October 30, 2017

SEBASTIAN KURZ; Kiongozi mbichi anayeugusa ulimwengu



NA MWANDISHI WETU

“ULIKUWA unafanya nini ulipokuwa na umri wa miaka 31? Hiyo ni sentensi ya kwanza iliyoandikwa na Mwanahabari wa Televisheni ya CNN, James Masters, kwenye tovuti ya CNN. Sentensi hiyo ilinivutia zaidi, ingawa aliendelea na mengine, lakini staili pekee haikuwa kivutio, bali mtu aliyekuwa akizungumzwa alivutia zaidi. 

Mwandishi James Masters alikuwa anamzungumzia kijana mmoja aitwaye Sebastian Kurz kutoka Austria. Ni kijana ambaye anazidi kuvutia duniani kutokana na siasa zake ambazo kwa namna moja au nyingine ziliibua nchi hiyo kwenye ramani ya kidiplomasia. 

Baada ya hapo nililazimika kufuatilia habari zaidi za Sebastian Kurz. Niliyokutana nayo ni somo, ingawa kwa Tanzania lilianza muda mrefu.
Nimekuandalia makala haya msomaji ili kujifunza jambo katika malezi ya familia na taifa kwa ujumla. Austria ipo tayari kwa kiongozi kijana? Fuatilia.

Sebastian Kurz ni nani?

 
Kijana huyu alizaliwaAgosti 27, mwaka 1986. Kwa sasa ana umri wa miaka 31 tu. Yeye ni mwenyekiti wa chama cha Austrian People’s Party (OVP) tangu Mei, mwaka huu. Baba yake ni Josef Kurz, ambaye alikuwa injinia. Mama yake ni Elizabeth Kurz, ambaye kitaaluma alikuwa mwalimu. Amekulia katika jiji la Vienna, ambalo ndilo makao makuu ya serikali na mji wa kibiashara nchini humo. Sebastian ni muumini wa Kanisa Katoliki. Anatajwa kuwa ni Mkatoliki mhafidhina. 

Miaka ‘mitatu mitatu’ ya dhahabu
Baaadhi ya wazungu wanahusudu sana mchezo wa namba. Katika mchezo wa soka namba 13 inatajwa kuwa yenye mkosi. Mifano mbalimbali inatolewa, lakini hali hiyo ni tofauti kwa miaka mitatu mitatu ya dhahabu kwa Sebastian. Iko hivi, mwaka 2009, akiwa na miaka 23, alichaguliwa kuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama cha OVP. 

Aidha, Sebastian alipokuwa na miaka 24 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Austria. Miaka mitatu baadaye alipotimiza miaka 27, yaani mwaka 2013, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Katika kipindi hiki aliwahi kuitisha mkutano wa mawaziri 30 wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Ulaya uliofanyika nchini Austria. Mnamo mwaka 2014, alichaguliwa kuwa mbunge kupitia chama cha OVP. 

Kutoka umri wa miaka 24 hadi 27, tofauti ni miaka mitatu. Kutoka umri wa miaka 27 hadi 31, tofauti yake ni miaka mitatu na nusu. Hii ina maana wakati mwaka huu ukiwa wa tatu tangu akabidhiwe cheo cha uwaziri wa mambo ya nje, amechaguliwa tena kuwa Kansela wa Austria. 

Kwanini amekuwa Kansela?
Katika umri wa miaka 31, Sebastian Kurz anakabidhiwa majukumu makubwa ya kuiongoza Austria, baada ya rais wa nchi hiyo, Alexander Van der Bellen, kumuomba aunde serikali ya kitaifa na chama kingine cha Freedom Party. Uchaguzi uliofanyika mwaka huu ulikipatia chama chake cha OVP asilimia 31.4 ya kura zote. Vyama vingine vilipata alama zifuatazo; Freedom Party (27.4%) na Social Democrats (26.7%). Kutokana na ushindi huo,  haukumwezesha kuunda serikali, hivyo kulazimika kuungana na chama cha Freedom Party kuunda serikali. 

Ni mtaalamu wa nini?
Sebastian ana shahada ya sheria aliyopata kutoka Chuo Kikuu cha Vienna mara baada ya kumaliza mafunzo ya lazima ya Jeshi la Kujenga Taifa la Austria.

Mdogo kama Kim, Macron
Nchini Ufaransa walijivunia kiongozi mwenye umri mdogo zaidi, Emmanuel Macron (39). Nchini Korea Kaskazini pia wanajivunia kiongozi mdogo zaidi, Kim Jong-Un, mwenye umri wa miaka 33. Pamoja na Canada ambao walimpa waziri mkuu mdogo kuliko wote, Justin Trundeau mwenye umri wa miaka 45.  Pia ni kama Leo Vardarkar mwenye umri wa miaka 38 na raia wa Ireland, ambaye aliteuliwa kuwa waziri wa Usafirishaji, Utalii na Michezo mwaka 2011.
Naam, wananchi wa Austria wanamwona Sebastian Kurz kama Emmanuel Macron, Justin Trudeau, Leo Vardarkar, Kim Jong-Un kutokana na umri mdogo, lakini wamebeba matumaini makubwa ya uongozi wa nchi zao. 

Nyerere, Salim na Kabila
Katika suala la uongozi hapa nchini pia zipo rekodi za viongozi vijana. Mwalimu Julius Nyerere alikabidhiwa urais akiwa na miaka 40. Salim Ahmed Salim alikabidhiwa ubalozi wa Misri akiwa na miaka 22. Naye rais wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, aliukwaa urais akiwa na miaka 29 tu. Kwa namna fulani utaona kuwa, dunia imekuwa na mabadiliko ya hapa na pale kwa viongozi wengi vijana kukabidhiwa majukumu makubwa. Sababu kubwa ni kwamba, wanakuwa na vitu vya ziada kuliko wengine pamoja na kuaminiwa au kuwa sehemu ya mtandao wa wanasiasa wenye kukabidhiana madaraka. 

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika ya habari.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako