NA MARY ASSENGA
KITABU hiki kimeandikwa na Jim Collins. Kinaeleza ni namna gani
wakubwa Huanguka, yaani jinsi gani taasisi, watu au makampuni imara sana huanguka.Baadhi ya kampuni, taasisi kubwa, nchi, hata watu binafsi
maarufu kama vile wasanii au wa taaluma nyingine wanaofikia mafanikio makubwa
hufika muda na kuanguka. kuna imani ambayo imejengeka kwamba mtu au taasisi
baada ya kupata mafanikio makubwa ni sheria ya asili kwamba lazima kuna wakati
unafika na ataanguka. hili si kweli, ukweli ni kwamba kuanguka kuna sababu na
hizo huanzia ndani na huwa zinaweza kuzuilika kama hatua zikichukuliwa mapema.
Twende
pamoja sasa tujadili yale nilikutana nayo
Kwa kawaida kuna hatua tano ambazo hupelekea taasisi kubwa,
kampuni au mtu maarufu kuanguka na kupotea kabisa, ambazo ni kama ifuatavyo;-
1. Hatua ya kwanza ni kiburi kinacholetwa na mafaniko, mara
nyingi mtu au taasisi ikipata mafanikio huwa na kiburi na majivuno na kuona
kwamba wamefanikiwa kwa sababu labda ni wa kipekee sana kwa kuwa wana akili
sana na hawawezi kuanguka tena kirahisi na kwamba wataendelea kuzidi
kufanikiwa, ambapo husahau ile misingi, juhudi na mbinu zilizowafanya
wafanikiwe hivyo hulewa mafanikio.
2. Hatua ya pili baada ya kiburi hujiona wanaweza kila kitu
hivyo huanza kujiingiza kwenye mambo mengine ambayo hawana uwezo nayo mkubwa au
kutaka kufanya mambo makubwa sana yaliyopo nje ya uwezo wao ambapo huwashinda
au kuwasumbua sana na kupelekea kuathiri hata yale waliyokuwa wanayafanya
vizuri, hii husababisha pia kupunguza nguvu na umakini katika yale waliyokuwa
wanafanya vizuri hivyo kuanza kuathiri utendaji au uzalishaji wa huku, ambapo
pia wanakuwa hawatengeneza watu sahihi wa kuendesha hayo mapya waliojiingiza
bila kujiandaa.
3. Hatua ya tatu ni kupuuzia hatari dalili za kuwepo
matatizo ambayo yameanza kuonekana kwa ndani ya kampuni au taasisi au mtu
binfasi. Viongozi wa taasisi husika hupinga kukataa kwamba kuna hatari inakuja
kwa sababu kampuni kwa muda huo kwa nje huonekana iko imara kumbe kwa ndani
imeanza kuanguka, hutetea na kusema kwamba hapana huu ugumu ni wa muda tu,
mambo yako sawa kabisa wala sio mabaya kiasi hicho na badala yake hulaumu tu
mambo mengine badala ya kukubali kuwajibika kwa kinachoendelea ambapo halii
hupelekea hatua ya nne ya anguko.
4. Hatua ya nne ni kampuni kuanza kutafuta ukombozi baada
ya mambo kwenda mrama na mambo kuwa hadharani, mara nyingi hukimbilia kutafuta
mkurugenzi mpya atakayeiokoa kampuni au kutafuta msaada serikali, huanza
kukimbia huko na huko na kufanya maamuzi mengi ya kukurupuka katika kutaka
kujiokoa, huweka mipango na mizito kwa haraka bila hata kujiridhisha au
kuichambua kwa kina kama itasaidia ambapo kampuni huonekana kama imeanza kupata
uhai lakini unakuta ndio inazidi kupoteza mwelekeo, na kadiri inavyohangaika
kujiokoa bila kuwa na mikakati sahihi ndivyo inavyozidi kujiangamiza vibaya.
5. Hatua ya tano ni baada ya kampuni au taasisi kupoteza
nguvu na pesa nyingi sana kujiokoa na kujikuta hata imepoteza nguvu yake ya
kifedha ambapo hupoteza matumaini ya kuendelea kukua tena na mwisho hufa
kabisa, au kwa kesi nyingine wahusika huamua kuuza kampuni au kampuni kuendelea
kuhangaika na kujiingiza katika hali mbaya zaidi na matokeo yake kufa moja kwa
moja.
6. Hata hivyo kampuni nyingi kubwa zinapoweza kutambua
tatizo baada ya hali kuwa mbayo zinaweza kuweka mikakati sahihi na kurudi
katika mafanikio kabla hazijafika katika hatua ya tano ya anguko lakini mpaka
hatua ya nne kampuni ina uwezo wa kurudi katika mafanikio pale inapoamua
kufuata njia sahihi. Utafiti wa Bwana Jim Collins unaonyesha kwamba anguko
huanzia ndani na husababishwa na wahusika wenyewe na linaweza kutatuliwa na
kutokana na maamuzi sahihi ya wahusika pia.
Tunaendelea kuangalia kwa undani zaidi hizi hatua
zinazopelekea kampuni kubwa, taasisi kubwa au mtu maarufu kama vile msanii
mkubwa au mtu mwingine yeyote mwenye mafanikio makubwa kuanguka
7. Huona wanastahili mafanikio na sio yatakuja kutokana na
kujituma na kupambana sana, huona kwamba mafanikio ni lazima yatakuja bila
kujali kama kampuni inafanya nini au haifanyi nini au bila kujali msanii
anajituma au hajitumi zaidi.
8. Kupuuzia changamoto zinazojitokeza na yale
yaliyomfanya/wafanya wakafanikiwa kwa mara ya kwanza na kufikiri
mambo yataendelea tu kuwa mazuri.
9. Kuacha kujifunza zaidi mambo mapya na mambo mengi zaidi
ya namna ya uendeshaji wa kampuni.
10. Kupuuza kwamba na bahati nayo imechangia wao kufika
hapo na badala yake kufikiri kwamba ni kutokana na uwezo na umakini wao peke
yake.
11. Kutaka kuzidi kukua kwa kasi zaidi bila kujali uwezo na
watu sahihi wa kuendesha hizo shughuli zaidi wanazoanzisha ambapo hupelekea
kuvuruga ule utamaduni wa kampuni husika na kushindwa kufanya mambo kwa ubora
unaistahili.
12. Kuendelea kuondoka kwa watu sahihi katika yale maeneo
muhimu kutokana na kupoteza watu bora na sahihi zaidi au kukuza kampuni kwa
kasi kiasi cha kukosa watu sahihi wa kutosha kushikilia nafasi mpya
zilizotokana na kukuza kampuni.
13. Kampuni au taasisi kupandisha bei za huduma au bidhaa
kutokana na kukua kwa gharama za uendeshaji badala ya kukuza nidhamu ya
utendaji na uendeshaji wa kampuni.
14. Wafanyakazi kutozingatia utamaduni na kauli mbiu za
kazi na kupoteza ile ari iliyojengwa na kampuni na badala yake kufanya kazi
kama kazi badala ya kazi kama majukumu na wajibu.
15. Mabadiliko ya uongozi wa kampuni yanayopelekea kupata
viongozi dhaifu, kushindwa kutengeneza viongozi bora ndani ya kampuni,
misukosuko ya kisiasa, mikosi na kushindwa kuchagua viongozi sahihi wa kurithi
nafasi za uongozi ndani ya kampuni.
16. Maslahi binafsi kuwa juu ya maslahi ya kampuni kama
vile utajiri binafsi, heshima binafsi, umaarufu, kufanya mambo yatakayokupa
ufahari wa muda mfupi badala ya kuwekeza katika kujenga kampuni itakayokuwa
imara kwa miaka mingi mbele.
17. Kulaumu hali ya nje ya kampuni na kukataa kuwajibika
kwamba matatizo yako ndani ya kampuni yenyewe na viongozi kuzungumza na kuona
zaidi matatizo kutokana nje ya kampuni kuliko kutoka ndani.
18. Kuongoza kampuni kutokana na takwimu zisizo sahihi na
kufanya maamuzi kutokana hizo taarifa zisizo na uhakika au za kutengeneza
lakini sio uhalisia.
19. Kutopenda kukosolewa na kuambiwa ukweli mchungu na
badala yake, kutaka zaidi kuungwa mkono kwa kila jambo na kuambiwa yale
yanayokufurahisha na unayotaka kusikia peke yake, pia kupenda kuheshimiwa na
kunyenyekewa kama mtu mwenye hadhi kubwa.
20. Kuhangaika kufanya mabadiliko mengi ya hovyo hovyo
haraka haraka kama kubadili mbinu, viongozi, miradi, programu mpya kila wakati
bila mafanikio yoyote.
21. Kuwa na mafanikio makubwa au ya kawaida sio kwa sababu
hakuna changamoto au nyakati ngumu bali uwezo na uimara wa kupambana na
changamoto hizo na kurudi kwenye mafanikio makubwa kuliko uliyokuwa nayo mwanzo.
Mataifa makubwa yanawezo kuanguka na kusimama upya, Makampuni makubwa zinaweza
kuanguka na kusimama upya, Taasisi za kijamii zinaweza kuanguka na kusimama
upya, watu wakubwa na maarufu wanaweza kuanguka na kusimama upya, ilimradi
huchoki wala kukata tamaa matumaini yapo makubwa.
©Mary Assenga
No comments:
Post a Comment
Maoni yako