu katika mkoa wa Dar
es Salaan na Taifa kwa ujumla.
“Hadi sasa tunashukuru kuona tunafanikisha kozi hii ambayo
wengi wameitikia wito, mwisho wa kozi hii ndio mwanzo wa kozi nyingine.
“Lakini haya ya kozi ya makocha ni moja ya majukumu ya
Kamati ya Ufundi ya DRFA yaliyoainishwa katika Katiba, hivyo hili ni moja ya
shabaha yetu na mengine mengi mazuri yanafuata,” alisema Mharizo.
Kozi hiyo ni ya
kwanza kuendeshwa na DRFA tangu kuingia madarakani kwa uongozi mpya wa chama
hicho Desemba 12, chini ya Mwenyekiti wake Almas Kassongo.
NB; imetolewa na Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako