October 06, 2017

ALFRED NOBEL: MHANDISI MWANZILISHI WA TUZO YA NISHANI YA AMANI YA NOBEL.


NA KIZITO MPANGALA, 0682 555 874

ALFRED NOBEL ni mtu aliye wazi masikioni mwa wengi lakini akifahamika zaidi kwa jina lake la mwisho yaani Nobel kutokana na tuzo aliyoianzisha katika amani, lakini kwa sasa tuzo hiyo imepanuliwa zaidi, haipo katika amani tu, bali ipo katika uga mwingi duniani na washindi wanapatikana kila mwaka kulingana na uga husika ambayo hubebwa na jina lake la mwisho yaani Nobel. 

Nobel alizaliwa Oktoba 21, 1833 jijini Stockholm nchini Sweden. Alikuwa ni mvumbuzi, mtaalamu wa Kemia, mfanyabiashara, mwanaphilanthropia na mhandisi katika viwanda mbalimbali ambavyo kati ya hivyo vipo vilivyomiliki yeye mwenyewe kikiwemo kiwanda cha Bofors ambacho kilikuwa kinajishughulisha na kufua vyuma na vyuma vya pua.
Alfred Nobel.
Alizaliwa katika familia ya kipato cha chini ambapo baba yake Mzee Emmanuel Nobel alikuwa mhandisi pia. Katika malezi yao Alfred Nobel na wadogo zake watatu walisalimika kuishi miaka mingi zaidi wakati wenzao waanne wakipoteza uhai kwa sababu mbalimbali. Hivyo kati ya watoto nane wa Mzee Immanuel Bernhard Nobel, bwana Alfred alijihusisha na kazi ya baba yake. Alijiunga katika mafunzo ya uhandisi katika himaya ya Mwanasayansi wa Sweden bwana Olaus Rudbeck ambapo alipendelea zaidi masuala ya milipiko (explosives) jambo ambalo alianza kulipenda kwa kujifunza misingi yake alipokuwa na baba yake nyumbani.


Baadae alilazimika kufuatana na baba yake huko Urusi na kuishi katika jiji la St. Petersburg na kufanya kazi ya uundaji wa mashine mbalimbali na baruti za kiwango cha kawaida. Hii  ni baada ya baba yake kushindwa katika harakati kadhaa za biashara ndipo alipoamua kwenda Urusi ambako kipawa cha Alfred Nobel kiliongezeka zaidi.  

Katikati ya mwaka 1867 na 1887 alifanya ugunduzi wa baruti kali ambayo inatumika katika silaha za kivita hasa milipuko, lakini lengo lake kuu lilikuwa itumike katika upasuaji wa miamba migodini, na katika kutobolea sehemu za milima ambazo zilihitajika kupitishwa reli. Alifanikiwa katika hilo na lilimuongzea kipato zaidi. Kutokana na utaalamu huo, leo hii katika Kemia kuna elementi ambayo inaitwa Nobelium ambayo ni elementi iliyo katika kundi la elementi za kisasa (Synthetic Elements) 

Hapo wazazi wake walipopata morali ya kumuendeleza zaidi Alfred. Walimpeleka katika shule mbalimbali ikiwemo Ufaransa, Marekani, na nyumbani kwao Sweden. Baada ya mafunzo ya miaka kadhaa, yeye na wazazi wake walirejea kwao Sweden kutoka Urusi na wakaanzisha kiwanda cha kisayansi kwa mara nyingine baada ya kiwanda cha kwanza kilichoanzishwa na baba yake kufilisika na kukumbwa na mlipuko ambao ulisababisha kifo cha mdogo wake wa mwisho, jambo hilo lilipelekea magazeti mengi kuchapisha taarifa inayofanana kimakosa ikimtuhumu Alfred Nobel kumfanyia mdogo wake majaribio ya kulipua baruti aliyoivumbua na ikasemwa na yeye mwenyewe amefariki. Magazeti mengi yalichapisha habari hiyo yenye kichwa cha “LE MERCHAND DE LA MORT ES MORT” ikiwa na maana ya “BEPARI WA KIFO AMEFARIKI” yaani “THE MERCHANT OF DEATH IS DEAD”. 

Alifaulu kuanzisha kampuni zake za masuala ya kisayansi ambazo ziliendelezwa na wengine baada ya kifo chake, na hivi sasa bado zipo. Kampuni hizo ni pamoja na AkzoNobel na Dynamite Nobel. Baruti alizozivumbua kwa ujumla ziligawanyika katika makundi matatu ambayo ni GELIGNITE, BALLISTITE, na CORDITE.

Licha ya kutopata elimu ya sekondari na chuo kikuu, aliweza kuzimudu     lugha sita ambazo ni Kijerumani, Kiswidishi, Kiitaliano, Kirusi, Kiingereza, na Kifaransa. Pia aijifunza fasihi na kuwa mwanafasihi hasa katika ushairi kutokana na kumbukumbu aliyoiacha katika kitabu chake cha ushairi (diwani) kilichoitwa NEMESIS, na tamthiliya katika kitabu cha ESPERANTO.
Mwanzilishi wa tuzo ya nishani ya Nobel Bw. Alfred Nobel akitafakari jambo.

Alfred Nobel alifikwa na wasiwasi mwingi katika ugunduzi wake wa baruti kali baada ya kuona matumizi yake katika silaha za kivita yamekuwa ni ya kuangamiza uhai wa wengine wengi duniani. Hakukata tamaa, alitafuta mbimu itakayoweza kusaidia kupunguza matumizi ya baruti hiyo katika mauaji mbalimbali yafanywayo kwa milipuko. Hapo ndipo alipata wazo kuu la AMANI. Baruti yake ilisifika na bado inasifika kwa kuwa na uwezo wa kuua watu wengi zaidi kwa wakati mmoja. Hii ni ile inayotumika katika mauaji ya kimbari. 

Aliiheshimu sana amani katika ulimwengu huu hasa zama alizokuwepo ambapo mbio za mapinduzi ya kisayansi katika viwanda zilishika kasi sana, hivyo alihofia sana suala la matumizi holela ya baruti aliyoivumbua ambayo inatumiwa katika silaha kama ilivyokwishasemwa awali. Hivyo basi, katika hati yake ya wosia alianzisha TUZO YA NOBEL kwa ajili ya mafanikio ya kisayansi lakini pia kwa ajili ya amani duniani ambalo ndilo jambo lililomsukuma sana. Baruti hiyo kwa sasa imekuwa msingi mkuu wa uundaji wa mabomu yanayotegwa chini ya ardhi. 

Mwaka 2001, mtoto wa mdogo wake Alfred Nobel  bwana Peter Nobel aliiomba Benki kuu ya Sweden kuanzisha nishani nyingine ya masuala ya uchumi ambayo itabebwa na jina la Nobel jambo ambalo limefanikishwa. Na zaidi ya hilo, nishani hii ya Nobel sasa imekuwa nishani kubwa zaidi duniani ambapo imejikita katika uga mbalimbali ikiwemo Sayansi, Hisabati, Uchumi, Fasihi, Amani na kadhalika. 
Mojawapo ya medali za tuzo ya nishani ya Nobel.


Mwaka huu 2017 kikundi kinachopinga matumizi ya silaha za nyuklia ndio kilichoshinda tuzo hii ya Nobe. Hatupaswi kumlaumu Alfred Nobel, yeye tayari alishaona dosari ya matumizi ya baruti hiyo ndipo alipobuni mbinu ya kuepuka matumizi holela ya baruti hiyo kwa utoaji wa tuzo kwa aneyekuwa mstari wa mbele kuhimiza amani duniani. Alifariki miaka minne kabla ya kuingia karne ya 20, yaani mwaka 1896, 10 Disemba.

Baadhi ya watu ambao wamewahi kutunukiwa nishani hii katika uga mbalimbali ni Nelson Mandela, Kalamcnand Mahatma Gandhi, Mama Teresa wa Kalkuta, Kazuo Ishiguro, Albert Einstein na kadhalika.

© Kizito Mpangala        

No comments:

Post a Comment

Maoni yako