September 20, 2017

SAMORA MACHEL: WEMA HAWADUMU

NA PASCAL MWAKYOMA

Samora Moisés Machel alizaliwa tarehe 29 Septemba,1933 katika kijiji cha Madragoa (kwa sasa Chilembene), mkoa wa Gaza nchini Msumbiji au Mozambique. Alikuwa Kamanda wa Jeshi la Msumbiji, Mwanamapinduzi, Mjamaa na mwenye msimamo mkali wa Kimarx na Kilenin aliyeiongoza nchi ya Msumbiji tangu uhuru wake mwaka 1975 hadi kifo chake kilichotokea usiku wa tarehe 19 Oktoba 1986 katika eneo la milima la Mbuzini, mpakani mwa Msumbiji, Swaziland na Afrika Kusini.
Katika harakati za kupigania uhuru wa Msumbiji kutoka kwa wakoloni wa Kireno, Samora Machel alihudhuria mafunzo ya kijeshi ya kujitolea mjini Dar es Salaam na baadaye alikuwa ni miongoni mwa wapiganaji wa chama cha FRELIMO waliopelekwa nchini Algeria kwa ajili ya mafunzo zaidi. Aliporejea Tanzania kutoka Algeria, Samora Machel aliteuliwa kuongoza kambi ya mafunzo ya wapigania uhuru wa FRELIMO iliyokuwa KONGWA mkoani Dodoma.


Baada ya FRELIMO kuanzisha vita vya kudai uhuru wa Msumbiji tarehe 25 Septemba, 1964, Samora Machel alitokea kuwa Kamanda mahiri na muhimu sana katika mapambano hayo ambaye jina lake lilivuma kwa kasi mno miongoni mwa Makamanda na wapigania uhuru wa FRELIMO kutokana na umahiri wake katika medani. Na kutokana na umahiri huo, alipanda vyeo kwa haraka ndani ya jeshi la wapigania uhuru wa msituni lililokuwa likijulikana kama FPLM hadi kufikia cheo cha Kamanda wa Jeshi baada ya Kamanda wa Kwanza wa Jeshi hilo, Filipe Samuel Magaia, kufariki mwaka 1966. Na katika uchaguzi wa mwaka 1970, Samora Machel alichaguliwa kuwa Rais wa FRELIMO.



Kamanda mpya wa Jeshi la Kireno la Msumbiji, Jenerali Kaúlza de Arriaga, alitamba kuwa angewasambaratisha na kuwaangamiza kabisa wapiganaji wa FRELIMO kwa muda wa miezi michache tu lakini hakufua dafu licha ya kuanzisha mashambulizi makali mno katika mpango wake wa Operation Gordian Knot mwaka 1970 akielekeza mashambulizi zaidi katika ngome za FRELIMO zilizokuwa Cabo Delgado kaskazini ya mbali ya Msumbiji. FRELIMO chini ya Samora Machel ilijibu mapigo na kuhimili vishindo hivyo ambapo ilianza mashambulizi kutoka kila upande na kuelekeza nguvu upande wa magharibi mwa nchi katika mkoa wa Tete. Mpaka kufikia mwaka 1974, Wareno walikuwa hoi bin taaban katika uwanja wa mapambano.

Baada ya kupigwa vya kutosha, Wareno walikubali kutia saini makubaliano tarehe 7 Septemba, 1974 mjini LUSAKA kwa ajili ya kukipa mamlaka kamili chama cha FRELIMO na tarehe rasmi ya Uhuru wa Msumbiji ikapangwa iwe 25 Juni, 1975. Serikali ya mpito iliundwa ikiwa na Baraza la Mawaziri lililojumuisha FRELIMO na Wareno ikiongozwa na Waziri Mkuu JOACHIM CHISSANO. Samora Machel aliendelea kuongoza akiwa Tanzania hadi aliporejea nyumbani Msumbiji kishujaa katika safari iliyoitwa “KUTOKA RUVUMA MPAKA MAPUTO”.

Siku ya tarehe 19 Oktoba, 1986, Rais SAMORA MACHEL alikwenda kuhudhuria mkutano mjini Mbala, Zambia, ulioitishwa kumshinikisha Dikteta MOBUTU SESE SEKO wa Zaire juu ya uungaji wake mkono kwa chama cha upinzani cha Angola cha UNITA. Mkakati wa nchi zilizokuwa Mstari wa Mbele ulikuwa ni kupingana na Mobutu Sese Seko na Hastings Kamuzu Banda katika nia ya kumaliza kabisa uungaji wao mkono kwa UNITA na RENAMO, vyama au makundi ambayo nchi hizo ziliyaona kama wasaidizi au vibaraka wa Afrika Kusini.

Japokuwa mamlaka za Zambia zilikuwa zimemwalika Samora Machel kukaa mjini Mbala usiku mzima, yeye alisisitiza kurejea Maputo usiku uleule kwa kuwa asubuhi yake, alikuwa amepanga kuwa na kikao chenye lengo la kufanya mabadiliko katika uongozi jeshini.

Kutokana na umuhimu wa kikao hicho kilichokuwa kimepangwa kifanyike asubuhi yake, Samora Machel alikiuka hata maelekezo ya Wizara ya Usalama kwamba Rais hakupaswa kusafiri usiku.
Na kweli Samora Machel aliondoka usiku wa tarehe 19 Oktoba, 1986 kwa ndege kurejea Maputo, lakini kwa bahati mbaya hakuweza kuiona tena Maputo kama alivyokuwa amepanga. Ndege yake ilianguka eneo la milima la Mbuzini mpakani mwa Msumbiji, Swaziland na Afrika Kusini, tena upande wa ndani ya Afrika Kusini; yeye Kamanda Samora Machel na watu wengine 33 walipoteza maisha huku watu 9 waliokuwa wamekaa viti vya nyuma ya ndege wakinusurika. Inaaminiwa kwamba ndege yake ilidunguliwa na utawala wa Kibaguzi wa Afrika Kusini wa wakati huo. Safari ya mwisho ya maisha ya Samora Moisés Machel wa Msumbiji ikawa imeishia hapo.

©Pascal Mwakyoma.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako