October 06, 2017

WAKOLONI WALITUPOTOSHA KWA ELIMU YAO

NA HONORIUS MPANGALA, 0628 994409

MIONGONI mwa mambo ambayo waafrika hatutakiwi kujiuliza kuhusu wakoloni na wawekezaji kwanini wanapenda kukimbilia kuwekeza au kama walivyokuja kutawala afrika,jibu ni jepesi tu, utajiri wetu. Utajiri wa bara la afrika unatokana na uwepo wa rasilimali alizotuzawadia mwenyezi mungu Tangu anaiumba hii dunia.

Wako wengi wanaoshangaa wanapoambiwa kuwa katika karne ya 15 maendeleo kati ya afrika na ulaya yalikuwa sawa. Ni miongoni wa maswali yaliyopendwa sana kuulizwa katika mitihani ya somo la historia kwa masomo kidato cha tano na sita, kuwa inasadikika katika karne ya 15 maendeleo kati ya Afrika na Ulaya yalikuwa sawa. 

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akiwa na baadhi ya watanzania wanaoishi nchini Marekani.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa na baadhi ya makatibu mbalimbali
 Hapo ndipo uliweza kuona watu wakitumia mifano mbalimbali ya kirejea kutoka kwa misafara kama ya mabaharia kina Bartholomew Diaz,Vasco Da Gama na Hata Christopher Columbus. Kitu pekee kilichosababisha kuliacha bara la afrika likawa na utofauti kuanzia karne ya 15 hadi sasa na kuonekana hakuna ulinganishi wowote utakaoweza kujionyesha uwiano wa kimaendeleo kati yao na sisi waafrika.


Ziko sababu lukuki zilizochangia tuendelee kupiga ‘mark time’ kama gwaride la mgambo wa jiji la Lubumbashi kule Kongo.  Sehemu kubwa ambayo wazungu walifanikisha ni kushika akili zetu na kutuaminisha katika mambo yasiyokuwa na msaada wa kutufanya tupige hatua ya kimaendeleo.

Upelelezi wa wazungu kabla ya kuja kututawala ulikuwa wa vitu vingi japo kuwa wanahistoria wetu wanaeleza tuu wapelelezi walitafiti maeneo yenye rutuba na hali nzuri ya hewa ili walowezi na wakoloni wanaweza kuishi na kufanya Kazi zao na kujiona wakiwa katika mazingira yanayofanana na wao kwa hali ya hewa.

Kitu ambacho naamini hakikuwekwa wazi ni upelelezi juu ya uwezo wetu wa kiakili katika utendaji wa Kazi na kuchanganua mambo. Hapo ndipo mzungu alipoona umahiri wetu wa matumizi mazuri ya akili lakini tulilwamishwa na mazingira yaliyotunzunguka tu.
Baada ya kugundua hilo waliona kuwa endapo tutawapa ujuzi ka upatikanao kwetu (ulaya) basi waafrika wangeweza kupiga hatua Kali zaidi katika maendele ya bara kiujumla. Labda tu niwaambie mwenyezi Mungu aliwaumba wanadamu na kuwaweka duniani kutazama mambo kadhaa ikiwapo ni wapi akae kutokana na uwezo wake wa kuhimili hali ya hewa ya maeneo husika. Ndio maana ni nadra kusikia seruji imedondoka Afrika, au kusikia Magonjwa ya Mafua ya ndege au Mafua ya nguruwe na mengineyo.

Uwepo wetu barani afrika ni kutokana na tabia ya nchi na hali ya hewa kiujumla ambayo watu wa ngozi nyeusi wamudu vyema kuwepo katika mazingira haya. Tukija katika suala la magonjwa kama Ebola ,malaria ni rahisi sana kusambaa ktk bara letu kutokana na hali ya hewa ya bara letu kwa ujumla.

Bara letu lina hali zote zinazopatikana katika Tabia ya nchi yaani Tabia ya kiikweta,kitropiki na kijangwa. Sababu ya elimu ndiyo pekee iliyokuwa chenga kubwa waliyotupiga wazungu kwa kutuchagulia aina hii ya elimu ambayo imeendelea kufuatwa karibia na mataifa mengi ya afrika.

Mfumo wa elimu waliotuanzishia tumekuwa tukipambana sana kuubadili katika maeneo tofauti lakini tumeshindwa kuwaondoa watu katika dhana ya kuajiriwa na kupata maarifa ya kuweza kujiajiri na kusaidia kuondoa tatizo la ajira katika bara letu kwa sababu tu ya aina ya elimu tuliyoipata.

Wazungu baada ya kuona babu zetu wana uwezo mkubwa wa kutumia akili na mikono yao katika kuunda vitu mbalimbali hivyo laiti kama wangekuwa na viwanda basi akili za vizazi na vizazi zingeegemea huko tofauti na walichokifanya cha kuvunja viwanda vyetu vya asili na kutuelekeza katika elimu ya kuelekea kuajiriwa katika serikali ya mkoloni tena kwa ngazi za chini sifa ikiwa tu anafanya kwenye serikali ya mkoloni.

Elimu ya ufundi ndiyo pekee iliyokuwa na msingi wa maendeleo ya viwanda kwa kuanzia chini hadi kufikia mambo ya teknolojia. Na hii ndiyo ambayo ingekuwa na msaada mkubwa kwa Afrika kwa sababu ingesaidia kuinua maendeleo ya bara la afrika.

Kunyimwa kwetu elimu ya ufundi ambayo Leo hii imeweza kudhihirika duniani kuwa sayansi na teknolojia imetokana na masuala ya ufundi ambayo yamekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo. Akili ya woga wa waafrika kupenda kufanya Kazi maofisini kwa kutumia kalamu ilikuwa ni heshima sana na kuwafanya wajione wana mazingira ya kizungu na kuona washika spana ni watu ambao hawana elimu yeyote.

Akili ya kujiona ni hadhi sana na kuthaminiwa kufanya kazi maofisini kwa kutegemea kalamu kulifanya akili za waafrika kuwa 'dormant' na kudhani aliyeko kiwandani ni mjinga na hajapata elimu. Tulijengwa katika mazingira ambayo leo hii babu zetu waliishia kutusimulia nilifanya kazi na wakoloni pasipo kuelezea faida iliyopatikana kimaarifa baada ya kuachana na wakoloni.

Laiti kama elimu ambayo wangetoa ingekuwa ya ufundi wa mambo mbalimbali ungetengeneza msingi bora wa kuwaandaa watu kuiljiajiri na kusaidia kuinua maendeleo ya nchi au bara letu. Ni dhahiri usemi wa asemaye kuajiriwa ni woga wa maisha unaweza kuwa kweli kutokana na mazingira yaliyopo kwa kuhusisha elimu tupatayo na ongezeko la wanaohitaji kuajiriwa na sio kujiajiri.

Akili tuliyonayo ukiona mtu kujiajiri tunaamini hakubahatika kusoma na aliyeajiriwa kabahatika kusoma jambo ambalo ni kinyume kabisa na linalotengeneza utegemezi wa akili katika kuishi. Hakuna tajiri duniani aliyeajiriwa ila tajiri anaajiajiri kwa kutenda mambo yake kwa elimu aliyoipata.
Nimetazama video moja ya mtoto wa kichina ambaye kwa mwonekano hajafikisha umri miaka 12 lakini elimu ya ufundi na teknolojia aliyoipata itamfanya apende zaidi na zaidi kitu anachokuwa nacho kwa sababu amejifunza angali mdogo na anakipenda.

Mtoto anaendesha Katapila na kunifanya nifikirie mbali zaidi juu ya msingi wa elimu yetu tuliyoachiwa na wakoloni nikatazama elimu yao,mwisho wa siku najipa majibu kuwa wakoloni kuna walichokigundua toka kwetu endapo tungepata elimu ya ufundi na teknolojia ambayo leo hii imekuwa msaada mkubwa katika maendeleo dunia kwa sasa.

Kuna watu kadhaa waliwahi kuniambia kuwa ukitaka kutazama utofauti wa elimu ya ufundi na ile ya kutumia kalamu basi wachukue watu waliosoma masuala ya mabomba (plumbing)' yule aliyeko vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) na yule aliyeko Chuo Kikuu kwa kozi hiyo hiyo na wakufanyie matendo ya namna ya kutengeneza ‘Intake’ ya maji.

Utakacho kipata ni mambo mawili tofauti yule wa VETA atakuwa mzuri sana katika elimu ya matendo wakati yule wa Chuo kikuu anaweza kuwa bora katika maelezo lakini kutenda ikawa tofauti, nafikiri unaweza kuwa shahidi wa maeneo yako.
Unakutana na injinia yeye ni injinia wa makaratasi tu na sio wa kufika eneo la kazi na kutenda. Hii yote ni kutokana na akili zetu za kuamini kazi ya matumizi ya kalamu na sio nyundo, koleo, au spana. Tunatakiwa kubadilika kiakili na kutambua kuwa elimu ya ufundi na teknolojia ndiyo ambayo ingekuwa msaada mkubwa sana kwa vizazi na vizazi.

Hatuwezi kutamani kuwa na nchi ya viwanda wakati akili za wanafunzi na wananchi kwa ujumla hazibadilika na kuona kuna kila sababu ya kuvitumia vyuo vyetu vya ufundi na teknolojia pamoja na mashule yetu ya ufundi kuwa ndiyo msaada pekee wa kutoa mazao ya hao watakaokuja kuwabadilisha wengine na kuhamasisha umuhimu wa elimu hii ya ufundi na teknolojia.

Kama tukawaanda watu wakasoma kozi mbalimbali na baadaye tukawajenga katika kutambua ujenzi wa nchi au bara unafanywa na wenyeji kwa kuwa na elimu nzuri ya ufundi na teknolojia kwa sababu tuko katika karne inayotumia teknolojia zaidi kuliko nguvuwatu. Hebu fikiria kama itatokea watoto wakapata maarifa kwa kutumia teknolojia huko madarasani unajiuliza Mwalimu amayetegemea kalamu ama nguvu yake kufundisha atakuwa na kazi gani.

Kila mmoja atathimini elimu tupatayo na mchango wake katika maendelo ya nchi hii. Tukumbuke neno maendeleo linatoa taswira ya uchumi wa nchi au mahali fulani. Ulaya tunao waona wanamaendelo ni kutokana na kujikita katika teknolojia na ufundi.

Ifike mahali tutambue nini tunataka , tuna watu gani wanaoweza kutupatia hicho tunachokitaka. Unaposema viwanda lazima uandae akili ya watu wako kimtazamo kujielekeza katika viwanda kwa kuvipa hadhi vyuo vya ufundi ambayo ndiyo kichocheo cha maendeleo ya viwanda.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako